Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Maida Hamad Abdallah

Supplementary Questions
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria wale wote walioshiriki vitendo hivi, lakini pia kuna wengine ambao tayari sasa hivi wameshakamatwa, yaani watuhumiwa wameshakamatwa, je, Serikali itakubaliana nami kwamba baada ya kugundulika watu hawa waliofanya vitendo hivi kwa raia wa Zanzibar, Serikali iko tayari pamoja na hatua kali zitakazochukuliwa za kisheria, iko tayari kuwataka walipe fidia kwa wale wote waliowafanyiwa vitendo hivi?
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa wanavyojitahidi na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kuhusiana na kadhia hii au suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Katika uhakiki unaondelea kuchukuliwa hadi tarehe aliyoitaja Mheshimiwa Waziri ni hasara kiasi gani Serikali imepata hadi kufikia tarehe hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pamoja na mikakati ambayo Serikali imekuwa ikichukua kuhusiana na watumishi pamoja na maafisa waliohusika na swala hili. Serikali itambue kwamba kuna udhoroteshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa inakwama pamoja na ukosefu wa madawa pamoja na ufinyu wa bajeti uliokuwa unajitokeza.
Je, Serikali inaweza kukubaliana na mimi kwamba pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kwa watumishi kwamba iwepo adhabu ya kurudisha fedha ambazo walizipoteza?
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninalo swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hamasa pia mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya kuhamasisha uendelezaji wa zao hili, lakini bado hadi sasa kipo kiwanda kimoja tu kinachopokea mazao haya ambapo kipo Kisiwani Pemba. Je, Serikali inawaambia nini wananchi katika uendelezwaji wa viwanda hasa katika mkakati huu wa uendelezaji wa viwanda nchini? (Makofi)
MHE. MAIDA H. ABDALLAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa miradi mingi ya maendeleo ngazi ya Halmashauri imekuwa ikisuasua na ikikwama kutokana na ucheleweshwaji wa fedha kutoka Hazina. Je, Serikali inatoa kauli gani katika ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo iliyopitishwa na bajeti ya Serikali mwaka 2015/2016 na 2016/ 2017?
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Hata hivyo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Waziri kujibu swali hili na kunihakikishia/kukiri kwamba yapo baadhi ya maeneo Kisiwani Pemba ambayo yanapata shida ya mawasiliano, hata hivyo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la mawasiliano Kisiwani Pemba katika maeneo ya Makangale, Kipange, Tumbe Kiungoni, Mtambwe, Gando na maeneo mengine yaliyopo Kaskazini na Kusini Pemba na kupelekea wananchi wa mikoa hiyo kupata usumbufu wa mawasiliano hasa katika kipindi cha dharura…
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali kupitia Wizara hii inawaambia nini tena wananchi kuhusu kutatua changamoto hii ambayo imekuwa ikiwaletea shida muda mrefu na wakati mwingine wananchi hulazima kupanda kwenye miti mirefu kutafuta mawasiliano? (Makofi)
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuongozana na wataalamu wake kwenda Pemba kutafuta maeneo na vijiji mbalimbali kuweka minara ili kuwatatulia matatizo wananchi wa Pemba? (Makofi
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Je, Serikali inaweza kutuambia ni kwa nini wazee kama baba na mama wa Mbunge hawakuwekwa miongoni mwa wategemezi katika bima ya afya?
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kama alivyokwishasema Mheshimiwa Waziri kwamba mapato ya Halmashauri ndiyo vyanzo vikuu vinavyoendeleza maendeleo katika Halmashauri. Kwa kuwa makusanyo yanayotokana na mapato na kodi ya ardhi na majengo urejeshaji wake kutoka katika mamlaka husika umekuwa ukisuasua huku Halmashauri zikiwa zimejipangia majukumu mbalimbali na hivyo utekelezaji wake kuchelewa. Je, Serikali haioni kwamba mtindo huu unaathiri utekelezaji wa haraka wa vipaumbele ilivyojipangia Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ndani ya Halmashauri zetu kwa mujibu wa sheria wametakiwa kutekeleza agizo la kuwawezesha wanawake na vijana kwa kutenga asilimia 10 ili ziwaendeleze kiuchumi. Kwa kuwa changamoto hii imekuwa ikiathiri sana agizo hili, je, Serikali sasa ipo tayari kuleta waraka Bungeni wa mapendekezo ya kwamba mapato yanatokana na kodi za ardhi na majengo baada ya makusanyo zibaki kwenye Halmashauri husika? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's