Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Peter Ambrose Lijualikali

Supplementary Questions
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba taarifa nilizokuwanazo na ambazo ni sahihi ni kwamba daraja la Mto Kilombero lilipaswa kuwa limekamilika mwezi wa 10, 2015. Kutokana na Serikali ya CCM kushindwa kumlipa Mkandarasi kwa wakati, ameshindwa kufanya kazi hii kwa wakati.
Sasa naomba nijue ni lini Serikali ya CCM itaweza kumlipa Mkandarasi huyu ili aweze kufanya kazi yake vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lingine. Nataka nijue ni kwa nini Mkandarasi huyu amechukua mchanga kama sehemu ya material katika maeneo ya Lipangalala bila kuwalipa fidia yoyote wananchi wa Lipangalala. Nataka nijue, kama amelipa, kamlipa nani na kiasi gani? Nashukuru.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu haya mazuri ya Mheshimiwa Waziri na kwa namna ambavyo wafadhili wetu wameonesha nia ya kuweza kusaidia, lakini kwenye majibu ya Waziri ameonesha mradi utaanza kwenye robo ya tatu, lakini sijaona mradi unakamilika lini? Kimsingi, kwa Kilombero hii imekuwa ni kero. Tumechoka kuzika ndugu zetu, tumechoka kuharibu magari yetu, mazao yanakuwa na bei kubwa kwa sababu ya usafirishaji; kwa kweli imekuwa ni kero kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri sasa aniambie kwamba huu mradi unaisha lini ili hii kero iweze kwisha nasi tujione ni sehemu ya Tanzania? Kwa sababu imefika hatua sasa ukiwa unakwenda Ifakara unasema sasa naingia Tanganyika, maana kule ni vumbi! Hii imekuwa ni kero, kwa hiyo, naomba atuambie sasa huu mradi unakamilika lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine tunaomba atusaidie kwa sababu pale Ifakara na hii Wizara kwa sababu ni ya Uchukuzi na Mawasiliano, pale kuna daraja la Mto Lumemo, kutokana na mafuriko linakwenda katika muda wowote. Kwa hiyo, atuambie kama wako tayari kwenda kuangalia lile daraja na athari za mafuriko waweze kusaidia ili haya mafuriko yatoweke na daraja lipone. Nashukuru sana.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Suala hili la maji kwenye Kijiji changu na Kata ya
Zinginari kuna mradi wa maji ambao unagharimu shilingi milioni 400 umefanywa, muda umeisha lakini mpaka leo maji hayatoki, kimekuwa ni kilio kikubwa sana.
Je, Waziri anafahamu kwamba kuna hii shida na
kama afahamu atakuwa tayari kwenda na mimi kwenye Jimbo langu ili ashuhudie namna ambavyo shilingi milioni 400 hizi zimeliwa na maji hakuna? Nashukuru.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Juzi hapa tumetoka kwenye Uchaguzi Mdogo Ifakara tarehe 23 ambapo kwanza Mwandishi wa Mwananchi Juma Mtanda alitekwa na wanachama na wafuasi wa CCM, wakampora iPad, simu na Kamera, akaenda Polisi akalalamika. Matokeo yake Polisi wakawatafuta watu wa CCM na wakamrudishia. Maana yake ni kwamba Polisi wanawajua wanaofanya uhalifu huu, mpaka leo hakuna ambacho kimefanyika, hakuna kesi wala chochote, hiyo ni moja. (Makofi)
Pili, kwenye uchaguzi ule kuna Askari WP Huruma alipigwa na jiwe na tofali akapasuka, ameshonwa nyuzi tano na amepigwa na wanachama wa CCM, lakini Polisi wanamuachia anatembea, anafanya chochote taarifa ipo. Namwomba Mheshimiwa Waziri anaiambie kama CCM wanaruhusiwa kufanya vurugu mpaka kujeruhi Askari wetu halafu wakaachiwa huru?
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mimi naomba nifahamu, Jimbo la Kilombero lina Halmashauri mbili, Halmashauri ya Mji wa Ifakara wenye kata tisa na Halmashauri ya Kilombero yenye kata kumi. Kama ambavyo Jimbo la Bariadi ambalo lina Halmashauri mbili, Bariadi Vijijini kuna kata ishirini na moja na Bariadi Mjini kuna kata kumi. Hata hivyo, Mbunge wa Kilombero amezuiliwa na alizuiliwa kushiriki vikao vya Halmashauri ya Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipotaka kushiriki nimefungwa miezi sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwenzangu anashiriki mwanzo mwisho sehemu zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nifahamu, ni
kwa nini mimi wa Kilombero siyo tu kwamba nimezuiliwa kushiriki vikao hata kufanya maamuzi kwenye hizi kata zangu kumi sishiriki, lakini mwenzangu wa CCM anashiriki? Sasa naomba Waziri aniambie ni kwa nini ubaguzi huu unafanyika dhidi yangu halafu mwenzangu wa CCM anaachiwa afanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu inawezekana vipi Mbunge wa Kilombero nazuiliwa kushiriki vikao…
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri Mji wa Ifakara ni Halmashauri mpya, kutokana na upya wake bado ni changa. Barabara zetu bado ziko katika level ya tope, kutokana na mvua hizi ambazo kule zinanyesha barabara zinaharibika sana. Sisi kama Halmashauri tunajaribu kuziwekea vifusi lakini kwa sababu ni Halmashauri mpya, hatuna fedha za kutosha kuweza kujenga lami.
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Halmashauri ambayo ni mpya ili iweze kuboresha barabara zake, ziweze kuwa katika kiwango cha lami?
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nashukuru kwamba Serikali inajua hivi viwanda vimehujumiwa. Tuna viwanda ambavyo vilikuwa vinafanya kazi nzuri sana, lakini hao ambao tumewapa wamekata mashine na kuziuza kama scrapers, hasa kule kwangu MMMT imefanyika hivyo na Serikali inajua. Kitu kinachonishangaza ni huu upole wa Serikali kwenye kuwashughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu waliotuhujumu, walioharibu mali zetu wameharibu vitu vyote, halafu tunawabembeleza! Kwenye jibu la msingi hapa, Serikali inasema kwamba imewaambia hawa waliowekeza waje ofisini wapate mwongozo namna ya kuendesha au kuwapa walio tayari, yaani watu hawa wanabembelezwa. Sasa Serikali hii sijui, naomba nipate majibu, kwa nini watu hawa wanabembelezwa kiasi hiki wakati wameharibu rasilimali zetu? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye kiwanda changu cha MMMT kule kuna shida kubwa. Mwekezaji amepewa, amekata mashine, lakini bado ameongeza eneo la kiwanda, amenyang’anya ardhi karibu robo tatu ya kijiji. Serikali kama hamjui, naomba mjue na ninamwomba Waziri twende Ifakara, Mang’ula aende ashuhudie wananchi wa Mang’ula ambao wameporwa kiwanda na pia wameporwa na ardhi yao…
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri twende Ifakara. Je, yuko tayari kwenda au hayuko tayari kwenda?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's