Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Flatei Gregory Massay

Supplementary Questions
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mbulu ni Wilaya kongwe, imeanza 1905, sawa na Nairobi. Pamoja na ahadi zilizotolewa kwa muda mrefu na Marais waliyotangulia. Je, kwa kuchelewa kutengeneza barabara hii, huoni kwamba ni kuwadanganya wananchi wa Mbulu na kuwakatisha tamaa?
Swali la pili, kwa kuwa barabara hii ya kwenda Hydom, ipo Hospitali kubwa ya Rufaa ya Hydom ambayo ni Hospitali ya Kanda; na sasa hivi daraja la Enagao limevunjika na wananchi hawezi kwenda kwenye Hospitali hiyo: Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kutopitika barabara hii kunaweza kuendelea kupoteza maisha ya watu na wasipate huduma katika hospitali hiyo? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa miradi hii haijakamilika na wananchi sasa hivi wanapata adha ya kutopata maji hasa katika miji niliyoisema na vijiji vyake, je, Serikali itahakikisha vipi leo hii itapeleka pesa kule ili wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na adha ya maji katika maeneo yetu, yuko mwananchi mmoja amechimba maji na kuyapata katika Mji wa Hydom. Je, kwa nini Serikali isiweze kupata maji katika maeneo yale na kuweka hela nyingi namna hii? Waziri yuko tayari kufuatana na mimi akaone jinsi ambavyo wananchi wanapata adha katika mji wa Hydom na maeneo mengine ya Mbulu Vijini? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ninaomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa uhalifu umeongezeka katika bonde la Yayeda Chini, hasa ubakaji na mengineyo mengi; gari lililosemwa hapo kwanza ni bovu au chakavu katika eneo hilo la polisi au kituo cha polisi, Hydom. Lakini hiyo haitoshi hapo, mvua ikinyesha kidogo bonde la Yayeda Chini halipitiki kutoka Haidom kwa gari lolote.
Je, Serikali haioni kwamba bado wananchi wa Yayeda Chini wana haki ya kulindwa wao na mali zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa wananchi wa Yayeda Chini wanahitaji kulindwa: Je, tukiwahamasisha, Serikali iko tayari ku- chip in ili kujenga kituo hicho pamoja na wananchi?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ahadi za Rais, zimekuwa zikitolewa na moja ya Mji wetu wa Haydom, Mbulu na Dongobesh tumeahidiwa kujengwa barabara ya lami kwa kilometa tano. Je, lini Serikali inatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa Mbulu walishapewa ahadi ya kujengewa uwanja na Olympic na sasa wale wameondoka na eneo hilo lipo mpaka sasa na wananchi wa Mbulu wamekubali kutoa eneo hilo. Je, Serikali haioni ndiyo sasa wakati wa kuja kuwekeza au kujenga kituo hicho Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wanariadha wazuri ambao wamevunja rekodi ya dunia mpaka leo na haijawahi kuvunjwa mfano Philbert Bai ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania, je, Serikali haioni sasa ndiyo muda muafaka wa kujenga kituo hicho Mbulu kwa sababu uwezo wa Mbulu na uoto wa asili na hali ya hewa inawaruhusu wanariadha kuweza kufanya mazoezi na kushinda Olympic?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri je, ni lini sasa Serikali itaanza kutoa mikopo hiyo?
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Manyara hasa Mbulu Vijijini wako tayari kabisa kwa elimu hiyo ya ujasiriamali, je, Mheshimiwa Waziri anaweza kusema anaweza kuanza na Mkoa huo kwa kuwa uko tayari?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana.
Kwa kuwa, ni makosa ya uchapaji nashukuru amekiri kuwa Kata hii ya Qurus ipo na kwamba Kijiji hiki cha Gongali ndiko ofisi ya TANESCO ilipo. Sasa
kuna Vijiji ambavyo amevitaja hapa katika swali la msingi ambavyo vinaitwa Gendaa na Bashay;
Je, ni lini vitapata umeme?
