Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Raphael Michael Japhary

Supplementary Questions
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majibu ya namna hiyo kuhusu viwanda vya Moshi yamekuwa yakitolewa mara kwa mara katika Bunge lako Tukufu bila utekelezaji; na kwa kuwa ilikuwa ni moja wapo ya ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba kwa muda mfupi sana viwanda vile vingetwaliwa kwa waliovitumia bila utaratibu.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutoa muda halisi kwa maana ya time frame ya lini viwanda hivyo vitatwaliwa kwa watu ambao wameshindwa kuvifanyia kazi katika malengo halisi yaliyokuwa yametarajiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa majibu ya Serikali hayaakisi ukweli ulivyo kuhusu wafanyakazi, kwa sababu madai yao ni ya msingi na fedha wanazodai siyo za mikataba ya hiari na wamekuwa wakidai fedha hizo tangu mwaka 1998, na kwa kuwa Serikali haijataka kuwa karibu nao…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali tafadhali!
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Je, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuanza kufuatilia ukweli wa madai hayo na kuwa karibu na hao wafanyakazi ili waweze kutoa ufafanuzi unaoridhisha wafanyakazi hao kuondoa manung’uniko yao? Ahsante sana.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo lililojitokeza katika Jimbo la Chilonwa halitofautiani na hali iliyojitokeza katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kutokana na mvua iliyonyesha ambayo imeharibu miundombinu sana na sababu kubwa ya uharibifu huo ni kutokana na mwelekeo wa namna ambavyo TANROADS wameelekeza maji kwenye Kata za Msaranga, Shirimatunda na Ng‟ambo, kiasi kwamba madaraja yameharibika sana. Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wa Moshi kwamba itatoa maelekezo kwa TANROADS kuhakikisha wanarekebisha miundombinu iliyoharibika?
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa migogoro iliyozungumzwa katika hifadhi haitofautiani na malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na Jumuiya za Wapagazi, Waongoza Watalii na Wapishi katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi nyingine za Taifa, wakigombana au wakilalamikia Tours Operators wao.
Je, Serikali kwa sababu, inalifahamu hili, ni lini itatatua migogoro hii ili maslahi na mazingira ya kikazi ya Jumuiya hizo za Wapagazi, Waongoza Watalii na Wapishi yaweze kuboreshwa, kama mabalozi wema wa kustawisha utalii katika nchi yetu?
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, uwanja wa ndege wa Moshi umeharibika sana na ni uwanja wa muda mrefu sana tangu wakati wa Muingereza; na ni uwanja muhimu sana na wenye faida sana kiuchumi hasa utalii, kama ilivyoonekena hapa. Na unawezekana kujiendesha wenyewe na ukaleta faida wala hautategemea viwanja vingine kujiendesha. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, nilikuwa naomba time frame, je, ni lini Serikali sasa itapeleka hata hizi milioni 350 angalao basi kufanya huo ukarabati ili uwanja huo uweze kutumika? Kwa sababu hii inaonekana inaweza ikawa ni ahadi ya kibajeti, lakini fedha hii isiende kwa wakati; na labda bajeti iishe ikiwa haijapatikana. Naomba nipate uhakika ni lini fedha hii itaenda ili uwanja huo uweze kutumika na uweze kujengewa uzio wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kulikuwa na mpango wa Serikali wa kuwa na chuo cha mambo ya anga (school of aviation). Naomba kujua kutoka Serikalini, ni lini chuo hicho kitaanza ili kuweza kusaidia watu wetu kupata utaalam wa mambo ya anga katika nchi hii? Ahsante sana.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la kukatika kwa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara halitofautiani na tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro hasa Jimbo la Moshi Mjini. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuhakikisha kwamba
wanatatua tatizo la ukatikaji wa umeme katika Jimbo la Moshi Mjini?
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nilikuwa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kitengo cha Zimamoto kikiwa kipo kwenye Mamlaka za Halmashauri za
