Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Issaay Zacharia Paulo

Supplementary Questions
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili.
Kwanza, kwa kuwa mipango hii ya bajeti tunayoijadili sasa hivi katika Bunge letu inahitaji sana kada hizi za Watendaji na kwa kuwa nafasi nyingi katika kada hizi ziko wazi, je, ni kwa nini Serikali isione umuhimu mkubwa wa kutoa nafasi kwa wale vijana waliomaliza Vyuo vya Serikali za Mitaa na Vyuo vya Utawala, wakaanza kujitolea katika kipindi hiki cha mpito kutegemeana na makubaliano yao katika Serikali za Mitaa hususan kwenye maeneo yao, ili baadaye waweze kuingia katika mfumo wa ajira?
Pili, ni kwa nini sasa Serikali isione inapaswa kutenga fedha za kutosha katika kuwezesha ofisi za Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa sababu fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika ngazi za chini zinatumika kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uendeshaji katika ofisi hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri akiwa Mbulu aliwaahidi wananchi wa Mbulu kwamba Halmashauri ya Mbulu itafute jengo kwa ajili ya Mahakama. Namuomba Mheshimiwa Waziri katika mwaka huu wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu itafanikiwa kwa kuwa ina kesi nyingi za ardhi ili Baraza hilo liweze kuzinduliwa na tayari Hamshauri imepata jingo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ina shule ya viziwi kule Dongobesh na pia ina Kitengo cha Elimu ya Watoto Walemavu katika Shule ya Msingi Endakkot na kwa kuwa kundi hili ni kubwa katika jamii; je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kuweka Kitengo cha Elimu kwa Walemavu katika kila halmashauri kwa shule mojawapo ili kundi hili lililokosa nafasi wapate huduma stahiki?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na jitihada nzuri za Mheshimiwa Rais wetu; na pia pamoja na harakati kubwa ya kuwajengea Watanzania nia njema ya kulipa kodi; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa Uchaguzi na katika Kampeni zake aliahidi kuondolewa kwa tozo ndogo ndogo kutokana na wafanyabiashara wadogo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kuwa ina kila sababu ya kutazama upya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na makundi gani yanasamehewa katika hizo tozo ndogo ndogo?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Mbulu yenye majimbo mawili, tuna vituo vya afya ambavyo havijakamilika takribani vituo vitano. Kwa mfano, Tarafa ya Nambisi ina kituo cha afya ambacho hakina hadhi, Tarafa ya Daudi na Tarafa ya Dongobesh.
Je, ni kwa nini Serikali isichukue hatua za makusudi kukagua vituo vyote vya afya, na kwa kuwa Waheshimiwa Madiwani katika bajeti ya Halmashauri hawawezi kupitisha bajeti ikaenda kwenye kituo kimoja ili Serikali itenge fedha za kutosha kwa kila Halmashauri, kwa kila mwaka walau kuwa na kituo cha afya kitakachotengewa fedha kutoka Hazina, nje ya bajeti ya Halmashauri? Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nami naomba kuuliza maswali madogo mawili. Swali langu la kwanza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri…

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru. Naomba kuuliza, ni kwa nini Wizara ya Ujenzi haijaweza kupitisha barabara mpya za Halmashauri ya Mji wa Mbulu na kwa kuwa mji wetu wa Mbulu ni mji mkongwe kuliko miji yote Tanzania? Naomba kauli ya Wizara kuhusu barabara hizi mpya kwa kuwa sasa magari yameongezeka sana katika Wilaya zetu. