Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Pauline Philipo Gekul

Supplementary Questions
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro katika nchi yetu baina ya wananchi na hifadhi, lakini tatizo hili limekuwa haliishi kwa Wizara hizi mbili ya Ardhi na Maliasili kukaa pamoja na kumaliza matatizo haya.

Nahitaji kufahamu kutoka kwa Serikali ni lini Wizara hizi mbili watakaa pamoja kumaliza migogoro ya Wananchi katika Vijiji ambavyo vinapakana na hifadhi mfano, Wananchi wangu wa Wilaya ya Babati na hifadhi ya Tarangire.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja ulio mbele yetu, miundombinu si kipaumbele.
Kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli wakati akiomba kura aliahidi ujenzi wa barabara za lami nchini kote ikiwemo Jimbo langu la Babati Mjini ambako aliahidi ujenzi wa kilometa 20 za lami. Naomba nifahamu, ni lini ahadi hii itatekelezwa kwa wananchi wa Babati?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na mikakati ya Serikali kujenga barabara za lami, lakini kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa katika maeneo yetu wakati anaomba kura, ya ujenzi wa barabara za lami. Katika Bunge hili tuliomba tupatiwe time frame kwamba ni muda gani hizi ahadi zinatekelezwa. Nataka kufahamu ni lini Mheshimiwa Waziri atatuletea ratiba ya ujenzi wa barabara hizo za lami kwa ahadi ya Rais ili tufuatilie kwa karibu ikiwemo Jimbo langu la Babati Mjini kilomita ishirini za lami?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri unafahamu kwamba gawio la Halmashauri za Mfuko wa Barabara ni ndogo sana zinazoenda kwenye Halmashauri zetu, tatizo la barabara siyo la Nzega tu lipo kwa nchi nzima baada ya mvua kunyesha sana mwaka huu barabara nyingi zimeharibika na madaraja. Napenda kufahamu Mheshimiwa Waziri kama upo tayari kuzungumza na Wizara ya Ujenzi ili gawio la Halmashauri ya fedha za Mfuko wa Barabara ziongezeke badala ya hivi sasa Halmashauri zimeshindwa kutengeneza barabara hizo zikiwemo za Babati Mjini?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Haya mashamba ya NAFCO hata kwa Babati yapo, yaka-transform kwenda RIVACU. Hivi karibuni mwaka jana, Waziri wa Ardhi alitaka Ofisi ya DC katika Wilaya ya Babati, shamba la RIVACU - Dareda lirudishwe kwa wananchi ambalo wanalihitaji kwa kilimo. Lakini hadi leo jambo hilo halifanyiki ilihali wananchi hao wamekuwa wakihangaika sana. Naomba nifahamu kupitia kwa Waziri wa Kilimo, je, uko tayari sasa kushirikiana na Waziri wa Ardhi, kuhakikisha mashamba ya RIVACU Babati yanarudi kwa wakulima wa Babati?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imetangaza kwamba nchi yetu sasa masomo ya sayansi ni lazima kwa wanafunzi wetu; lakini hakuna maandalizi ambayo yamefanyika mpaka sasa, hatuna walimu hao kabisa. Nitolee mfano katika Jimbo langu la Babati Mjini, walimu wa mathematics katika shule kumi za sekondari, ni shule moja tu ndiyo ina mwalimu wa hesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu, Serikali haioni kwamba inawachanganya wananchi wa Tanzania katika kutoa kauli zao wakati hawajajiandaa kukabiliana na tatizo hilo? Ni lini wanaajiri walimu hao wa sayansi? (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa pamoja na mishahara ya watumishi hawa wa sekta ya afya, Serikali ilikuwa ikitoa motisha mbalimbali ikiwemo on call allowance kwa wauguzi wetu; lakini hadi hivi tunavyoongea Serikali haipeleki pesa hizi kwa wakati; na nitoe mfano kwa Hospitali yangu ya Mrara katika Jimbo la Babati Mjini, tangu mwezi wa pili wauguzi wale katika hospitali ile tangu mwezi wa pili hawajalipwa fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu, ni kwa nini Serikali haipeleki fedha hizi kwa wakati kama ilivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika bajeti iliyopita OC katika Halmashauri zetu na katika hospitali zetu zilipunguzwa kwa zaidi ya asilimia 60; nitoe mfano wa hospitali yangu ya Mrara, ilikuwa inapokea OC ya shilingi milioni 154 lakini ikapunguzwa hadi shilingi milioni 46 kwa mwaka na hizi fedha sasa zilipe likizo za watumishi, maji na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu kauli ya Serikali, ni kwa nini fedha hizi zimepunguzwa ilhali mambo haya sasa yamekwama? Mfano sisi, zaidi ya shilingi milioni 10 hospitali inadaiwa, imeshindwa kulipa BAWASA bili ya maji. Serikali iko tayari kufikiria kuhusu uamuzi huu wa kupunguza OC katika hospitali zetu za Wilaya ili waweze kuziendesha hospitali hizi? (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tatizo la soko la chai kuna tatizo kubwa sasa linaendelea katika Mkoa wangu wa Manyara kuhusu soko la mbaazi. Wafanyabiashara wamekataa kununua mbaazi kabisa katika Wilaya ya Babati na katika Wilaya zote za Mkoa wa Manyara na wakulima wamebaki na mbaazi zao kwa sababu India mwaka huu ambao walikuwa wanunuzi wakubwa wao wamelima, Uganda wamelima na Kenya wamelima.
Naomba nipate kauli ya Serikali juu ya wakulima hao wa mbaazi katika Mkoa wa Manyara ambao wameshindwa kuuza mbaazi zao kwa sababu wafanyabiashara wamegoma kabisa kununua mbaazi hizo.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa miongoni mwa sababu ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezitaja, ambazo zinasababisha uharibifu wa barabara, magari na wakandarasi wasio waaminifu, sababu kubwa mwaka huu iliyosababisha barabara zetu kuharibika ni mvua za masika ambazo hazikutegemewa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa kauli humu ndani katika Bunge la Bajeti kwamba TANROADS watoe fedha katika Halmashauri zetu kwa sababu ni dharura, wasaidie Halmashauri kujenga hizo barabara. Naomba nifahamu hii kauli ya Serikali imetekelezwa kwa kiwango gani, hususan katika Mkoa wangu wa Manyara na Jimbo la Babati Mjini maana hizo barabara hazijatengenezwa kabisa?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watoto wenye mtindio wa ubongo wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali sawasawa na wale watoto wenye ulemavu wa ngozi, hususan suala la haki ya kupata elimu. Naomba nifahamu Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watoto hawa ili wapate haki ya kupata elimu kwa kuanzisha madarasa maalum au shule maalum walau kwa kila Wilaya ili watoto hawa wapate haki hiyo ya elimu ikiwemo Wilaya yangu ya Babati?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sababu ambazo Madaktari Wakuu au Waganga Wakuu wamekuwa wakitoa kwa suala zima la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu ni kwamba, kundi hili la msamaha la wazee, akinamama wajawazito na watoto ni wengi na wanaugua mara kwa mara. Naomba nifahamu, Serikali mmefanya utafiti kwa kiasi gani ili kuona kwamba hili kundi halilemei makundi mengine na kusababisha ukosefu wa dawa?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama kuna maamuzi mabaya yalishawahi kufanyika ni maamuzi tuliyoyafanya katika Bunge la bajeti hii iliyopita ya 2016/2017 kwa kuondoa au kufuta vyanzo vikubwa ambavyo vinazipatia Halmashauri mapato na kuvipeleka Serikali Kuu.
