Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Aida Joseph Khenani

Supplementary Questions
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini ni aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Majibu hayo ni ya Arumeru na siyo ya Mkoa wa Rukwa. Halafu mnajiita Serikali ya kazi tu, hapa! Swali hili sijaleta jana, lakini kwa sababu madai ya walimu yako nchi nzima, nitauliza maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa madeni kwa wakati walimu ambao wamekuwa wakilia kila siku na ni malalamiko ya kila siku!
Swali la pili, mpaka sasa walimu wanadai fedha walizosahihisha mitihani ya mwaka 2015 ya kidato cha nne, ni lini Serikali itawalipa walimu hawa na kuwatendea haki kama wafanyakazi wengine wa nchi hii?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa uwiano kati ya walimu na wafunzi limekuwa tatizo sugu, katika shule zetu hasa kwamadarasa ya awali hususani Mkoa wa Rukwa, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kukamilisha au kuweka uwiano sana ili kuweka ufanisi wa ufundishaji na uelewa wa watoto wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa walimu hawa walipokuwa wakiwafundisha watoto walikuwa wanatumia mikakati mbalimbali ikiwepo nyimbo, michezo pamoja na kuwapatia uji ili wapende elimu. Toka Serikali imetangaza elimu bure mpaka sasa imetoa kiasi gani kuweza kukidhi mambo hayo ili watotowaendele kupenda shule? (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa mradi wa maji unaoendelea Manispaa ya Sumbawanga umechukua muda mrefu na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga mpaka sasa hawajui huo mradi utaisha lini: Je, Serikali inawaambiaje wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga ikiwepo wanawake ambao wanapata athari mpaka sasa na wengine kupata vifo kwa ajili ya kufuata maji kwenye umbali mrefu?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa,
tathmini imefanyika toka mwaka 2009 mpaka leo hakuna kitu kinachoendelea.
Wananchi wa Sumbawanga wanataka majibu ya uhakika ni lini watalipwa pesa
zao, kwa sababu ahadi zimekuwa za kila siku?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa bidhaa nyingi zinazoonekana nchini kuwa ni feki kwa asilimia kubwa zinatoka nchi ya China na kupitia Bandari ya Dar es Salaam; mpaka sasa Serikali imewachukulia hatua gani TBS, FCC, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyosababisha bidhaa hizi kupita na baadaye kuwaathiri wananchi wasiojua chochote kinachoendelea? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano alitangaza kuzima simu ambazo zilionekana ni fake, wakati zinaingia nchini zililipa kodi na zikaonekana ni sahihi mpaka kuingizwa kwenye maduka na baadaye wananchi wakazinunua. Lakini baadae Serikali hii hii ya Chama cha Mapinduzi ikaona hazifai na zikazimwa, badala yake wananchi ndio wakapata gharama ya kuingia tena kununua simu nyingine. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia au kuwalipa gharama wananchi kwa kuwa uzembe huu ulifanyika na Serikali yenyewe ya Chama cha Mapinduzi?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa utaratibu wa Serikali wa kuajiri unaeleweka kwa kufuata taratibu mbalimbali na wapo vijana ambao wana sifa hizo, elimu, uzoefu na vitu vingine. Ni lini Serikali itawapa ajira vijana wa Kitanzania ili kuwaepusha kujiingiza kwenye masuala ya ukabaji, wizi na mambo mengine?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Pamoja na agizo la Serikali kwenye Halmashauri kuagiza kutenga asilimia kumi kwa vijana na wanawake, kumekuwa na utaratibu wa Halmashauri kugawa pesa hizi kipindi cha Mwenge. Kwa sababu Halmashauri nyingine wanawake wanapata changamoto sana kipindi cha kilimo, Serikali haioni ni hekima au busara kutoa pesa hizi kipindi cha msimu wa kilimo?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa, ni Wizara hiyohiyo ya Uchukuzi, ingawa niliomba swali namba 70.
Kwa kuwa mawasiliano ni haki ya kila Mtanzania, lakini
toka nchi imepata uhuru kuna maeneoa ambayo hayajapata mawasiliano, ikiweko kata ya Kala na Ninde. Ni lini Serikali itatimiza wajibu wake wa kupeleka mawasiliano katika hizo kata, ikizingatia ziko pembezoni? (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia nashukuru kwa ufafanuzi alioutoa Naibu Waziri ambao utaleta mwanga kidogo kwa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wameamua sasa kufuata utaratibu ili wapate hati, shida yao siyo kumiliki tu hati, ziwasaidie kwenye taasisi pia za kifedha, lakini hati zimekuwa zinachelewa sana. Hamuoni kwamba kuendelea kuchelewa kwa hati hizo mnawanyima fursa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa masuala ya maendeleo kwa sababu wanakosa mambo muhimu hasa katika taasisi za fedha?