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Ni kweli kuwa taifa letu lina changamoto kubwa ya ajira kwa vijana. Kwa kuwa vijana hawa wengi wako kwenye mazingira ya vijijini, ni kwa nini sasa Serikali isianzishe Jukwaa la Vijana katika Halmashauri zetu ili vijana wetu walioko vijijini na wale walioko kwenye miji midogo kama Mbulu na kwingineko waweze kujadiliana na Maafisa Uchumi, Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii changamoto na fursa zilizoko na jinsi vijana wetu wanavyoweza kupata ajira zile ambazo si rasmi kutokana na ukosefu wa ajira? Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kufahamu, kule Jimboni Mbulu kuna Bwawa la Dongobesh lililokamilika takriban miezi sita. Mkandarasi ameshaleta certificate yapata miezi miwili. Waheshimiwa Mawaziri wanajibu majibu hapa, lakini kule Wizarani hakuna mchakato wa kuwalipa hao Wakandarasi. Naomba, kama itawezekana, Waziri ana kauli gani kumlipa Mkandarasi wa Bwawa la Dongobesh?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza swali dogo. Kwa kuwa sasa kuna wimbi kubwa la ujenzi wa vituo vya afya katika ngazi za kata, kwa mfano, Wilaya yetu ya Mbulu ina tarafa tano, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kupitia tarafa zote hizo tano na kuona ni kituo gani cha afya chenye mahitaji madogo ya fedha ili iweze kutoa huduma kwa kutengewa fedha za kutosha? Kwa mfano tarafa zote zina vituo vingi lakini hakuna kituo kinachotoa huduma stahiki? Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusu vyuo hivi viwili vilivyoko Wilayani Mbulu, nami naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa katika Chuo cha MCH - Mbulu hadi sasa wanafunzi wetu wamesitishiwa huduma ya chakula kutokana na madeni makubwa walionayo wazabuni. Je, ni lini Serikali itarudisha huduma hiyo ya chakula ili wanafunzi wetu wasome kwa amani? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu kuna jengo la ghorofa lililojengwa takribani miaka mitatu na liko chini ya kiwango na kwa sasa halitoi huduma iliyokusudiwa. Je, Serikali inachukua hatua gani kuja kubomoa hilo jengo na kujenga jengo lingine jipya ili liweze kutoa huduma kwa hospitali yetu na chuo kwa ujumla?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na nimpongeze Naibu Waziri kwa maelezo ya swali la msingi. Tatizo la ujenzi holela wa miji katika Tanzania yetu inakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fedha, watumishi kwa maana ya Maafisa Mipango miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu takribani miaka sita tulikuwa tunatafuta fedha kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe wa Master Plan ya Mji wa Mbulu na hatimaye kushindikana, hivyo ni kwa nini Serikali isifanye mapitio upya kuona rasilimali watumishi kwa maana ya wataalam wa Mipango Miji, fedha za kuhakikisha kwamba miji midogo na miji mikubwa inayopanuka inafanyiwa utaratibu wa mipango miji ili nchi yetu isikumbwe mara nyingi na bomoabomoa zinazojirudia mara nyingi? Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nichukue nafasi hii kuuliza maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa kilio cha barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara – Mbulu ni ya muda mrefu na kwa kuwa barabara hii ndiyo inaunganisha Mji wa Babati na Mji wa Arusha kwa ajili ya wananchi wa Mbulu na kwa kuwa taarifa anayosoma Mheshimiwa Naibu Waziri ni taarifa aliyoandikiwa; wakati wa bajeti tulikubaliana fedha zote, karibu shilingi bilioni moja na milioni 200 zitumike kujenga daraja la Magara, na kwa sasa fedha zinazozungumzwa, shilingi milioni 300, ni hela ndogo sana.
Je, ni lini Naibu Waziri au Waziri mwenyewe mwenye dhamana ya Wizara hii atafanya ziara kujionea hali halisi ya mateso wanayopata wananchi wa Mji wa Mbulu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika uwanja wa Mbulu Mjini, aliahidi kuweka kilometa tano za lami katika Mji wa Mbulu kutokana na Mji wa Mbulu kuwa Mji mkongwe sana na kwa kuwa Rais aliahidi kwamba ahadi hii itatekelezwa katika bajeti ya mwaka 2015/2016.
