Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Josephine Tabitha Chagulla

Supplementary Questions
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru sana Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kututia moyo wananchi wa Mkoa wa Geita. Nina swali moja tu la kumuuliza. Kwa kuwa vijana wetu wangependa sana kujiajiri au kuajiriwa, lakini hawana ujuzi; je, Serikali iko tayari kuwapa ujuzi?
MHE. JOSEPHINA T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba nimwulize swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wagonjwa wa kisukari katika jamii yetu na inavyoonekana, jamii bado haijapata uelewa mkubwa kuhusu kujikinga na ugonjwa huu wa kisukari. Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuja na mpango mkakati wa kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kujikinga na baadhi ya vyakula pamoja na kubadilisha staili ya maisha yetu tunayoishi? (Makofi)
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ni kubwa sana; watumishi hawa hulazimika kutembea umbali wa kilometa 50 mpaka 80, lakini wengine wanaishi Mkoani kabisa Geita ambako ni umbali wa kilometa 100. (Makofi)
Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuharakisha majengo haya ili watumishi hawa waweze kuishi karibu na ofisi zao?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kiukweli majibu ya Mheshimiwa Waziri yapo kiujumla zaidi na inasikitisha kwa sababu tunapokuwa tunatoa maswali yetu tunatarajia mwende sehemu husika kujua uhalisia wa sehemu husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mahabusu waliopo Gereza la Tarime, zaidi ya asilimia 65 ni kesi au makosa ambayo yanatakiwa yapewe dhamana; na kwa kuwa kesi nyingi ni kesi za kisiasa za kubambikwa na nyingine ni kesi za watoto chini ya miaka 15; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alikuja Tarime na hakupata muda wa kuingia Gerezani, ningependa sasa leo mtuambie ni lini Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkurugenzi wa Mashtaka watakuja Tarime kuangalia hali halisi ya mahabusu walioko Gereza la Tarime ili waweze kuondoa zile kesi ambazo jana Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba nyingine ni za juice, ili Watanzania warudi uraiani na wafanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna msongamano mkubwa sana kwenye Gereza la Tarime, capacity yake ilikuwa ni watu 260 wakiwa wamezidi sana. Sasa hivi ni zaidi ya watu 600; na kwa kuwa ukitokea mlipuko wa magonjwa tutapoteza Watanzania wengi waliopo kwenye lile Gereza; na kwa kuwa gereza lile linahudumia Wilaya ya Rorya na Tarime: ni lini sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi mtajenga gereza katika Wilaya ya Rorya, mtajenga Mahakama ya Wilaya kule Rorya ili wale Watanzania wa Rorya waweze kushtakiwa kule na kuhudhuria kesi zao kule ili kuondoa msongamano ambao upo katika Gereza la Tarime?
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kutia moyo wananchi wa Nyang’hwale.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Kharumwa kilipopandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale lakini bado hakijapata watumishi wa kutosha kulingana na hadhi hiyo ya Hospitali ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kutosha katika Hospitali hiyo ya Wilaya ya Nyang’hwale?(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa na msongamano mkubwa sana katika Hospitali zetu hizi za Rufaa kama vile Bugando na kwingine ukitaka kuonana na Daktari Bingwa; je, Serikali, haioni ni muda muwafaka sasa kuweza kupeleka Madaktari Bingwa wa watoto pamoja na akina mama katika hospitali zetu za Wilaya, ili kuondoa usumbufu huo usiokuwa wa lazima kwa wananchi? (Makofi)
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nampongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kututia moyo wananchi wa Mkoa wa Geita, lakini nina swali moja tu la nyongeza naomba nimuulize.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Benki ya Wanawake iko Mjini Dar es Salaam, lakini asilimia kubwa ya wanawake wanaishi vijijini. Je, Serikali ina mpango gani basi wa kuweza kupeleka Benki ya Wanawake katika Mikoa yote, ikiwepo Mkoa wangu wa Geita? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's