Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Supplementary Questions
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Migogoro ya ardhi kati ya hifadhi zetu na wananchi wanaozunguka hifadhi imekuwa ni migogoro ya muda mrefu na imeenea katika nchi nzima. Katika Jimbo langu la Liwale sisi ni miongoni mwa tuliozungukwa na Hifadhi ya Selous.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mgogoro mkubwa sana kati ya hifadhi ya Selous pamoja na Kijiji cha Kikulyungu wakigombea bwawa la Kihurumila. Mgogoro huu umeshapoteza maisha ya watu kwa muda mrefu na hata Mbunge aliyepita wa Jimbo la Liwale mgogoro huu umemfanya asirudi tena Bungeni pale alipotamka Bungeni kwamba anasikia watu wamefariki katika bwawa hilo, badala ya yeye kwenda kujiridhisha na kuangalia hali halisi ya mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini basi Mheshimiwa Waziri atashiriki katika kutatua mgogoro huu ili maisha ya watu wa Liwale yasiendelee kupotea wakigombea bwawa la Kihurumila? Naomba majibu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nasikitika sana kwa majibu ya kukatisha tamaa yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Wilaya ya Liwale ina umri wa miaka 41 leo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inasema haina mpango wowote wa kujenga Kituo cha Polisi pale, anaposema kwamba ni zaidi ya Wilaya 65, sidhani kama hizi Wilaya nyingine ambazo anazi-include yeye zina umri wa miaka 40. Wilaya ya Liwale ina jumla ya kilometa 66,000 na hizi tarafa anazozisema zipo umbali wa kilometa zaidi ya 60 kutoka Liwale Mjini… (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, swali sasa!
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, najenga hoja. Wilaya ya Liwale mpaka leo, nimetembelea kile kituo, mafaili yale wanafunika na maturubai, lile jengo walilopanga la mtu binafsi linavuja. Sasa ninachoomba, nipewe time frame, ni lini Kituo cha Polisi Liwale kitajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile katika Tarafa ya Kibutuka, ndiyo tarafa inayoongoza kwa ufuta na wafanyabiashara wakubwa wako pale na Kata ya Lilombe sasa hivi kuna machimbo na wafanyabiashara wengi wako pale, ni lini Kata hizi zitajengewa vituo vya Polisi?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, natoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri kwa majibu ya kutia matumaini. Lakini nataka ieleweke kwamba Wilaya ile ya Liwale ipo mbali sana na makao makuu ya Mkoa, Wilaya ya Liwale haina usafiri, haina barabara za kutosha yaani za kuaminika, Wilaya ya Liwale haina mtandao wa simu unaoaminika, Wilaya ya Liwale haina usikivu wa redio. Sasa muone jinsi Wilaya hii ilivyo kisiwani, hawa ni miongoni mwa walipa kodi wa nchi hii, sijui kama kodi zao watanufaika nazo vipi? Nashukuru kwa jibu la kwanza nimepata timeframe na mimi nitafuatilia kuhakikisha hii timeframe inafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa swali la pili napata wasiwasi, nimepata tu majibu ya moja kwa moja. Nahitaji kujua ni lini Redio Tanzania itasikika Liwale? Hapa nimepewa tu majibu ya jumla jumla. Mwisho kabisa hapa amesema kwamba mpango wa muda mrefu sasa hata huo mpango wa muda mfupi nao haujatajwa, huo ni wa lini? Naomba nipatiwe majibu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Matatizo yaliyopo kwenye hii Wilaya ya Busanda yanafanana kabisa na yale yaliyoko katika Wilaya ya Liwale. Wilaya ya Liwale hatuna Chuo cha Ufundi, je, ni lini Serikali itatujengea Chuo cha Ufundi Wilayani Liwale?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kukamilika kwa daraja la Mto Kilombero ni wazi kwamba sasa Mkoa wa Morogoro unafunguliwa kibiashara. Nini mipango ya Serikali kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Lindi kwa barabara inayopitia kutoka Liwale kuelekea Morogoro? Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo kubwa la miradi hii ya umwagiliaji ni ule upembuzi yakinifu sijui na usanifu. Kwa sababu, katika Jimbo langu la Liwale kuna Mradi wa Umwagiliaji wa Ngongowele umetumia zaidi ya shilingi bilioni nne na mradi ule sasa hivi uko grounded, hautegemei tena kufufuka. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya pesa zile zilizopotea pale na hatima ya mradi ule?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Moja ya sababu zinazofanya ucheleweshwaji wa malipo ya korosho ni pamoja na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, alitamka kwamba korosho zote za Mkoa wa Lindi na Mtwara zipitie Bandari ya Mtwara kitendo ambacho bandari ya Mtwara ilishindwa kusafirisha korosho hizo kwa wakati na wanunuzi wakaacha kulipa kwa sababu korosho zao mpaka ziingie kwenye maji ndipo waendelee kufanya malipo. Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, sababu ya pili; ni kwamba hata hayo makampuni mnayosema kwamba mnayadhibiti pale ambapo yanakuwa yanachelewesha kulipa lakini bado kuna mtindo wa hayo makampuni kubadilisha majina. Unalifutia jina kampuni hili, mwenye kampuni ni yule yule anatengeneza kampuni nyingine…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Je, Serikali inatoa kauli gani namna ya kukabiliana na matatizo hayo?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Wilaya ya Liwale iko katika Mkoa wa Lindi na ndiyo Wilaya pekee ambayo bado mpaka leo hii inatumia umeme wa mafuta na mashine zile tumezitoa Rufiji, mashine zile zimechoka. Nini kauli ya Serikali kuipatia umeme wa gesi Wilaya ya Liwale ili tuweze kuwa na umeme wa uhakika?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Sambamba na Sheria ya Ndoa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia Sera ya Wazee tangu mwaka 2003. Ni lini Serikali italeta sheria kamili ya wazee ili waweze kutambuliwa katika nchi yetu?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Barabara ya Nangurukulu – Liwale, Nachingwea – Liwale, ni barabara ambazo zimo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini mara nyingi nimekuwa nikiuliza barabara hizi, naambiwa itajengwa, itajengwa; sasa wana-Liwale wanataka kusikia ni lini barabara hizi zitaingia kwenye upembuzi yakinifu na hatimaye kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niseme tu nasikitika kwa majibu ambayo ni rahisi, majibu mafupi, majibu ambayo hayaoneshi matumaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri...
...anasema ubinafsishaji wa matawi 22 yaliyokuwa National Milling tumepata shilingi bilioni 7.4, ni masikitiko makubwa sana; na hii inaonyesha moja kwa moja kwamba sisi huu umasikini umetuandama. kwa sababu kama tunaweza tukatupa…
..ni masikitiko makubwa sana. Msheshimiwa Mwenyekiti, najenga hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matawi kama Plot 33, Plot 5, Tangold yale matawi sasa hivi yote ni ma-godawn. Watu walionunua matawi ya National Milling ambayo yanafanya kazi ni Bakheresa na Mohamed Enterprises peke yake, lakini matawi mengine yote yaliyobaki yamekuwa ma-godawn na ninyi mnasema mnaenda kwenye viwanda, mimi hapa sijapata kuelewa. Nini hatima ya hayo mashirika ambayo sasa hivi ni ma- godawn badala ya kuwa viwanda? (Makofi)
(b) Kwanza niseme wazi kwamba na mimi ni mmoja kwenye taaluma hii ya usindikaji wa nafaka. Nimefanya kazi National Milling si chini ya miaka 10. Kwa upande wa Kurasini mnamo tarehe 31 Aprili, 2005 waliletewa barua aliyekuwa Meneja pale kwamba kiwanda hicho akabidhiwe Mohamed Enterprises anayekaribia kununua, alikabidhiwa tu kwa sababu anakaribia kununua. Si hivyo tu, wafanyakazi waliokuwepo pale mpaka leo hii wanaidai Serikali hii zaidi ya shilingi milioni 234.3, bado hatima yao haieleweki na kesi imekwisha. Vilevile si hivyo tu, tarehe 20…Hazina wameitwa mahakamani hawataki kwenda, nini hatima ya wafanyakazi wale?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza kuhusu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nimekuwa nikisimama hapa mara nyingi naongelea Barabara ya Nangurukuru – Liwale na Barabara ya Nachingwea – Liwale. Majibu ninayoyapata ni kwamba barabara hizi zitajengwa katika kipindi hiki cha miaka mitano, lakini barabara hizo sasa hivi hazipitikia kutokana na mvua za masika zilizokatika sasa hivi. Je, nini commitment ya Serikali kwa kuwaokoa hawa Wanaliwale ili waweze kupata barabara inayopitika masika na kiangazi? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuelekea kwenye nchi za viwanda; na ninavyofahamu mimi ili twende huko, lengo kubwa ni kuchakata mazao yanayolimwa hapa nchini; lakini kama ambavyo swali namba 206 lilivyojibiwa, sijaona mkakati unaowekwa kwenye zao la ufuta. Ni namna gani Serikali imejipanga kutangaza ili tupate wawekezaji kwenye kusindika mazao ya ufuta?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri anasema kwamba mpango mkakati mmojawapo ni kutangaza kuingiza hiyo tovuti na filamu. Hapa swali lilikuwa linataka kujua mkakati thabiti wenye dhamira ya kweli kwa sababu hapo wanaposema, hata barabara ya kufika kwenye hivyo vivutio hakuna. Sasa huu mkakati, hata hao watu unaoingiza kwenye filamu, watafikaje kule Kilwa ambapo kwenye hivi vivutio hamna barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba Pwani ya Afrika Mashariki ni mahali ambapo kwanza walikuwa na currency yao, yaani walikuwa na pesa yao; ni Kilwa, lakini haya yote watu hawayajui.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa mfano, ukiangalia Vita ya Majimaji; asili ya vita hii ni Kilwa, lakini makumbusho ya Vita ya Majimaji yako Songea. Sasa Wananchi wa Kilwa walitaka waone, Serikali inafanya taratibu gani kuirudisha Vita ya Majimaji Kilwa na kuitangaza Kilwa kama sehemu ya Utalii? Hilo ni swali la kwanza.(Kicheko)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Kama ambavyo Halmashauri ya Itilima ilivyokuwa na tatizo la Hospitali ya Wilaya, Wilaya ya Liwale ni Wilaya ya zamani sana na lile jengo lake la Hospitali ya Wilaya limeshachakaa na limezidiwa uwezo. Kwa kutambua hilo Halmashauri yetu ya Wilaya ya Liwale imetenga eneo kama hekari 50 hivi kwaili ya mradi wa hospitali mpya ya Wilaya ya Liwale. Je, Serikali ipo tayari kutuunga mkono katika mradi huu?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kunakuwa na matatizo mengi ya miradi mingi ya maji nchini ambayo haikamiliki kutokana na matatizo ya fedha, lakini mara nyingi tukiuliza hapa, nakumbuka Bunge lililopita, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii alikuwa anasema kwamba Wakurugenzi wetu wakamilishe taratibu za manunuzi, pesa zipo kwenye Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokwenda kwenye halmashauri yangu kwa mfano, nilienda kuulizia suala hili wakasema wameshaandika maandiko mengi kupeleka Wizarani, lakini mpaka leo hawajaletewa hizo pesa na miradi mingi imekwama . Sasa naomba kupata Kauli ya Serikali; ni nini Kauli ya Serikali kwa miradi ile ya maji iliyokwama kwenye halmashauri zetu mbalimbali hapa nchini?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika,ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuharibikaharibika kwa mara kwa mara kwa kinu cha gesi pale Kilwa na kutokana na uchakavu wa mitambo ile, hitajio la Wilaya za Kilwa, Lindi pamoja na Liwale, I mean Kilwa pamoja na Rufiji pamoja na Liwale kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba Waziri atueleze hapa ni nini kinachelewesha wilaya hizi kuongizwa kwenye Gridi ya Taifa kwa sababu ya uchakavu wa mitambo ya Kilwa kunafanya umeme usiwe wa uhakika katika Wilaya hizi tatu? Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa sababu tunataka tuingie kwenye Tanzania ya viwanda na Tanzania ya viwanda ni lazima iende sambamba na uwekezaji kwenye ardhi lakini uwekezaji kwenye ardhi unakumbwa na matatizo makubwa. Tatizo la kwanza vijiji vyetu vingi havijaingia kwenye matumizi bora ya ardhi, matokeo yake mwekezaji anakosa nafasi na hata pale ambapo vijiji vimeshaingia kwenye matumizi bora ya ardhi kuna tatizo kwenye Makamishna wa Kanda katika upatikanaji wa ardhi lakini sio hivyo tu, hata kwenye Ofisi ya Rais ambapo nako kuna matatizo...
