Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Barabara ya Ipole - Mpanda yenye urefu wa kilometa 359 iliyoko kwenye mpango wa kujengwa kwa lami iko kwenye hali mbaya sana kutokana na kuharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha, maji maji yamejaa kuvuka barabara na maeneo mengine yanatitia kiasi kwamba mabasi ya abiria na magari ya mizigo yanapata shida kupita na wananchi wa Tabora, Sikonge na Katavi nao wanataabika sana na barabara hiyo. (a) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura za muda mfupi kuwasaidia wananchi wa Tabora, Sikonge, Katavi na maeneo mengine wanaoathirika na tatizo hilo? (b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya mapitio ya haraka ya usanifu wa barabara hiyo ili kunyanyua zaidi tuta na kuongeza madaraja na makalvati ili kudhibiti maji ya mvua yasiharibu barabara mpya itakayojengwa? (c) Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa lami na kukamilika?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa matengenezo aliyosema Mheshimiwa Naibu Waziri yalihusu kukwangua tu na kusawazisha barabara, badala ya kuweka kifusi na kushindilia, hali ambayo imesababisha mvua kidogo tu iliyonyesha, tatizo la mashimo kurudi pale pale. Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara hiyo, kwa kuweka kifusi na kushindilia ili iwe imara kabla hata ya lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti iliyosomwa jana, imepangiwa shilingi bilioni 120 kujengwa kwa lami kuanzia mwakani, ambayo ni asilimia 17 tu ya mahitaji yote ya fedha yanayohitajika. Pia Mheshimiwa Waziri hajajibu swali langu la mwisho sehemu (c); Je, ni lini barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha lami?

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

Naibu Spika, wakati mvua inanyesha, suala la kuweka kifusi nadhani lisingekuwa muafaka, kwa sababu ukiweka kifusi kitaharibu zaidi badala ya kujenga. Hivi sasa mvua kwa kuwa imekwisha suala sasa la kuimarisha kikamilifu hiyo barabara litafuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka kwamba nilishatoa maelekezo kwa Mameneja wote wa Mikoa sasa kuelekeza nguvu zao kufungua barabara zote nchini ambazo zilijifunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, namwomba Mheshimiwa Mbunge akiri kwamba hiki kiasi ambacho amepangiwa, kinatosha ukilinganisha na mahitaji makubwa ya Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani.

WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niongezee baada ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Barabara hii inafadhiliwa au inajengwa kutokana na pesa za Benki ya Afrika (ADB).
Kwa kawaida, barabara hii tutaigawa kwenye lots mbalimbali kwa sababu ni barabara ndefu sana. Kwa kawaida barabara hii kuanzia mwakani inaweza kuchukua baina ya miaka mitatu mpaka miaka minne, itakuwa imekamilika, itategemea hali ya hewa inavyokwenda.