Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MHAGAMA) aliuliza:- Miongoni mwa mambo yanayokwamisha ukuaji wa sekta ya kilimo nchini ni pamoja na kukosekana kwa maduka ya pembejeo za kutosha maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wakulima wengi. Miongoni mwa sababu za kukosekana maduka hayo ni gharama kubwa ya kufuzu (certifications) kama vile TOSC 1 – Sh. 100,000; TPRI – Sh.320,000; TFDA - Sh.100,000; leseni na kadhalika na hivyo kufanya gharama kuwa zaidi ya Sh.600,000:- Je, ni kwa nini Serikali isiondoe gharama hizi ili kutoa hamasa kwa wajasiriamali kupata mafunzo, kufuzu na kuwekeza maduka ya pembejeo ili kusogeza huduma kwa wakulima wadogo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa kilimo?

Supplementary Question 1

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Mikoa ambayo imekuwa ikijishughulisha na kilimo cha chakula na biashara na kwa kufanya hivyo, wakulima wengi wanahitaji kupata mbolea kwa ukaribu.

Pamoja na maelezo mazuri ambayo yametolewa na Naibu Waziri, naomba Serikali ione sasa wakati umefika wa kuondoa hizo tozo zote kwa hao wafanyabiashara ambao watakuwa wamekidhi vigezo ili kuwaruhusu sasa waende wakafungue maduka huko vijijini ambako ndiko waliko wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya Mawakala ambao siyo waaminifu, wamekuwa wakiuza mbolea kinyume na bei elekezi na hii inapelekea kuwafanya wakulima wetu kununua mbolea na pembejeo kwa gharama ya juu sana. Je, Serikali inakuja na kauli gani kwa Mawakala ambao wamekuwa wakiongeza bei za pembejeo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la tozo, Wizara ya Kilimo sasa hivi inapitia upya tozo na gharama mbalimbali ambazo zinaweza kupunguza na kurahisisha shughuli za biashara katika sekta ya kilimo. Kwa kuwa Serikali inakuja na Blue print nataka nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla, huo utakuwa ni wakati mzuri sana wakati tunafanya mapitio ya Sheria ya Kurahisisha Mazingira ya Kufanya Biashara kuweza sote kushauriana na kuja na mwelekeo sahihi. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha unaokuja, zipo baadhi ya tozo ambazo tutazileta Bungeni kwa ajili ya kuomba namna ya kuweza kuzibadilisha na kurahisisha mazingira ya kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la wafanyabiashara wasio waaminifu, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa hatua alizochukua za kupita katika maduka na kuwakamata wafanyabiashara ambao wanakwenda kinyume na maelekezo ya Serikali. Kumekuwa na tatizo la wafanyabiashara wa viuatilifu na mbolea, kuhusu suala la bei elekezi, tumeagiza kwamba yeyote anayekwenda kinyume na maelekezo ya Serikali katika kuuza mbolea tofauti na bei elekezi, viongozi walioko katika ngazi za Wilaya na Mikoa waweze kuwakamata na kuwachukulia hatua na kuwapeleka katika vyombo vya Sheria kwa sababu hiyo itakuwa ni dhuluma na wizi kwa wakulima na ni jambo ambalo kama Serikali hatuwezi kuliruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, tunaendelea kusisitiza wafanyabiashara wote walioko katika sekta ya kilimo wanaouza mbolea na pembejeo na mbegu ambao wamekuwa siyo waaminifu kwa kuuza mbegu feki, kwa kutoa viuatilifu feki, Serikali inafuatilia kwa karibu. Tunatumia nafasi kuwaomba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanakagua na nawataka wananchi wanaponunua wahakikishe wanaomba risiti ili watakapokutana na tatizo iwe rahisi sisi Serikali kuweza kuchukua hatua na kuwafuatilia na kuwapeleka katika vyombo vya sheria.

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MHAGAMA) aliuliza:- Miongoni mwa mambo yanayokwamisha ukuaji wa sekta ya kilimo nchini ni pamoja na kukosekana kwa maduka ya pembejeo za kutosha maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wakulima wengi. Miongoni mwa sababu za kukosekana maduka hayo ni gharama kubwa ya kufuzu (certifications) kama vile TOSC 1 – Sh. 100,000; TPRI – Sh.320,000; TFDA - Sh.100,000; leseni na kadhalika na hivyo kufanya gharama kuwa zaidi ya Sh.600,000:- Je, ni kwa nini Serikali isiondoe gharama hizi ili kutoa hamasa kwa wajasiriamali kupata mafunzo, kufuzu na kuwekeza maduka ya pembejeo ili kusogeza huduma kwa wakulima wadogo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa kilimo?

Supplementary Question 2

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakulima wanapata adha hii kubwa ya kununua mbolea kwa bei kubwa, kwa nini Serikali sasa isianzishe maduka haya ya pembejeo huko vijijini kupitia Mawakala ili kuwaletea unafuu wakulima kwa ajili ya ununuzi wa mbolea?

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Chatanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali haifanyi biashara, tuna encourage private sector kufanya biashara na kuwekeza na kuhakikisha kwamba wanafika maeneo ya wakulima vijijini. Jukumu letu ni kujenga mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanzisha mfumo wa Bulk Procurement ili ununzi uwe wa pamoja kupunguza gharama. Tunaendelea kuuangalia mfumo huo kwa sababu katika soko la dunia kuna nyakati ambazo bei ya mbolea inakuwa juu na kuna nyakati ambazo inakuwa chini. Tunachokifanya sasa hivi ni kuangalia ni nyakati gani ambazo bei ya mbolea inakuwa chini ili tiuweze kuutumia mfumo wa Bulk Procurement wafanyabiashara waweze kununua wakati huo, mtaona mwaka hadi mwaka bei za mbolea zimekuwa zikishuka. Hata sisi tunaamini kwamba bado bei hizi hazijashuka kiwango kinachostahili lakini tunaendelea kufanya jitihada hizo na kwa mfumo wa Bulk Procurement ndiyo itakuwa njia sahihi ya kuweza kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mbolea bora na kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu biashara, hatutafungua maduka ya Serikali vijijini bali ni kuhamasisha sekta binafsi na kuwajengea mazingira ili kupunguza gharama na kupunguza utitiri wa regulatory bodies ili wafanyabiashara waweze kwenda kufungua maduka haya vijijini na kuwapatia huduma wakulima. Dhumuni la Serikali ni kuwawezesha wafanyabiashara na Watanzania waweze kufanya biashara na wala siyo Serikali kufanya biashara katika eneo hilo. Tuta-intervene pale ambapo kuna jambo la muhimu kufanya namna hiyo.