Je, nini kauli ya Serikali kwa wawekezaji wanaohangaika kutafuta ardhi ya kufanya uwekezaji katika kilimo? (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwenye matatizo ya mazao ya mbaazi vivyo hivyo kuna tatizo la zao la ufuta, lakini tatizo kubwa la mazao haya ni Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Ni nini kauli ya Serikali katika kuiboresha hii Bodi ya Mazao Mchanganyiko iwe na mipango endelevu ya kuendeleza haya mazao ili wananchi wetu waweze kupata soko la uhakika?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kutokamilika kwa miradi ya maji katika Halmashauri zetu kumekuwa ni tatizo sugu, niliwahi kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wakati huo ambaye sasa ndiyo Waziri alisema pesa Wizarani zipo ila watu wapeleke certificate. Ninasikitika kumwambia kwamba hapa ninayo makabrashi ambayo ni copy ya hizo certificate ambazo zimeshafika kwenye Wizara yake sasa ni zaidi ya mwaka mzima hizo pesa hazijawahi kutolewa, na kuna miradi kadhaa katika vijiji vya Kipule, Ngongowele pamoja na Mikunya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kauli ya Serikali ni lini miradi hii itakamilika ili wananchi wa vijiji hivi waweze kupata maji. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nitoe shukrani kwa Serikali, wanasema kwamba usiposhukuru kwa kidogo basi hata kikubwa hutaweza kupata, kwa sababu nililalamika hapa sina hata kituo cha afya kimoja, lakini sasa hivi nimepewa pesa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha pili na pesa za kuboresha kile kituo cha afya cha zamani ambacho nilisema ni mfu, kwa hiyo nasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado Hospitali ya Wilaya ya Liwale ina tatizo la nursing officers na mpiga picha wa x-ray. Ni lini Serikali itaweza kutupatia watumishi hawa wa kada mbili; mpiga picha wa x-ray na nursing officers? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali la nyongeza.
Matatizo ya mawasiliano katika Halimashauri ya Wilaya ya Liwale na Wilaya nzima ile ni makubwa sana na ujio wa Kampuni ya Halotel pamoja na TTCL tuliona kwamba inaweza kuwa kama mkombozi kwa ajili ya mawasiliano katika Halmashauri ile. Kwa bahati mbaya zaidi, miradi ambayo ilikuwa tayari wananchi wametoa maeneo yao kwa ajili ya kujenga minara katika Kata za Mirui, Ngongowele, Mpigamiti, Mkutano, Ndapata na Igombe na Mtunguni miradi ile yote imesimama hatuwaoni tena wale Halotel…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali juu ya kukwama kwa miradi hii katika hizo Kata nilizozitaja?
MHE. ZUBER M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Mpigamiti pamoja na Kikulyungu ni vijiji ambavyo vimepakana na hifadhi ya Selous katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, lakini kuna mgogoro mkubwa sana wa ardhi kati ya Kikulyungu pamoja na Selous.
