Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Janet Zebedayo Mbene

Supplementary Questions
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kuwa masuala mengi yanayohusiana na mambo ya wanawake yanatafutiwa kila sababu yasifanyike yakakamilika. Tunataka kupata majibu ni lini sasa hizi sheria zitapitiwa na zilete majibu yanayotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake ni zaidi ya asilimia 51 ya nchi hii lakini mambo yao yanapigwa danadana kila siku. Tunataka hili jambo likamilishwe sasa, lilikuwa lisingoje Katiba kwa sababu ni la miaka mingi kabla hata ya Katiba. Ahsante sana.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini vile vile Ileje ina changamoto kubwa sana ya shule ya sekondari ya bweni ya wasichana. In fact hakuna shule ya bweni ya wasichana peke yake, hii inaleta changamoto kubwa kwa watoto kusafiri kwenda Wilaya nyingine au Mikoa mingine na ni gharama kubwa kwa wazazi na inaleta usumbufu. Watoto wengine wameshindwa hata kumaliza masomo yao. Je, Serikali iko tayari kutusaidia kujenga shule ya bweni ya wasichana kwa kuchangia nguvu na wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Ileje vile vile ni katika wilaya ambazo hazina vyuo vya ufundi vya aina yoyote. Tumejitahidi sana, tumepata mfadhili ametujengea VETA, hivi sasa karibu imalizike. Je, Serikali iko tayari kuchukua ile VETA kuiendesha, kuiwekea vifaa na kuwalipa Walimu?
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Hizo huduma zinazosemekana kuwa zinatolewa kwa out growers, Je kuna mkakati maalum au inategemea na huruma ya huyo mwekezaji mkubwa?
Swali la pili linahusiana na soko; Kwa kuwa sasa hivi huu utaratibu wa minada ya Kahawa unaathiri kwa kiasi kikubwa mapato yanayopatikana kwa wakulima wadogo. Je, Serikali iko tayari kuruhusu wakulima wa kahawa na wao wenyewe kujitafutia masoko katika maeneo ambayo ni nish kwa ajili yao ili na wao waweze kupata mapato makubwa zaidi kwa ajili ya kahawa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Je, hii minada ni lazima iwe Kilimanjaro tu, hatuwezi kuwa na minada katika maeneo makubwa ambayo Kahawa inalimwa? Ahsante sana
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kuitikia wito wetu wa kusaidia kupokea hiki chuo kiwe cha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu kubwa Ileje na maeneo mengi ya pembezoni ni upimaji wa ardhi kwa ajili ya kuweka taasisi muhimu kama hizi za vyuo na masuala mengine. Naomba Serikali kwa ujumla itusaidie kwa sababu kupima viwanja muhimu kama hivi kwanza ni gharama lakini vilevile hatuna wataalam katika maeneo yetu wa kutupimia kwa haraka ambayo tungeitegemea. Je, Serikali ipo tayari kupitia Wizara nyingine yoyote ambayo inahusika na mambo haya kusaidia Wilaya ya Ileje tuweze kupima viwanja vyote muhimu tulivyoviainisha kwa ajili ya taasisi kwa mfano viwanda, elimu kama hivyo, vyuo vya unesi na vyuo vingine mbalimbali vya ualimu ili tuweze kupata maendeleo haraka zaidi? La sivyo tukiendelea kungojea tu mpaka sisi wenyewe tuwe na uwezo wa kupima tutachelewa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine, kwa kuwa sasa hivi tumeshaanzisha mkakati wa kuwa na chuo cha ufundi, tungeomba sasa tunapoendelea na mipango basi hiki chuo kiwe na mitaala ambayo itatusaidia kuzalisha vijana watakaokuja kufanya kazi katika viwanda kwa sababu sasa hivi tunalenga kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Ahsante
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.Ningependa kupata jibu, kwakuwa masuala ya madini hasa yale ambayo si ya kawaida yapo hata katika Mkoa wa Songwe; tuna migodi ya marumaru hususan Mbozi, Ileje, Chunya, yote haya bado hayajaendelezwa kwa kiasi ambacho yangeweza kuleta tija, je, Wizara ya Nishati na Madini itafanya lini utafiti wa kuja kutuletea na sisi uchimbaji wa migodi hii kwa sababu ina faida sana. Badala ya kuagiza tiles nje tungeweza kutumia za kwetu na ubora wake ni mzuri kuliko ule wa nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, je, mgodi wa Kiwira ambao uko Ileje na haujawahi kuifaidia Ileje utazinduliwa lini? Ahsante sana
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa kumekuwa na matamshi yanayotofautiana kutoka Serikalini kuhusiana na maendeleo ya mgodi huu, tungependa sasa kupata tamko rasmi ambalo wananchi watalielewa kuhusiana na uendelezwaji wa mgodi huu. Mwaka jana mwishoni tuliambiwa kuwa tayari mwekezaji ameshapatikana na karibu ataanza kazi. Tukaja kuambiwa mwekezaji yule ameonekana hafai na anatafutwa mwingine. Sasa tunaambiwa wako kwenye hatua za mwisho za kumtambulisha mwekezaji. Napenda kupata tamko rasmi kuwa ni lini huyo mwekezaji atapatikana na wananchi wategemee kuanza kufaidika na mgodi huo lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mgodi huu umetolewa leseni kwa miaka 25 na kwa muda mrefu sana huu mgodi umekaa bure. Je, huo muda wa leseni utaongezwa pindi atakapopatikana huyo mwekezaji au la sivyo mategemeo ni yapi mwekezaji huyo akija?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutupa moyo na kutuhakikishia kuwa tayari mikakati ya kutuwekea kituo cha forodha iko njiani. Hata hivyo, nataka vilevile nimtake
