Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. David Ernest Silinde

Supplementary Questions
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, asante sana. Tatizo la maji Tanzania ni kubwa na ndiyo maana kwenye Bunge letu kila Mbunge akiulizwa atakueleza hilo. Sera ya Maji ya Taifa inataka mwananchi wa kawaida apate maji umbali wa mita 400 toka makazi anayoishi. Sasa Mheshimiwa Waziri, na Naibu Waziri atueleze ni lini Sera hiyo ya Taifa itaanza kutekelezwa kikamilifu ili Watanzania waondokane na hii kero ya maji?
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niseme Serikali inaonekana haiko serious katika hizi Halmashauri mpya ambazo tumekuwa tukizianzisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2014/2015 Halmashauri ya Wilaya ya Momba tuliomba shilingi bilioni mbili fedha maalum, maombi maalum, kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa Makao Mkuu yaani kwa maana ya kujenga boma na nyumba za watumishi ili watumishi watoke katika Halmashauri mama ya Mbozi kwenda Momba eneo la Chitete wakaanze kazi maalum. Mwaka 2014/2015 ukiangalia hapa hapa Serikali haijatenga kitu chochote, ni kwa nini Serikali inakuwa haiko serious inapoanzisha Wilaya mpya kwa ajili ya maandalizi ya watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali (b), Halmashauri ya Momba ipo katika Mkoa mpya wa Songwe ambao na wenyewe umeanzishwa hauna Mkuu wa Mkoa, hauna ofisi, hauna chochote. Ni kwa nini Serikali imekuwa ikianzisha jambo la msingi lakini utekelezaji imekuwa ikishindwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kupata majibu lini Mkoa Mpya wa Songwe utapelekewa Mkuu wa Mkoa na ofisi itakuwepo pamoja na Halmashauri ya Mombo? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kuna changamoto katika ujenzi wa nyumba za Polisi pamoja na vituo. Sasa swali langu ni je, kwenye Polisi kuna kitengo cha Usalama Barabarani yaani Trafiki, ambacho kimekuwa kikikusanya fedha nyingi, almost kwenye bajeti huwa tunatenga ni zaidi ya bilioni 10 kwa mwaka.
Je, ni kwa nini sasa Serikalli isiamue kuruhusu Polisi kutumia fedha zinazotokana na Polisi wa barabarani kwa ajili ya kuondoa kero ya ujenzi wa nyumba za polisi, pamoja na Vituo vya Polisi katika Wilaya zote nchini?
Swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, amesema Serikali inatajarijiwa kukopa kutoka Benki ya Exim China; je, haijatueleza ni kiwango gani mnatarajia kukopa na namna ambavyo mtalipa, kwa sababu suala la Polisi siyo miradi ya maendeleo? Ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ningependa kuuliza maswali mado mawili.
Moja ya kero inayowakuta wafugaji wanapokuwa minadani, inatokea mahali mtu amekwenda kuuza bahati mbaya akiwa pale mnadani hajauza mfugo wake, na anapotoka pale anadaiwa ushuru wakati hajapata hiyo fedha. Sasa nilitaka nifahamu kauli ya Serikali juu ya wale wote ambao wanashindwa kuuza mazao ama mifugo yao katika maeneo hayo?
Swali la pili, je, ni kiwango gani ambacho mtu anapaswa kulipa, kwa sababu kuna watu wanatoka mashambani labda ana mahindi wanakwenda nyumbani kwao kuyatunza. Sasa wakikutana na kizuizi, mtu ana gunia mbili, gunia tatu anaambiwa lazima alipe ushuru hata kwenye yale mahindi ya kutumia.
Je, ipi ni kauli ya Serikali juu ya hili jambo? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchakato mzima wa uzalishaji umeme katika Mto Malagarasi umetumia vilevile fedha za Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC I). Ninataka nifahamu kwamba watu wa MCC wamekuwa wakipeleka fedha zao nyingi kwenye mradi wa umeme, na sasa hivi wamejitoa.
