Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Oran Manase Njeza

Supplementary Questions
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, kwanza napenda kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na vilevile kuipongeza Wizara hii kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kusambaza umeme karibu vijiji vyote vya Tanzania hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuwapongeza Mainjinia wa TANESCO waliopo pale Mbeya akiwemo Engineer Maze na Engineer Kiduko pamoja na Engineer Mbalamwezi. Pamoja na hayo, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Wizara ina mpango gani wa kusambaza umeme pamoja na hii REA kwenye vitongoji vilivyobaki katika vijiji hivyo vilivyotajwa? (Makofi)
Swali la pili, kutokana na ongezeko la usambazaji wa umeme vijijini, inaelekea capacity ya watumishi wa TANESCO ikiwemo vifaa, haitoshelezi tena.
Je, Wizara ina mkakati wa kuhakikisha kuwa inaongeza capacity ya watumishi ili iendane pamoja na usambazaji wa umeme vijijini?
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mwenyekiti, na pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa haya madini adimu duniani pamoja na joto ardhi ni muhimu sana kwa uchumi wa viwanda, naomba commitment ya Serikali, moja, je, ni lini wataanza uchimbaji wa joto ardhi ili tuweze kutumia kwenye viwanda vyetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na pili, naomba pia commitment ya Serikali pamoja na mradi wa Ziwa Ngozi, je, Serikali imetoa leseni ngapi za uchimbaji na uzalishaji wa madini na nishati ya joto ardhi katika sehemu zingine hapa kwetu Tanzania? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Kwa kuwa Waziri amepotoshwa kwenye jibu (b) sehemu ya kwanza ya swali langu na hivyo kuwapotosha wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi na pia kulipotosha Bunge; je, Waziri atachukua hatua gani kwa Afisa huyo aliyempotosha?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ndani ya Mji Mdogo wa Mbalizi kuna ardhi ya zaidi ya ekari 5,000 iliyokuwa Tanganyika Packers, na haijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 30 sasa na kwa kuwa Halmashauri ya Mbeya imetenga eneo mahsusi kwa kunenepesha mfugo na kwa ajili ya kiwanda cha nyama, je, ni lini Serikali itarudisha ardhi hiyo kwa Halmasahuri ya Mbeya kwa madhumuni ya makazi bora na huduma za jamii? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pia nashukuru kwa juhudi za misaada ya UNICEF kwa kuboresha elimu kwenye Halmashauri ya Mbeya na sehemu nyingine za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, changamoto nyingi, hasa kwa shule za vijijini ni miundombinu. Ukichukulia mfano wa Jimbo langu la Mbeya Vijijini, Shule ya Msingi Ipwizi ya ina walimu wawili na wanafunzi wanaozidi 200; Shule za Iyanga, Shule za Ivwanga hazina hata mwalimu na hizo ziko karibu sana na Jiji la Mbeya.
Mheshimiwa Spika, shule nyingine kama za Kitusi na Ivwanga wanafunzi wanatembea zaidi ya kilometakumi kwenda Mkoa mpya wa Songwe kwa ajili ya kujipatia elimu.
Je, ni kwa nini misaada hii haijalenga kwenye changamoto muhimu za miundombinu katika shule zetu za vijijini? Ahsante.
MHE ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwenye Mji mdogo wa Maswa tuna tatizo kama hilo kwa Mji wetu Mdogo wa Mbalizi, ambapo Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kumalizia kipande kidogo cha barabara ya kilometa moja na pia aliahidi kumalizia ujenzi wa stand pale Mbalizi lakini mpaka leo hakuna chochote kinachofanyika labda ningepena Waziri ajaribu kutoa ufafanuzi ni lini ujenzi huo utaanza? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na Jimbo la Mbeya Vijijini kuwa na vyanzo vya uhakika wa maji kutoka Mlima Mbeya, lakini maji yamekuwa yakipelekwa Jijini Mbeya badala ya kupelekwa kwenye sehemu zenye uhaba mkubwa wa maji kwenye vijiji vya kata ya Mjele na Utengule Usongwe. Je, ni lini Wizara itapeleka maji safi kwenye vijiji vya kata za Mjele na Utengule Usongwe?
