Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Martha Jachi Umbulla

Supplementary Questions
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kususua kwa barabara ya hizi za Busokelo inafanana sana na kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya kutoka Dodoma kwenda Babati na hasa kipande cha Mayamaya kwenda Bonga, naomba kujua Serikali inasema nini kuhusu changamoto hiyo kubwa ambayo imechukua muda mrefu na ahadi ilikuwa mwisho wa mwaka 2015 kumalizika?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Nishati ya umeme ni nishati muhimu sana hasa kwa maendeleo ya elimu. Hivi sasa sekondari zetu nyingi za kata, hasa kwa mikoa ya pembezoni kama Manyara na kwingineko hakuna umeme kabisa. Je, ni kwa nini usambazaji huu wa umeme vijijini unaofanywa na REA usilenge kwanza sekondari hizi za kata ambazo zina hali mbaya na ambazo zinahitaji kuboreshwa kielimu na kuboreshewa mazingira ya kusoma?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayajaweza kutia matumaini makubwa, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitenga fedha kwa bajeti ya 2015/2016 kwa ajili ya miradi ya kipaumbele na ya kilio cha muda mrefu cha wananchi hususani mradi wa maji katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Haydom ambayo inatumikia mikoa zaidi ya minne ikiwepo Manyara, Singida, Simiyu na kwingineko na ambayo hadi leo haijakamilika kutokana na kukosa fedha lakini pia ikiwepo na bwawa la maji la Dongobeshi ambacho ni kilio cha muda mrefu. Hata Mheshimiwa Rais alipopita wakati wa kampeni walimpa mabango na ni kilio cha muda mrefu kweli kweli na sasa mkandarasi ameacha hiyo kazi kwa sababu pia hajalipwa fedha zake. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu miradi hii ya kipaumbele cha wananchi na kilio cha muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miradi ya maendeleo ambayo inatengewa fedha kwa kipindi kilichopita huwa zile fedha zinakwenda kwenye dharura nyingine ambazo zinapangwa na Serikali kuliko fedha kwenda kwenye miradi iliyokusudiwa kama ilivyoidhinishwa na Bunge. Je, Serikali ina mikakati gani sasa kwa bajeti ya 2016/2017 kuhakikisha kwamba fedha zote zinakwenda kwenye miradi yenye kilio cha muda mrefu cha wananchi kuliko kwenda kwenye miradi ya dharura kama ambavyo ilikwenda kwenye miradi ya maabara kipindi kilichopita?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa maeneo yaliyotajwa kwenye swali la msingi, Naberera iko Simanjiro na Kibaya iko Wilaya ya Kiteto na ni maeneo yanayozalisha sana mahindi hapa nchini, kwa hiyo, ni maeneo muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, lakini hakuna barabara hata moja inayounganisha hata na Makao Makuu ya Mkoa ambayo ni Babati na barabara zake ni za vumbi na hivyo zinaharibika sana kwa ajili ya kubeba mahindi nyakati za mvua.
Je, Serikali ina mikakati gani sasa kwa umuhimu nilioutaja kuhakikisha kwamba angalau kuna barabara hata moja inayounganisha maeneo hayo muhimu kwa uchumi na Makao Makuu ya Mkoa wa Babati?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vifo vya wanawake wanapokwenda kujifungua katika mikoa yetu tunaposomewa, kwenye RCC bado iko juu sana na tena kwa muda mrefu sasa na hii ni kutokana na kukosa vifaa tiba, vitendanishi na huduma stahiki kwa ajili ya kujifungua. Je, sambamba na ukarabati wa zahanati na vituo vya afya sasa hivi kama mkakati wa Serikali, nini kauli ya Serikali hasa kutokana na vifo hivi, takwimu hizi ambazo zipo kwa muda mrefu, mama kwenda kujifungua anafariki?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa umuhimu huohuo wa wanawake wa Mkoa wa Morogoro kupata mikopo kutoka Benki ya Wanawake, Mkoa wetu wa Manyara, wanawake wengi ni wa kutoka jamii ya wafugaji na jamii ya wafugaji hawana elimu pana ya kukopa katika vyombo vya benki hasa tutakapokuwa tumefikiwa na Benki ya Wanawake. Je, Wizara ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inaandaa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na elimu ya uelewa ili wanawake wa jamii ya kifugaji nao waweze kunufaika na Benki ya Wanawake?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zote za Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini zinapita kwenye Halmashauri za Wilaya na katika vikao vya Halmashauri za Wilaya hasa Kamati hiyo ya Fedha na Mipango Wabunge wa Viti Maalum hawashiriki na ndiyo watu wenye dhamana na maendeleo ya wanawake.
