Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wakunga wa Jadi ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto hasa maeneo ya Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na mwongozo huo ambao Serikali imeutaja lakini ni ukweli kwamba bado tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya afya na hivyo vifo vinaendelea kuongezeka. Je, Serikali haioni umuhimu bado wa kuwatumia hawa wakunga kwa kuwapa mafunzo ili waweze kusaidia uzalishaji ili tuendelee kupunguza vifo hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sasa upungufu katika sekta ya afya kwa maana ya watumishi wataalam ni asilimia 50, kiwango ambacho ni kikubwa sana na watu wetu wanaendelea kupata taabu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tunapunguza upungufu huu kwa kuongeza ajira katika sekta ya afya? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, kutokana na kuwa na vifo vingi vya akina mama na watoto sisi kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapunguza sana vifo hivi kwa kuwekeza katika miundombinu ambapo zaidi ya Hospitali za Wilaya 352 zimeboreshwa lakini kuhakikisha akina mama wanakwenda kliniki. Sasa hivi tumepiga hatua kubwa sana idadi ya akina mama ambao wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka asilimia 51 mpaka asilimia zaidi ya 63.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna-encourage kabisa akina mama wajifungulie katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya. Hawa wakunga wa jadi tunaendelea kushirikiana nao kwa sababu nao wana mchango kwenye jamii lakini katika lengo la kuhamasisha akina mama kwenda kliniki na kujifungulia katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ili kupata huduma sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili lilikuwa kuhusiana na ajira, ni kweli tuna changamoto ya rasilimali watu lakini tumeendelea kuajiri watumishi wa afya kadri vibali vya Serikali vinavyopatikana. (Makofi)

Name

Khadija Nassir Ali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wakunga wa Jadi ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto hasa maeneo ya Vijijini?

Supplementary Question 2

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali duniani zinaonesha kwamba mwanaume mmoja ana uwezo wa kuwapa ujauzito wanawake tisa (9) kwa siku moja wakati mwanamke mmoja ana uwezo wa kushika mimba moja (1) kwa miezi tisa (9). Je, Serikali haioni sasa kuendelea na programu za uzazi wa mpango kwa wanawake ni uharibifu wa rasilimali na badala yake programu za uzazi wa mpango zielekezwe sasa kwa akina baba? Ahsante. (Makofi/ Vigelegele)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Khadija Nassir, kama ifatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhana potofu kudhani kwamba suala la uzazi wa mpango ni la wanawake peke yake. Suala la uzazi wa mpango linawahusu wanaume vilevile. Sisi kama Serikali tuna-encourage akina baba na akina mama wote kushiriki katika suala zima la mpango wa uzazi salama.