Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Esther Nicholus Matiko

Supplementary Questions
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwenye swali langu la msingi nimeelezea dhahiri kwamba hospitali ya Mji wa Tarime inatoa huduma kwa Wilaya nzima ya Tarime na baadhi ya wananchi wa Serengeti na Wilaya ya Rorya. Serikali imekuwa ikileta fedha za OC na bajeti ya dawa, kwa kufuata population ya Mji wa Tarime ambayo ni watu 78,000. Ppia imekuwa ikileta, fedha la kapu la pamoja kwa maana ya basket fund, milioni 106 tu ambayo haikidhi haja na zamani tulikuwa tukipokea zaidi ya milioni 500 bado huduma za afya zilikuwa siyo dhahiri.
Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwa nini Serikali sasa, isiweze kuleta fedha za OC na za basket fund kwa kufuata population walau ya Tarime Rorya na siyo ya Mji wa Tarime, ukizingatia kwamba tunatoa huduma kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wanaopata huduma ya afya kwenye hospitali ya Mji wa Tarime, wamekuwa wakitozwa sh. 6,000 lakini wakifika ndani hawapati madawa, hawapati huduma zinazostahili, ni kwa nini sasa Serikali kwa maana katika Hospitali ya Mji wa Tarime tayari tuna jengo ambalo liko tayari, kuweza kufungua duka la dawa kwa maana ya MSD ni kwa nini sasa Serikali isiweze kuja na kufungua hilo duka pale kwenye hospitali ya Mji wa Tarime ili wananchi waweze kupata huduma ya madawa wanavyoenda kutibiwa pale kuliko kuhangaika tena wanatoa sh. 6,000 halafu akitoka nje anaambiwa hamna dawa? Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa masikitiko makubwa sana nimefedheheshwa na majibu ya Wizara kwa sababu amenijibu kuhusiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mimi nimeuliza kuhusiana na Halmashauri ya Mji wa Tarime ambapo Mnada wa Magena upo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu, kwa kuwa katika majibu yao ambayo hayajakidhi wametamka dhahiri kwamba walifunga mnada huu kwa sababu za wizi wa ng’ombe na usalama. Kwa kuwa Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi imeanzisha Kanda Maalum ya Tarime - Rorya ambapo hivi sasa usalama umeimarika ingawa bado wanaongelea suala la wizi. Vilevile wameainisha kwenye majibu yao kwamba 1996 tu waliweza kupata Sh.260,000,000 na sasa hivi 2015 wanapata Sh.212,000,000, hawaoni kuwa Serikali inapoteza mapato mengi sana kwa kutokuanzisha ule mnada ambao ulikuwa umeshajengwa ambapo kwa sasa hivi unaweza kupata zaidi ya Sh.1,000,000,000? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni dhahiri kabisa na hata kwenye majibu yao wamesema Mnada wa Mtana, Kewenja, Nyamwaga na Chemakolele ipo katika Halmashauri ya Wilaya na ni dhahiri kabisa pia kwamba huu mnada ulihamishwa kwa sababu za kisiasa kwa sababu huwezi ukasema Kirumi ipo mpakani na Kenya. Napenda kujua sasa ni lini Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itaacha siasa iweze kufanya mambo ya kimaendeleo na Mnada wa Magena ufunguliwe ili wananchi wa Tarime wafaidike? ((Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kweli majibu yaliyopatikana leo, ni dhahiri kabisa hata Serikali haijui mipaka ya Kata. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwa kinywa kwamba wanatwaa ardhi kwa kufuata Sheria ya mwaka 1999 na kwa kuwa JWTZ hawakufuata sheria, mwanzoni waliomba hifadhi ya miezi mitatu katika Kata ya Nkende, walivyopewa wakaamua kuhodhi na Kata ya Nyamisangura na Nkende na Nyamisangura, siyo eneo la Nyandoto. Kikosi cha Jeshi kinatakiwa kukaa Kata ya Nyandoto na siyo Nyamisangura na Nkende.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu hawakufuata Sheria ya mwaka 1999, kama alivyotamka mwenyewe, haoni sasa kwamba ni dhahiri wananchi hawa wanatakiwa kuhodhi maeneo yao kama mlivyoyateka mwaka 2008 mpaka sasa hivi, mwaache waendeleze shughuli zao za kiuchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Waziri anasema kwamba wanaenda kukamilisha utathmini, ifahamike kwamba waliwazuia wananchi hawa kufanya shughuli za maendeleo kuanzia mwaka 2008, hawafanyi shughuli zozote za maendeleo. Sasa hiyo tathmini ambayo Waziri anakiri kwamba anaenda kuikamilisha mwaka huu, napenda kujua na wananchi wa Tarime wajue kwamba mtazingatia hali halisi ya mwaka 2007, ambapo Wanajeshi hao waliwakataza wananchi wasifanye shughuli zozote za maendeleo; nyumba zimebomoka, vyoo vimebomoka, mashamba yameshakuwa chakavu sasa hivi ni ardhi tu; huo utathmini ambao mnaenda kuufanya sasa hivi, unazingatia vigezo vipi? Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba, posho za Madiwani kwa maana ya vikao na posho za Wenyeviti wa Mitaa, Vitongoji na Vijiji zinalipwa na Halmashauri na kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwamba wanatambua kuna Halmashauri zingine hazina uwezo, makusanyo ya ndani ni madogo kama ilivyo Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini sasa Serikali isione ni vema mathalani kwenye vikao vya Madiwani ambavyo tumeona vinatofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine, wengine wanalipwa 60,000, wengine 80,000 wengine 250,000 wengine 300,000, kwa nini wasi-standardize iwe kama tunavyolipwa posho Wabunge kwa Tanzania nzima na iweze kutenga fedha, isitegemee mapato ya Halmashauri ili Madiwani wanavyokaa vikao vyao waweze kulipwa fedha ambazo ni uniform kwa Tanzania nzima, vilevile kwa Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kuhusuiana na suala la Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji na Vijiji. Tumeshuhudia wananchi wakienda kupata huduma majumbani kwao. Serikali inajibu kwamba, inategemea mapato ya Halmashauri. Narudi pale pale tuna Halmashauri zingine mapato ni madogo sana na haiwezi kujenga Ofisi za Wenyeviti. Kwa mfano, kwangu Halmashauri ya Mji tuna Mitaa 81 Halmashauri ya Mji wa Tarime haiwezi ikajenga hizo ofisi. Kwa nini sasa Serikali isione umuhimu kuwapatia hawa Viongozi ofisi zao iwajengee, itenge fungu kutoka Serikalini ishuke chini kwenye Halmashauri zote nchini iweze kujengewa ofisi ili kuepuka adha ambayo inaweza kupelekea hata wengine kushawishika na kutoa na vitu vingine?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Matatizo yaliyopo kwenye Kituo cha Afya cha Chamwino ni sawa sawa na matatizo yaliyopo kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo inahudumia takribani wananchi zaidi ya 500,000, hawana kifaa cha ultra sound. Ningependa kujua sasa ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa dhati kabisa wa kuleta huduma hii ya kifaa cha ultra sound kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ili kuondoa hizi adha kwa wananchi?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa magereza mengi nchini ni kweli miundombinu ni michakavu sana; na kwa kuwa asilimia zaidi ya 75 mahabusu waliopo magereza ni wale ambao wana kesi za kudhaminika lakini wananyimwa dhamana. Swali langu linakuja kwamba Gereza la Tarime linachukua mahabusu na wafungwa kutoka Wilaya ya Rorya na unakuta ina msongamano mkubwa kutoka 209 mpaka 560 mpaka 600.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa Serikali ni lini itajenga gereza Rorya, kwa sababu ile ni Wilaya inajitegemea, ili kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa Tarime ambayo inaweza ikapelekea magonjwa mbalimbali na ukizingatia miundombinu ni mibovu sana? Lakini pia kwa haki za kibinadamu wanatoka kule Rorya kufuatilia kesi Tarime, kuja kuona mahabusu Tarime, kuja kuona wafungwa Tarime. Ni lini sasa mtajenga Gereza la Rorya kupunguza msongamano katika Gereza la Tarime? Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Askari Magereza wapo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa kuwa Askari Magereza na wenyewe wanajiendeleza, wanapata shahada, wanapata elimu ya juu zaidi, lakini mishahara yao imekuwa ikibaki kuwa ile ile ambayo haitofautiani na askari wa kawaida aliye na cheti cha form four. Ukiangalia Jeshi la Polisi mtu mwenye shahada anapata sh. 860,000 lakini pia anapata posho ya ujuzi asilimia 15, kwa Askari Magereza wanalipwa sh. 400,000 wakikatwa inabaki 335,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwalipa Askari Magereza kulingana na ujuzi wao maana imekuwa ikiwaahidi kwamba itawaongezea mshahara kulingana na ujuzi wao, lakini mpaka leo bado. Ni lini sasa itakwenda kuwalipa Askari Magereza kulingana na ujuzi wao ili kuwapa motisha kama askari wengine?