Miji na Manispaa, Manispaa ya Moshi ilikuwa ina uwezo wa kuhudumia magari makubwa mawili na gari moja dogo ambalo tuliazima kutoka Japan. Tangu magari yale yachukuliwe na Kitengo cha Zimamoto Mkoa wa Kilimanjaro, leo tunahudumia gari moja tena tunahudumia kwa taabu na hicho kigari kimoja tulichokiomba Japan ndicho kinachofanywa kama ndiyo gari wanalotembelea Maafisa wa Zimamoto.
Je, Serikali imetumia kigezo gani kuonesha kwamba ufanisi umeongezeka baada ya kuhamisha kitengo hiki
kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani tofauti na kilivyokuwa Halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kama Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kusaidia Mkoa wa
Kilimanjaro kwa kuazima gari moja ya zimamoto kutoka KIA kwa sababu KIA wanaonekana wana magari ya ziada ili iweze kusaidiana na gari lililopo sasa hivi Mkoa wa Kilimanjaro ili kutoa huduma ya zimamoto kwa watu wa Mkoa wa Kilimanjaro? Ahsante.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imekuwa na maombi ya muda mrefu ya Hospitali ya Wilaya na tulikuwa tayari na majibu ya Serikali kwamba wakati wowote watajibu maombi yetu, lakini mpaka sasa hatuoni mwelekeo wowote. Nini tamko la Wizara ya TAMISEMI katika suala hilo la Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Moshi? (Makofi)
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Serengeti linafanana na tatizo lililopo Manispaa ya Moshi na ukizingatia kwamba Manispaa ya Moshi ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Kilimanjaro na ndiyo eneo ambalo watalii wote wanaoenda mlima Kilimanjaro hupitia pale. Tumekuwa na ombi la muda mrefu la kuomba Hospitali ya Wilaya Serikalini kwa zaidi ya miaka sita au saba hapa. Swali langu, je, Serikali itatusaidia lini kutekeleza ombi letu maalum la kujenga Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Moshi?
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa suala la Kigoma – Uvinza lipo sawa la Kiwanda cha Magunia Moshi na Kiwanda cha Kiritimba ambapo nimeshauliza swali la msingi hapa Bungeni na Serikali ikajibu kwamba ipo tayari kwenda kuonana na wale wafanyakazi ambao hawakulipwa mafao yao ili waweze kuwaeleza, kwa nini hawakuwalipa na kama wamewalipa, waliwalipa kwa vipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali inipe commitment kama ni lini itakwenda kuonana na wafanyakazi wa magunia waliostaafishwa na wafanyakazi wa Kiritimba wa Mkoa wa Kilimanjaro. Ahsante.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Gereza la Karanga lina tatizo kubwa sana la vyombo vya usafiri kwa maana ya magari. Naomba majibu ya Serikali kwamba ina mpango gani wa kununua gari ili kusaidia wafungwa wanaokata rufaa pamoja na askari ili kulinda usalama wa wafungwa kwa sababu gari lililopo ni chakavu sana na hata matairi halina?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Gereza la Karanga limekuwa na tatizo la madeni makubwa kwa matibabu ya wafungwa wanaotibiwa nje ya zahanati ya gereza hilo. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba madeni yanayodaiwa gereza yanalipwa ili wafungwa waendelee kupata huduma ya matibabu? Ahsante sana.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali kuhusu tatizo hilo, lakini bado tatizo hili ni kubwa na linaendelea. Mijadala juu ya wapagazi, waongoza watalii na wapishi imekuwa ya muda mrefu baina ya Serikali na waajiriwa hawa, lakini utekelezaji wa makubaliano umekuwa hafifu sana.
Swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba kuna haja kwa sasa kwenda kuonana na waajiriwa kuongea nao ana kwa ana, kujua ni kwa kiwango gani miongozo hii ambayo wameipeleka imetekelezwa na imekuwa na tija kwa hao watu ambao ndio waathirika wa tatizo hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na utaratibu kwamba wanaoshughulikia matatizo ya watalii imekuwa ni kampuni ya nje na sio watu wa ndani. Ni kwa nini Serikali haioni haja ya kushirikisha kampuni za ndani kuhakikisha kwamba inasimamia suala la porters na waongoza watalii na inaliacha katika kampuni za nje? Ahsante sana.(Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Dr. Tulia Ackson

Nominated (CCM)

Profile

Hon. Salim Hassan Turky

Mpendae (CCM)

Contributions (4)

Profile

View All MP's