Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Japhet Ngailonga Hasunga

Supplementary Questions
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Tatizo la ajira katika nchi yetu, na hasa kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu limekuwa ni kubwa sana, kama kwa mwaka mmoja inaonyesha idadi hiyo bado hawana ajira.


Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuliambia Bunge hili ni lini hasa watakuja na mkakati wa kuanza kutoa labda mikopo midogo midogo ambayo itakuwa ni mitaji kwa hawa vijana ambao wanamaliza Vyuo vya Elimu ya Juu ambao hawana kazi kwa muda mrefu?, hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa inaonekana kwamba Serikali bado haina orodha kamili ya wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana kazi.


Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kukubaliana na mimi kwamba umefika wakati sasa kuanza kuwa na data bank ya kujua wahitimu wote wa Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuweza kujua ni ujuzi wa aina gani na weledi wa namna gani ambao upo katika nchi hii, na kuweza kuwashauri waajiri mbalimbali na sehemu mbalimbali? Nakushukuru sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, ulipaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali kuweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi ni wajibu wa kila raia wa nchi hii na kwa kuwa kumekuwa na matatizo mengi katika mfumo wa ulipaji wa kodi katika Serikali Kuu na Halmashauri, kodi usumbufu mkubwa kwa walipa kodi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mfumo wa ulipaji kodi ili uwe wazi zaidi na kuwawezesha wananchi kuweza kulipa kodi zile zinazotakiwa kulipwa?
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa wananchi wengi hawajui umuhimu wa kulipa kodi, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi na hasa walipa kodi ili waweze kuzijua aina zote za kodi na kuweza kulipa kama inavyotakiwa.ambazo zimekuwa zikileta
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa imeonekana taasisi nyingi hazifuati mfumo huu wakati Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 iliweka ni lazima kwa kila mtumishi kujaza hizo fomu na kutekeleza mfumo huu. Je, ni hatua gani ambazo Serikali imekusudia kuchukua kwa taasisi na watumishi ambao hawafuati huu mfumo ambao ni wa lazima kwa mujibu wa sheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kutangaza hadharani taasisi ambazo zimefanya vizuri katika kutekeleza mfumo huu kungesaidia sana kuwapa motisha wafanyakazi wanaofanya kazi katika taasisi hizo. Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba umefika wakati sasa taasisi zinazofanya vizuri na zile ambazo zinafanya vibaya zitangazwe moja kwa moja hadharani?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu haya ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mazingira ya kimondo chenyewe yako kwenye hali mbaya sana, na ukiangalia miundombinu na barabara zinazoenda kule ziko kwenye hali mbaya sana, hivi sasa hivi kimondo kile hata uzio wa kukizunguka kimondo kile ku-protect haupo. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya kimondo kile ili kiwe ni kivutio kizuri sana kwa utalii pamoja na kuinua pato la Mkoa mpya wa Songwe na Jimbo langu la Vwawa?
Mheshimiwa MWenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ilishaandika barua ya kuomba Wizara hii ikikabidhi kimondo kwenye Halmashauri ili waweze kukiendeleza na kuweka vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na migahawa, hoteli na vitu mbali mbali vitakavyowavutia watalii wa ndani na nje, Serikali ni lini sasa itakubali kukikabidhi kimondo hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ningependa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo zinafanya kazi zinazofanana na hii inasababisha kwamba bado gharama ziendelee kubaki kuwa kubwa. Serikali ina mpango gani wa kupitia upya taasisi zake zote ili kuhakikisha kwamba zile zinazofanana zinaunganishwa, kusudi kuweza kupunguza matumizi zaidi?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba niulize maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mfumo wa ugatuaji wa madaraka ulikuwa na lengo la kuwapa madaraka wananchi kuweza kuwa na maamuzi yao na kutekeleza masuala yao yanayohusiana kufuatana na mazingira yaliyopo; na kwa kuwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu hayo katika maeneo husika: Je, Serikali haioni haja ya kuupitia upya huu mfumo ili Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wabaki badala ya kuwa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji, Halmashauri za Wilaya pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri za Majiji ambao kidogo wamekuwa wakiongeza gharama kwenye Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya sasa hivi zimekuwa zikikabiliwa na upungufu mkubwa sana wa mapato na kwa sababu Serikali kuu imekuwa haina fedha za kutosha kuweza kuzipatia hizo Wilaya. Je, Serikali haioni haja kwamba Wakuu wa Wilaya sasa iwe ni sehemu ya kutegemea mapato yanayotokana na hizo Halmashauri ili waweze kuendesha majukumu yao na kusimamia sera vizuri katika maeneo husika?