Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Primary Question

Kumekuwa na tatizo kubwa katika jamii yetu la ubakaji wa watoto wadogo chini ya miaka mitano na vikongwe:- Je, Serikali imeshawahi kufanya utafiti ili kujua chanzo cha tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vitendo hivi vinasikitisha sana. Huwezi ukakuta ng’ombe dume anapanda ndama, huwezi ukakuta jogoo anapanda kifaranga lakini binadamu aliyepewa utashi anafanya vitu hivyo. Ukiangalia trend ya matukio yanaongezeka kwa kiasi kikubwa. Matukio 13,457 mwaka 2018 yameongezeka kwa 1,000 lakini ukienda Mahakamani hukuti hizi kesi. Je, Wizara ina mkakati gani kuhakikisha haya matukio yote inasimamia upatikanaji wa ushahidi na kuhakikisha yanakwenda Mahakamani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sehemu kubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinasababishwa na mila na desturi potofu. Kwa mfano, katika mila za Kihehe kuna utamaduni unaitwa Nyangusage, katika tamaduni za Kisukuma kuna mila inaitwa Chagulaga na Kigoma kuna Teleza. Wizara ina mkakati gani wa kutoa elimu kuhakikisha mila na tamaduni potofu zinatokomezwa?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matukio haya yamekuwa yanaongezeka na changamoto kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba asilimia zaidi ya 60 ya matukio haya yanafanywa na watu ambao wako karibu na familia na tumekuwa tunapata changamoto kama Serikali kuyafikisha na kuchukua hatua kwa wale wahusika kwa sababu ndugu na jamaa wanakaa vikao vya familia wanaamua kumalizana kwa kutozana faini au kwa kumtorosha yule mwathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba haya mambo hayamalizwi katika mazingira ya nyumbani na badala yake mkondo wa sheria uruhusiwe kuchukua hatua. Kama Serikali ama kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto tunafanya kazi kwa karibu sana na Idara ya Mahakama, tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani na tuna mpango unaitwa MTAKUWA ambao ni mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha 2021/2022. Katika mpango mkakati huu, taasisi zote za kisekta ambazo zinashirikiana kwa pamoja tuna lengo la kuhakikisha kwamba suala hili la ukatili wa kijinsia tunaweza kulidhibiti ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mlinga ameuliza swali lake la pili kuhusiana na mila na desturi potofu. Hili kama Wizara tunaendelea kulifanyia kazi na tumekuwa tunafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa kidini, kimila, wanazuoni na sasa hivi tumeanza hata kufanya kazi na wasanii mbalimbali kuhakikisha kwamba tunafikisha ujumbe huu kwa jamii. Suala lililotokea kule Kigoma la Teleza, lile siyo mila, ni suala la uhalifu, nasi kama Serikali tulichukua hatua na kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa ninavyoongea wako Mahakamani na mkondo wa sheria unachukua hatua zake. (Makofi)

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

Kumekuwa na tatizo kubwa katika jamii yetu la ubakaji wa watoto wadogo chini ya miaka mitano na vikongwe:- Je, Serikali imeshawahi kufanya utafiti ili kujua chanzo cha tatizo hilo?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ukiangalia matukio yote haya yanatokana na sababu kwamba wananchi wengi hawajapata elimu. Hapa Mheshimiwa Naibu Waziri anazungumzia suala la mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini sisi kama wadau wakubwa hatujapata hata semina wala hatujui huo mpango. Nataka kujua, Serikali italeta lini mpango huo ili sisi kama Wabunge tuujue na tuweze kuupeleka katika maeneo yetu. Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baada ya kubaini ukubwa wa tatizo hili, tulikuja na mpango unaitwa MTAKUWA ambao ni Mpango Mkakati wa Serikali wa Kutokomeza au Kudhibiti Ukatili wa Kijinsia wa Wanawake na Watoto. Ndani ya Mpango huu kuna mambo mbalimbali mbayo tumeyaainisha, moja ni kuanzisha Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto, kuanzisha huduma za mkono kwa mkono na masuala ya kutoa elimu mbalimbali katika nyanja mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Wabunge, wote kwa ujumla tutafanya utaratibu wa kuhakikisha tunatoa elimu kuhusiana na mpango mkakati huu. Tunawaomba sana Waheshimiwa Wabunge nanyi muwe mabalozi wa mpango huu wa MTAKUWA kwenda kukemea masuala haya ya ukatili wa kijinsia katika sehemu ambazo mnatoka.