Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING (K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda cha maziwa Wilayani Makete?

Supplementary Question 1

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Makete tumekwenda pale na Waziri kutembelea kile kituo tukaona kwamba idadi ya ng‟ombe wanaotakiwa kuwepo pale ni 4,000 lakini sasa hivi wako ng‟ombe 750 tu. Ni Lini Serikali itapeleka ng‟ombe wa kuzaliana Kitulo? Ahsante.

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa majibu yaliyokuwa yakiendelea Mheshimiwa Naibu Waziri na swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na Kituo cha Kitulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namuunga mkono kabisa kwamba Kituo chetu cha Kitulo ndiyo Kituo pekee cha uzalishaji wa Ng‟ombe wa maziwa bora hapa nchini kwetu, na ni kweli kabisa kwamba idadi ya Mifugo imepungua kwenye lile shamba letu; na kama yeye mwenyewe alivyosema hivi karibuni nilikuwa kwenye ziara katika eneo hilo.

Nataka tu nimhakikishie kwamba tunakamilisha mipango ya kuhakikisha kwamba shamba letu hilo tunaliboresha upya kuanzia uoteshaji wa nyasi katika shamba lenyewe pamoja na miundombinu mingine iliyochakaa. Vilevile kuhakikisha kwamba ng‟ombe wanarejeshwa mle, kwa maana ya kuongeza idadi ya ng‟ombe, ili iendane na ukubwa wa eneo na mahitaji ya wananchi ambao kwa sasa wanahitaji mitamba mingi sana kila sehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tukuhakikishie kwamba ujio wangu ule ndiyo ilikuwa mipango ya kuanza kununua ng‟ombe wengine na kujaza kwenye hilo shamba lakini na kuhakikisha kwamba mahitaji ya wananchi wa Tanzania wanaohitaji mitamba bora kutoka Kitulo wanaipata mitamba hiyo.

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING (K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda cha maziwa Wilayani Makete?

Supplementary Question 2

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa swali la nyongeza Mkoa wa Njombe ni moja ya Mikoa yenye hali ya hewa nzuri ambayo inaruhusu ng‟ombe wa maziwa kuweza kustawi na kuzalisha maziwa ya kutosha. Je, ni nini Mkakati wa Wizara kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao wanapenda kufuga wanapata ng‟ombe bora wa kisasa ili uzalishaji uongezeke na pia ili Viwanda viweze kupata malighafi za kutosha? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati wa Serikali katika kuhakikisha tunaongeza idadi ya ng‟ombe katika Mkoa wa Njombe. Majibu ya msingi na majibu ya ziada yaliyojibiwa na Mheshimiwa Waziri yameeleza wazi juu ya Mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya mitamba katika mashamba yetu ya Serikali likiwemo Shamba la Kitulo lililopo katika Mkoa huo wa Njombe; pia vilevile shamba letu la sao hill lililoko pale Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hii kwa pamoja, pamoja na mikakati mingine ya kuanzisha makambi ya uhimilishaji wa ng‟ombe mikoani, ambao tunaendelea nao hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini ya kuongeza mbali ama breed za kisasa za ng‟ombe watakaotuletea tija zaidi inayokwenda sambasamba na kutuhakikishia kufikia katika lengo la kuwa na ng‟ombe wa maziwa wa kutosha nchini kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa tuna takribani ng‟ombe milioni moja wa maziwa wazuri; na mkakati wetu ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2021/2022 tuwe na jumla ya ng‟ombe milioni nne watakao kuwa ng‟ombe wazuri wa maziwa kwa ajili ya uzalishaji mkubwa wa maziwa na kuingiza katika viwanda vyetu.