Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. David Mathayo David

Supplementary Questions
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naipongeza Wizara hii kwa kuwa makini katika kufanya kazi katika sekta hii ya nishati na madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza maswali
mawili ya nyongeza ningependa kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, hususan kata ya Hedaru ambao wamepoteza nyumba nyingi pamoja na mifugo na mazao kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataallah, aweze kutupa mvua za kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuuliza
maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, katika Mradi wa REA Awamu ya Pili, mkandarasi ambaye anaitwa SPENCON alishindwa kufanyakazi na kwa hiyo, vijiji vingi pamoja na vitongoji vingi vya Jimbo la Same Magharibi hususan vijiji 48, umeme haujakamilika kutokana na kwamba, mkandarasi huyo alishindwa kazi.
Je, REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi ambavyo vilikosa umeme pamoja na vitongoji vyake, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba, vitongoji vyote vinapata umeme na vijiji vyangu vyote vya Jimbo la Same Magharibi katika Awamu hii ya Tatu ya REA?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili la Bajeti kuongozana na mimi kwenda katika Jimbo la Same Magharibi, ili akajionee mwenyewe vijiji na vitongoji ambavyo havina umeme katika Jimbo langu? Ahsante sana.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wangu wa Kata za Kisiwani, Vumari na Mji Mdogo wa Same wamebanwa sana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi; na kwa kuwa Mwenyezi Mungu wakati anaumba dunia alimuumba binadamu akamwambia atawale viumbe vyote viishivyo kwenye maji na kwenye nchi kavu; na kwa kuwa wakati wa uhuru tulikuwa na idadi ya watu milioni 10.3 na sasa hivi tuko takribani milioni 50, tulikuwa na ng’ombe milioni nane sasa hivi milioni 28; tulikuwa na mbuzi milioni 4.4 sasa hivi ni milioni 16.6; tulikuwa na kondoo milioni tatu na sasa hivi ni milioni tano, tulikuwa na nguruwe 22,000 sasa hivi ni milioni mbili, astaghfilillah nimetaja nguruwe wakati ni mwezi wa Ramadhani, mnisamehe sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza je, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo, TAMISEMI pamoja Ardhi ili waweze kutathmini eneo na idadi ya watu pamoja na mifugo wanayofuga ili kusudi kama kuna uwezekano maeneo ya hifadhi za misitu pamoja na Hifadhi za Wanyamapori zipunguzwe ili binadamu waweze kupata maeneo ya makazi pamoja na mifugo na kilimo?
Swali la pili, kwa kuwa Botswana, Afrika ya Kusini na Namibia wameweza kuzuia wanyamapori kutoka kwenye mapori kwenda kwa binadamu ama kwenye wanyama wanaofugwa, je, Serikali iko tayari sasa kuandaa mpango rasmi wa kuweka fence ili wanyamapori wasiweze kwenda kwenye makazi ya watu kuwasumbua na kuwaletea madhara ikiwa ni pamoja na vifo? (Makofi)
MHE. MATHAYO D. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza.
Aidha, napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa kujibu maswali yake vizuri na kitaalam. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Benki Kuu imepunguza riba ya mabenki ya biashara yanapokopa kutoka kwenye Benki Kuu hadi kufikia asilimia tisa na kwa kuwa pia, imepunguza amana kutoka asilimia kumi hadi asilimia nane ya kiwango cha fedha ambazo mabenki haya ya biashara yanatakiwa yahifadhi Benki Kuu. Je, Benki Kuu imefuatilia na kuona kwamba, mabenki ya biashara yanatoza riba nzuri au yametoa punguzo zuri la riba kwa wananchi ambao wanakopa kwenye mabenki hayo?
Swali la pili, kwa kuwa katika nchi zinazoendelea asilimia 70 ya fedha zinakuwa mikononi mwa wananchi na asilimia 30 inakuwa kwenye mabenki pamoja na Serikali. Je, Benki Kuu imefanya utafiti na kuona, kwa sababu sasa hivi tukiangalia fedha katika mzunguko kwa wananchi wa kawaida zimepungua sana.
Je, Benki Kuu imefanya utafiti na kujua kwamba, fedha hizi ziko wapi ili waweze kutunga Sera ambazo zitarudisha fedha hizi kwenye mabenki ya biashara pamoja na wananchi ili maisha yaweze kuwa mazuri, lakini wananchi pia washiriki vizuri katika shughuli za kujenga nchi yao? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's