Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Hassan Elias Masala

Supplementary Questions
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa juu ya Mkoa wa Lindi, lakini naomba pia nitumie nafasi hii kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ambavyo yeye amekiri, Mkoa wa Lindi kwa ujumla ulikuwa na viwanda vingi ambavyo sasa hivi vyote vimebinafsishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nachingwea viko viwanda viwili, Kiwanda cha Korosho pamoja na Kiwanda cha Kukamua Mafuta lakini Lindi pia imekuwa na rasilimali ya bahari ambayo tukiitengenezea mazingira bado tunaweza tukatengeneza viwanda vidogo kwa ajili ya usindikaji wa samaki. Pamoja na majibu hayo aliyoyatoa je Mheshimiwa Waziri anatuahidi nini katika mpango huu ambao tunaelekea na tukiangalia Mkoa wa Lindi haujaguswa kwa namna yoyote ile? Asante sana.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru kwa majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini sambamba na hilo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kampuni ambayo ameitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa muda huo wa miaka nane ambao wamekuwa wanafanya utafiti, wamekuwa wanatumia mashine, wamekuwa wanatumia magari ambayo yamekuwa yanaharibu barabara zinazounganisha, Nditi, Nero, Namakwia pamoja na Lionja.
Je, Mheshimiwa Waziri ananiambia nini kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea juu ya fidia ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unafanywa na kampuni hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni eneo la upatikanaji wa leseni. Wananchi walio wengi wanaozunguka Wilaya ya Nachingwea wana kipato cha chini na wanatamani kujinufaisha na rasilimali ambazo zinapatikana katika maeneo yao kama taarifa inavyojionesha, lakini upatikanaji wa leseni hizi umekuwa na mlolongo mkubwa.
Je, Wizara inaweka utaratibu gani rahisi ambao utawawezesha watu wa Nachingwea kujimilikisha na kupata leseni waweze kuchimba wao wenyewe badala ya kuwa vibarua? Ahsante sana.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Swali la kwanza, kwa sababu mradi huu unagusa Wilaya zaidi ya tatu, Wilaya ya Nachingwea, Wilaya ya Ruangwa pamoja na Wilaya ya Masasi, kiasi cha pesa ambacho kimetengwa ni shilingi bilioni moja. Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa tayari kunitajia ni vijiji gani ambavyo vitaanza katika awamu hii ambayo imetengewa bilioni moja, hasa vile vinavyogusa Wilaya ya Nachingwea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa kujua, mwezi Februari mwaka huu Mheshimiwa Naibu Waziri tulifuatana mimi na yeye ndani ya Wilaya ya Nachingwea kwenda kukagua miradi ya maji ya Chiola, Nampemba pamoja na maeneo ya Mkoka. Miradi ile bado haijakamilika na yako mambo ambayo yamefanyika ambayo siyo mazuri, alituahidi ataleta wataalamu kwa ajili ya kuja kufanya uchunguzi ili tuweze kuchukua hatua za kisheria kwa hujuma iliyofanyika kwenye miradi ile.
Je, Mheshimiwa Waziri anatoa jibu gani kwa Wananchi wa maeneo haya ambayo nimeyataja ambao wanasubiri majibu yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza;
Swali langu la kwanza ninataka tu nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, hii project ya Road to Independence, nimepitia bajeti zote za Wizara ya Ulinzi, nimepitia bajeti ya Wizara ya Utamaduni, sijajua kama anaweza akaweleza wananchi wa Nachingwea ni kipindi gani haswa inaenda kutekelezwa hii program ili tuweze kujua kwa sababu miundombinu ya eneo lile bado inaendelea kuharibika mpaka sasa hivi tunavyozungumza, ikiwemo eneo ambalo ameisha Mheshimiwa Samora Machel.
Swali la pili ambalo ninapenda kuuliza, ni nini kazi za Mabalozi wetu katika nchi hizi ambazo zilinufaika na maeneo haya, ukienda Msumbiji leo hii kuna Chuo Kikuu kinaitwa Nachingwea University kinapatikana pale Msumbiji. Je, hawaoni umuhimu wa kushirikisha Balozi zetu na nchi zilizohusika kuweza kusaidia maeneo haya ili kuweza kuweka kumbukumbu za Viongozi ambao waliishi katika maeneo haya? Ahsante.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri hayajaonyesha ni muda gani ambao pesa inayotafutwa na Serikali itapatikana. Naomba sasa atoe ufafanuzi wa kutosha ili wananchi wa Nachingwea waweze kujua pesa hii ambayo kimsingi inatakiwa ikae kwenye bajeti, ni wakati gani au ni muda gani ili iwe ni rahisi kwangu kufuatilia kujua barabara hii itajengwa lini ukizingatia upembuzi yakinifu ilishafanyika?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri, naomba nipate vigezo vinavyotumika vya ku-allocate pesa katika barabara zetu kwa kiwango cha lami na ukizingatia barabara ya Nachingwea ni barabara kongwe na ya muda mrefu lakini bado haijatengewa pesa kwa muda huu wote ambao tulitazamia tayari itakuwa imepata pesa? Ahsante.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa masjala za ardhi ambazo zimejengwa katika Vijiji vya Nakalonji, Mbondo, Namatunu pamoja na Nahimba hizo ambazo zilikuwa zinadhaminiwa na watu wa MKURABITA. Maana ni muda mrefu toka zimeachwa mpaka sasa hivi zinataka kupotea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili nataka nijue, ni nini mantiki ya Serikali kuanzisha Vijiji vya mfano; kwa mfano hivyo vijiji vinne ambavyo nimevitaja ambavyo jukumu hili limeachwa mikononi mwa Halmashauri wakati wanajua Halmashauri zetu hazina uwezo au hazina uchumi wa kutosha kuweza kugharamia kukamilisha hizi hati ambazo mpaka sasa hivi zimesimama na wananchi bado hawajapata?
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Nachingwea tuna jumla ya Tarafa tano. Tarafa nne tayari zimeshafanikiwa kuwa na mitandao ya simu, lakini Tarafa moja ya Kilimarondo mpaka sasa hivi bado hamna mawasiliano ya uhakika na wako watu wa TTCL wameshafunga mitandao yao katika maeneo ya Kata ya Mbondo, Kegei pamoja na Kilimarondo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo ninapozungumza ni mwaka wa tatu sasa, bado hawajawasha mitambo yao kwa ajili ya kutoa huduma. Naomba kuuliza swali. Nini mkakati wa Serikali juu ya kuhakikisha maeneo haya yanapata mawasiliano ya uhakika?
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini pia naomba nitoe pongezi kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sambamba na haya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu Nachingwea tayari tumeshatenga maeneo na kupitia fedha ya Halmashauri peke yake kwa hizi 5% haiwezi kutosha kuwafikia vijana wengi, sijajua Serikali inatuambia nini ili tuweze kuona namna gani tunaweza kunufaika na fedha zinazotolewa na Mifuko ya Vijana kupitia Taifa badala ya kuachia Halmashauri peke yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, naomba nipate majibu juu ya jitihada gani ambazo zinafanywa kwa vijana wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ukizingatia ziko baadhi ya Kanda tayari wameshaanza kuwasogezea huduma za kuwafungulia milango ya kupata ajira ikiwemo Kanda ya Ziwa, vijana wengi wanatakiwa waende kule kwa ajili ya kujiunga na vikundi vya kushona viatu. Lindi na Mtwara tunavyo Vyuo vya VETA, nini kauli ya Serikali juu ya vijana wa kanda hii na hasa vijana wanaotoka Nachingwea ambao hawana chuo cha namna hii? Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's