Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Philipo Augustino Mulugo

Supplementary Questions
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza na-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyoongea, kuna vikao kadhaa vinaendelea kati ya Wamiliki, Mameneja na Serikali, Ofisi ya Kamishna Wizara ya Elimu, lakini mpaka sasa hatujafikia muafaka kwa sababu ya hiki ambacho amekiongea Mheshimiwa Naibu Waziri. Tunaonekana kama vile tunafanya mchezo, lakini jambo hili ni gumu sana. Shule zimetofautiana, wapo wamiliki wamewekeza na wamekopa fedha benki. Zipo shule zina utofauti wa vijijini na mjini. Menu ya chakula huwezi kulinganisha menu ya chakula shule za Dar es Salaam na shule za Rukwa, Mbeya ama Mwanza. Hata hivyo, mpaka wiki iliyopita, tumekutana na Serikali kwamba hata hawajafanya utafiti kwenye shule za msingi lakini ada elekezi inataka kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali, ni lini Serikali itaita tena kikao cha mwisho TAMONGSCO pamoja na Serikali wakae pamoja waweze kufanya utafiti wa pamoja? Serikali ifanye utafiti na shule binafsi zifanye utafiti ili wakae pamoja waweze kufanya negotiation ili ada elekezi itolewe si kwa upande mmoja tu?
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi niweze kuuliza swali lanyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Songwe naomba niiulize Serikali. Rais Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Songwe ambapo sasa ni Wilaya mpya aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbalizi - Mkwajuni - Makongorosi na tayari Serikali 2013 imeshafanya upembuzi yakinifu lakini baada ya hapo hakuna kinachoendelea. Je, Serikali ni lini itaanza sasa ujenzi wa lami wa barabara hiyo?
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Sika, Mji wa Mkwajuni ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Songwe hatuna maji kabisa, hivi ninavyoongea ule Mji unakua, watu wanahamia kwa wingi sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura na kwa haraka tuweze kupata maji katika ule Mji ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya na Mkuu wa Wilaya atakuja hivi karibuni pamoja na Wakurugenzi na Watumishi wengine wa Serikali?
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza nipende tu kusikitika tu kwamba sijui Serikali inafanya kazi kwa upendeleo baadhi ya Wilaya zingine. Tumekaa RCC iliyokuwa Mkoa wa Mbeya na Mheshimiwa Mwambalaswa na Mheshimiwa Mary Mwanjelwa mashahidi hapa. Tumepitisha barabara za Chunya mbili kutoka Ngwala mpaka Kapalala na kutoka Gua ziende ziwe hadhi kwa Mkoa ziwe kwenye TANROADS, toka mwaka 2011 tulikaa RCC tukapitisha leo bado Serikali inasema tunafanyia kazi, miaka sita mnafanyia kazi? Mimi binafsi nimesikitika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti narudia tena, naomba Serikali inijibu kwasababu tayari Songwe imeshakuwa ni Wilaya mpya ni lini watatupatia fedha tupandishe hadhi barabara ya hiyo kutoka Kininga kwenda Ngwala ni kilometa 46. Nikitaka kufanya ziara kule nitembee kwa bodaboda na watu wananielewa hivyo na kuna wanyama wakali na kuna ndorobo nahangaika sana.
Naomba leo Serikali inipe majibu tunahangaika sana wenzenu. Mbona sehemu zingine barabara mnatengeneza? Kutoka mwaka 2011 mpaka leo hatujatengeneza barabara. Naomba Mheshimiwa Waziri uniambie hapa hapa, utaniletea lini barabara hiyo? (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kule jimboni kwangu, Jimbo la Songwe na wilaya mpya, kuna kampuni moja inaitwa Sun Marie, walipata leseni mwaka jana mwezi Aprili kwa ajili ya kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe Kata za Magamba na Namkukwe Jimboni Songwe, lakini mpaka sasa hawaonekani walipo. Walikuwa wanafanya utafiti wa kujenga barabara mpaka sasa hatujajua wako wapi, Halmashauri haiwajui, tunaomba msaada wa Serikali, hawa watu kwanza wako wapi na ni lini wataanza kazi za uchimbaji wa madini haya?
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali maswali mawili tu ya nyongeza. Katika mpango wa Serikali wa kujenga nyumba 4,136, nataka tu kujua: je, Wilaya yangu ya Songwe ambayo ni wilaya mpya, itajengewa nyumba ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mgao huo, ni pamoja na Askari Magereza pamoja na hawa Askari Polisi wa kawaida? Ahsante.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mkwajuni ambao ndiyo makao makuu ya Wilaya ya Songwe, kila wiki umeme upo siku tatu na umeme haupo siku nne mpaka hivi ninavyoongea, hata wiki iliyopita nilikuwa huko. Nini tatizo la
kukatika katika kwa umeme hasa ule unaotoka Mbeya Lwanjilo, Chunya, Makongolosi mpaka Mkwajuni. Tatizo ni nini kila mwaka maana huu ni mwaka wa nne sasa hatuna umeme wa uhakika pale Mkwajuni?