Pia, kwa kuwa Wilaya hii ya Karatu ni pacha kabisa na jimbo la Mbulu Vijijini; Je, Vijiji vya Mbulu Vijiji ambavyo vinafanana kabisa kwa majina haya ya Gendaa ambavyo viko Mbulu Vijijini na Bashay ambavyo viko Mbulu Vijijini na Vijiji vingine vya Endara Gadati na Vijiji na Haidereri, Kantananati, Bashay, Yaeda Ampa lini vitapatiwa umeme?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo hili la Same Mashariki linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kwa mahitaji. Same Mashariki wanalima kitu kinachoitwa tangawizi, Mbulu Vijijini tunalima vitunguu na tuna tatizo hili la soko. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia wananchi wa Mbulu Vijijini kwa zao hili la vitunguu swaumu maana yake ni maarufu sana pale Bashineti Mbulu ili kuhakikisha kwamba maisha haya yanakwenda vizuri?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia muda wa kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema amefika mikoa hii 23, kwanza nimshukuru sana kwa kuweka plan ya kujenga barabara ya Mbulu - Karatu, Mbulu - Haydom - Singida kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kuanzia na upembuzi yakinifu? Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa umeme umefika Dongobesh miaka 11 iliyopita na haujawahi kwenda kijiji hata kimoja na pia miaka ya tisini umefika Haydom. Je, Serikali iko tayari sasa kusogeza umeme huo kutoka Kata hizo ambazo nimezisema kuelekea kwenye Kata ambazo amezitaja? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa tuna miradi ambayo ni ya maji, na inahitaji umeme na kwenye REA phase two, hatujawahi kupata mradi huo: Je, Serikali iko tayari kukubali sasa kuanza na Vijiji hivi vya Kata ya Hayderer, Getanyamba, Dinamu, Maretadu, Masieda, Laba na Dinamu?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Hospitali ya Haydom inahudumia Mikoa ambayo umeitaja ya Singida, Simiyu, Arusha, Dodoma na Mara; na nashukuru Serikali kwa kutoa fedha na kupanga kiwango hiki cha shilingi milioni 570.
Je, kwa kuwa Serikali sasa imesema haya na hela iliyopelekwa ni kidogo, haioni sasa ni muda wa kuongeza ruzuku hii ili hospitali hii ikaweza kutoa huduma nzuri kwa watu wanaozunguka?
Swali la pili, kwa kuwa tumeleta maombi ya hospitali hii kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya Kikanda na kwa kuwa Wabunge wanaozunguka hospitali hii na Mikoa niliyoitaja tumeomba namna hiyo.
Je, ni lini sasa Serikali itajibu maombi haya ya kuipandisha Hospitali ya Haydom kuwa Hospitali ya Kanda?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imefanya feasibility study (upembuzi yakinifu) kwenye malambo mengi na kwa kuwa swali la msingi la Bunda linafanana na Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini, je, Serikali ina mpango gani kuyajenga malambo hayo?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa majibu mazuri sana, kwanza nampongeza. Pili kwa kuwa kundi la walemavu limekuwa likisahaulika sana hasa katika suala hili la mikopo, ukizingatia wapo vijana wa kike na wa kiume, lakini je, kwenye mpango huu wa milioni 500, kundi la walemavu limekuwa considered namna gani. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kunithibitishia hilo?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Mheshimiwa Profesa Maji Marefu la Korogwe Vijijini ni pacha kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kutokana na hali ya kukosa mawasiliano. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano kwenye Kata ya Ari, Tumati, Mung’ahai, Ng’orati, Masieda, Endagi, Chani kule Mbulu Vijijini?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Morogoro Mjini linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini juu ya tatizo hili la ukosefu wa maji. Kwa kuwa Waziri alishaniahidi kwamba tukipeleka certificate atawasaidia wakandarasi kuwalipa fedha waendelee na mradi. Je, ni lini sasa watapatiwa fedha, miradi ya Mbulu iliyopo Haidom na Dongobeshi ili wakandarasi waweze kumalizia na wananchi wapate maji? Ahsante