Kwa kuwa sheria hiyo iliyotungwa ambayo inawakataza Wabunge wa Viti Maalum kuingia kwenye Kamati hizo ilitungwa zamani sana kabla hata utaratibu wa Ubunge wa Viti Maalum haujaanza bali kulikuwa na Wabunge wa Majimbo na Wabunge wa Kuteuliwa na Rais; na kwa kuwa mwaka jana kwenye Bunge la Kumi, Mheshimiwa Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri alipokuwa anajibu swali hapa Bungeni, alitueleza kwamba sheria hiyo ni kandamizi na tunahitaji kuileta hapa Bungeni ili tuirekebishe Wabunge wa Viti Maalum washiriki.
Je, Serikali italeta lini hiyo sheria ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki katika Kamati hii muhimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri zetu za Wilaya hasa kwa Mkoa wetu wa Manyara zinatenga asilimia kumi za fedha kwa ajili ya miradi ya wanawake. Utaratibu na mfumo wa utoaji wa fedha hizo kwa ajili ya miradi ya wanawake hauko vizuri na kuna upotevu mkubwa sana wa fedha hizo za Serikali.
Je, ni kwa nini Madiwani wa Viti Maalum wakisaidiana na Wabunge wao wasisimamie kikamilifu utoaji na urejeshaji wa fedha hizo ili ziweze kuwafikia walengwa?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Taasisi nyingi za fedha zinawakwepa wakulima na wafugaji kuwapatia fursa za mikopo, lakini nashukuru katika maelezo yake sasa hivi amefafanua hasa kwa wakulima. Sasa je, Serikali ina mikakati gani hasa kuwapa wafugaji mikopo ili waweze kuendeleza mifugo yao?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kutia matumaini, naomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kiteto kwa sehemu kubwa inakaliwa na jamii ya wafugaji ambao shule haijawa kipaumbele sana, hasa kwa watoto wa kike. Kwa sehemu kubwa ukombozi mkubwa ni kuwa na shule za bweni ambako wasichana wanaweza wakabaki shuleni badala ya kurudi nyumbani kukwepa kuolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha ni kwamba kuna baadhi ya sekondari za kata tena za muda mrefu zenye mabweni, kama sekondari ya Ndedo na Lesoit ambazo ni za bweni na zina wasichana wengi wa Kimasai, lakini inasikitisha kwamba hizo shule za kata hadi leo hazina umeme. Na sio hizo shule tu hata Kituo cha Afya cha Osteti ambacho kinasaidia sana huduma za afya kwa akina mama hakuna umeme.
Je, ni lini Naibu Waziri sasa atachukua jukumu la makusudi kutembelea Wilaya ya Kiteto, hasa maeneo haya niliyoyataja, ili kujionea mwenyewe jinsi ambavyo sekondari hizo hazina walimu na hata maabara tulizojenga hazitumiki kwa ajili ya kukosa umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba ku-declare interest kwamba nimetoa mikopo kwa takribani miaka 20 sasa katika Mkoa wangu wa Manyara. Uzoefu unaonyesha kwamba ufanisi mkubwa kwa kurejesha mikopo kwa wanawake na vijana ni katika vijiji vile vyenye umeme wa uhakika. Je, nini kauli ya Serikali kabla ya kutoa hizo shilingi milioni 50 katika maeneo haya ya wafugaji na mikoa ya pembezoni kuhakikisha kwamba vijiji hivyo vitakuwa na umeme kabla ya kusambaza hizo fedha?
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mimi nina swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa suala la rasilimali watu katika Wizara ya Elimu hasa kwenye vyuo vyetu na hata shule za sekondari bado ni changamoto kubwa na kwa kuwa hali hii inasababisha pia baadhi ya Waratibu wa Elimu kupangiwa masomo ya kufundisha sawasawa na Walimu wengine hali inayopelekea kuona kwamba ni kazi iliyopo nje ya job discription zao. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kufikiria kwa kuwa hiyo ni kazi ya ziada basi waweze kupewa posho ya ziada hawa Waratibu wa Elimu kuliko hali ya sasa ambayo wanafundisha kama Walimu wengine lakini hawana nyongeza ya mishahara?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's