Je, ni kitu gani kilipelekea ahadi ile isitekelezwe mpaka leo?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwezesha elimu bure, upatikanaji wa madawati na pia watumishi hewa kuondolewa, naomba kufahamu, kwa sasa Watanzania wengi hasa akinamama katika SACCOS zao wamekuwa na hamu kubwa ya kufanya biashara. Je, Serikali inachukua hatua gani kuwezesha SACCOS za akinamama katika halmashauri zote zipate hela za kutosha?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana. Tatizo hili la wazabuni kushinda tender na baadae kuchelewesha huduma kwa Watanzania kwa muda uliokusudiwa imekuwa tatizo kubwa katika nchi yetu. Mifano ya wazi zipo katika Halmashauri za Wilaya ya Mbulu kwa miradi ya maji na miradi ya afya. Mifano hiyo ni kama ambavyo kupewa tender makampuni ambayo hayana uwezo na hatimaye baadaye kuchelewesha huduma hizi. Je, Seriakli yetu sasa kutokana na hali hii ambapo tenda hutolewa na wataalam ndani ya Halmashauri, inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma kwa wakati uliokusudiwa kutokana na muda wa mikataba?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichukue nafasi hii kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri hayakugusa ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika barabara ya Mji wa Mbulu na ahadi hiyo iliwagusa wananchi wa Mji wa Mbulu wakati wa uchaguzi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambia nini kuhusu utekelezaji wa ahadi hii ambayo imesahaulika, hadi sasa mwaka mmoja umeisha baada ya uchaguzi?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri niwashukuru Naibu Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa kuja Mbulu na kutembelea baadhi ya Halmashauri za Wilaya ya Mbulu na vituo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika swali la msingi muuliza swali alitaka pia mpango mkakati wa Serikali kuajiri kada za afya kwa maelezo ya swali la msingi. Je, Serikali ina mkakati gani na ajira ya kada za afya ili kupunguza tatizo
hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ongezeko la asilimia 9.7 ni dogo sana ukilinganisha na tatizo la huduma ya afya hususan dawa na vifaa tiba katika nchi yetu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kukaa chini na kwenda katika Halmashauri zote nchini kufanya tafiti ili waweze kuleta mpango mkakati wa kuondoa tatizo la
upungufu wa dawa na vifaa tiba katika nchi yetu?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Hivi sasa Serikali inatumia gharama kubwa sana katika kuanzisha mabwawa mapya kupitia maji ya mvua; lakini rasilimali hizi za asili nyingi zimeelekea kutoweka, kwa hiyo, nilidhani Serikali pia itakuwa na mkakati.
Mheshimiwa Spika, hivyo nina maswali madogo mawili, la kwanza, fedha zilizotajwa katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017 hazikuweza kupatikana hadi sasa na hivi sasa tunaingia Bajeti ya Mwaka 2017/2018, lakini hali inayotishia ziwa hili inaonesha hivi punde litakauka; je, Serikali itatoa lini fedha milioni mia moja kupitia Mradi wa DADP’s ambayo imekusudiwa kwa nia njema katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amewajibu Watanzania pamoja na mimi na wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutuma timu ya wataalam kupitia maziwa yote ya asili katika nchi yetu ili iweze kutoa ushauri wa kitaalam na kuchukua hatua za kunusuru maziwa hayo kwa haraka na wataalam hao watakwenda lini?
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mji mkongwe wa Mbulu ni mji wa zamani. Umekumbwa na tatizo kubwa la maji hivi karibuni, lakini tatizo hili la miradi ya maji kusuasua katika utekelezaji limeikumba Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Serikali mwaka huu ilitenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa maji Mbulu Mjini. Mradi huu hadi sasa utaratibu umeshafanyika wa tenda kwa kupitia Mamlaka ya Maji Mji wa Babati, lakini hakuna hatua iliyofikiwa umebaki mwezi mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika Mheshimiwa Naibu Waziri mwenye dhamana, alifika Mbulu akafanya ziara. Mradi wa Maji ulioko katika kijiji cha Moringa Daudi una takribani miaka minne, hadi sasa mradi huo umeshindikana kukamilika na mkandarasi alimdanganya Mheshimiwa Naibu Waziri alipotembelea site.
