Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wawi

Primary Question

MHE. AHMED JUMA NGWALI aliuliza:- Tanzania iko kwenye mikataba mbalimbali na ushirikiano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama Green Climate Fund (GCF), Adaptation Fund (AF), Last Developed Countries Fund (LDCF), UNEP na kadhalika. Je, Serikali imepokea fedha kiasi gani toka kwa wafadhili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi tangu mwaka 2010 hadi 2015?

Supplementary Question 1

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, fedha zilizotolewa na wahisani ni zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa kipindi cha miaka mitano; je, ni fedha kiasi gani zilizopelekwa Zanzibar na kwa miradi ipi kwa lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, kuna harufu kubwa ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha hizi za wahisani, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuliambia Bunge hili Tukufu ni hatua gani hadi sasa zimechukuliwa na Serikali katika kukabiliana na ufisadi huo? Ahsante.

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ngwali kwa swali lake zuri na jinsi ambavyo amebobea katika mambo ya mazingira na ndiyo maana swali lake hapa limekuwa refu sana. Kwanza katika hizo fedha shilingi bilioni 224 ambazo nimezitaja, tumepeleka Zanzibar zaidi ya sh. 17,234,056,000.80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi ambazo tumezipeleka Zanzibar ni 7.7% ya fedha zote ambazo zilipokelewa na wafadhili, ambazo ni zaidi ya kiwango kilichowekwa cha General Budget Support cha asilimia 4.5. Kwa miradi ipi? Tumepeleka kwa miradi mingi Zanzibar.
Moja, ni mradi ule wa Kilimani ambapo tunajenga makingio, lakini na Kisiwa Panza, pia pamoja na miradi mingine ya upandaji mikoko kwenye maeneo hayo kwa maana ya Kilimani pamoja na Kisiwa Panza. Tunapanda mikoko pamoja na kujenga kuta na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ameuliza kwamba Ofisi hii imechukua hatua gani kwa ufisadi uliozungumzwa, hasa katika hotuba ya Kambi ya Upinzani wakati ule akiwasilisha hapa. Tuliahidi siku hiyo hapa Bungeni kwamba tutafuatilia tujue ukweli wa tuhuma hizi ukoje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie kwamba tarehe 12 tulishamwagiza Chief Internal Auditor wa Ofisi yetu kufanya mapitio ya matumizi ya fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi zilizotolewa kutoka muda ule wa mwaka 2010 mpaka mwaka 2015 ili kujua uhalali wa matumizi yake. Kazi hiyo imeanza na itamalizika baada ya siku 30 tu. Kwa hiyo, Bunge hili litapata taarifa nini kilichojiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama taarifa ile itakuwa imekwenda vizuri, maana yake hakuna ubadhirifu wowote, tuwapongeze watumishi wetu kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini kama tutagundua kwamba kuna ufisadi wa aina yoyote, nilihakikishie Bunge hili kwamba hakuna atakayepona wala atakayechomoka, tutachukua hatua kali stahili.