Je, sasa Serikali itupe commitment ya miradi yote ya umeme ambayo fedha zake zilikuwa za MCC, sasa Serikali itatumia vyanzo gani kuhakikisha kwamba miradi iliyopangwa inakamilika kwa wakati.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu yaliyotolewa. Naomba tuweke rekodi vizuri. Hakuna ujenzi wa miundombinu uliokamilika katika Mkoa wa Kigoma hilo la kwanza, Pili, Kampuni ya Kigoma Sugar haifanyi utafiti wa miwa wala BTC hawafanyi utafiti wa chai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa ruhusa yako naomba swali langu kipengele (a) litafutiwe majibu muafaka kwa sababu hayo siyo majibu yake. Kwa sababu shamba la chai limeachwa limekuwa poro kwa muda mrefu na hakuna utafiti kama huo. Swali la kipengele cha (b) limejibiwa sawasawa. Swali (c)….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nsanzugwanko kuna nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa hiyo umechagua kusahihisha jibu au utauliza swali la nyongeza? Kwa sababu kama una malalamiko kuhusu jibu umeshayaleta na Kiti kimepokea kitatoa uamuzi. Kama ni hayo tu tumalize au kama unauliza swali la nyongeza uliza swali, suala la kulalamikia jibu tumeshalipata.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la Bugaga ambalo Mheshimiwa Waziri anajibu kwamba halikuendelezwa kwa sababu ya ufinyu wa fedha ni kwamba shamba hili hata mwaka huu wa fedha halina fedha. Kwa hiyo ni vizuri tu Wizara waturudishie shamba letu kama wameshindwa kuliendeleza shamba hili la Bugaga tunaomba waturudishie shamba letu ili tulitumie kadri tutakapoona inafaa, kwa sababu inaonekana Serikali haina nia hata kidogo ya kufufu shamba hili la Mbegu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ukiliangalia jibu unaona kweli fupi na linaridhisha.
Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, ni nini kinachochelewesha Wizara kuchukua hatua ya kujibu barabara zote ikiwemo hii ya Kakozi - Kapele mpaka Ilonga, kupata majibu mapema iwezekanavyo tofauti na jibu ambavyo limewekwa hapa?
Jambo la pili, barabara hii tulikuwa tunaiombea kupandishwa hadhi karibu mara tatu kukamilisha vigezo, mwaka 2011, mwaka 2013 na mwaka 2015 kupitia Road Board ya zamani tulipokuwepo ya Mkoa wa Mbeya. Wizara mlitushauri tuombe special funds kwa ajili ya kuikarabati barabara hii, tumeomba fedha na mpaka sasa hazijaja.
Kwa nini mnatushauri tuchukue maamuzi ambayo hamuwezi kutekeleza? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Pamoja na uhaba wa Maafisa wa Ardhi na uhaba wa fedha, lakini zoezi la kupima ardhi nchini limekuwa likisuasua na mahitaji ya wananchi kujenga yamekuwa yakiongezeka, kwa hiyo ukiangalia katika hali ya kawaida wananchi wengi wamekuwa wakijenga katika maeneo ambayo hayajapimwa, sasa nataka kauli ya Serikali, ipi ni kauli ya Serikali juu ya wananchi wote wanaojenga katika maeneo ambayo hayajapimwa na Serikali bado inasuasua kwenye kupima maeneo hayo ya ardhi? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Suala la idadi ya wanafunzi ambao wametokana na bajeti linaendana na sifa za wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na vyuo vikuu. Ningependa kuuliza swali dogo tu, kwamba, sasa hivi Serikali imetoa kauli mbili tofauti, mwezi Julai iliweka vigezo vya wanafunzi kujiunga na Chuo Kikuu vya GPA ya 3.5 kwa watu wa diploma, si zaidi ya hapo. Hata hivyo, juzi wametoa tena tamko lingine la GPA ya 3.0 kwa watu wa ordinary diploma. Je, Serikali itueleze hapa, ni kwa nini inawasumbua wanafunzi katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wengi walikuwa wameshakata tamaa na hawaku-apply katika Vyuo Vikuu? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla ya kuanza kwa Mradi wa REA III, kuna baadhi ya maeneo Miradi ya REA I na REA II bado haijakamilika ikiwemo katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Momba. Sasa tunataka assurance ya kukamilisha miradi kwanza ya REA I na REA II kabla ya hiyo REA III, lini itakamilika miradi hii, REA I na REA II? Ahsante Sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, changamoto katika sekta ya afya ukiacha vifaa tiba, sasa hivi pameibuka changamoto kubwa mpya, ambao wananchi wanakuwa wakilipa bima zao za afya, wanakwenda katika hospitali, wanaandikiwa tu dawa lakini wanashindwa kupatiwa pale. Kwa hiyo, nilitaka nijue ipi ni kauli ya Serikali kwa wananchi ambao wamelipia bima zao lakini hawapati matibabu katika hospitali husika?