Je, ni hatua gani ichukuliwe kwa mkandarasi wa namna hii ambaye alimdanganya Mheshimiwa Waziri hadi leo ni miezi minne hajakamilisha mradi huo, ambapo aliahidi mbele ya Mheshimiwa Naibu Waziri wetu? (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, hivi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu katika majimbo yote mawili tulikuwa na mradi wa maji takribani zaidi ya miaka minne na hao wamekosesha Halmashauri zetu kupata mpya za miradi ya maji. Ni kwa nini sasa Serikali isitoe maelekezo ya Waraka kwa Halmashauri za Wilaya kwa jinsi ambavyo watajiondoa katika mikataba ya awali ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora na kwa wakati?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na riba kubwa inayotozwa kwa wafanyabiashara wadogo lakini pia wafanyabiashara wadogo wanachangamoto kubwa ya tozo za ada na ushuru katika makundi haya ya bodaboda, mama ntilie na wauza mbogamboga. Na kwa kuwa Serikali yetu kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliahidi Itazitazama upya tozo hizi ambazo ni kikwazo kwa wafanyabiashara wadogo, sasa ni lini Serikali yetu itatazama upya tozo hizi ili wafanyabiashara wadogo waweze kupunguziwa mzigo mkubwa katika uendeshaji wa biashara yao?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wetu, hali hii ya makorongo na jiografia inayobadilika kutokana na tabianchi imesababisha jamii yetu hasa akinamama kukosa huduma za afya, watoto na wanafunzi kukosa masomo na kwa kuwa ni tatizo la nchi nzima, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuona ni namna gani hata madaraja ya dharura kama yale ya chuma kuwekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sasa hivi tunabadilika kutoka Watendaji wa Halmashauri na barabara zote zinazohudumiwa na Halmashauri zinapelekwa kwa Wakala wa Barabara za Vijijini. Je, ni kwa namna gani Serikali itatazama suala hili kutokana na kwamba fedha zinazotengwa ni kidogo sana kulingana na fedha za Mfuko wa Barabara kwa zile barabara zilizokuwa zinahudumiwa na halmashauri za wilaya katika maeneo ya vijijini ili fedha zitakazotengwa kwa dharura ziweze kusaidia tatizo hili na jamii ipate huduma stahiki na kwa wakati kuliko sasa ambavyo inapoteza maisha katika hali ya dharura na mvua nyakati za masika? Ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa Wilaya kongwe hapa nchini. Wilaya hiyo kongwe huko mbele ilikuwa na kiwanda cha kutengeneza vigae vya kuezeka maghorofa na pia kulikuwa na kiwanda kilichokuwa kinamilikiwa cha kutengeneza chokaa na gypsum powder. Hivi sasa hivyo viwanda havifanyi kazi.
Je, ni lini Wizara itaenda Mbulu ili ikae na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Vijijini waweze kufufua viwanda hivi ambayo vilianzishwa na wenzetu huko awali?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii niseme kwamba kwanza Serikali haitutendei haki sisi Wabunge. Neno italipa fedha au kifuta machozi pindi hela itakapopatikana haliwafurahishi Watanzania kwa tukio lililotokea la Watanzania kupoteza maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kadhia hii kwa Jimbo la Mbulu Mjini ina changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa Askari Wanyamapori na pia ratiba isiyoonekana ya wenzetu wa TANAPA na jamii zinazopakana na mipaka ya hifadhi na makazi ya watu. Tukio hili la mwaka 2015 lilipoteza maisha ya wananchi saba, siyo watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine niishukuru Serikali kwa sababu, Mheshimiwa Waziri ameleta tu majibu ambayo hajayafanyia kazi kwa sababu, hadi sasa muda mchache uliopita, kama miezi miwili, mitatu, Serikali tayari imetoa fidia kwa wahanga hao wapatao wanne, lakini wale wengine hawakupatiwa hata fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu sasa, kwa kuwa tatizo hili linagusa maisha ya Watanzania, je, ni kiasi gani cha fidia au cha kifuta machozi kinatolewa kwa wale wote waliopoteza maisha yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kwa kuwa tatizo hili linavunja mahusiano kati ya wananchi na wenzetu wa TANAPA ama Serikali, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuandaa ratiba rasmi itakayowaunganisha wadau wa mpakani katika Tarafa yangu ya Daudi ili waweze kujadiliana matukio yanayotokea na hatimaye kudumisha uhusiano kati ya Shirika la TANAPA na wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini? (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Waziri wa Maji na Waziri wa TAMISEMI kwa kuteua Bodi ya Maji na pili kuwatuma wataalam kule Mbulu kwa ajili ya suala hili la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Mbulu na hasa Mji wa Mbulu, hali ya maji imekuwa mbaya kwa takribani sasa miezi sita. Katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tulitenga fedha shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya utafiti na usanifu wa maji katika Mji wa Mbulu. Je, ni lini mpango huu sasa Wizara itatusaidia ili tuweze kupata maji ya uhakika kuepukana na adha hii ya ukosefu wa maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Mjini limekuwa na migogoro ya ardhi hususani shule zetu za msingi na sekondari na kwa sasa karibu shule mbili ziko mahakamani kwa ajili ya kutetea ardhi zake.