Mheshimiwa Waziri na Serikali kuharakisha mipango hiyo kwa sababu hivyo vituo vya jirani anavyovizungumza bila shaka anazungumzia Kasumulo iliyopo Kyela, anazungumzia Tunduma ambavyo vyote viko mbali sana na Ileje na Ileje
kama inavyofahamika hakuna barabara hata moja
inayopitika vizuri, kwa hiyo kutuambia sisi twende tukatumie vituo vile ni kama kutudhihaki. Pamoja na hayo, tayari ardhi imeshaanza kupimwa na inamaliziwa, tayari maeneo yameshaainishwa, tayari wahusika wameshakuja kukagua maeneo, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri anihakikishie
kuwa sasa hatua itakayofuata ni ujenzi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Malawi; Malawi
tayari wana kituo, wanatungojea sisi. Miundombinu yetu sisi ndiyo inachelewesha kile kituo cha Malawi kushirikiana na cha kwetu. Kwa hiyo, naomba sana hilo lifahamike na
atuhakikishie hapa ni lini sasa hatua hizo zitafanyika? Ahsante sana.
MHE. JANET Z. MBENE: Mhehimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mazingira anayozungumzia Mheshimiwa Chagula hayana tofauti na mazingira mengi ya Wilaya zetu na mikoa yetu ya pembezoni.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ileje ilibahatika kupata fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa na sasa hivi imesimama karibu miaka miwili. Nataka kuomba kuuliza, je, Wizara ya TAMISEMI iko tayari kuimalizia hospitali hiyo kwa sababu ni hospitali kubwa na kwamba kama ingetumika vizuri ingesaidia kiasi kikubwa sana. Sasa hivi wagonjwa wetu wa-referral wanakwenda Malawi. Kwa sababu Mbeya ni mbali zaidi, wanakwenda Malawi kutibiwa sasa hii si sahihi. Mheshimiwa Waziri atuambie, je, itawezekana kututengea fedha bilioni 1.3 kwa ajili ya kumalizia hosptali ile?
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Mkoa wa Songwe hususan Wilaya ya Ileje iko katika ukanda River Songwe Basin na kulikuwa kuna mpango katika mojawapo ya vitu vya kufanya katika mradi ule wa kuwa na mabwawa kwa ajili ya kufugia samaki na mpaka sasa hivi watu walizuiwa kutumia eneo hilo la Bupigu kwa sababu hiyo.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza ni lini sasa mpango huo utafanyika ili vijana wetu wapate ajira na vipato? Ahsante.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Waziri lakini halijanipa faraja hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ina fursa nyingi, kuwa mazao mengine sasa hivi hayajajitosheleza, ni kwasababu hakuna masoko, lakini fursa zipo. Sasa hivi hayo maeneo tuliyotenga, nilimuita Meneja wa SIDO Mbeya, alikuwa hajawahi kufika Ileje hata siku moja. Amekuja pale akatuambia tengeni eneo, hakutupa viwango, tutenge eneo kiasi gani? Hakutupa maelekezo yoyote. Miaka miwili imepita, wala hajarudi tena kuangalia kitu gani kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna fursa kubwa sana ya viwanda vidogo vya usindikaji wa nafaka. Tunalima mahindi mengi, karanga nyingi na ulezi mwingi. Hivyo ni vitu ambavyo tunaweza kuanzia kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaposema sisi tutayarishe miundombinu yote wezeshi, kwa uwezo gani wa Halmashauri zetu masikini watu wa pembezoni kama sisi? Nini maana ya ile Sera ya Kuendeleza Viwanda ya 1996 mpaka 2020 inayosema mtapeleka viwanda nchi nzima na mtakwenda mpaka maeneo ya pembezoni? Sisi ndio watu wenyewe wa pembezoni, mnakuja lini kutusaidia kuweka viwanda? Msituachie huo mzigo wa kutengeneza miundombinu, hatuna uwezo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, lini Mawaziri watakuja Ileje? Naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo waje Ileje. Mkija mkajionea wenyewe hali halisi ndiyo mtajua majibu ya kutupa humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naipongeza Serikali kwa kuja na huu mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa Bonde la Mto Songwe linaendelea kuwa endelevu kwa ajili ya matumizi ya wananchi wanaozunguka mto huo. Lakini nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji iliyowasilishwa hapa Bungeni kwa ajili ya mwaka 2016/2017 tulielezwa kuwa kuna mambo ambayo tayari yameshafanyika kuhusiana na juhudi za kuendeleza rasilimali za bonde hili, lakini vilevile katika masuala mazima ya kutengeneza mpango wa biashara kwa ajili ya kuendeleza bonde hili. Nataka kujua na ilisemekana kuwa vingekuwa vimekamilika kwa mwaka 2015. Je, jambo hili lilifanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumzia mkakati mzima wa uendelezwaji wa Bonde la Mto Songwe, wananchi wa kawaida katika maeneo ambayo yanahusika na yanaguswa na bonde hili hawana taarifa zozote wala elimu ya aina yoyote wala hawajui ni nini kinachoendelea.