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Tatizo la viongozi kukosa semina elekezi juu ya masuala ya uongozi yamekuwa yakionekana kuanzia ngazi za juu, kwa mfano mdogo tu hapa katika swali lililopita unakuta Mawaziri wamejibu, Naibu Waziri naye anajibu kwa hiyo, protocol inakuwa inaonekana pale haijafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala langu ninalotaka kujua ni kwamba taratibu kama hizi, viongozi ambao wanakosa semina za mafunzo elekezi na contradiction inaonekana ndani ya Bunge lako Tukufu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka nijue makosa kama haya yataendelea mpaka lini kwa viongozi ambao hawana semina kama Mawaziri? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na ukubwa wa tatizo la maji, Bunge lako liliidhinisha Sheria hapa ya kuweka zuio la fedha ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri hapa amekiri kwamba fedha zipo, lakini maji hakuna. Sasa swali ambalo nataka watupatie majibu, tumewapa fedha, lakini kwenye miji na vijijini kwetu kule maji hakuna. Nini kinachowafanya wanakwamisha miradi ya maji mpaka sasa hivi inashindwa kukamilika? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Hili swali la ujenzi wa daraja ninaliuliza leo ni mwaka wa saba mfululizo nikiwa ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada ambazo nimeanza kuziona ambazo zinaweza kuzaa matunda hivi karibuni, ni kwamba wametangaza tender tarehe 11.01.2017; sasa ninachotaka kujua ni kwamba, ili tupunguze maneno maneno mengi, je, Serikali itakamilisha lini utaratibu wa tenda ili ujenzi huo uanze? Wananchi wangu kule wameshachoka story hizi wanataka waone daraja likiwa limejengwa kwahiyo hicho ndiyo kitu cha kwanza, commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili; ni kwamba palipokuwa na ahadi ya ujenzi wa daraja ilikuwa inaambatana na muendelezo wa ujenzi wa barabara ambayo Mheshimiwa Haonga alikuwa ameuliza katika swali la nyongeza kutokea pale Kamsamba mpaka Mlowo kilometa 166.
Sasa ninachohitaji kujua ni kwamba wakati wa awamu ya nne Waziri Mkuu alipokuwa analijibu hili swali alisema umeingizwa katika mradi wa MCC 3 lakini bahati mbaya wale watu wa Marekani wa MCC 3 walishajitoa katika kuhudumia miradi ya ndani ya nchi yetu. Sasa, je, Serikali ile miradi ambayo iliondolewa na MCC katika Serikali hii ya Awamu ya Tano itatekelezwa vipi ili kuhakikisha kwamba daraja linakamilika na liendane na ujenzi wa lami? Ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, natambua jitihada ambazo zimefanyika kwenye hii barabara ikiwemo ujenzi wa daraja la Momba.
Mheshimiwa Spika, nataka tu niulize swali dogo, barabara hii imekuwa katika ahadi, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2009 alipokwenda kwenye Halmashauri ya Momba aliweka ahadi ya kujenga hii barabara. Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokwenda kule vilevile alitoa ahadi ya kuhakikisha hii barabara inakamilika kwa sababu hili bonde linaunganisha Mikoa mitatu na ni muhimu kwa mazao yetu.