Mfano kodi ya majengo ambayo mpaka sasa TRA wameshindwa kukusanya, kodi ya ardhi inapelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina lakini mpaka sasa hazijarudishwa, Halmashauri hazina fedha. Swali, Mheshimiwa Waziri ni kwa nini msifikirie upya uamuzi huu na kurudisha vyanzo hivi kwenye Halmashauri zetu kwa sababu hata Serikali Kuu mkikusanya hamzirudishi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri juzi hapa kwenye Bunge hili kwamba Halmashauri zetu nyingi hazina set za upimaji viwanja, hakuna vile vifaa na katika majibu yake amesema kwamba ataangalia utaratibu wa kurudisha fedha hizi. Ni kwa nini sasa hizi pesa zisitumike kununua vifaa vya upimaji katika Halmashauri zetu ilhali amekiri mwenyewe kwamba hakuna vifaa hivyo?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakulima wa Tanzania wanaelekea sasa kwenye msimu mwingine wa kilimo ikiwa mazao yao bado wanayo manyumbani hawajauza. Tuliona wakulima wa nyanya, mbaazi, mahindi na mazao mengine, na Serikali ilitoa kauli katika Bunge hili kwamba wanatafuta masoko nje ya nchi nilijibiwa na Naibu Waziri wa Kilimo. Naomba nifahamu mchakato huo umefikia hatua gani maana wakulima mpaka sasa wana mazao yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Waziri ni kwamba, wanaanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ili mazao haya yapate soko na mtawezesha sekta binafsi na Serikali haitoi moja kwa moja fedha kwa ajili ya viwanda hivyo watu binafsi waanzishe. Wakulima wa Tanzania wasubiri kwa muda gani mpaka hivyo viwanda vianzishwe ili mazao yao yapate soko?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Miongoni mwa matatizo ambayo tunayapata katika Wilaya ya Babati kwa Hospitali ya Mrara ni ranking ya hospitali hiyo ambapo mpaka sasa inaitwa Kituo cha Afya wakati hospitali hiyo imekuwa ikihudumia watu wa Kondoa na watu wa Babati Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tumekuwa tukipendekeza kwamba hospitali hii tuipandishe rank iwe Hospitali Teule ya Wilaya, lakini Serikali imekuwa haitupi ushirikiano. Je, sasa wako tayari kutusaidia ili hospitali hiyo ipate dawa na vifaa tiba kuhudumia watu wote hao?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, juzi Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake walijibu kuhusu suala hili la makundi maalum (akina mama wajawazito, watoto na wazee), walisema kwamba sasa wameiagiza Halmashauri zetu waorodheshe wazee ili wapatiwe kadi za bima ya afya. Naomba nifahamu kama Serikali ipo serious huo mwongozo umeshatolewa na TAMISEMI katika Halmashauri zetu ili Madiwani wapange fedha hizo za kuwalipia wazee bima ya afya katika bajeti inayofuata?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TANESCO wameondoa service charge na hawa ndiyo wanatusaidia kusukuma maji katika vyanzo vyetu lakini wenzetu wa Wizara ya Maji kwenye bili zetu za maji bado kuna service charge. Je, ni lini hii service charge itaondolewa kwa wananchi wetu kwa sababu kwa kweli ni gharama kubwa pamoja na bili hizi ambazo zimepanda?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti tarehe 12 Januari, 2017 nilifika kwenye Gereza la Babati nikakuta watuhumiwa wa kesi ya mauaji na dawa za kulevya wamekaa zaidi ya miaka minne na sheria haijaweka time frame, hizo siku 60 ni kwa makosa ya kawaida. Mheshimiwa Waziri tuambie ni lini mtafanya marekebsho ya sheria ili hata kwa makosa haya ya mauaji na dawa za kulevya watu wasikae magerezani au mahabusu kwa muda mrefu kama ilivyo sasa?
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika,
ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa gharama kubwa ambazo Hifadhi ya Ngorongoro inatumia ni pamoja na kumtunza faru Fausta ambaye chakula chake kwa mwezi ni shilingi milioni zaidi ya 64. Naomba kufahamu, Serikali ina mpango gani juu ya faru huyu Fausta ambaye analigharimu Taifa au hifadhi ile kwa fedha nyingi sana kwa mwezi na
hata kwa mwaka?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Job Yustino Ndugai

Kongwa (CCM)

Contributions (1)

Profile

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Special Seats (CCM)

Supplementary Questions / Answers (3 / 0)

Contributions (1)

Profile

View All MP's