Swali la pili, Maafisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga wanajitahidi sana kwa jitihada zao kuwafuata wananchi kwenda kupima maeneo, lakini wanakabiliana na changamoto za usafiri, pamoja na vitendea kazi vingine kwenda kupima ardhi.
Je, Serikali hamuoni kuna umuhimu zaidi wa kuwapa kipaumbele ili wale wakafanye kazi kwa mujibu wa sheria ili wasipate malalamiko kama yanayoendelea kwa sasa?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa ni zaidi ya miaka 53 toka nchi imepata uhuru sehemu yenye hadhi ya mkoa kama Mkoa wa Rukwa hatuna Hospitali ya Wilaya hata moja. Serikali haioni umuhimu sasa wa kuondoa aibu hiyo angalau hata wilaya mbili zipate hospitali ya wilaya?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mkoa wa Rukwa tunalima sana mazao ya chakula na sasa ni msimu wa mavuno… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkoa wa Rukwa tunalima sana mazao ya chakula na sasa ni msimu wa mavuno, lakini wananchi wa Mkoa wa Rukwa mpaka sasa hawajapata soko la uhakika la kuuza mazao yao wala kiwanda hakipo. Ni lini kiwanda kikubwa kitajengwa Mkoa wa Rukwa ili kiwanufaishe wakulima hao?
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Serikali ya Awamu ya Tano imepunguza wafanyakazi kwenye kada mbalimbali kwa kigezo cha kutokuwa na sifa, ni lini sasa Serikali itatoa ajira kwa kuwapa kipaumbele vijana wa nchi hii ambao kwa sasa ni wengi wamerundikana mtaani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Kwa kuwa mikopo hiyo anayoizungumza Waziri, Halmashauri inatenga asilimia tano ambayo kwa sasa haiwezi kukidhi haja kulingana na idadai au wimbi kubwa la vijana waliopo mtaani. Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuwa na mpango mkakati wa kuwapa mafunzo maalum au kuanzisha vyuo kwenye mikoa yote ili kuwapa ufanisi vijana waweze kujiajiri? (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata pembejeo za kutosha na wanapata masoko ya uhakika, jambo ambalo Serikali hii imeshindwa kutimiza wajibu wake.
Swali langu, Serikali ina mkakati gani wa kuandaa masoko ya uhakika badala ya taabu ambazo wanazipata wananchi wetu na kupata umaskini unaosababishwa na Serikali? (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha migogoro hii pia kinatokana na hifadhi ambazo zinatolewa bila utaratibu, tunajua mpaka eneo litangazwe kuwa hifadhi kuna utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa. Hivi karibuni kumekuwa na utaratibu wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kushirikiana na halmashauri kuwaondoa wananchi na kusema maeneo fulani ni hifadhi na wakijua kabisa maeneo hayo hayajatangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Nini tamko la Serikali juu ya Halmashauri ambazo zinaondoa wananchi hao na ikiangalia kabisa hawajafuata taratibu na sheria za nchi yetu? (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu, anasema ni askari 105 ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Katika matukio ambayo yametokea ambayo hayana shaka, ni matukio ya wazi, ni matukio ambayo yametokea kwa Mheshimiwa Nape Nnauye ya kutolea bastola hadharani lakini pia Mdude Nyangali ambaye amepigwa mpaka sasa hawezi kutembea vizuri, Husna Amri ni kiongozi wetu wa CHADEMA ambaye amefanyiwa hicho kitendo mpaka sasa hivi tuko hospitali. Je, katika hao askari ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu ni miongoni mwa hao 105?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna askari ambao umekiri kwamba wamechukuliwa hatua za kinidhamu na hawa watu wanaoteswa wengine hawawezi tena kuendelea na shughuli zozote, wanapata fidia gani kulingana na madhara ambayo wamekuwa wameyapata? (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Na mimi niseme tu kwamba mimi ni miongoni mwa Wenyeviti wa Tanzania wa Serikali ya Mtaa wa Vodacom Kata ya Chanji kwa hiyo, ninaloliuliza ninalijua na changamoto zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya Serikali inayotengwa watekelezaji wa kwanza ni Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, kauli hii ya kwamba wataanza kulipwa posho sio mara ya kwanza ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba time frame ni lini sheria italetwa hapa ili Wenyeviti waanze kulipwa posho kwa sababu sio hisani wanafanya kazi kubwa? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's