Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Joseph Leonard Haule

Supplementary Questions
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naomba niongeze maswali mawili ya ziada. Serikali iliagiza Wakurugenzi wa Halmashauri waorodheshe mashamba ambayo yametelekezwa na wameshafanya hivyo. Je, ni lini Serikali itakwenda kutupa majibu ya moja kwa moja?
Swali la pili, kwa kuwa kuna wawekezaji wana mashamba makubwa mfano mashamba ya Miombo Estate, Kilosa Estate, SUMAGRO, Isanga Estate ambao wamebadilisha matumizi na kuvunja sheria na utaratibu, Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuyarudisha mashamba hayo kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi? (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Suala la Arumeru Magharibi linafanana sana na tatizo ambalo lipo Mikumi, je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kero ya maji katika Kata ya Mikumi, Ruaha, Uleling’ombe na maeneo ya Tindiga?
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Suala hili la Mbeya Vijijini linafanana sana na tatizo sugu la umeme katika Jimbo letu la Mikumi.
Swali langu ni kwamba, je, ni lini Serikali itapeleka umeme huu wa REA kwenye Kata za Tindiga, Mabwerebwere, Ulaya, Zombo, Muhenda, Uleling’ombe na Vidunda?
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la Nachingwea linafanana sana na tatizo la Mikumi. Ningependa nipate majibu ya Serikali ni lini itatengeneza barabara ya lami ya kutoka Kilosa kwenda Mikumi yenye urefu wa kilometa 78, ambayo ni kichocheo kikubwa sana cha uchumi wa Kata za Mikumi, Muhenda, Ulaya, Zombo, Masanze pamoja na Magomeni?
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kutenga bajeti ya daraja hili la Ruhembe kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017. Hata hivyo, kutokana na kilio na mateso makali pamoja na vifo vya watu wa Ruhembe ambao wamekuwa wakilia kwa muda mrefu, Serikali ipo tayari kuleta pesa hizi kule Mikumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016/2017?
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza ninasikitika sana kwa majibu ya Naibu Waziri anaposema kwamba wafugaji hawapati maji kwa sababu wakulima wamekuwa wakikinga hayo maji, nadhani wana upungufu wa research. Inaonesha kwamba mto Mkondoa na mto Miyombo inafika mpaka sehemu ambazo wafugaji wapo na tatizo lao kubwa siyo maji, tatizo lao kubwa ni malisho. Ndiyo maana wameonekana sehemu za Malangali wakilisha katika sehemu za mashamba ya watu na sehemu ambazo watu wamehifadhi mazao yao.
Mheshimiwa Spika, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Tindiga pamekuwa siyo mahali salama kwa watu kuishi na kwa kilimo kwa sababu wafugaji wameonekana ku-take over maeneo yale na hapa nnavyozungumza na wewe pamekuwa na mauaji kila mwezi; tarehe 8 Juni ameuawa kijana anaitwa Ally Mbarouk Makakala na juzi tarehe 6 Septemba wameuawa watu wawili Elia Emmanuel Mbwane na Ramadhani John Mashimba.
Je, Serikali inawahakikishiaje usalama wa wakulima wa pale Tindiga lakini pia inawahakikishiaje usalama wananchi wa Tanzania ambapo suala la migogoro ya wakulima na wafugaji limeonekana kuwa kero kubwa sana hapa nchini? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilikuja Tindiga na kutoa baadhi ya maagizo ambayo mpaka sasa hayajafanyiwa kazi na kupelekea vifo vya hao watu wawili vilivyotokea juzi.
Je, Naibu Waziri pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wapo tayari kuambatana pamoja na mimi kuelekea Tindiga kuona hali halisi ya mauaji na hali ya kutotulia katika Jimbo la Mikumi? (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa
kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Miundombinu ya mradi
wa umwagiliaji wa Bwawa la Dachi lililopo katika Kata ya Malolo liligharimu
takribani sh. 600,000,000 ambazo zilifadhiliwa na Shirika la JICA la Japan lakini
miundombinu hiyo imeharibika vibaya na imejengwa chini ya kiwango.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwashughulikia wale wote waliofanya
ubadhilifu huu na inachukua hatua gani ya kuokoa mradi huu ambao sasa Mto
Mwega umejaa mchanga na kuharibika na wananchi wakiwa wanategemea
sana bwawa hili kwa ajili ya umwagiliaji pale Malolo?
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na jitihada za Serikali za kukamilisha huu mradi wa World Bank, Mji wa Mikumi ni Mji wa kitalii na umekuwa ukipata wageni mbalimbali na idadi ya watu imeongezeka wamekaribia wakazi 30,000, lakini Mikumi kuna vyanzo vingi kama Iyovi, Madibila na pia Mto Muhanzi.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweza kutumia
vyanzo vingine ili viweze kusaidiana na mradi huu ili iweze kusaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi na kadhia hii?
Swali la pili, katika ziara ya Naibu Waiziri ulipokuja uliagiza watalaam waje kuangalia chanzo cha maji cha Sigareti pale Kata ya Ruaha ambapo kingeweza kusaidia Kata ya Ruaha na Rwembe, wameshafanya hivyo na kukuletea taarifa na imeonekana takribani shilingi bilioni mbili zinahitajika ili kuwezesha wananchi wa Ruaha waweze kupata mradi huo.
Je, Mheshimiwa Waziri unaweza kuwaahidi vipi wananchi wa Ruaha ambao sasa wanakutazama kwamba je, huu mradi utaingizwa katika Bajeti ya 2017/2018 ili uweze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi kwa ujumla?
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika ziara yake Naibu Waziri pale Wilayani Kilosa alitembelea bwawa la Kidete na alijionea jinsi ambavyo limekuwa likileta madhara makubwa ya mafuriko na kuharibu mpaka reli kwenye Wilaya yetu ya Kilosa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa hili la Kidete ambalo ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa? (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nisikitishwe sana na majibu haya ya Serikali ambayo wamekuwa wakiyajibu mara kwa mara, kiukweli yanakatisha sana tamaa. Kwa sasa huu utaratibu wa Serikali wanaosema ni kifuta jasho kwa wananchi ambao wanakuwa wameuliwa na tembo au mazao yameharibiwa kiukweli haina uhalisia na haileti haki kwa wananchi ambao wamekaa kwenye mazingira hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii yote inatokana na sheria ya wanyamapori ambayo imeonekana kuwa na usumbufu na upungufu mkubwa sana. Ni lini Serikali itaileta sheria hii hapa Bungeni ili iweze kubadilishwa ili iweze kwenda na uhalisiana kurudisha fidia na hili neno la kifuta jasho libadilishwe iwe fidia iliyokuwa imetathiminiwa kutokana na matatizo ambayo wamepata wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juzi kuamkia jana katika Kijiji cha Kikwaraza pale Mikumi ambapo Mbunge wa Mikumi anaishi, simba alivamia zizi la mfugaji anaitwa Agrey Raphael na kuua ng’ombe mmoja pamoja na kujeruhi ng’ombe wawili.Sasa hayo matatizo na changamoto kama hizi zimekuwa nyingi sana kule Mikumi kwenye Kata kama Mikumi, Luhembe, Kidodi, Kilangali, pamoja na maeneo ya Mhenda. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuelekea kule mikumi ili akasikilize changamoto nyingi za wananchi ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu kutokana na matatizo kama haya ya wanyamapori kabla hawajaamua kuchukua sheria zao mikononi kwa kutumia silaha za jadi? Ahsante. (Makofi) [Maneno haya siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's