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ambayo kidogo hayajatosheleza, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hamu na haja ya Waheshimiwa Wabunge wengi, toka nimeingia Bungeni hapa mwaka 2010, Wabunge wengi wanahitaji sana mabadiliko ya sheria ndogo ndogo ili mambo yaweze kuendana na wakati. Iko Sheria ya Ndoa ambayo inasema lazima mtoto awe na miaka 14 kuweza kuolewa; lakini mimi nimekuwa mwalimu muda mrefu, najua miaka 14 kwa sheria ya leo ilivyo ya elimu msingi, anakuwa bado ni mtoto yupo form two na tunasema elimu msingi mtoto atoke chekechea mpaka form four na ni elimu ya lazima. Kwa hiyo, unakuta ile sheria imepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi nilisema hapa kuhusu Sheria ya TMAA ya Madini kwamba Halmashauri kule zinapata ile ruzuku (service levy) ambayo unakuta hawajui source yake imetoka wapi kwa sababu hawashiriki katika kuangalia pato lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ipo Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, imepitwa na wakati. Sasa yote hayo nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka 1980 Serikali iliunda Tume kwa ajili ya kuangalia Sheria Mbalimbali na mabadiliko ili iweze kuletwa Bungeni, mpaka leo Tume hiyo ni kama vile imeshindwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Bunge liwe na Tume yake, Serikali iwe na Tume yake ili na sisi tuonekane kweli tunatunga sheria. Maana toka nimekuja mwaka 2010 hapa sijawahi kuona Mbunge kaleta hoja binafsi hapa na ikapita. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wana hoja binafsi nyingi, lakini wakileta hapa hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iruhusu Bunge liwe na Tume ili sisi wenyewe tuanze kutunga sheria na Serikali iwe na Tume, tuzilete pamoja tuweze kujadili ili tuweze kufanya marekebisho ya sheria kadri mambo yanavyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali italeta hoja ya kuruhusu Bunge iwe na Tume yake binafsi?
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa upendeleo wa kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Songwe lina uhaba mkubwa sana wa maji lakini niongelee Kata moja inaitwa Totowe ambapo mimi mwenyewe kwa juhudi za Mbunge niliomba mradi wa Mheshimiwa Sabodo nikachimba kisima kikubwa sana na kisima hicho mpaka ninavyosema hivi bomba hilo linatoa maji kutoka mwaka 2012 mpaka leo yanatiririka na yamesambaa pale kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuomba pale Halmashauri angalau watupe fedha hata shilingi milioni 50 tuweze kujenga tanki la kutunzia maji yale angalau yaweze kusambaa vizuri kwa kujenga mabomba kwa wananchi wa Totowe na maeneo ya Namambu. Je, Serikali inanisaidiaje mimi kama Mbunge nimefanya juhudi kutafuta maji halafu maji yanatiririka bila kujengewa tanki ili angalau wanipe fedha nikajenge tanki maji yaweze kuenea pale Totowe? Ahsante.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku nimekuwa nikilalamika hapa kwamba Wilaya ya Songwe, Mkoa mpya wa Songwe na hasa Jimbo langu lina Vijiji sita tu vyenye kutoa maji, vijiji vingine vyote 28 hakuna maji. Je, ni lini yeye mwenyewe kama Waziri anakuja Songwe mimi na yeye tutembee siku nzima nimwoneshe sehemu ambazo wananchi wa Songwe wanalalamika maji, hususan ni maeneo ya Mbangala, Mbotoe na Mkajuni. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Jimboni kwangu Kata ya Mbangala nina Kampuni inaitwa Shanta Gold Mining. Kampuni hiyo imefunga Mto Lwika na kusababisha wananchi wa Mbangala kutopata maji. Miezi miwili iliyopita kulitokea vurugu kubwa sana kati ya Polisi na vijana wa pale Mbangala lakini Serikali ipo na wanaona kabisa bwawa limefungwa na mto hautiririki kwenda hata vijiji vya Maleza. Je, Serikali inaniambia nini juu ya Ashanti wafungue ili na sisi kijiji cha Mbangala tuweze kupata maji?
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo itakuwa ni mara ya pili nipende tu kusikitika kwamba swali hili tena halijajibiwa na Bunge lililopita mwezi Novemba, swali langu nalo halikujibiwa vizuri sasa sijui nina mkosi gani. Kwa sababu swali la msingi haliendani kabisa na majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali langu la kwanza liwe hivi. Naomba Serikali iniambie inatumia mfumo gani wa kuwajibu maswali Wabunge humu ndani, kwa sababu Wabunge wengi wamekuwa wakilalamika maswali hayo hayajibiwi vizuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, bado niseme namuomba Waziri tena Waziri mwenye dhamana aje Jimbo la Songwe afanye ziara aangalie jinsi ambavyo vijiji vyangu na kata vilivyo scattered ili aone umbali wa kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine, karibuni kilometa 20 hapa, ndipo wanaweza kujenga vituo vya polisi. Lakini kunijibu kwamba kipaumbele ni RPC na OCD wala haviingi akilini naomba Mheshimiwa Waziri mwenyewe anijibu.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kuweza kupata muda wa kuuliza swali moja la nyongeza. Mamlaka ya Wanyamapori maeneo ya Ngwala, Itiziro na kule Guwa wamevamia vijiji hivyo na hivyo wamewasambaza wananchi, wamewanyang’anya mashamba, wamenyang’anya mbao na mali zao nyingine; na Mheshimiwa Naibu Waziri nilikwambia. Sasa nataka Mheshimiwa Naibu Waziri anithibitishie humu ndani mbele ya Bunge kwamba ni lini tutaongozana mimi na yeye twende tuka-solve mgogoro huo kwa ajili ya wanyamapori maeneo ya Ngwala?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's