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Mpwapwa linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kwa ukosefu wa maji kwa eneo kubwa mno, je, ni lini Serikali itakuwa tayari kuja kuviangalia hivi vijiji na kata za Labay, Bisigeta, Maretadu, Endamilay, Endahagichan, Bashnet na Dinamu, ili kuzipatia visima virefu na wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kupata maji?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri amefika katika hospitali ya Hydom, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kwamba hospitali hii imepandishwa hadhi miaka sita toka 2010 hadi leo ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na haijapata hata siku moja ile haki ya kibajeti ya hospitali ya Mkoa. Je, sasa ni lini hospitali hii itatengewa bajeti ili ifanane na hospitali zote za Rufaa za Mikoa ya Tanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa kwenye majibu ya msingi amesema hospitali hii ina tatizo la miundombinu na watumishi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuijengea uwezo na kuipatia watumishi ili hospitali ya Haydom iweze kutoa huduma kwa sababu na yeye amekiri kwamba inafikika na maeneo ya jirani na mikoa hii?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa hali ya barabara za Lulindi ni nafuu kuliko Mbulu Vijijini; na kuna barabara imeahidiwa ya Karatu - Mbulu; Mbulu – Hydom; Hydom – Sibiti na Mheshimiwa Rais, kwa kujengwa kwa lami; na majibu ya MheshimiwaWaziri yalikuwa yanasema mwanzoni uchambuzi yakinifu umeshaanza. Je, barabara hii inajengwa lini sasa ili wananchi wa Mbulu na maeneo mengine wapate nafuu ya kiuchumi na kupita hasa kuelekea kwenye Hospitali ya Hydom?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa sasa wanafunzi wa vyuo vikuu wamekuwa wengi ukizingatia Chuo hiki cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kimeanza kujaa. Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha vyuo vidogo vya diploma kama vile vya Monduli CDTI ili kuwa university kuweza kuwa-accommodate vijana waweze kusoma kwa wingi maana elimu inayotolewa na vyuo hivi ni nzuri sana kwa ajili ya Taifa letu?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu. Mbulu Vijijini tuna tatizo linalofanana na Ngara.
Mheshimiwa Spika, tuna Bwawa la Dongobesh ambalo limejengwa zaidi ya shilingi bilioni mbili; na kwa kuwa limekaribia kukamilika na Naibu Waziri ameshafika; kilichobaki ni njia tu ya maji ya kwenda kuwafikia watumiaji. Je, Mheshimiwa Waziri atuambie lini anapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia tu hilo bwawa ambalo kimsingi limekamilika bado tu njia ya kwenda kupeleka maji kwa watumiaji?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Daraja la Magala na barabara yetu ya Karatu - Mbulu - Haydom - Sibiti Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba itaanza upembuzi yakinifu, sasa swali, je, barabara hii iko kwenye hatua gani, upembuzi yakinifu na lini anafikiri kwamba itaanza ujenzi?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali
mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeleta maombi haya muda mrefu; na vikao hivi vimekaa muda mrefu; na tuna miji miwili ya Dongobesh na Haydom; na kwa kuwa muda umepita, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa
kutuma wataalamu wake kutoka TAMISEMI ili kushirikiana na wataalamu walioko Wilayani kusaidia vigezo hivi kutimia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari, je, ni lini sasa atawatuma wataalamu hawa ili
