Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Frank George Mwakajoka

Supplementary Questions
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua barabara ya Tunduma - Mpemba yenye kilometa 12 itajengwa lini na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu barabara ile inasababisha msongamano mkubwa sana wa magari kwenye Mji wa Tunduma na wananchi kushindwa kutimiza majukumu yao. Kwa hiyo, nataka Waziri atueleze ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwenye Mji wetu wa Tunduma haraka iwezekanavyo? Ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa sababu matatizo ya maji katika jimbo langu yanafanana sana na Jimbo la Kigoma Kaskazini, ninapenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali hii itakamilisha Mradi wa maji katika Mji wa Tunduma kwa sababu imekuwa inaahidi mara nyingi kwamba itatengeneza maji na hata wakati Mheshimiwa Rais anaomba kura kwa wananchi pia alisema kwamba ataweza kuwaletea maji haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka mmoja mradi utaanza kutekelezwa. Leo hii kuna kampuni ambayo tayari imekubali kujenga…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, swali si umeshauliza? Nadhani swali umeshauliza, kwamba huo mradi utakamilika lini?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nikumbushe kidogo kwa sababu kuna kampuni leo imekuja hapa na mradi ule umeshapitishwa na Wizara lakini tunashangaa Wizara ya Fedha hawataki kukubali mradi ule uanze kujengwa haraka. Kwa sababu mradi ule ulitakiwa uanze kujengwa mwanzoni mwa mwaka huu lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea. Tunataka kupata majibu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara hii ahadi yake ilikuwa ni kujengwa kwenye bajeti ya mwaka 2009/2010 na daraja lile ilikuwa ni 2009/2010, lakini mpaka leo daraja lile halijajengwa. Je, majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri yataleta matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Momba hasa eneo la bondeni kwamba itaanza kujengwa mapema mwaka 2016/2017?
Swali la pili, Momba ni Wilaya mpya ambayo inaunganisha Mji wa Tunduma na kutoka Tunduma kuelekea Makao Makuu ya Momba, eneo la Chitete ni Kilometa 120. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kutujengea daraja katika Mto Ikana katika Kijiji cha Chitete, Kata ya Msangano ili wananchi wa Tunduma waweze kufika kule wakiwa wanatumia barabara ile ambayo itakuwa na kilomita 68?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika na kwa sababu Mheshimiwa Waziri amenihakikishia kwamba mradi mkubwa wa maji utajengwa kwenye Mji wa Tunduma lakini kuna mradi ambao ulijengwa mwaka 1973, mradi wa maji wa kutega kwenye Kijiji cha Ukwire ambapo ulikuwa unahudumia Kata za Mpemba, Katete na Chapwa na sasa hivi mradi ule hautoi maji ya kutosha. Ni lini Serikali itakwenda kukamilisha mradi ule wa Mpemba ambao unalisha kata tatu katika Mji wa Tunduma?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanavyokwenda katika nchi ya Zambia hasa katika Jimbo la Copperbelt wamekuwa wanakamatwa wakiwa stand na wanapelekwa gerezani bila kupelekwa Mahakamani. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na jambo hili kwa sababu kuna vijana wengi sana ambao wako magereza na hawajapelekwa Mahakamani mpaka sasa hivi? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wangu wa Mji wa Tunduma. Swali la kwanza; Mji wa Tunduma ni mji uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia na ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika. Kwa tafsiri hiyo ni kwamba wageni wote kabla hawajingia katika nchi ya Tanzania ni lazima wapitie Tunduma kutoka katika nchi hizo.
Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka wa kupima ardhi katika Mji wa Tunduma ili kuondoa ujenzi holela unaoendelea kwa hivi sasa? (Makofi)
