Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA Aliuliza:- Kutokana na kuwepo kwa magonjwa sugu yanayoathiri mazao ya ndizi, mihogo, minazi na matunda kama michungwa, miembe na kadhalika kumesababisha wakulima kutozalisha kwa kiwango kinachostahili lakini pia mazao haya kukosa masoko ya uhakika nje ya nchi. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha magonjwa haya yanapatiwa suluhisho la haraka ili kilimo kiwe na tija na kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi?

Supplementary Question 1

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na kuwepo kwa wataalam watafiti wenye uwezo na weledi, taasisi nyingi za utafiti zinakabiliwa na changamoto kubwa za miundombinu mibovu lakini pia ukosefu wa rasilimali fedha pamoja na madawa kwa ajili ya kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba kushindwa kutenga asilimia moja ya bajeti kwenda kwenye utafiti inasababisha Serikali kushindwa kuhudumia taasisi hizi na hivyo kusababisha magonjwa kuendelea kutesa mimea na wananchi kuendelea kuathirika kwa kulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali ina mkakati wa kuweza kusambaza mbegu bora na miche bora ambazo zinahimili magonjwa wakati huo huo zinapandwa maeneo ambapo pambeni yake kuna mazao yaliyoathirika, kuna mimea iliyoathirika. Kwanini Serikali isije na mkakati sasa na program maalum ya kuondoa mimea iliyoathirika yote na kuwezesha wakulima kupata mbegu nzuri na miche bora ili kuhakikisha kwamba miche mipya inayopandwa haiathiriki na hivyo kusaidia wakulima kuinua uchumi wa familia na uchumi wa Taifa? Ahsante.

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sakaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni maamuzi ya Kikanda na Kimataifa kwamba tutenge asilimia moja ya pato letu kwa ajili ya research na development lakini vilevile ni ukweli usiopingika kwamba bado mapato ya nchi na vipaumbele na matatizo yanayotukabili kama nchi ni mengi. Kwa hiyo, uwekezaji katika research pamoja na kuwa ni muhimu lakini hatujafikia lengo ambalo tumejiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tulichoamua kama Wizara ya Kilimo ni kwamba all resource zinazokuja kutoka kwa development partners na tarehe 19, Wizara ya Kilimo tutakuwa na kikao na development partners wanaowekeza katika sekta ya kilimo, fedha zote tutaelekeza katika research na seed multiplication program ili uwekezaji katika vyuo na taasisi za utafiti uweze kupata resource inayotosheleza. Tuondoe uwekezaji unaofanywa katika capacity building ambao unatolewa na taasisi za Kimataifa zinazowekeza katika sekta ya kilimo. Kwa hiyo, focus yetu katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu ni uwekezaji mkubwa wa fedha zote za donors na development partners zinazokuja katika sekta ya kilimo pamoja na uwekezaji wetu wa ndani kuwekezwa katika maeneo ya research na uzalishaji wa mbegu bora ambazo zitakabiliana na matatizo yanayotukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna changamoto pale ambapo ardhi imekumbwa na tatizo halafu tunapeleka mbegu mpya. Kama Wizara tumeamua kufanya mapping na tumeanza programu katika Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Kondoa ambao wameathiriwa na sumukuvu. Maeneo yote haya sasa hivi tunaanza utaratibu wa kwenda kwa wananchi katika kata zilizoathirika kuondoa mbegu walizohifadhi kwa ajili ya msimu ujao na kuanza utaratibu wa kuwapatia mbegu mpya na ku-treat ile ardhi ili tatizo hilo lisiweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu wa kufanya mapping na kuelewa wapi kumeathirika na nini unaendelea ndani ya Wizara. Tunaamini kwa mpango mpya wa miaka mitatu wa Wizara ya Kilimo wa kuwekeza katika research na development katika taasisi hizi, tutaondoka katika matatizo haya yanayotukabili sasa hivi kama nchi.