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa tatizo la maji lililopo Jimbo la Mpwapwa linaonesha uhalisia wa ukosefu wa maji Tanzania nzima likiwepo Jimbo la Tarime Mjini, na kwa kuwa maji safi na salama ni muhimu kwa afya za binadamu; ni lini sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaona kuna umuhimu wa kuwapatia maji wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini maji safi na salama kwa kutekeleza bajeti ambayo tuliipitisha hapa, ambayo bado hamjaanza kuitekeleza mpaka sasa hivi, ili wananchi wa Tarime Mjini na Tanzania kwa ujumla waweze kupata maji safi na salama?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kiukweli majibu ya Mheshimiwa Waziri yapo kiujumla zaidi na inasikitisha kwa sababu tunapokuwa tunatoa maswali yetu tunatarajia mwende sehemu husika kujua uhalisia wa sehemu husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mahabusu waliopo Gereza la Tarime, zaidi ya asilimia 65 ni kesi au makosa ambayo yanatakiwa yapewe dhamana; na kwa kuwa kesi nyingi ni kesi za kisiasa za kubambikwa na nyingine ni kesi za watoto chini ya miaka 15; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alikuja Tarime na hakupata muda wa kuingia Gerezani, ningependa sasa leo mtuambie ni lini Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkurugenzi wa Mashtaka watakuja Tarime kuangalia hali halisi ya mahabusu walioko Gereza la Tarime ili waweze kuondoa zile kesi ambazo jana Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba nyingine ni za juice, ili Watanzania warudi uraiani na wafanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna msongamano mkubwa sana kwenye Gereza la Tarime, capacity yake ilikuwa ni watu 260 wakiwa wamezidi sana. Sasa hivi ni zaidi ya watu 600; na kwa kuwa ukitokea mlipuko wa magonjwa tutapoteza Watanzania wengi waliopo kwenye lile Gereza; na kwa kuwa gereza lile linahudumia Wilaya ya Rorya na Tarime: ni lini sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi mtajenga gereza katika Wilaya ya Rorya, mtajenga Mahakama ya Wilaya kule Rorya ili wale Watanzania wa Rorya waweze kushtakiwa kule na kuhudhuria kesi zao kule ili kuondoa msongamano ambao upo katika Gereza la Tarime?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, kiukweli nasikitika kwa majibu ya Waziri wa Katiba na Sheria kuhusiana na umuhimu wa kuwa na Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Rorya. Tangu Bunge la Kumi nakumbuka nikiwa Mbunge wa Viti Maalum nimekuwa nikiongelea suala zima la kupatikana kwa Mahakama ya Wilaya ya Rorya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kukiwa hakuna Mahakama Wilaya ya Rorya, Mahakama ya Wilaya ya Tarime inakuwa na kesi nyingi na ndiyo maana mwisho wa siku tunakuwa na mrundikano wa kesi ambazo hazifanyiwi uamuzi kwa muda muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Rorya tayari wana ardhi na kwa sababu tumekuwa tukiongea umuhimu kuwa na Mahakama ya Wilaya ya Rorya tangu Bunge la Kumi, ni vegezo vipi ambavyo vilitumika kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 wasipeleke Mahakama ya Wilaya Rorya wakaamua kupeleka sehemu nyingine Tanzania ikizingatiwa jiografia ya Wilaya Rorya ni kubwa, watu wanatoka mbali sana kuja Wilaya ya Tarime. Naomba kujua ni vigezo vipi vimetumika kwa Serikali isiweze kujenga Mahakama ya Wilaya ya Rorya mwaka huu wa fedha hadi waseme ni mwaka ujao wa fedha?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naitwa Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa kwamba ukosefu wa nyumba za walimu na kukaa mbali na shule unasababisha kutokuwa na kiwango kizuri cha ufundishaji kwenye shule zetu. Hivi karibuni tulisikia kauli ya Waziri Mkuu akitoa msisitizo kwamba walimu waishi kwenye shule ambazo wanafundisha. Kwa majibu ya Naibu Waziri ni dhahiri bado Serikali haijawa na mpango madhubuti wa kuhakikisha walimu wanakaa kwenye maeneo ambayo wanafundisha.
Ni nini mpango mkakati wa Serikali hasa kwa pale ambapo wananchi wamejenga maboma wanashindwa kuyamalizia ili watoto wetu waweze kupata elimu mbadala kwa Walimu kukaa maeneo ya shule. Napenda kupata mkakati ambao unatekelezeka siyo wa kuandikwa tu kwenye makaratasi, ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Tarime Mjini lina kata nane na kati ya kata nane, kata nne ziko pembezoni na hazina umeme kabisa na kata mbili zina umeme kwa asilimia chache. Ningependa kujua commitment ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini wanapata umeme kwa asilimia zaidi ya 90.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru. Kwa kweli niendelee kusikitika kwamba Serikali inashindwa kuona barabara ambazo zinaweza zikaongeza chachu ya ukuaji wa uchumi kwenye nchi yetu kupitia utalii.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua ni lini Barabara ya Tarime – Nata kwa maana ya kwenda Mugumu itakamilika kwa kiwango cha lami? Mheshimiwa Naibu Waziri anatueleza
