Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Omary Tebweta Mgumba

Supplementary Questions
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini napata mashaka na majibu yake, kwa sababu hivyo vikao vyote vya ushauri vya DCC na RCC vimeshafanyika na nina uhakika kabisa Serikali hii ina taarifa ya maombi ya watu wa Morogoro Vijijini kuhamia kule Mvuha.
(a) Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba kwa sababu mchakato huu ulianza tangu mwaka 2009 wakati huo Mbunge akiwa Mheshimiwa Hamza Mwenegoha na Serikali hii imeshaleta shilingi milioni 500 kwa ajili ya maandalizi ya kuhamia Mvuha; hizo hela zimetumika kwa ajili ya udongo na kupima viwanja. Sasa leo Serikali inapokuja kusema haina taarifa, napata mshangao kidogo.
Mheshimiwa Spika, swali langu, sipendi kuidhalilisha Serikali yangu, namwomba Mheshimiwa Waziri arudi akatafute majibu sahihi ili aniletee kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Morogoro Vijijini.
(b) Ni lini Serikali italeta majibu hayo sahihi ili tuweze kuwapelekea watu wa Morogoro Vijijini?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, matatizo yaliyopo Nzega yanafanana kabisa na Halmashauri ya Morogoro hatuna high school hata moja katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia ambao ukizingatia juhudi za wananchi tumejitahidi tumejenga ile Sekondari ya Nelson Mandela. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea nguvu ili kuimalizie shule ile angalau Halmashauri hii iwe na shule hata moja ya sekondari?
MHE. OMAR T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yaliyoko Tabora Kaskazini ya kukosa soko la tumbaku na bei zake kushuka yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika jimbo langu la Morogoro Kusini Mashariki hususan katika zao la bei ya ufuta, ukizingatia kwa mfano mwaka jana bei ya ufuta ilifika mpaka shilingi 2500 mpaka 3000 lakini mwaka huu 1500, 1600 mpaka 2000. Na kwa kuwa mazao haya yanategemea soko la dunia na soko la dunia kila siku bei zinashuka kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi kwenye tumbaku na mazao mengine. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuwafidia wakulima kwa kutoa ruzuku hasa pale bei zinaposhuka katika soko la dunia ndogo kulinganisha na gharama za uzalishaji wa mazao hayo hususan ufuta katika vijiji vyangu na jimbo langu na Tanzania kwa ujumla?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la ufidiaji liko pia katika Jimbo langu la Morogoro Kusini hasa kwenye Kijiji cha Kivuma. Kuna mwekezaji amekuja pale ameanza kuchimba mawe bila kulipa fidia kwa wahusika. Je, nini kauli ya Serikali kwa mwekezaji huyu ambaye hajalipa fidia kwa wahusika wenye umiliki wa ardhi wa pale Kivuma?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazao mengi ya biashara tunategemea sana soko la nje ambalo lina ushindani mkubwa kuzingatia nchi nyingi zinalima mazao hayo na wakati mwingine wakulima wanalima kutokana na mazoea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kitengo cha Utafiti wa Masoko hayo ili kujua mahitaji halisi ya soko la dunia kuliko kama sasa ufuta umeshuka mpaka Sh.1,500 kutoka bei ya mwaka jana ya Sh. 3,000? Nataka kujua tu Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kitengo hicho cha Utafiti wa Masoko Ulimwenguni ili kutoa habari nchini kwa wakulima kulima mazao kutokana mahitaji ya soko badala ya kulima mazao kwa mazoea.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Sheria ya Mipango Miji Namba Nane ya Mwaka 2007 inasema mashamba ya kilimo na mifugo kwa mijini na mamlaka za miji yasizidi ukubwa wa heka tatu. Ukizingatia Ngerengere sasa hivi ni mamlaka ya mji mdogo na shamba lile lina ukubwa wa zaidi ya hekta 4,562 ambazo ni sawa na heka 10,036, ambapo ni kinyume na sheria hii namba nane ya mwaka 2007. Je, Serikali haioni uwepo wa shamba hili katika Mamlaka ya Mji wa Ngerengere inakiuka sheria hii namba Nane na ukizingatia Serikali inafuta mashamba mengi sasa hivi kwa kuzingatia shabaha hii kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri ya Morogoro ina ardhi kubwa nje ya Mamlaka ya Mji wa Ngerengere, je, Serikali iko tayari wakatupa ardhi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Ngerengere na Serikali tukawapa ardhi nyingine kwa ajili ya kuendeleza shamba la mifugo, kwa kuzingatia Sheria ile Namba Nane ili iwe nje ya hapo?