Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Primary Question

MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kata ya Ilemba ambao ulijengwa na wananchi na ukabomolewa na mvua msimu wa 2018/2019?

Supplementary Question 1

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla sijaenda kwenye maswali, nami niungane na wewe kumpongeza Mheshimiwa Mzindakaya, nami ndio mrithi wake katika Jimbo, naomba wananchi waniunge mkono miaka 45 washuhudie maendeleo. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naenda kwenye swali. Namshukuru sana kwa majibu yenye ufanisi aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri, japo tatizo hili nimelisema hapa Bungeni mara nyingi sana, sasa ifike wakati Serikali iende kwenye utekelezaji iwasaidie wananchi hao ambao wanajisaidia wenyewe Serikali iwaunge mkono.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri afike kwenye eneo hili ili aone wananchi hawa wanavyohangaika kujinasua na umasikini. Waswahili wanasema kuona kunaongeza huruma kuliko kuambiwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha anataka kufahamu hatua za utekelezaji wa mradi huu umefikia wapi kwa sababu ameshasema mara nyingi. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, ni kwamba mradi huu umeibuliwa na nguvu wananchi na Serikali hii inawaunga mkono wananchi na ndiyo maana tumeanza kwanza kuboresha mfumo wa utendaji kazi wa Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji. Kuanzia sasa tumeanza kujipanga Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ipo katika ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda na Taifa.

Mheshimiwa Spika la pili, nachukua nafasi hii kuwaelekeza wataalam wa Taifa ya Umwagiliaji kwenda kwenye mradi huu haraka iwezekanavyo kufanya tathmini hiyo ili tuweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kufahamu ni lini nitaenda pale kuona? Baada ya Bunge hili nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, kuanzia tarehe 22 mwezi wa Tisa, nitakwenda huko kwenye Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa ajili ya kufuatilia miradi hii. (Makofi)

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kata ya Ilemba ambao ulijengwa na wananchi na ukabomolewa na mvua msimu wa 2018/2019?

Supplementary Question 2

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tukitaka kufanya mapinduzi ya kilimo, hakika kilimo cha umwagiliaji ndicho ambacho kinaweza kumsaidia mkulima wa Tanzania. Katika Bonde la Eyasi Wilayani Karatu, wananchi wale wanatumia kilimo cha umwagiliaji lakini hakuna miundombinu ya uhakika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inawejengea miundombinu ya uhakika ili umwagiliaji wao uwe endelevu na kilimo chao kiweze kuwasaidia?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli bonde hili la Eyasi ambalo mimi mwenyewe nilifika, ni bonde muhimu sana kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na ni chanzo kikubwa cha uchumi kwa watu wa Tarafa ile hasa kwenye zao la vitunguu.

Mheshimiwa Spika, katika bonde hili mikakati tuliyokuwa nayo kama Serikali, kwanza kama nilivyosema ni kwamba hatuwezi kusubiri pesa za kibajeti miaka yote hii. Kwa hiyo, sasa hivi kupitia Sheria ile ya PPP tumekuja na mpango kabambe kwa ajili ya kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza miundombinu hii kwa utaratibu ule niliosema kwenye jibu la msingi la jenga, endesha na kabidhi baada ya yule mdau anayeendesha ule mradi kurudisha gharama zake.

Mheshimiwa Spika, pili, kupitia Serikai ya Halmashauri, ukizingatia Halmashauri hii ya Karatu zaidi ya 33% mapato yake yanatoka kwenye bonde hili. Kwa hiyo, tukasema zaidi ya mapato hayo ya ndani 20% warudushe kuwekeza katika bonde lile ili liweze kurudisha maendeleo kwa wananchi.