Mheshimiwa Spika, Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli alisema katika Serikali yake hataki kusikia mambo ya michakato, ahadi, tunatafuta fedha, alisema mwenyewe. Watu wa Mikoa wa Songwe, Rukwa pamoja na Katavi tumekuwa tukilia kila mwaka ni kwa nini sasa mwaka huu msiweke commitment katika barabara zote mkatenga tu fedha kuelekeza katika Mkoa huu wa Rukwa, hususan hii barabara kutoka Mlowo mpaka Kamsamba na Kilyamatundu kwa kiwango cha lami ili tuache
kuwasumbua tena katika kipindi cha miaka mitano. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa tatizo la maji limekuwa ni kero ya nchi nzima, ni kwa nini sasa Serikali, hususan kupitia kwenye bajeti ya Bunge hili, isikubali kutengeneza Wakala wa Maji Vijijini ambaye atasaidia kupeleka maji vijijini kote kama ambavyo tumefanya katika REA ambapo kwenye suala la umeme wameweza kufanikiwa vizuri. Kwa nini wasifanye hivyo ili maji yafike hata kule Momba, Chitete, pamoja na vijiji vingine? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwenye majibu ya Mheshiwa Waziri amesema, endapo mtumishi hajaridhika na hatua za kinidhamu alizochukuliwa, akate rufaa. Sasa endapo mtumishi huyo ametumbuliwa na Mheshimiwa Rais na hajaridhika na hayo matokeo, wapi achukue hatua za kuja kukata rufaa?
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Masasi mpaka Nachingwea ni kama kilometa 42 na kutoka Masasi mpaka Ndanda ni kama kilometa 40; na kwenye bajeti iliyokuwa imeitengwa ambayo imeombwa mwaka 2017/2018 kama shilingi bilioni tatu, ni fedha ndogo ambayo haiwezi kukidhi kumaliza barabara hiyo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alikuwa ameomba, kwa sababu fedha iliyotengwa ni ndogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili la nyongeza ni kwamba, matatizo ya Jimbo la Ndanda yanafanana kabisa na Jimbo la Momba kule; sasa naomba niulize kwamba barabara ya kutoka Kakozi kwenda Kapele mpaka Namchinka kilometa 50.1 imepandishwa hadhi na Wizara yako, lakini mpaka sasa haijawahi kuhudumiwa na hiyo barabara ni mbovu. Ni kwa nini barabara hizi mnazipandisha hadhi na hamzihudumii kwa wakati? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la maji nchini ni kubwa na Tanzania ni moja ya nchi ambayo tuna sifa ya kuwa na Maziwa makubwa pamoja na mito mingi; yaani ni nchi ya Maziwa Makuu tofauti na zile nchi za kwenye jangwa kule kama Libya ambao wana maji zaidi ya asilimia 80. Sasa ni kwa nini Serikali isione aibu ya kushindwa kutatua hili tatizo kwa muda mrefu ilhali tuna maji mengi? Sasa hivi ukiangalia moja ya sifa ya nchi yetu ambayo tumekuwa tukijitamba na Serikali mmekuwa mkijisifu kwamba mmekuwa mkikusanya mapato mengi. Ni kwa nini sasa…
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kukubali kwamba watafanya mazungumzo na mmiliki ambaye ni Chama cha Mapinduzi, shule hii ni muda mrefu sana imefungwa, karibu miaka kumi hamna mwanafunzi anayesoma pale. Ni kwa nini msione sasa ni wakati muafaka wa kuirudisha kwa wananchi ili tuweze kuitumia?
Mheshimiwa Spika, ombi letu la pili, tunaomba shule hii tuitumie kwa ajili ya kidato cha tano kwa sababu Halmashauri ya Wilaya Momba haina shule ya kidato cha tano? Ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu yanayoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, mimi nilikuwa tu nataka niweke msisitizo kwenye hili jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, Mheshimiwa Rais amekuwa akirudia na wewe leo hapo umejaribu kuweka msisitizo, lakini bado kuna shida kule chini kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kukataa hili agizo kwa maana circular bado haijafika.
