Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Devotha Methew Minja

Supplementary Questions
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Kwa kuwa matatizo ya ukosefu wa huduma katika Hospitali za Mkoa wa Morogoro hayana tofauti na matatizo ya Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Morogoro una Hospitali ya Rufaa ambayo inatoa huduma katika wilaya zake zote lakini cha kusikitisha hospitali hiyo haina huduma ya X-ray. Huduma ya X-ray iliyopo ni ya zaidi ya miaka 20 iliyopita hali ambayo inawalazimu wagonjwa waliolazwa hata wodini kwenda kupata huduma za X-ray nje ya hospitali hiyo katika Hospitali za Mzinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapeleka huduma hizo za X-ray katika Hospitali hii muhimu ya Rufaa ambayo inategemewa na wananchi wa Mkoa wa Morogoro?
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu mazuri aliyotoa Naibu Waziri kuhusu kushughulikia tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali imekuja na mpango wa kuanzisha Bwawa jipya la Kidunda ambalo litakuwa likitoa huduma ya maji katika mikoa mingine lakini siyo kwa Mkoa wa Morogoro. Serikali haioni kama si vyema kuanzisha bwawa hilo pasipo kwanza kushughulikia kero ya maji ya wananchi hasa wa Manispaa ya Morogoro kuliko kuitumia mito yao kuendelea kutoa huduma katika mabwawa ambayo yatahudumia mikoa mingine nje ya Mkoa wa Morogoro? (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri kwa majibu yake, amesema mwaka 2018 ndio mradi huo utakamilika, ni nini commitment ya Serikali kwa kuwa hadi kufikia mwaka 2018 na wananchi wanaihitaji nishati hii muhimu kwa ajili ya maendeleo. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia njia mbadala kuweza kusaidia wananchi hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tatizo la nishati ya umeme katika Mkoa wa Katavi linafanana kabisa na matatizo ya umeme katika Mkoa wa Morogoro hasa katika Manispaa ya Morogoro katika Kata za Mindu, Kihonda na Mkundi ambapo wananchi hawa kwa muda mrefu hawana nishati ya umeme ingawa wanapitiwa na Gridi ya Taifa. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kuhakikisha wananchi hawa wanapata umeme?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimesikiliza majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambapo amesema hivi sasa Serikali ime-stick kupima kwenye Sh. 300,000/= kwa hekta moja lakini pia amesema Serikali inashirikiana na wapima binafsi. Je, Serikali imeweka mikakati gani ya kuzuia hao wapima binafsi wasiendelee kuongeza bei kwa maana ya kuwaumiza wananchi ambao wanahitaji huduma hii ya kupimiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali inasema nini juu ya wananchi wa Mtaa wa CCT Mkundi katika Manispaa ya Morogoro ambao walifuata taratibu zote za kupata hati, lakini hivi sasa wamevunjiwa nyumba zao na wengine wanalala nje huku wakiwa na hati zao mikononi. Je, Serikali ina mpango wowote wa kulipa fidia kwa wananchi hao ambao wana hati?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la maji Ngara linafanana kabisa na tatizo la maji katika Mkoa wa Morogoro, licha ya Mkoa Morogoro kuwa na mito mingi, lakini wananchi wa Morogoro hawapati maji safi na salama. Je, Serikali haioni kama kuna haja sasa ya kujenga bwawa lingine liweze kusaidiana na Bwawa la Mindu ili kutosheleza maji kwa wakazi wa Morogoro?
MHE DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kukuniona. Licha ya Mkoa wa Morogoro kuwa na mito mingi na hatimaye kuweza kulisha Mikoa mingine kama Pwani, Dar es Salaam na Mkoa wa Tanga lakini Mkoa wa Morogoro hauna maji safi na salama. Sasa ni lini Serikali itahakikisha Manispaa ya Morogoro hususan katika Kata za Bingwa, Kiegea A na B, Mkundi, Kingolwira na Kihonda zinapata maji safi na salama?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa na viwanda vingi sana. Baada ya ubinafsishaji, viwanda vingi vimekufa na vingine vimegeuka kuwa ma-godown. Je, Serikali ina mpango gani wa uhakikisha inafufua viwanda hivi viweze kutoa ajira kwa wakati wa Mkoa wa Morogoro? (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Magereza mengi nchini yanaendeshwa kinyume kabisa na Kanuni Namba 10 ya Umoja wa Mataifa ambayo inazungumzia namna ya kuwahifadhi wafungwa kwamba ni lazima wakidhi vigezo ikiwemo afya, hali ya hewa, joto na nafasi ya kutosha. Magereza mengi nchini likiwemo Gereza la Songea ni mojawapo ya magereza kongwe nchini ambalo lilijengwa tangu mwaka 1948. Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba gereza hili nalo linakidhi vigezo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tangu Rais aseme maneno ka-ta yameleta athari kwa magereza mengi nchini ikiwemo magereza 14 ya Mkoa wa Morogoro ambayo hivi sasa yako kwenye giza tororo. Serikali haioni kama magereza haya kuendelea kuwa na giza ni kinyume kabisa na haki za Umoja wa Kimataifa na pia inasababisha Askari Magereza kushindwa kufanya kazi zao vizuri? (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inaitaja kazi ya uandishi wa habari kuwa ni jukumu la kisheria. Serikali inawachukulia hatua gani watu wanaowazuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi zao kama vile RC kuvamia kituo cha Clouds, baadhi ya waandishi kuvamiwa wakiwa kwenye mkutano wa CUF, baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuwakamata waandishi wa habari na kuwaweka ndani na hata jana kule Arusha katika Shule ya Msingi ya Lucky Vincent waandishi wa habari kumi walikamatwa wakiwa wanatimiza majukumu yao. Ni lini Serikali itaacha tabia hii mbaya ya kuwakamata kamata waandishi wa habari wakiwa kwenye majukumu yao? (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara ya Kichangani - Tubuyu katika Manispaa ya Morogoro ambayo ina urefu wa kilometa nne imejengwa kwa kilometa moja kwa shilingi bilioni tatu yaani kilometa nne imejengwa kwa shilingi bilioni 12. Je, Serikali iko tayari kupeleka wataalam kwenda kubaini ubadhirifu wa ujenzi wa barabara hii ambayo imejengwa kwa Mfuko wa Benki ya Dunia? (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Waziri amesema Serikali haitarajii kuwepo kwa ucheleweshwaji wa mikopo kwa wanafunzi ambao wamekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita mamia ya wanafunzi wenye vigezo walikuwa wakishinda katika Bodi ya Mikopo wakifuatilia upatikanaji wa mikopo. Wengi wa wanafunzi hao wanatoka katika familia maskini, na Bodi ya Mikopo vigezo wanavyoviangalia ni ufaulu. Wanafunzi wengi ambao wanasoma katika shule binafsi zikiwemo Feza na nyinginezo wana ufaulu wahali ya juu ukilinganiswa na shule za Serikali. Hata hivyo hivi sasa wanafunzi hao wanaotoka kwenye shule za private ambao wana ufaulu mkubwa wanapata fursa hii ya mikopo ikilinganishwa na wanafunzi maskini wanaotoka katika shule za Serikali. Je, ni lini Serikali sasa itaangalia vigezo stahiki vya wanafunzi ambao wana uhitaji wa kuingia vyuo vikuu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ilikuwa ni kwa wenye uhitaji, lakini sasa lengo lile limebadilika na sasa hivi mikopo inatolewa kwa kozi, kwa mfano wanaosoma udaktari, engineering wanapata mikopo kwa asilimia 100. Ni nani amesema kwamba nchi hii haihitaji accountants? Nani amesema nchi haihitaji waandishi wa habari? Nani amesema haihitaji lawyers? Naomba majibu ni kwa nini sasa Serikali isiangalie namna ya kutoa mikopo kwa kuangaliwa mahitaji ya wanafunzi wa hali ya juu?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la Ranchi ya Mbarali linafanana kabisa na tatizo la Ranchi ya Mkata iliyoko Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ambapo Ranchi ile hivi sasa imegeuka kuwa pori na Serikali imeshindwa kuiendeleza. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kubinafsisha Ranchi ile, mashamba yatolewe kwa wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro ya muda mrefu?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa ni Sera ya Serikali kwa Wazee kupata matibabu bure, Kambi ya Funga Funga ya Mjini Morogoro, ambayo inahudumia wazee wengi hivi sasa wanakosa huduma ya matibabu kutokana na hospitali ya Mkoa wa Morogoro kukosa madawa ya kutosha, hivi sasa wazee wale wakifika hospitali wanapewa panado na madawa mengine wanaambiwa wakanunue kwenye pharmacy za nje ya hospitali. Nataka kujua, je, Sera hii ya matibabu bure kwa Wazee inatekelezeka?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kukosekana kwa mipaka limeendelea kuleta migogoro na kuwaumiza wananchi wengi hapa nchini. Tatizo hilo limeendelea kuwaumiza wananchi wa Mtaa wa CCT Mkundi pale Manispaa ya Morogoro ambao wamevunjiwa nyumba zao, takribani miaka miwili imepita baada ya kuambiwa kwamba wamejenga kwenye Hifadhi ya Msitu wa Kundi. Hata hivyo wananchi wale walikuwa na vibali halali na walipewa ramani zote na mji kujenga nyumba zao. Je, Serikali ipo tayari kuwalipa fidia wananchi hawa wa Mtaa wa CCT Mkundi?
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoeleza Naibu Waziri, kazi za wasanii ni kuburudisha, kuelimisha, kuonya na kukosoa, wasanii wamekuwa wakifanya kazi hizi hata wakati wa kampeni tulishuhudia wasanii walivyofanya kazi yao vizuri na wakati mwingine waliimba nyimbo za kuponda upinzani na mlikuwa mkishangilia. Jambo la kushangaza hivi sasa wasanii wakiimba nyimbo za kukosoa Serikali wanashughulikiwa na mfano mzuri ni Ney wa Mitego pamoja na Roma Mkatoliki.
• Swali la kwanza, je, ni wakati gani sasa kazi hizi za wasanii zinathaminika?
• Swali la pili, kwa bahati mbaya sana Rais ametoa maagizo ya wale ambao wamehujumu kazi za wasanii na kuacha kabisa kuwawajibisha Serikali yake ambayo imeshindwa kabisa kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na Marehemu Mzee Francis Ngosha ambaye amekufa akiwa maskini wa kutupwa.
Je, Serikali inataka kukamata kazi za wasanii wakati ninyi wenyewe mmemuhujumu Mzee Francis Ngosha ambaye mpaka sasa hivi hana lolote, amekufa na hakuacha alama yoyote katika familia yake? (Makofi)
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Matatizo ya afya katika Mkoa wa Songea yanafanana kabisa na matatizo ya afya katika Hospitali ya Mkoa Morogoro ambapo licha ya kazi nzuri inayofanywa na Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro lakini hospitali ile inaelemewa na wagonjwa wengi. Kwa mwezi mmoja Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro inatibu zaidi ya wagonjwa 15,000. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kupeleka vifaa muhimu kama MRI, CT- Scan na X-ray machines za kisasa ili kuwapunguzia mzigo wagonjwa ambao wanalazimika hivi sasa kwenda Muhimbili kwa matibabu?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's