Je, hii ofisi ndogo ya muda iliyoundwa imeanza kufanya kazi gani ili wananchi wetu waanze kupata uelewa ili hata mkakati huu utakapoanza kufanya kazi wawe tayari kuupokea? Ahsante sana.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nami niulize swali la nyongeza kuhusiana na masuala ya matumizi ya Maafisa Maendeleo ya Jamii na nipendekeze kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, vilevile kuna kundi zima la vijana wengi wanaomaliza shule kuanzia Darasa la Saba, Kidato cha Pili, Kidato cha Nne mpaka Kidato cha Sita. Je, kuna uwezekano wa kuwatumia hawa kuwapa mafunzo ili watumike katika Vijiji vyao kama Maafisa Maendeleo ya Jamii hata kama ni Para Community Development Officers wa kufanya uraghibishi wa aina mbalimbali ili waweze kusaidia katika nguvu ya maendeleo ya jamii yaliyopo? (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kweli nasikitika hili jibu ni la juu juu mno. Hii Wizara imeshafanya mambo mengi tunayoyajua, ningetegemea hapa ingekuwa ndio wakati Serikali ingetueleza ambayo wameshafanya na yale ambayo bado. Hata hivyo, tumeletewa taarifa ambayo mwananchi wa kawaida anayesikiliza sasa hivi wala haelewi kama Serikali imefanya chochote katika masuala ya viwanda katika maeneo maalum wakati nafahamu kuwa yameshafanyika mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi baada ya kusema hivyo nina maswali mawili ya nyongeza. Sasa katika hayo maeneo ambayo yametengwa ambayo nayafahamu kuna industrial parks, stand alones na kuna maeneo mengine ambayo ni ya Wilayani; ni mangapi ambayo mpaka sasa hivi yameshawekewa hiyo miundombinu saidizi na miundombinu wezeshi na kiasi gani ambacho tayari kinazalishwa na mapato kiasi gani nchi inapata na ajira kiasi gani kimeshazalishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuzingatia kuwa katika changamoto ambazo zinakwamisha na ambazo zimekuwa zikikwamisha kuendelezwa maeneo haya nyingi ziko katika uwezo wetu kuzitekeleza. Hiyo miundombinu inayozungumzwa ni kitu ambacho kiko kwenye uwezo wetu tukiamua. Haya masuala ya utata kati ya special economic zones na economic processing zones yanaweza kutatuliwa. Sasa ni kwa nini basi hatujakamilisha japo tuwe tuna maeneo mawili kila mwaka yanayofanyiwa kazi? Maana yameshatengwa na wananchi wamezuiwa kuyaendeleza lakini sisi hatujayafanyia chochote zaidi ya miaka 10 sasa. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Na mimi naomba kuuliza swali la nyongeza kuwa hili suala la kutenga asilimia 10 wa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu linaonekana kama halijakaa kisheria sana na ndiyo maana wakati mwingine wanatumia hiyo loopholes za kuepuka kutenga hilo fungu.
Je, Serikali ina mkakati wowote wa kuhakikisha kuwa sheria au kanuni zinarekebishwa ili kuhakikisha kuwa hili jambo linakuwa kisheria zaidi? Ahsante. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza kuhusiana na VETA ya Ileje. VETA ya Ileje mimi ndiyo nilienda kuomba fedha kwa wafadhili zikapelekwa pale na VETA imejengwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hayo masharti kuwa lazima tuwe na hati ndiyo yametukwamisha mpaka sasa hivi. Kupima na kupata hati pia ni suala la Serikali vilevile. Sasa kwa nini hicho Chuo kisianze wakati suala la upimaji linaendelea? Kwa sababu ni miaka miwili sasa Chuo kimesimama na kile Chuo kingekuwa tayari kinasaidia vijana wetu wengi sana wakati suala la hati likiendelea maana nalo ni sehemu ya Serikali vilevile.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's