Sasa nataka nijue tu kabisa kwamba, je, circular hiyo inahusu ile mizigo ya wakulima ama wananchi wa kawaida wenye chini ya tani moja, kama Rais alivyoagiza kwamba ukisafirisha mzigo kutoka eneo moja kwenda lingine, chini ya tani moja hutakiwi kulipa ushuru; kwa hiyo, nilitaka nijue kama circular na yenyewe inazungumzia hivyo? Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya kuridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza, miradi ya umeme ya REA III imezinduliwa karibu nchi nzima katika kila Mkoa, lakini utekelezaji wake mpaka sasa hivi haupo, isipokuwa ipo katika mipango kama hivi ambavyo inaonesha. Nini ambacho kinasababisha au kimesababisha kucheleweshwa kwa miradi ya REA III kuanza kukamilika tofauti na iliyopo katika maandishi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba pamoja na majibu yake, Miradi ya REA tuliiwekea zuwio la fedha, yaani tuli-ring fence fedha zake ambazo zilitakiwa zisiguswe, lakini mpaka sasa hivi miradi hii haitekelezeki kwa sababu hizi fedha hazieleweki mahali ziliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu nataka niulize je, hizi fedha ambazo tumezi-ring fence kwa ajili ya utekelezaji wa hii miradi, kwa nini hazitumiki kutekeleza mradi ikizingatiwa kuna fedha ambazo tunakata katika mafuta shilingi 50 kwenye kila lita ya mafuta? Kwa nini zinashindwa kutumika kwa ajili ya kumalizia hii miradi? Ahsante. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri kujaribu kueleza sheria mbalimbali za kudhibiti fedha za umma, lakini kuna changamoto moja kubwa. Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ndio mtu pekee ambaye amekuwa akisimamia na kudhibiti hili suala la umma na kutuonesha wapi kwenye mapungufu na matumizi sahihi. Lakini Serikali imekuwa haipeleki fedha za kutosha kwa CAG ili aweze kudhibiti hizi fedha.
Je, Serikali haioni kwamba yenyewe ndio yenye jukumu la kuzorotesha Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kushindwa kufanya kazi yake ili tuweze kujua hayo mapungufu, kwa kushindwa kupeleka hizo fedha?
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri hapa amesema wataongeza kipato kwa Madiwani ikiwa mapato ya Serikali yataongezeka; lakini kwa mwaka sasa Serikali imekuwa ikitangaza kuongezeka kwa mapato, yaani makusanyo yamekuwa makubwa, ninachokitaka badala tu ya kuwalipa posho kwa nini sasa Madiwani wasilipwe mishahara kama tunavyolipwa sisi Wabunge ili wafanye kazi hiyo kwa moyo. Ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa, swali lilivyoulizwa na majibu ni kwamba Chuo hicho ambacho kinataka kuanzishwa kipo katika Jimbo la Momba ambalo mimi naongoza. Sasa nataka tu nimuulize pamoja na ahadi hii ambayo imetolewa na tunaamini kwamba kitaanza hivi karibuni na nina uhakika ni mwaka huu wa fedha. Je, endapo hicho anachokizungumza kisipotekelezwa ni hatua gani tumchukulie yeye kama Waziri kuwadanganya wananchi wa Momba? (Makofi/Kicheko)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa ya jumla kwa sababu swali nililouliza nilitaka nijue kama Momba kitapatikana kiwanda, kitajengwa au hakitajengwa. Kwa hiyo, jibu ni kwamba wananchi wa Momba huko mnakonisikia hamna kiwanda kitakachojengwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Mheshimiwa Waziri yanaainisha kwamba jukumu la ujenzi wa viwanda ni la sekta binafsi, lakini kauli za Serikali na viongozi wa Serikali mitaani huko, kila siku statement ambazo wamekuwa wakizitoa ni kwamba Serikali inajenga viwanda. Ni kwa nini sasa Serikali isibadilishe kauli yake ikawaambia wananchi jukumu la kujenga viwanda sio la Serikali, Serikali kazi yake ni kuwezesha mazingira wezeshi kama ambavyo mmekuwa mkitamka hapa. Ninayasema haya kwa sababu tumekuwa tukisia hapa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio nataka niulize kabisa kwamba kwa nini sasa wasibadilishe hiyo kaulimbiu kwa sababu mind set ya wananchi ni kwamba Serikali inajenga viwanda wakati ukweli ni kwamba Serikali haijengi viwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali imejinasibu hapa kwamba inaweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi pamoja na wafanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachotaka nijue jitihada za Serikali juu ya hawa watu wa sekta binafsi kwa sababu moja kumekuwa na malalamiko, mazingira wezeshi kwa mfano huko Momba barabara mbovu, maji hayapatikana, umeme unayumbayumba, mitaji hakuna, riba zimekuwa zinapitiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nijue jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto hizi ili hii sera ya viwanda iweze kuwa inatekelezeka.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Ruangwa (CCM)

Contributions (4)

Profile

Hon. Salim Hassan Turky

Mpendae (CCM)

Contributions (4)

Profile

View All MP's