Je, ni lini Mheshimiwa Waziri utaweza kutatua mgogoro huu ambao umedumu zaidi ya miaka 10 na watu tayari washapoteza maisha?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utangulizi tu nipende kusema kwamba jibu ni jibu hata kama halikutosha kwa muuliza swali huwa ni jibu. Hii bla bla yote iliyotolewa kwenye aya ya pili mimi sioni kama ni jibu linalijitosheleza kwa sababu mradi huu umehujumiwa kwa kiwango kikubwa sana. Kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye Jimbo langu, mimi na Mkuu wetu wa Wilaya na Mkurugenzi wetu wa Halmashauri tulipanga ziara Mheshimiwa Waziri Mkuu akakague aone nini kimefanyika kwenye mradi ule. Hata hivyo, hao watu wa Kanda wa Umwagiliaji wakishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi waliifuta hiyo ziara katika mazingira yasiyofahamika na ni kwa sababu tu huu mradi umehujumiwa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari sasa kama hii awamu wanayotaka kuisema awamu ya tatu, kutukabidhi Halmashauri mradi huu tuutekeleze badala ya kuwaachia hawa watu wa Kanda ambao wamekuwa wakiuhujumu mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutembelea mradi huu ili aangalie pesa hizi shilingi milioni 746 za Serikali ambavyo zimepotea bila sababu zozote zile za msingi? (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninachotaka kujua TARURA ni chombo ambaco kimeundwa hivi karibuni, nataka kujua TARURA sasa kwa sababu barabara wanazoshughulikia ni zile zilikuwa zinashughulikiwa na Halmashauri chini ya Madiwani. Je, hiki chombo sasa kinasimamiwa na mamlaka gani kwa niaba ya wananchi, kwa sababu hawaingii kwenye Baraza la Madiwani?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nataka kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kuridhisha.
Lakini kwa niaba ya wananchi wa Dar es Salaam na hasa wa hili eneo la Kawe, huu mgogoro ni wa muda mrefu sana. Kama ambavyo Naibu Waziri anasema anataka kushirikisha sasa jamii kuona namna ya kuwapa fidia wale wamiliki wa mwanzo mimi naomba kwamba ushughulikiaji wa suala hili Mheshimiwa Naibu Waziri bado ni mdogo sana. Sasa nataka tu nipate majibu ya uhakika kwamba Mheshimiwa Naibu Wziri unawahakikishia nini watu wa Kawe juu ya upatikanaji wa ardhi ili waweze kuondokana na adha hii ya upatikanaji wa ardhi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili la migogoro ya ardhi Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hii alishawahi kutuletea taarifa Wabunge hapa Bungeni kwamba tuorodheshe migogoro mingi kwenye majimbo yetu, lakini asilimia kubwa ya migogoro ile bado haijashughulikiwa, nini kauli ya Serikali juu ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini? (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ambavyo Naibu Waziri ameitambua Kitowelo kwamba atatenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Vilevile eneo hilo liko ndani ya kijiji cha Lilombe, lakini tangu uchimbaji huu mdogo umeanza kijiji kile cha Lilombe hakijawahi kunufaika kwa lolote na Halmashauri nzima ya Liwale haijawahi kunufaika kwa lolote, kwa sababu vibali vya uchimbaji vinatoka Kanda, halafu wale wakitoka kwenye Kanda wanaingia moja kwa moja vijijini wanaanza uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, nini kauli ya Serikali juu ya manufaa wanayoyapata vile vijiji ambavyo tayari machimbo hayo yapo? (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa ninasikitika tu kwamba hili swali halijajibiwa; kwa sababu hapa nilizopewa ni story tu, nimeona hapa zimepatikana story tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tatizo letu Liwale ni kwamba Mji wa Liwale unategemea maji kutoka Mto Liwale na Mto Liwale sasa umekauka, kwa hiyo, shida yetu ni kutafuta chanzo cha pili mbadala cha maji. Sasa hapa Mheshimiwa Waziri anasema kwamba hatua ya awali yaani kwa muda mfupi wanakarabati matenki, wanakarabati chanzo cha maji na wananunua dira. Sasa unakarabati chanzo cha maji, unakarabati vipi? Mto umekauka unaukarabati vipi? Matenki unayokarabati unataka uweke nini na mita unazokwenda kufunga unataka zitoe nini? Hapo naona swali bado halijajibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, katika muda mrefu wanasema wametenga shilingi bilioni 3.5 lakini hizi shilingi bilioni 3.5 kuna Halmashauri 14 zimewekwa hapa. Kwa nini sasa Mheshimiwa Waziri hajatenganisha kujua kwamba Halmashauri fulani ina kiasi gani maana kuzifumba hapa ni nini?