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme kwenye huduma zingine za jamii kama vile zahanati, Vituo vya Polisi na Ofisi za Serikali ya Kijiji katika Kijiji hicho cha Lugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu matatizo yaliyopo Malinyi yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika Vijiji vya Luholole, Misala, Mmalazi, Kivuma, Ludewa na Amini kule kwenye Kata ya Kinole?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Mkoa wa Lindi yanafanana kabisa na yaliyopo katika Mkoa wa Morogoro kwenye Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hasa kwenye Kata za Maturi, Mkulazi, Seregeti na Tununguo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka minara katika kata hizi na Vijiji vyake vile vya Usungura, Kidunda na vinginevyo ili kuimarisha mawasiliano katika vijiji hivyo?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Mkoa wa Lindi yanafanana kabisa na yaliyopo katika Mkoa wa Morogoro kwenye Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki hasa kwenye Kata za Maturi, Mkulazi, Seregeti na Tununguo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka minara katika kata hizi na Vijiji vyake vile vya Usungura, Kidunda na vinginevyo ili kuimarisha mawasiliano katika vijiji hivyo?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, lakini swali langu la msingi lililenga mahsusi vyanzo vya maji vilivyopo katika
Mkoa wa Morogoro hususan katika Milima ya Uluguru katika Vijiji vya Tegetero, Kinole, Mgeta na

Hewe lakini majibu yamekuwa ya jumla mno. Sasa nataka
kujua katika pesa hizi zilizotengwa shilingi 2.1 bilioni kwa ajili ya utunzaji wa maji ni kiasi
gani kimetengwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro ambao ndiyo chanzo cha
Mto Ruvu ambao unategemewa kwa ajili ya maji ya Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na kadhalika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Mkoa wa Morogoro tuna Chuo cha cha Kilimo cha Sokoine
ambacho kina wataalam waliobobea katika masuala haya ya utunzaji wa mazingira hususan katika kilimo na wako tayari kutumika kama muda wote wanavyojitolea lakini tatizo ni uwezeshaji. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuwawezesha wataalam hawa ili washiriki katika utunzaji huu wa mazingira kwa weledi zaidi?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.Kwa kuwa matatizo yanayowakabili watu wa Kwera yanafanana kabisa na matatizo yanayotukabili watu wa Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Vijijini kwa ujumla, kuna Barabara ya Bingwa – Mkuyuni – Kisaki mpaka kuelekea Rufiji kule Mloka kuelekea Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara na pia kuelekea katika Mbuga ya Selous.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii iliahidiwa kuwekwa kiwango cha lami tangu Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Waziri wa Ujenzi aliyekuwa katika Serikali ya Awamu ya Nne ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; na kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshamalizika, je, Mheshimiwa Waziri, ni lini barabara hii itaanza kutengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuinua hali ya kiuchumi ya wananchi hawa? (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kuna mradi mwingine unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Mji Mdogo wa Malinyi unaosuasua toka mwaka 2013. Kwa sasa mabomba ya usambaji maji ya mradi huo yamekwama katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu ya tozo ya storage. Halmashauri tumeomba kuondolewa kwa tozo hiyo lakini mpaka sasa hatujafanikiwa. Je, Serikali inatusaidiaje katika ombi hilo ili kukamilisha mradi huu ili wananchi wapate maji safi na salama?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa matatizo ya maji yanayowakabili wananchi wa Malinyi yanafanana na matatizo yanayotukabili wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki; na kwa kuwa vijiji vya Mtego wa Simba na Newland vilikuwa ni vitongoji wakati wa mradi wa maji Fulwe - Mikese unafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2006; na kwa kuwa mradi huo sasa unatekelezwa tangu mwaka 2016 na vitongoji hivi viwili vya Newland na Mtego wa Simba sasa ni vijiji kamili.
