Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Willy Qulwi Qambalo

Supplementary Questions
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, Naitwa Willy Qambalo Mbunge wa Jimbo la Karatu.
Kwa kuwa, matatizo ya maji yaliyoko Busekelo yanafanana kabisa na matatizo ya maji yanayoukumba Mji wa Karatu na vijiji vinavyouzunguka. Na kwa kuwa Mji wa Karatu unakua sana kutokana na shughuli za utalii zinazoendelea katika maeneo ya jirani. Je, ni lini Serikali itamaliza kabisa matatizo ya maji katika Mji wa Karatu na vijiji vinavyozunguka?
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2002 mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ilifanya uhakiki wa mipaka yake na ndipo hapo ilipochukua maeneo ya wananchi katika Vijiji vya Endamaga na Lostete na tangu mwaka huo hadi wa leo kuna migogoro ambayo haiishi ni lini maeneo hayo ya wananchi sasa yatarudishwa kwao?
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Tunayo sera katika nchi hii inayotoa kipaumbele kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara zinazounganisha mikoa. Barabara hii tunayoongelea inaunganisha Mkoa wa Arusha na Simiyu. Kutokana na jiografia ya maeneo hayo, barabara hii ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri katika jibu lake anasema barabara hii itajengwa fedha zitakapopatikana. Sasa naomba swali, kutokana na sababu hizo za kisera na kijiografia, je, utafutaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii umefikia hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha katika maeneo ya barabara hii na hata ile inayounga Mji wa Karatu na Mbulu, zimeharibika sana na usafiri umekuwa wa shida na maeneo mengine barabara zimekatika. Kwa kuwa mvua sasa zinaelekea mwisho, ukarabati na ujenzi wa barabara hii utaanza lini?
MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza pamoja na majibu yenye matumaini ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kisima hiki cha Karatu Mjini kimeombewa umeme sasa ni mwaka mmoja na nusu lakini bado haujaunganishwa na nikiangalia fedha zinazoongelewa kukamilisha kazi ile ni shilingi milioni 33, naona hizi ni fedha kidogo sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano Serikali ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Waziri kwa nini Serikali isitafute fedha hizi shilingi milioni 33 ili kisima hiki kiweze kukamilika ili wananachi wapate huduma hii muhimu?
Swali la pili, Awamu ya Tatu ya REA inasubiriwa kwa hamu sana katika nchi yetu kwa sababu ni awamu ya kuiwasha karibu Tanzania yote. Hivi sasa tuko mwezi wa tatu ndani ya awamu hiyo; je, ni lini utekekezaji au ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo yetu utaanza ili wananchi wetu waweze kujiandaa? (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo ya ardhi ambayo haijapata kuendelezwa yaliyopo katika eneo la Mbozi yanafanana kabisa na matatizo ambayo tunayo kwenye Wilaya yetu ya Karatu. Katika Kijiji cha Mang‟ola Juu kuna mwekezaji, Tembotembo ambaye amemilikishwa eka zaidi ya 3,000 lakini ameweza kuendeleza chini ya asilimia 25. Katika kijiji hichohicho pia kuna mwekezaji anaitwa Acacia naye ameendeleza eneo alilopewa kwa chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo sasa yamebadilika kuwa hifadhi na mapori bubu ya kuhifadhia wanyama wa porini ambao ni hatarishi kwa wananchi wanaolizunguka. Je, ni lini Serikali itatoa mashamba hayo na kuwarudishia wananchi hao ili waweze kuyatumia? Ahsante.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni fursa kubwa kwa Halmashauri hasa kama ile ya Karatu yenye vivutio vingi vya kitalii na hizi hoteli za kitalii hasa katika kipindi hiki ambacho Halmashauri zetu nyingi zinachechemea katika eneo la mapato ya ndani. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, huoni sasa umefika wakati wa kubadilisha sheria hiyo ili kodi hiyo ya hotel levy ikusanywe na Halmashauri zetu ili iweze kuchangia katika eneo lile la mapato ya ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika swali la msingi uliulizwa suala la Serikali inamkakati gani, lakini majibu bado yamerudi kwa Halmashauri ya Karatu kujitangaza pamoja na kwamba kuna kipengele kidogo cha Serikali kusaidia. Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zetu nyingi hazina mapato ya kutosha ya ndani, je, Mheshimiwa Waziri tunachouliza, ni mkakati wa Serikali wa kutangaza hoteli zile za kisasa ili wale wageni badala ya kulala hata Nairobi waje Karatu ili waondokee pale kwenda Ngorongoro na Manyara? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mamlama ya Maji ya Mji wa Karatu (KARUWASA) ina zaidi ya umri wa miaka mitatu, lakini uendeshaji wake umekuwa ukisuasua kwa sababu mamlaka hiyo bado haina
bodi ya usimamizi; majina ya wajumbe waliopendekezwa kwenye bodi hiyo yalishapita kwenye ngazi ya Baraza la Madiwani zaidi ya miezi sita. Ni lini bodi hiyo itaundwa ili isaidie uendeshaji wa mamlaka hiyo? Ahsante.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Karatu (KARUWASA) ina kisima kimoja na kisima hicho kimeharibika na ni miezi miwili wananchi hawana huduma ya maji; na Mamlaka hiyo iko katika kundi la Mamlaka Daraja la C ambalo zinapata ruzuku kutoka Serikalini:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kuokoa kisima hicho ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo? (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi wa maji wa kijiji cha Getamok katika Wilaya ya Karatu uliojengwa kwa zaidi ya gharama ya shilingi milioni 600 chini ya Programu ya Kwanza ya WSDP hivi sasa haufanyi kazi kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango. Mabomba yaliyofungwa kwenye mradi huo yanapasuka kila kukicha na hata matenki yanavuja. Halmashauri ya Wilaya imejaribu kurejesha huduma kwa kutumia vyanzo vyake lakini imeshindikana kwa sababu fedha nyingi zinahitajika.
Je, Serikali itawasaidiaje wananchi wa kijiji hicho kupata huduma hiyo ya maji safi na salama na pia wale waliofanya ujenzi huo chini ya kiwango Serikali itawachukulia hatua gani?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Nimrod Elirehemah Mkono

Butiama (CCM)

Supplementary Questions / Answers (1 / 0)

Profile

Hon. Khamis Ali Vuai

Mkwajuni (CCM)

Profile

View All MP's