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ninalouliza mo wamba, scheme ya Umwagiliaji ya Ngongowele itakamilika nini? Nimepewa story tu. Sasa nataka nijue hatua gani imefikiwa ili tuweze kupata chanzo cha maji mbadala kwa Mji wa Liwale, hilo ndio swali ambalo naomba niulize. Vilvile naomba nirudie, tunaomba mradi wa Ngongowele ukamilike. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kwenda na mimi kuangalia huo mradi?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kama ilivyo Mahakama ya Kasulu ni chakavu, lakini Wilaya ya Liwale ni Wilaya ambayo ina umri wa miaka 42 mpaka leo haina jengo la Mahakama. Jengo linalotumiwa ni lile jengo ambalo lilikuwa Mahakama ya Mwanzo ambalo sasa hivi limechakaa limefika mahali ambapo mafaili yanafunikwa na maturubai. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kuijengea Liwale Mahakama ya Wilaya?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ina misitu mikubwa miwili; kuna ule msitu ambao unahifadhiliwa na WMA (Ustawi wa Vijiji) na ule msitu wa Serikali ambao ni Msitu wa Nyera, Kipelele. Msitu huu ni msitu ambao tumeurithi kutoka enzi za Wakoloni, lakini mpaka leo harversting plan ya msitu ule haijatoka. Nini kauli ya Serikali kuharakisha harvesting plan ya msitu huu ili wananchi waweze kupata faida ya kuwepo kwa msitu huu wa Nyera, Kipelele? (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri anasema kwamba mpango mkakati mmojawapo ni kutangaza kuingiza hiyo tovuti na filamu. Hapa swali lilikuwa linataka kujua mkakati thabiti wenye dhamira ya kweli kwa sababu hapo wanaposema, hata barabara ya kufika kwenye hivyo vivutio hakuna. Sasa huu mkakati, hata hao watu unaoingiza kwenye filamu, watafikaje kule Kilwa ambapo kwenye hivi vivutio hamna barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba Pwani ya Afrika Mashariki ni mahali ambapo kwanza walikuwa na currency yao, yaani walikuwa na pesa yao; ni Kilwa, lakini haya yote watu hawayajui.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa mfano, ukiangalia Vita ya Majimaji; asili ya vita hii ni Kilwa, lakini makumbusho ya Vita ya Majimaji yako Songea. Sasa Wananchi wa Kilwa walitaka waone, Serikali inafanya taratibu gani kuirudisha Vita ya Majimaji Kilwa na kuitangaza Kilwa kama sehemu ya Utalii? Hilo ni swali la kwanza. (Kicheko)
Swali la pili...
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Liwale ulikuwa na miradi ya maji wa vijiji 10, lakini mpaka sasa hivi vijiji vyote 10 vimeshatobolewa lakini vijiji vilivyofungwa miundombinu ya maji ni vijiji vitatu tu. Vijiji ambavyo sasa hivi vina maji ni Kijiji cha Mpigamiti, Barikiwa, pamoja na Namiu. Je, vile vijiji saba vilivyobaki lini watatoa pesa kwa ajili ya kujenga miundombinu kumalizia vile visima ambavyo tayari vimeshatobolewa?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale yenye kata 20 na kituo kimoja cha aya haina gari ya wagonjwa. Shida tuliyonayo ni kubwa sana ukizingatia mtawanyiko wa kata zetu zile pale Wilaya ya Liwale mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi, umefika, umeona jinsi shida ya Wilaya ya Liwale ilivyo juu ya kupata gari la wagonjwa. Ni lini sasa Serikali itatupatia gari la wagonjwa katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Liwale? (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Liwale ni mji unaokua kwa kasi sana hasa baada ya korosho kufanya vizuri na kuna mradi wa kutafuta chanzo cha maji mbadala kwa Mji wa Liwale. Mradi ule sasa hivi una zaidi ya miaka minne umesimama. Nini kauli ya Serikali juu ya kuwapatia maji wananchi wa Mji wa Liwale? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's