Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Je, ni vigezo vipi vinatumika kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yatakuwa na afya katika Ushirika wetu. Hata hivyo, bado kuna upungufu kwenye kaguzi zinazofanywa katika Vyama vya Ushirika. Mkaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) anakagua na ripoti yake inapelekwa kwa Vyama vya Ushirika hivyo kuwepo kwa mgongano wa maslahi. Je, Serikali haioni ni muda muafaka Vyama Vikuu vya Ushirika vikakaguliwa na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama cha Ushirika Nyanza, SHIRECU na SIMCU vina mali nyingi na Serikali inafanya juhudi ya kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa vinu vya kuchambulia pamba. Nimeshudia Naibu Waziri akifanya ukaguzi wa vinu hivyo kujiridhisha na kuona hali halisi. Hata hivyo, tukumbuke katika maeneo hayohayo kuna vinu vya kuchambulia pamba vinavyomilikiwa na watu binafsi wanaofanya biashara kwa faida hivyo kuwepo na ushindani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinajisimamia na kuwa endelevu? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama Serikali nikiri kumekuwa na udhaifu katika mfumo wa Ushirika na ndiyo maana Serikali imeamua kufanya mapitio makubwa ya Sera pamoja na Sheria ya Vyama vya Ushirika. Kama alivyosema kuhusu suala la COASCO na kushauri kwamba CAG akague Vyama Vikuu vya Ushirika; kwa mujibu wa sheria, CAG anakagua fedha za umma zinazopitishwa na Bunge, Vyama vya Ushirika ni private entity kwa muundo wake, ni vyama vya hiari.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mapendekezo tunayokuja nayo ili kuifanya COASCO iwe na taasisi nyingine inayoifanyia oversight, bado ndani ya Serikali tunaangalia ni namna gani tutaifanya COASCO iweze kufikia malengo tuliyonayo ya kuweza kusimamia Vyama vya Ushirika na kuwa na nguvu ambayo tunaitarajia. Ni kweli sasa hivi wakifanya ukaguzi, taarifa pamoja na kuipeleka kwa Mrajisi lakini vilevile wanaipeleka kwa wanachama husika wa Chama cha Ushirika. Hii imekuwa ikileta matatizo na pale ambapo kunakuwa na viongozi wasiokuwa waaminifu huweza kutumia nafasi hiyo vibaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwa sasa COASCO wanafanya kazi nzuri, kwa miaka hii miwili wame-produce report ambayo imeweza kutuonyesha taswira ya Vyama vyetu vya Ushirika vina hali gani na sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua. Kutokana na report hiyo, tumeona upungufu ambao unatulazimu sisi kama Serikali kuja na mabadiliko katika muundo wa Ushirika na namna ambavyo COASCO itafanya kazi na pale ambapo tunaamini kwamba kuna umuhimu wa kumuingiza CAG hatutasita kuchukua hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Nyanza, SIMCU na SHIRECU; moja, ni sahihi kwamba ginnery nyingi na miradi mingi iliyokuwa chini ya Ushirika imefeli. Nini tunafanya kama Serikali? Tumepitia ginnery zaidi ya nane na tumeshazifanyia feasibility study ili kuweza kuziinua zikiwemo ginnery za Chato, Mbogwe, Kahama (KACU), Lugola na Manawa. Ginnery hizi tumezipitia na kuziangalia kama zinaweza kuanza kufanya biashara. Taarifa hii imeshakamilika, tunaifanyia kazi tukishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini muundo wa uendeshaji tumesema clearly kwamba ginnery hazitaendeshwa na Wenyeviti wa Vyama vya Ushirika. Ginnery zitakuwa ni business entity zinatazoendeshwa na professional people ambao watazisimamia kibiashara ili ziendeshwe kibiashara. Mara nyingi tumekuwa tukitoa mifano, Kampouni kama Vodacom, Airtel na multi-nation zingine, shareholders hawaendeshi wana contract management na hiyo ndiyo model tutakayotumia kuendesha ginnery hizi ili ziweze kujiendesha kibiashara, hatutaziendesha kama taasisi za huduma.

Name

Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Je, ni vigezo vipi vinatumika kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika?

Supplementary Question 2

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niipongeze Serikali kwa juhudi kubwa ambazo imefanya kwa kurejesha Vyama vya Ushirika. Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu vyama hivi na matatizo yake ni mengi. Wakulima wanapokuwa wamepeleka mazao yao mara nyingine hawalipwi kwa wakati au fedha zao kupotea kabisa. Sasa nataka kuiuliza Serikali, je, itakuwa tayari yenyewe kama Serikali kuweza kufidia pale ambapo Vyama vya Ushirika vimeshindwa kuwalipa wakulima hawa fedha zao kwa wakati ama kuwafanya wakulima wapate bima zao za mazao ambazo zinakuwa ni kwa ajili ya majanga mbalimbali kama mafuriko, nzige, ukame na kadhalika, pamoja na kutokulipwa iwe ni kama janga mojawapo? Ahsante.

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Martha Mlata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu suala la bima; wakati wa Nane Nane Serikali ilizindua Bima ya Mazao. Nitumie nafasi hii kuwahamasisha wakulima kuhakikisha kwamba wanajikatia insurance za mazao yao. Pamoja na hatua hiyo kama Serikali na Wizara tumeanza kupitia gharama za bima ya mazao na hivi karibuni tutakutana na insurance companies ambazo zinatoa bima katika sekta ya kilimo ili tuweze kukubaliana nao na kutengeneza road map itakayo-guide suala la insurance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ushirika, napenda tena kurudia kusema ndani ya Bunge hili Tukufu. Ushirika haununui mazao, wao ni conduit ya kumkutanisha mkulima na mnunuzi. Tunatumia Ushirika kama sehemu ambayo wakulima wadogo wadogo watapeleka mazao yao na watakuwa na bargaining power juu ya hatima ya mazao yao. Vilevile niseme pale ambapo Chama cha Ushirika kitashiriki katika ubadhirifu wa kumuibia mkulima, tutawachukulia hatua stahiki na kali kama ambavyo tumekuwa tukifanya. Navyoongea sasa hivi viongozi wa ushirika sehemu mbalimbali ambao wamekula fedha za wakulima wako magerezani na wamechukuliwa hatua na kupelekwa kwenye kesi za uhujumu uchumi. Hivi karibuni tumewaweka ndani viongozi wa Chama cha Chai cha MVYULU kilichopo Wilaya ya Lupemba ambao walikuwa wamejibinafsishia mali za wakulima ziwepo magari, mashamba na nyumba na tutaendelea kufanya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Watanzania na Waheshimiwa Wabunge hatuwezi kukimbia changamoto. Ubadhirifu ulikuwepo hatuwezi kuua mfumo mzuri wa sekta ya kilimo kwa sababu ya viongozi wabadhirifu. Sisi kama Wizara tutasimamia kuhakikisha kwamba ushirika unakuwa safi na kuweza kufikia malengo ya Serikali. (Makofi)