kwamba upembuzi yakinifu unakamilika 2018, watalii wengi wanaotoka Kenya wanapita Tarime wanaenda Serengeti, tukiboresha ile barabara kwa kiwango cha lami tutakwenda kukuza uchumi wetu kwa sababu watalii wengi watapita
kwa sababu barabara inapitika. Ni lini sasa Serikali itajicommit, isiseme leo itamaliza upembuzi yakinifu 2018, ione kuna uhitaji wa haraka sana wa kujenga barabara ya Tarime – Mugumu na iweze kumalizika ndani ya mwaka mmoja kama ikiwezekana tuweze kukuza uchumi wa nchi yetu? (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nasikitika kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani leo hii inaita kwamba ni Wilaya ya Tarime/Rorya haijui kwamba ni Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya masikitiko yangu, nipende kumwambia Naibu Waziri kwamba tayari tuna miuondombinu kwa maana ya mtandao wa TRA pale, tayari wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamejenga hilo jengo na tuna rasilimali watu. Sasa nataka kujua ni lini sasa baada ya kutambua kwamba Tarime/Rorya ni Mkoa wa Kipolisi na hivyo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Kipolisi, ni lini mtakuja kufunga huo mtambo ili kupunguza adha ya wananchi kwenda kwenye Mkoa wa Polisi wa Mara kutafuta huduma? (Makofi)
Swali la pili ni kuhusiana na kujenga ofisi ya Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya ambao Mheshimiwa Waziri amesema ni mkoa mpya. Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya ni wa siku nyingi ukilinganisha na Katavi, Simiyu na Geita. Kwa mikakati yenu ya ndani ningependa kujua ni lini mtakuja kujenga jengo zuri lenye hadhi ya Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya ili kuondokana na kukaa kwenye magodauni ambayo wanakaa sasa hivi na kushusha hadhi ya Kipolisi Mkoa wa Tarime/Rorya?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Tarime miundombinu yake ni mibovu sana na haina hadhi ya kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Kwa bajeti ya mwaka jana 2016/2017, Serikali iliahidi hapa kwamba Vyuo vyote vya Wananchi vitapandishwa hadhi na kuwa VETA. Napenda kujua sasa ni lini Serikali itaenda kutimiza azma yake ya kupandisha Vyuo hivi vya Wananchi kuwa VETA kwa kuanzia na Chuo cha Wananchi cha Tarime? (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina Hospitali ambayo ni Hospitali ya Mji, lakini inahudumia Wilaya nzima, ningetaka kujua ni lini Serikali itajenga Hospitali kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati inasubiria kujenga, iipe ile hadhi kama Hospitali ya Wilaya na kuweza kuleta mahitaji kama inavyotakiwa kwa idadi wa watu wa Tarime nzima na siyo Halmashauri ya Mji tu?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, wakati Naibu Waziri anajibu alielezea ni jinsi gani moshi wa bangi unamuathiri si tu mtumiaji bali hata watu wa pembeni.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiona wakati Serikali inafanya operation ya kukata au kuzuia bangi, inavuna yale mabangi yaliyokwisha komaa, na wanaenda wanachoma zile bangi, sasa Naibu Waziri atueleze ni kwa kiasi gani Jeshi la Polisi wameweza kuathirika na ile bangi na je, hawaoni kwamba zile bangi zinawaathiri ndio maana wanatenda kinyume na wajibu wao wanavyowatakiwa kufanya?(Makofi/ Kicheko)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ametueleza kwamba waliondoa watumishi hewa 19,708. Ni dhahiri kwamba kuondolewa kwa wafanyakazi wenye vyeti fake kumeathiri zaidi maeneo ya elimu na afya. Napenda kujua statistically ni vipi Serikali, maana yake ametuambia wataajiri; mpaka sasa hivi Serikali imeajiri walimu wangapi na wafanyakazi wa sekta ya afya? Maana yake kuna zahanati nyingine hazina kabisa watumishi.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine unakuta shule zina walimu watatu tu, tunaweza kuona ni madhara gani watoto wetu watapata. Sasa kama walikuwa na hili zoezi la vyeti fake, walijiandaa vipi ku-replace hawa wafanyakazi kwenye sekta ya elimu na afya? Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni kweli kabisa kwamba wastaafu wanateseka sana na wengi wao wanapoteza maisha. Ni katika Bunge hili hili, Mheshimiwa Naibu Waziri aliliahidi Bunge kwamba wastaafu wote wanaodai malimbikizo baada ya marekebisho ya kima cha chini kutoka shilingi 50,000 kwenda shilingi 100,000 watalipwa fedha zao kwa maana arrears zote lakini ni takribani miaka miwili sasa wastaafu hawa hawajalipwa fedha zao sana sana ni wale ambao walikuwa kwenye PSPF na PPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningetaka kujua ni kwa nini Serikali haijaweza kuwalipa hawa wastaafu haya malimbikizo kama ambavyo Naibu Waziri uliahidi Bunge hili na je mnavyoenda kuwalipa…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kufuatia majibu ya Mheshimiwa Waziri, ni dhahiri kabisa imeonyesha ni jinsi gani miundombinu ya kujifunzia na kujifunza katika Halmashauri ya Mji wa Tarime hairidhishi na inapelekea matokeo mabaya kwa ufaulu wa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Tarime wameitikia sana wakishirikiana na wadau mbalimbali ikiwepo mimi mwenyewe Mbunge. Tumejenga madarasa mengi lakini mengi yamekaa bila kuezekwa na kwa kuwa kuna Shule ya Msingi Mtulu ambayo imejengwa na wananchi kwa kujitolea madarasa sita pamoja na ofisi lakini Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji amezuia ile shule wananchi wasiendelee kujenga kwa kile anachokiita kwamba ni mgogoro wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sasa kupitia Wizara hii ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais na Rais ana mamlaka ya kubadilisha matumizi ya ardhi, wawatie moyo wananchi wale waliojenga yale madarasa ili sasa waweze kuamuru ile shule iendelezwe ili kupunguza adha ya upungufu wa madarasa katika Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Halmashauri ya Mji kuna shule moja ambayo inatumiwa na shule tatu, Shule za Msingi Azimio, Mapinduzi na Sabasaba. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kipindi hicho akiwa Naibu Waziri alitembelea sisi kama Halmashauri ya Mji tunataka ile shule ijengwe ghorofa ili sasa walimu wasikae kwenye mti kama Ofisi, wanafunzi wasifundishiwe nje chini ya mti, wanafunzi wasirundikane 120 kwenye darasa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini sasa Serikali isiweze kutumia ile asilimia tano ambayo walisema Waziri anaweza akapeleka kwenye matumizi mbalimbali kama tulivyoona ilivyoenda Chato kwenye uwanja wa ndege. Kwa nini msijenge ghorofa katika shule ile kwenye zile asilimia tano ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 1.7 ili sasa kupunguza adha ya ukosefu wa madarasa katika Mji wa Tarime? (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mkoa wa Mara una shughuli nyingi sana ambazo zingeweza kuliongezea Taifa letu uchumi kwa maana ya utalii, tuna Ziwa Victoria lakini pia makumbusho ya Baba wa Taifa. Katika majibu yake Naibu Waziri ametueleza kwamba wamefanya usanifu pia kwenye uwanja wa ndege wa Musoma, ningependa kujua uwanja wa ndege wa Musoma na wenyewe upo kati ya viwanja vilivyopewa priority maana yake umetaja Tanga tu kama ndiyo umepewa kipaumbele na unaanza kukarabatiwa? Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ingawa kwa kweli majibu ya Waziri, Naibu Waziri yanakatisha tamaa maana tumekuwa tukisikia siku zote kadri fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa raia na mali zao ni muhimu sana katika nchi yetu. Kwenye Jimbo la Tarime Mjini katika Kata zote nane tuna kituo cha poilisi kwenye Kata ya Bomani tu, na Kata zingine ambazo za pembezoni wananchi wamejitolea kujenga vituo vya polisi. Tunataka kujua mkakati thabiti wa Serikali katika ku-support zile juhudi za wananchi hasa Kata ya Nyandoto, Kenyamanyoli, Nkende na Kitale ambazo ni mbali na mji, na kuna gari moja tu ambayo inafanya patrol.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mkakati wa Serikali maanake mnakusanya mapato mengi, muweze kuelekeza kwenye kumalizia vituo vya poilisi ili tuweze kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Sadifa Juma Khamis

Donge (CCM)

Contributions (1)

Profile

Hon. Makame Kassim Makame

Mwera (CCM)

Contributions (1)

Profile

Hon. Justin Joseph Monko

Singida Kaskazini (CCM)

Supplementary Questions / Answers (1 / 0)

Profile

View All MP's