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ningependa kuuliza swali dogo tu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa hapo nyuma, shule nyingi zilikuwa zinategemea sana michango ya wazazi ili iwasaidie katika kuweza kutoa mafunzo hasa katika zile fani ambazo hazikuwa na Walimu wa kutosha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fungu maalum kwa ajili ya wale Walimu ambao watakuwa wanatoa mafunzo hasa ya masaa ya ziada baada ya ule muda wa kazi kukamilika?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 Serikali kupitia Ofisi ya Rais - Utumishi ilikipa Chuo cha Utumishi wa Umma kikishirikiana na chuo kimoja cha Macintosh cha Canada kuandaa framework ya kuwandaa viongozi ambayo ilijulikana kama Leadership Competence Framework. Na katika framework hiyo ilikuja na sifa 24 yaani leadership competencies 24. Sasa, je, ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kuziingiza hizo competencies katika mafunzo ambayo tayari yameandaliwa na Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika utaratibu wa majeshi yetu kuna utaratibu kwamba mtu hawezi kupata cheo chochote mpaka kwanza apate mafunzo fulani. Sasa kwa kuwa Serikali imesema inaandaa utaratibu wa kozi ambazo zitakuwa ni lazima kwa watumishi wa umma waandamizi. Je, ni lini sasa tamko la Serikali hizo kozi zitaanza ili watumishi hawa wawe wanafundishwa na wanaandaliwa ili wawe mahiri kabla hawajapata uteuzi wa madaraka ya aina yoyote?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na mazingira ya wakulima wa Wilaya ya Mbozi na hasa katika Jimbo la Vwawa. Kwa kuwa, moja ya gharama kubwa ambazo wakulima wa kahawa wanazipata ni pamoja na kusafirisha kahawa yao kupeleka kwenye mnada kule Kilimanjaro. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba Mnada wa Mloo unafunguliwa ili kupunguza ushuru na tozo mbalimbali ambazo zinawakabili wakulima wa zao la kahawa wa Wilaya ya Mbozi?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kwamba Watanzania ambao ni zaidi ya miaka 15 na ambao hawazidi miaka 54 wako takribani milioni 25 na kuendelea; na kwa kuwa asilimia 22.4 ni kubwa sana, maana yake ni kwamba karibu takribani watu 5,813,066 hawajui kusoma na kuandika.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha sasa vituo vya kufundishia kama ilivyokuwa zamani katika kila kijiji, kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana na hasa katika Jimbo la Vwawa na maeneo mengine nchini?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri umesema kwamba mmeziagiza Halimashauri kutenga fedha ili wahakikishe kwamba huo mfumo wa KKK unatekelezwa.
Je, mmeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kutakuwa na uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hili?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata hii nafasi. Kwa kuwa Mheshimiwa waziri amesema kwamba wana mpango wa kupeleka vitendea kazi na magari katika Ofisi za Ukaguzi wa Elimu, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa fedha za uendeshaji, unaweza ukapeleka magari kama hakuna fedha za uendeshaji bado hawataweza kufanya kazi; na kwa kwa muda mrefu wakaguzi wamekuwa wakifanya ukaguzi katika shule ambazo ziko jirani tu kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea OC ofisi hizo zote za kanda ili ziweze kufanya kazi yao sawasawa? (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya walimu wamekuwa wakijiendeleza wao wenyewe katika vyuo mbalimbali na kupata vyeti lakini kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikivikataa vyeti hivyo, imekuwa haivitambui. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvitambua hivyo vyeti ili waweze kupandishwa madaraja zaidi?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na hatua ambazo zimechukua katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo ambalo limekuwa na matatizo makubwa katika taasisi za umma ni eneo linalohusu ununuzi wa vipuri na matengenezo ya magari pamoja na mafuta.
Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote walioko katika Menejimenti za Mashirika hayo wanakopeshwa magari badala ya kutumia magari ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndiye mwenye wajibu wa kukagua hesabu zote za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma, lakini kwa muda mrefu tumeona kwamba hesabu za taasisi za umma, Mkaguzi Mkuu amekuwa akizipatia sekta binafsi zimekuwa zikikagua kwa niaba yake, lakini sekta hizo binafsi zimekuwa ziki-charge fedha kubwa sana ya ukaguzi. Je, ili kupunguza matumizi Serikali ina mpango gani wa kuimarisha ofisi ya CAG ili iweze kufanya kazi hiyo sawa sawa badala ya kutumia sekta binafsi?
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na hali halisi iliyopo katika Jimbo la Vwawa hasa katika Wilaya ya Mbozi. Kwa kuwa, Wilaya ya Mbozi inajishughulisha sana na kilimo na niwazalishaji wakubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Tawi la Benki ya Kilimo ili liweze kutoa mikopo kwa wakulima hawa wa Wilaya ya Mbozi?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's