Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. George Malima Lubeleje

Primary Questions
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la njaa, na katika msimu wa mwaka 2014/2015 mvua hazikunyesha kabisa na kusababisha wananchi wengi kukosa chakula kutokana na ukame; na Serikali imekwisha tamka kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kugawa chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza napenda niishukuru sana Serikali kwa kutupatia kiasi kidogo cha chakula katika Wilaya ya Mpwapwa.

Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapwa ina Majimbo mawili, Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la Kibakwe, na kwa kuwa chakula hicho ambacho tumepatiwa ni kidogo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?

Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wameacha kulima mashamba yao wanalima vibarua ili wapate hela ya kununua chakula. Je, utakubaliana na mimi kwamba iko haja sasa ulete chakula hicho haraka kwa Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa?

MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami; na barabara hiyo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Barabara kutoka Gulwe - Berege - Chitemo- Mima- Sazima - Igoji Kaskazini - Iwondo - Fufu inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ni mbaya sana na inapitika kwa shida sana hasa wakati wa mvua/masika.
Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba ipo haja kubwa ya barabara hiyo kuhudumiwa na Serikali Kuu (TANROADS) badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambayo uwezo wake kifedha ni mdogo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Mji wa Mpwapwa wenye wakazi zaidi ya 41,000 unakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji, ambapo wananchi wanapata shida kubwa sana kutembea mwendo mrefu zaidi ya kilometa tano kufuata huduma ya maji; na kuna baadhi ya mitambo imeharibika na Mamlaka ya Maji Safi na Salama hawana fedha za kukarabati mitambo hiyo. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja kubwa ya kusaidia ukarabati wa mitambo hiyo ili wananchi wa Mji wa Mpwapwa na vitongoji vyake waweze kupata huduma ya maji karibu na makazi yao?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikwishaanza kujenga vituo vya afya katika vijiji vya Mima na Mbori na ujenzi huo umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma za afya?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Vijiji vya Iyoma, Kisokwe, Idilo, Lukole, Lupeta, Bumila, Makutupa, Mkanana, Igoji Kaskazini (Isalaza), Nana, Kisisi, Ngalamilo, Godegoge, Mzogole, Mugoma, Kiegea, Kazania, Igoji Kusini, Chamanda, Simai, Makawila, Iwondo, Lupeta, Gulwe, Majami, Mwenzele na Mlembule katika Wilaya ya Mpwapwa vina matatizo makubwa sana ya maji na hivyo kusababisha wananchi wa vijiji hivyo kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tano hadi kumi kutafuta maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima vya maji katika maeneo hayo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Jukumu la MSD ni kununua na kusambaza dawa na vifaa tiba; na MSD
inakabiliwa na tatizo kubwa la fedha za kununua dawa na vifaa tiba:-
Je, Serikali itakubaliana nami kwamba ipo haja kubwa ya MSD
kuwezeshwa kuwa na Fungu (Vote) maalum kutoka Hazina?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Kila mwaka Bunge limekuwa likipitisha Bajeti ya Serikali kuhusu Wizara, Mikoa na Wilaya lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hususan katika Mikoa na Wilaya na kupelekea miradi mingi kutokamilika.
Je, ni sababu gani za msingi zinazofanya Serikali kuchelewa kuleta fedha za Miradi ya Maendeleo katika Mikoa na Wilaya?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha Kata mpya ya Mkanana ambayo ina vijiji vya Mkanana na Chibwegele na vipo mlimani ambapo hakuna huduma yoyote kama vile barabara ambayo ni mbaya sana na hupitika kwa shida wakati wote.
Je, mpango huo wa kuanzisha Kata mpya umefikia wapi?
Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba kuanzishwa kwa kata hiyo kutawezesha kuwasogezea karibu huduma mbalimbali wananchi wa kata hiyo kuliko ilivyo sasa ambapo Makao Makuu yapo Kijiji cha Chitemo, umbali wa kilometa 45?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikuwa na mpango wa kuchimba mabwawa katika vijiji vya Msagali, Bumila, Makutupa, Lupeta, Inzomvu, Vibelewele, Kimagai, Chunyu na Ng’ambi ambayo yatahudumia wananchi pamoja na mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Je, Serikali imefikia hatua gani ya utekelezaji wa mpango huo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Mpango wa MKURABITA ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo lakini unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha na hivyo kushindwa kuendesha shughuli za urasimishaji kwa ufanisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfuko wa urasimishaji utakaokuwa maalum katika Serikali za Mitaa ili kutatua tatizo la ukosefu wa fedha za kuendeleza shughuli za urasimishaji?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mima hadi Mkanana ni mbaya sana na inapitika kwa shida sana wakati wote; na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa haina uwezo kifedha wa kuifanyia mategenezo makubwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's