Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. Mary Michael Nagu

Supplementary Questions
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii adimu ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ilivyo Wilaya na Mlalo, Wilaya ya Hanang‟ ina bwawa ambalo lilikuwa likikusanya maji ya Mlima Hanang‟ kwa scheme ambazo zinaweza zikatumika kwa umwagiliaji. Ni miaka mitano sasa tumekuwa tukiomba bwawa hilo likarabatiwe na bado hatujafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunisaidia kuwahakikishia wananchi wa Hanang‟ kwamba kama anavyoomba Mbunge wa Mlalo na Mbunge wa Jimbo la Hanang‟ analiomba hilo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri alilotoa. Pamoja na jibu hilo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, Hanang ni Wilaya ya pili kuwa na CHF iliyoboreshwa na CHF hii iliyoboreshwa haitaweza kunufaisha wananchi kama hakutakuwa na dawa za uhakika. Je, Serikali haioni ni vizuri pamoja na CHF iliyoboreshwa kuwe na duka la MSD?
Pili, Wilaya ya Hanang ina upungufu wa Wodi za akina mama na watoto na nimeshukuru sana kuona kwamba wodi ambayo italaza wanawake 16 inajengwa, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba ni wanawake 200. Je, kuwa na wodi itakayolaza wanawake 16 itatosheleza mahitaji hayo?
Pamoja na hivyo, naomba Serikali ione umuhimu wa Wilaya ya Hanang ambayo imezungukwa na Wilaya nyingi kuwa na wodi za kutosheleza akina mama kulazwa.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile fedha za Mfuko wa Barabara ni asilimia 30 kwa TAMISEMI na asilimia 70 kwa Serikali Kuu, hatuoni kutokana na mahitaji kama haya ya makorongo aliyoyasema Mheshimiwa Bashe, sasa wakati umefika wa kugawa fedha hizo asilimia 50 kwa 50 na Wilaya ya Hanang‟ ina makorongo makubwa kutokana na uharibifu wa mazingira lakini Halmashauri kama alivyosema Mheshimiwa Waziri haina uwezo kabisa wa kujenga makorongo hayo?
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ya kijito cha Endagaw yamekuwa mengi kuliko utaalamu ulivyoona na kwa hivyo mfereji mmoja unaweza ukafanya ukuta uliojengwa kubomoka.
Je, Waziri anaweza kuwahakikishia watu wa Endagaw na wa Hanang kwamba huu upande wa pili utajengewa mfereji mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, palipokuwa na kijito cha Endagaw kulikuwa na wananchi ambao walikuwa na shughuli zao na makazi yao na wakaondolewa kwa ajili ya skimu hiyo.
Je, Serikali inaweza kutusaidia kuwapa fidia wale watu ambao wameondoka pale kwa ajili ya mradi huu? Namuomba Mheshimiwa Waziri aweze kutembelea eneo hilo na kuona umuhimu wa maswali haya mawili ya nyongeza niliyoyauliza, ahsante.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii.
Kwa kuwa, Wilaya ya Hanang ni Wilaya ya wafugaji, na wananchi wamejitahidi sana kujenga hosteli kama ya shule ya Mreru, Mulbadau, Endasak na kwa kufuatia suala hilo; je, Serikali ipo tayari kusaidiana na wananchi, kuona kwamba zile hosteli na mabweni yaliyokuwepo toka wakati wa uhuru, tunaimarisha na kuboresha miundombinu ambayo ipo?
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kuwaletea matumaini wananchi wa Hanang. Sasa naomba niulize maswali madogo mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa kutambua kwamba, Wilaya ya Hanang ilisahauliwa katika Awamu ya kwanza na ya pili, sasa atakubaliana na mimi, na ninahakika atakubaliana na mimi kwamba, vijiji hivyo vya Hanang alivyovitaja sasa vitakuwa Awamu ya tatu viwe vya kwanza katika kupewa umeme katika Awamu hiyo ya tatu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; najua kwamba, awamu ya kwanza na ya pili ilipewa vijiji vichache mpaka sasa havijapata umeme. Je, Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, katika muda mfupi unaokuja vijiji hivyo vichache vipate umeme basi, ili viwape matumaini wananchi wa Hanang?
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kufanya bidii yote ya kutengeneza madawati kwa ajili ya watoto wa shule na kwa sababu madarasa hayatoshelezi kuna hatari ya madawati hayo kuharibika. Je, wakati haujafika sasa kuwa na mpango mzuri kama ulivyokuwa wa madawati kutengeneza madarasa hasa pale ambapo tunazingatia wananchi wameshajitolea kwa kiasi kikubwa? Je, ni mpango gani ambao Serikali unaweza ukaufanya ili tuwe na madarasa ya kutosha kuweka madawati ambayo tumeyatengeneza wote? Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Serikali ningependa ijue kwamba kuna wananchi waliojitolea kwa kujua umuhimu wa walimu kujenga maboma kwa ajili ya nyumba za walimu, pamoja na madarasa.
Je, Serikali itatoa kipaumbele kwa wale wananchi ambao wameonesha umuhimu wa walimu na umuhimu wa elimu?
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali langu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Bwawa la Gidahababieg siyo la umwagiliaji tu, maeneo yote yale hayana maji ya uhakika kwa hivyo litakuwa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo pamoja na umwagiliaji ikiwezekana. Baada ya bwawa lile kuvunjika kutokana na athari za mvua mwaka 2006, nilifikisha suala hilo kwenye Serikali mwaka 2007 na mpaka leo hakuna lililofanyika. Nataka kujua kama ni kweli mchakato utaanza na bwawa hili lirudi kwa sababu ndiyo linakusanya maji ya mlima Hanang yanayomwagika na kupotea bure?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Vijiji vya Hirbadaw, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela vyote vilikuwa kwenye Mradi wa Benki ya Dunia na maji hayakuweza kupatikana. Naomba nijue ni lini vijiji hivyo vitaanza kutafutiwa vyanzo vingine ili watu wale waweze kupata maji kwani Bonde la Ufa halina maji? Nashukuru sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's