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama ilivyo kwenye Jimbo la Busokelo kuna barabara ya Mbalizi kwenda Makongorosi ambayo inapitia kwenye Bonde la Ziwa Rukwa ambayo tumegundua neema ya gesi nyingi sana. Sasa ni lini Serikali itajenga barabara hiyo ya Mbalizi - Makongorosi kwa kiwango cha lami ambayo ni ya Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, suala la Mji Mdogo wa Mbalizi kuna changamoto kubwa za maji kama iliyokuwa kwa Mji wa Mikumi. Je, ni lini mtatatua changamoto kubwa ya maji kwenye Mji Mdogo wa Mbalizi? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupewa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo kwa mkutano tuliofanya na wakulima na wawakilishi wa Wanunuzi mwishoni mwa mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huo tulikubaliana kuwa wanunuzi wadogo wapewe leseni ya muda na vile vile wajiunge kwenye vikundi na pia hii Kampuni ya pareto ambayo ilikuwa imebinafsishwa kutoka Serikalini kulikuwa na asilimia 10 ambazo walipewa wakulima. Vilevile katika hicho kikao tulikubaliana kuwa zichunguzwe hizo asilimia kumi ziko kwa nani kwa vile wakulima hawakupewa hizo asilimia kumi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na makubaliano yote hayo, hakuna hata kimoja kilichozingatiwa na leo hii kuna kampuni mpya mbayo imejenga kiwanda eneo la Inyara, Mbeya ambayo imezingatia vigezo vyote na ilipewa leseni ya kununua pareto kwenye vijiji viwili tu kati ya vijiji zaidi ya 20 vinavyolima pareto. Sasa ni kwa nini Serikali isiboreshe hii Bodi ya Pareto ili tuweze kuboresha kiwango cha zao la pareto?
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
La pili vilevile nilitaka kupata uhakika wa Serikali, kwa sababu inavyoelekea hakuna ushindani sasa hivi, watatuhakikishia vipi ya kwamba hawa ambao wametimiza vigezo vyote wanaruhusiwa kununua pareto ili inunuliwe kwa ushindani? Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kama ilivyo kwa Jimbo la Kwela, kuna barabara mbili ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais; Barabara ya Mbalizi kwenda Makongorosi ambayo inaunganisha Mbeya na Mkoa mpya wa Songwe. Pia kuna barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete mpaka Njombe ambayo vile vile inaunganisha Mikoa ya Mbeya na Njombe ziliahidiwa na Rais kwamba zitajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini hizi barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kulipa fidia wale wote ambao ni waathirika.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa ajili ya matatizo ya migogoro ya wafugaji na wakulima, maeneo mengi yanahitaji sasa hivi kuwe na vituo vidogo vya Polisi. Je, Serikali au Wizara inatupa commitment gani kuwa kutakuwa na vituo vya Polisi katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga vituo vya Polisi kama ilivyokuwa kwa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mbeya ambao wamejenga kwa asilimia karibu zaidi ya 50. Je, Serikali inawaahidi nini wale wananchi wa Mbalizi kuwaunga mkono kuwamalizia kile kituo chao cha Polisi? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuna shule Shikizi nyingi ambazo zina Walimu wa kujitolea na hawapati posho. Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho hawa Walimu wanaofundisha kwenye Shule Shikizi? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata tafsiri ya jina langu.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo, pamoja na kuwepo na jitihada za kuweka mfumo mzuri wa masoko, bado mfumo wa masoko umedhoofishwa na kuwepo kwa wanunuzi wachache ambao wamekuwa wakiwadidimiza wakulima kwa bei isiyokuwa ya ushindani.
Swali la kwanza, je, ni kwa nini zao la pareto lina mnunuzi mmoja ambaye anajipangia bei anavyotaka mwenyewe?
Swali la pili, je, ni kwa nini tumeshindwa kuanzisha soko la bidhaa (commodity exchange) ambayo imekuwepo toka mwaka 2014?
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana vilevile nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kazi zilizokuwa zinaendelea zilizokuwa zinafanywa na Halmashauri na hizo zimehamishiwa kwenye TARURA sasa hivi. Je, ni lini TARURA wataanza na kuendeleza hizo kazi?
Swali la pili, kama ilivyo katika Mji Mdogo wa Rujewa vilevile Mheshimiwa Rais aliahidi kumalizia ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbalizi katika Mji Mdogo wa Mbalizi.
Je, ni lini kazi hiyo ya kujenga kituo cha mabasi cha Mji Mdogo wa Mbalizi kitaanza? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika Halmashauri ya Mbeya na katika ziara yake tuliahidi kuwa mradi wa Iwindi wananchi wangeanza kupata maji kabla ya Desemba mwaka 2017, je, ni lini mradi wa maji kwa Vijiji vya Izumbwe, Iwindi, Mwashiwawala na Mbalizi utakamilika? Ahsante.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, napenda vile vile kushukuru majibu ya Serikali na pia nipende kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya mkoa na TANAPA vile vile kwa kushiriki katika ujenzi wa kituo cha afya pale Ilungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwa vile hii fidia ni ya muda mrefu 1965; je, Serikali inathibitisha kuwa hii fidia itakayolipwa mwaka huu itazingatia thamani na sheria zilizopo sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile Mji wa Mdogo wa Igoma unakua kwa haraka sana na pale kuna eneo la hifadhi ambalo limezungukwa na mji; je, Serikali itakuwa tayari kuliachia lile ili liweze kutumiwa na shule pamoja na huduma zingine za kijamii? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's