kiu ya wananchi wa Mbulu Vijijini itimie?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Mbulu Vijijini katika REA Awamu ya Pili tumepata vijiji viwili tu na sasa Mbulu Vijijini hatuna sub-station tunapata umeme kutoka Katesh na Mheshimiwa Waziri anafahamu, amekuja, tunapata kutoka Babati na Mbulu Mjini. Je, mtatuhakikishiaje sasa katika awamu hii REA itafika maeneo yote ya kata na hasa katika vijiji vya mwanzo vya Mbulu Vijijini?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nimpe taarifa kwamba katika Kata ya Hayderer kuna mnara wa Airtel umeanzishwa, una miaka miwili, haujamalizika kabisa, uko kwenye foundation. Sasa kwa kuwa Kata za Yaeda Ampa na Tumati zinakaribiana. Je, Wizara iko tayari sasa kujenga mnara katikati ya kata hizi ili angalau katika mnara huu uliotangazwa tender, kata hizi mbili zikapata mawasiliano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa maeneo mengi mitandao haifiki, maeneo ya Endagichan, Endamasak, Enargatag, Runguamono, Munguhai, Gembak na Gidamba. Serikali sasa ituambie, ina mpango gani tena wa kuingiza vijiji hivi na kata hizi ili angalau basi Jimbo langu lipate mawasiliano? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alifika Jimboni kwangu na amekiona Kituo cha Dongobesh na tukaleta ombi la kujengewa theater, je, Mheshimiwa lini sasa theater ile inajengwa ili wananchi wangu wapate matibabu hayo ya upasuaji? Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa pembejeo nyingi mwaka huu mawakala wengi walipewa muda wa kupeleka kwa wakulima na hazikufika kwa wakulima mwaka huu, mawakala wameshapewa na Kamati ile ya pembejeo za Wilaya na sasa pembejeo hazijafika.
Je, Serikali inatuambia nini kwa pembejeo hizi ambazo hazijafika wakulima bado wanasubiri na msimu umeshapita?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, Kwa kuwa, Serengeti Boys vijana wale walionesha umahiri mkubwa wa kiwango kile cha soka kinachotakiwa na wakatutangaza sana kule nje na sasa wamerudi. Je, Wizara ina mpango gani sasa kuwaendeleza vijana hawa ili kutokuwa na ile kazi ya zimamoto, wachezaji hawa wakaendelea kufanya vizuri wakati mwingine wa ligi za kimataifa. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi wa Maji wa Haydom unafanana kabisa na jinsi ambavyo matatizo ya Ngara yalivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi huu wa Haydom umekaa miaka saba, mkandarasi amechukua pesa na muda wa kukabidhi mradi umeshafika. Mkurugenzi kafanya jitihada mpaka leo mradi haujaisha.
Je, Mheshimiwa Waziri atanisaidiaje sasa kuisaidia Halmashauri yangu ule mradi wa Haydom ukaisha na wananchi wakapata maji?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali ilitoa ahadi ya kujenga Kituo cha Polisi katika bonde la Yaeda Chini na muda umepita sasa na wananchi wanaibiwa mifugo na kutokea mauaji katika lile bonde.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kutengeneza Kituo cha Polisi ya Yaeda Chini? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Mheshimiwa Rais aliahidi maeneo mengi hasa wakati wa kampeni katika Jimbo la Mbulu Vijijini aliahidi ujenzi wa barabara kilometa tano katika Mji wa Haydom na Dongobesh kilometa mbili. Je, ni lini sasa ahadi hizi za Mheshimiwa Rais zitatekelezwa?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kutaja vizuri vijiji hivi, nina swali la nyongeza. Mwaka jana bajeti yetu ilikuwa shilingi bilioni 2.4 ikarudi na sasa hivi Mheshimiwa Waziri amesema tumetengewa shilingi bilioni, tatizo lililoko pale ni kwamba wakandarasi wanaojenga miradi hiyo baadhi yao hawako site ndiyo maana bajeti mwaka jana imerudi na kadri inavyoendelea hivi bajeti ya mwaka huu kuna wasiwasi wa kurudi. Je, atanisaidiaje kusukuma sasa bajeti hii iishe kwa kuwa wakandarasi wengi hawako site?