Swali la pili; nini mwongozo wa Wizara ya Ardhi ikishirikiana na TAMISEMI kupitia Halmashauri zetu kwenye Idara ya Ardhi ili kutoa fursa kwa Halmashauri kukopa fedha katika taasisi za fedha, lakini pia kukubali makampuni binafsi ambayo yanaweza yakapima ardhi mfano UTT katika maeneo yetu ili kuhakikisha kwamba tunapunguza ujenzi holela katika maeneo yetu ya Mji wa Tunduma na maeneo yote nchini? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Tatizo la ardhi kwenye Wilaya ya Mbozi linafanana sana na tatizo lililopo kwenye Mji wetu wa Tunduma. Katika Mji wa Tunduma katika Kata ya Mpemba kuna ardhi karibu ekari 500 ambazo zinamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa na mpaka sasa hivi eneo lile halijaendelezwa zaidi ya miaka minane. Je, Serikali inasema nini ili kuikabidhi halmashauri, ambayo haina hata eneo la kujenga makao makuu ili iweze kutumia ardhi ile?
MHE. FRANK MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio mimi, naitwa Frank George Mwakajoka. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa kipindi hiki cha miaka miwili kumekuwa na tatizo kubwa sana la malalamiko ya wafanyabiashara katika nchi hii na wafanyabiashara wengi sana wamekuwa wakifunga biashara zao, wafanyabiashara wa maduka pamoja wafanyabiashara wa hoteli, lakini pia wawekezaji wa kutoka nje, wamekuwa wakifunga shughuli zao na kuondoka. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaendelea kuwekeza katika nchi yetu?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wananchi wa Mji wa Tunduma, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wa Mji wa Tunduma wamekubali ushauri wa viongozi wao na kuondoa nyumba katika maeneo mbalimbali na kuhakisha kwamba barabara 42 zimepatikana kwenye Mji wa Tunduma, Serikali ina mpango gani wa kuwaunga mkono ili kuhakikisha kwamba barabara zile zinakuwa kwa kiwango cha lami kwenye Mji wa Tunduma, ukizingatia mji unaendelea kukua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo ya usalama katika eneo la Bunda yanafanana sana na Jimbo langu la Mji wa Tunduma.
Mwaka 2016 katika swali langu la msingi, niliuliza kuhusiana na ujenzi wa kituo chenye hadhi ya Wilaya, lakini pia niliuliza kuhusiana na nyumba zenye gharama nafuu kwa ajili ya polisi wetu kwenye Mji wa Tunduma. Majibu yake ni kwamba walisema katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 nyumba hizi zingeweza kujengwa pamoja na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na changamoto hizi katika mji wetu wa Tunduma? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa sana katika Halmashauri mbalimbali nchini baada ya kauli ya Mheshimiwa Rais katika sherehe za Mei Mosi juzi kule Kilimanjaro alivyosema kwamba Halmashauri yoyote au Baraza lolote la Madiwani litakalojitokeza na kutaka kumuondoa Mkurugenzi kazini au kumfukuza, Baraza hilo litavunjwa mara moja na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kumteua Mkurugenzi kwa hiyo atahakikisha anaifuta Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa mujibu wa Sheria
za Serikali za Mitaa, Waheshimiwa Madiwani ndiyo wasimamizi wa shughuli na miradi ya maendeleo na mapato na matumizi ya fedha za Halmashauri.
Je, Mkurugenzi akiwa ametumia fedha vibaya na akatumia madaraka yake vibaya, ni utaratibu gani ambao Waheshimiwa Madiwani watautumia kama siyo kumuondoa Mkurugenzi wakati Rais tayari ameshawaonya na amewaambia kwamba ataivunja Halmashauri hiyo? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Sera ya nchi na ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kila kijiji na kila kitongoji kuna kuwa na zahanati, na katika mji wa Tunduma katika mtaa wa Makambini eneo la Sogea wananchi wameamua kujenga zahanati katika eneo ambalo lilikuwa limetengwa na Serikali, lakini kutokana na mgogoro uliokuwepo na ambao alikuja kuumaliza Naibu Waziri wa Ardhi, alitoa maelezo kwamba eneo hilo lisianze kujengwa mpaka atakavyotoa ruhusa ya wananchi kuendelea kujenga Zahanati pale. Je, ni lini atatoa ruhusa ili wananchi wa mji wa Tunduma eneo la Makambini waweze kuendelea na ujenzi wa zahanati kama ambavyo sera za nchi zinasema?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Edwin Mgante Sannda

Kondoa Mjini (CCM)

Supplementary Questions / Answers (5 / 0)

Contributions (10)

Profile

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Singida Magharibi (CCM)

Contributions (5)

Profile

View All MP's