Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mgeni Jadi Kadika

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:- Mwenge wa Uhuru umekuwa ukileta maendeleo makubwa nchini na kuchangia pato la Taifa:- Je, kwa mwaka mmoja Mwenge wa Taifa unafungua miradi mingapi?

Supplementary Question 1

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu yake ya kuridhisha, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenge wa Uhuru unaleta maendeleo ni sawa lakini kuna changamoto na kuna hasara kubwa, kwa sababu mkesha wa Mwenge unapolala unakuwa kishawishi na maambukizi makubwa mapya ya UKIMWI jambo ambalo linapelekea vijana wengi kuathirika. Je, kwa nini Serikali haiweki mfumo mwingine kwa kulaza Mwenge huu kwenye Vituo vya Polisi au Ofisi za Halmashauri ili kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI kwa vijana wetu? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgeni, hilo la UKIMWI halina uthibitisho.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watu wanalazimishwa wakalale kwenye mkesha wa Mwenge wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara. Je, hii ni kwa mujibu wa kanuni au sheria gani? Nataka kufahamu kuhusu suala hili. (Makofi)

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niuambie umma wa Watanzania kwamba Mwenge una faida kubwa sana. Pia niuambie kwamba hakuna Taifa ambalo halina chimbuko lake. Mwenge ni chimbuko la Watanzania na ni utamaduni wetu. Hivyo, Mwenge utaendelea kuwa chombo muhimu na alama ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba mkesha wa Mwenge unasababisha maambukizi ya VVU, siyo kweli, kwa sababu kitu kimojawapo ambacho kinafanywa na Mbio za Mwenge ni kuelimisha mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya UKIMWI, Malaria pamoja na Kupambana na Dawa za Kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala haya ya UKIMWI, tunaelimisha nini kupitia Mwenge? Tunaelimisha kwamba ni lazima Watanzania wapime wafahamu afya zao, matumizi sahihi ya ARV’s na kuondoa unyanyapaa kwa waathirika wa magonjwa ya UKIMWI. Suala lingine ni mabadiliko ya tabia, Watanzania tunapaswa tubadilike tabia ili kuondokana na maambukizi mapya ya VVU. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Mwenge unasababisha maambukizi ya VVU kupitia hii mikesha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la nyongeza amesema kwamba watu wanalazimishwa kwenda kwenye hii mikesha, siyo kweli. Hakuna mtu anayelazimishwa, kila mtu kwa mapenzi yake anaenda kwenye mkesha wa Mwenge. Mimi mwenyewe nilikesha hakuna mtu ambaye aliniambia Ikupa njoo ukeshe kwenye Mwenge, nilienda nilikesha.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanafunzi mbalimbali wanakwenda kwenye mikesha hiyo kutokana na hamasa ambazo zinafanywa na mbio za Mwenge. Kwa hiyo, hamasa za mikesha hii ndiyo zinafanya watu wanajitokeza kwenda kukesha na kusikiliza ni nini kimefanywa na Serikali yao lakini pia kujua ni nini kinaendelea kutekelezwa na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:- Mwenge wa Uhuru umekuwa ukileta maendeleo makubwa nchini na kuchangia pato la Taifa:- Je, kwa mwaka mmoja Mwenge wa Taifa unafungua miradi mingapi?

Supplementary Question 2

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Serikali imezuia mikesha ikiwemo ngoma na mambo mengine ili kuondokana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, hiyo ni dhahiri kabisa. Pili, kazi ambazo zinafanywa na Mbio za Mwenge zinaweza kufanywa na baadhi ya Watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali na tumeshuhudia uzinduzi wa miradi ya aina mbalimbali ukifanywa na watendaji hao. Je, kwa kuwa condom zimekuwa zikigaiwa maboksi na maboksi katika mikesha ya Mwenge, hamwoni sasa kuna haja Mwenge wa Uhuru ukawekwa makumbusho badala ya kutembezwa katika maeneo mbalimbali? (Makofi/ Kicheko)

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeweza kujibu wakati najibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mwengenge wa Uhuru una mambo mengi, mwenge wa uhuru ni tochi ambayo inaangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ambayo yanafanwa na mwenge wa uhuru kama ambavyo nimesema. Hii itaendelea kuwa alama yetu. Mbio hizi zitaendelea kukimbizwa kila mahali kwa sababu mwenge huu wa uhuru tukisema kwamba tunauhifadhi, je, hii miradi, kwanza nikielezea faida moja, mwenge wa uhuru unakagua miradi mbalimbali, miradi ambayo kama mwenge wa uhuru usingepita; sasa hivi tunaona kwamba Wakandarasi wengi wamekuwa wanahofu, wanajitahidi kuhakikisha kwamba mwenge unapofika mahali pale, ukute ule mradi wake uko vizuri. Sasa kama tukisema kwamba tuuhifhadhi huu mwenge wa uhuru, Mheshimiwa Mbunge nadhani tutakuwa hatujafanya kitu. Faida ambazo zinapatikana na mwenge wa uhuru ni kubwa kuliko vile ambavyo tunafikiria. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri, amefanya kazi nzuri sana na ametoa majibu fasaha kabisa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, napenda tu niwakumbushe na niwarudishe kwenye dhana yenyewe ya mwenge wa uhuru. Tunapokwenda kwenye dhana ya mwenge wa uhuru tujue falsafa yake na chanzo chake ndani ya Taifa letu. Sasa tukifika mahali hapo, nadhani sisi wote tutakuwa na uelewa wa pamoja. Tukumbuke kwamba, chombo hiki mwenge wa ukuru ni ukumbusho wa uhuru wa Taifa letu la Tanzania ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa hili la Tanzania, ukiwa na falsafa ya kujenga umoja, mshikamano, ukombozi ndani ya Taifa letu na Bara zima la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenge huu umekimbizwa miaka hii yote na faida ya kuendelea kuenzi falsafa ya Baba wa Taifa imekuwa ni mfano mzuri hata kwenye Mataifa mengine kwenye Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeona, ziko nchi katika Bara la Afrika kwa sasa nao wameanza kuwa na mienge yao katika matukio ya Kitaifa ambayo yanaashiria mambo yao ya msingi na ya muhimu kabisa katika Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, hakuna jambo linalofanywa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambalo halijaratibiwa kwa faida ya Watanzania tu ni kwa faida ya Taifa letu na nchi nzima kwa ujumla, hata Mataifa ambayo yako nje ya mipaka ya nje ya mipaka ya nchi ya Tanzania. Tuungane pamoja, tuenzi falsafa ya mwenge wa uhuru, tumuenzi Marehemu Baba wa Taifa na chombo hiki ni muhimu katika historia ya ukombozi wa Taifa letu. (Makofi)