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mradi wa Haydom mpaka sasa una tatizo la kwisha pamoja miradi hii ambayo ameitaja mwenyewe ya Arri-Harsha, Barshai, Quantananat na mradi wa Mongahay kuja Tumati. Je, atakuja lini kule na kuwaahidi wananchi wangu ili aweze kuona jinsi ambavyo wakandarasi wanawadanganya kutomaliza miradi na pesa za maendeleo kurudi?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa majibu mazuri ya kueleweka katika maswali haya na katika majibu yake ya msingi. Je, yupo tayari sasa kuandika maelekezo haya yaende kwenye Halmashauri yetu ili hizi Community Centers zifanye kazi yake iliyokusudiwa? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuandaa mpango huu wa kunusuru kaya maskini. Katika jimbo langu Mheshimiwa Waziri alishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu anajua Bonde la Yaeda Chini kwa Hadzabe kule wana tatizo hili la umaskini. Je, ataweza kutuongezea angalau Vijiji vile Mungwamono, Eshkeshi na Endagechani tukapata zaidi msaada huu wa TASAF?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hii ya Haydom kwenye swali la msingi iko katika jimbo langu na inaihudumia Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Singida na Shinyanga. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alishafika na kutuahidi kwamba atatupatia watumishi zaidi na Mheshimiwa Ummy amefika kwenye hospitali hiyo. Je, lini sasa Serikali inatimiza ile ahadi yake ya kutupatia watumishi katika hospitali hii ambayo inahudumia mikoa mingi niliyoisema?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kueleza masikitiko yangu kuhusiana na mradi huu, mwaka 2014 alikuja Katibu Mkuu wa Chama akadanganywa kuhusu mradi huu. Akaja Waziri Kamwelwe Januari mwaka jana akadanganywa kuhusu mradi huu, mimi nimekuja Ofisi na hao uliowasema mwaka jana Desemba mradi ulikuwa uishe tukadanganywa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitaji muda gani na mara ngapi kuja hapa kuuliza maswali haya na uwongo wa kudanganywa namna hii, wananchi kule umetaja 17,000 hawana maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa miradi ya maji katika Jimbo la Mbulu Vijijini iko mingi, nayo hakuna muda ambao umetajwa wa kumalizika na mikataba imeisha, na mimi kule sina fundi kabisa au Mhandisi wa Maji ndani ya Halmashauri yangu.
Je, unanisaidia pamoja na kwamba tutakaa baadae kuhusu ya watumishi katika Wizara hii au katika sekta ya maji?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wanafanya kazi nzuri na imekuwa ikiwategemea kwenye kazi zote na hata kualika mikutano yote ya Wabunge, Madiwani na kufanya kazi kubwa, asilimia 20 ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja katika majibu yake ya msingi haijawahi kupelekwa hata siku moja.
Je, kwa nini sasa Serikali isilete namna nzuri ya kuwalipa moja kwa moja hawa Wenyeviti kwa sababu, ni viongozi ili pasiwe na utaratibu huu wa asilimia ambayo haijawahi kupelekwa tangu wameanza kazi hizi mpaka sasa? (Makofi)
Swali la pili, kwenye swali langu la msingi nilieleza habari ya Madiwani. Madiwani kimsingi wanapata posho ndogo ya shilingi 300,000 na kitu kama sikosei. Je, ni lini sasa mnaongeza posho hizi ili walau basi wafanye kazi nzuri katika chini ya Halmashauri zetu huko Wilayani? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la msingi linahusiana na usalama wa wasafiri, na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja maeneo ya Mbulu na kwa kuwa ile barabara ya lami ya kilometa tano ya Hydom na Dongobesh bado. Je, Mheshimiwa Waziri lini sasa atakuja Hydom kuangalia barabara ile ambayo haina usalama kwa wasafiri? Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa kutokana na vyeti feki vimeondoa kabisa watumishi wa afya katika zahanati zetu. Je, ni lini hasa hawa watumishi wataenda kuajiriwa yaani wanayo time frame kwa sababu sasa hivi zahanati zina shida katika huduma hii ya afya? Ahsante sana. (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's