Je, Serikali haiwezi kuchukua utaratibu sasa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote ya shule za msingi na sekondari nchini zinapata kupimwa ili ziweze kuepukana na adha hii ya migogoro ya ardhi kwa taasisi hizi za Serikali?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze Waziri kwa kuteuliwa kwake pamoja na Mawaziri wengine wote.
Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali ilikuwa na nia njema ya kuajiri watumishi 52,000; je, Serikali sasa itatekeleza mpango ule wakati gani ili vijana wetu waliopo mitaani waweze kupata nafasi ya ajira?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi mimi ni kwa namna gani Serikali itoe utaratibu wa jamii, Halmashauri na Serikali Kuu kuweza kuweka nguvu pamoja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu hivi sasa maboma yaliyo mengi katika Halmashauri zetu yamechukua miaka mingi ningeomba basi Mheshimiwa Waziri atume wataalamu kwa baadhi ya maeneo machache ili kunyambulisha ni gharama gani zitakazotumika katika ujenzi wa nyumba hizi za walimu na tuwe na lengo kwa kila Halmashauri kwa zile nyumba ambazo ziko katika lenta ili tuweze kukamilisha kuungana na wananchi. Nashukuru.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na hatua kubwa inayochukuliwa na Serikali yetu.
Je, kutokana na gharama kubwa inayotumika ya matengenezo ya kawaida katika barabara hii inayounganisha mikoa minne kwa kiwango cha changarawe na kwa kuwa katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri hakueleza mkataba huu unaisha lini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuharakisha kazi hii ya usanifu ili barabara hii ipate kutengenezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais aliahidi ahadi nyingi wakati wa kampeni kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za wananchi. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu aliahidi kilometa tano kwa barabara ambazo zinamilikiwa na Serikali za Mitaa wakati ule. Kwa kuwa sasa barabara zile zimehamia kwa TARURA, je, ni nani atakayetekeleza ile ahadi ya kilometa tano katika barabara zile kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa sasa haziko tena kwenye utaratibu wa kuzihudumia?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na changamoto nyingi zilizokuwa zinakabiri kundi hili la walimu, moja ya changamoto kubwa inayokabili kundi la walimu ni mazingira magumu ya kufanyia kazi. Na kwa kuwa hivi sasa Serikali yetu inatekeleza mpango kabambe wa vituo vya afya kwa nchi nzima, je ni kwa nini Serikali isione umuhimu sasa wa kushirikiana na jamii, Halmashauri na Serikali Kuu ili kuona ni namna gani kwa kila Halmashauri katika mwaka wa fedha tunajenga nyumba kadhaa za walimu hasa mazingira yale ya vijijini ili walimu waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naipongeza Serikali kwa hatua kubwa inayochukua ya kutekeleza miradi ya barabara nchini.
Swali langu dogo, katika utaratibu wa awali nilijibiwa hapa Bungeni kwamba barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Shinyanga iko katika hatua ya mwisho a kupatiwa fedha za usanifu kina.
Je, Serikali kwa mwaka huu wa fedha imetenga kiasi gani kwa ajili ya kufanya usanifu wa Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Shinyanga kwa kiwango cha lami?
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo la Mbulu Mjini mipaka yake kwa asilimia 50 inazungukwa na misitu ya asili na maji wanayotumia viumbe wakiwemo binadamu yanatoka katika misitu hiyo. Hivi sasa maji hayo yameanza kupungua ndani ya misitu. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam watakaofanya utafiti katika misitu inayozunguka Jimbo la Mbulu Mjini ili iweze kufanyia kazi taarifa yake ya utafiti kwa ajili ya kushauri jamii inayozunguka misitu hiyo? (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii ya madini kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wachimbaji wa Jimbo la Mbulu Mjini, ni kwamba wanakosa mitaji, lakini pia uchimbaji wao ni wa kubahatisha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia fursa za uwezeshaji, lakini pia na vifaa vya kubaini madini yako wapi na njia rahisi ya uchimbaji?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's