Je, Serikali inavisaidiaje vijiji hivi vya Mtego wa Simbana Newland kupata maji safi na salama ukizingatia vilikuwa ni sehemu ya mradi huo?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serilkali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 368.5 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika vijiji vya Mkuyuni na Madam. Na kwa kuwa mwaka wa fedha 2016/2017 umebaki mwezi mmoja tu kumalizika, lakini mpaka sasa pesa hizi hazijafika; na kwa kuwa bajeti ya maji kwa ajili ya Morogoro imepunguzwa kutoka shilingi bilioni 4.2 ya mwaka jana mwaka huu imekuwa ni shilingi bilioni 1.5.
Je, Serikali inanipa commitment gani ya kuleta hela hizi shilingi milioni 368.5 kabla ya mwaka wa fedha uliobaki mwezi mmoja kuisha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika mpango wa muda wa kati, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kupeleka maji katika Vijiji vya Lolole, Madam, Mwalazi, Kibuko na kitongoji cha Misala katika Kijiji cha Mkuyuni. Na kwa kuwa huu mradi wenyewe kwamba…
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna mradi wa maji katika kijiji cha Kibwaya ambao unakamilika muda si mrefu, je, Serikali badala ya kutafuta chanzo kingine cha maji, kwa nini isiongeze pesa katika mradi huu ili kupeleka maji katika vijiji hivi ambavyo nimevitaja vya Lolole, Misala, Madam na Kibuko?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yanayowakabili wananchi wa Bagamoyo yanafanana kabisa na ya Morogoro Kusini Mashariki. Kwenye mipango ya Serikali ya REA awamu ya tatu, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tumepata vijiji saba tu na kuacha vijiji 47 kati ya vijiji 64 ambavyo vyote havina umeme katika Kata za Tegetero, Kibuko, Tomondo, Maturi, Mkulazi na Seregeti. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika huu mradi wa REA awamu ya tatu, katika Kata hizo na vijiji vyake vyote?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa gharamba za uzalishaji wa korosho za wabanguaji wa ndani wadogo na wakubwa ni kubwa pamoja na korosho yenyewe kuzalisha, na kwa kuwa wabanguaji wadogo na wakubwa wanashindanishwa kupata korosho kama malighafi katika mnada wa stakabadhi ghalani pamoja na wabanguaji kutoka nchi za nje kutoka India na Vietinam ambao wanapata ruzuku.
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwawezesha wabanguaji wadogo na wakubwa waliowekeza nchini, kupata korosho kama malighafi katika minada hapa nchini ili kutoa ajira na kuongeza thamani korosho zetu. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Matatizo yaliyopo katika Jimbo la Mufindi Kusini yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Tuna mradi wa maji katika vijiji vitano una miaka zaidi ya tisa. Serikali imejitahidi kujenga miundominu yote ya kuhifadhi na kusambaza maji kwa kutegemea chanzo cha Mto Ruvu katika mradi wa Chalinze III lakini mpaka leo maji hayatoki. Nataka kujua ni lini Vijiji hivi vitano vya Maseyu, Kinonko, Kidugalo, Ngerengere, Sinyaulime pamoja na kambi mbili zetu za Jeshi za Kizuka na Sangasanga vitapata maji?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na Sera nzuri ya Serikali ya CCM ya Elimu Bila Malipo imesababisha mwamko wa elimu na wanafunzi kufauli kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu wa madarasa zaidi ya vyumba 45 katika Jimbo langu. Je, Serikali imejipangaje katika kutatua tatizo hili la ujenzi wa vyumba 45 ukizingatia kipindi hiki wananchi wengi wako kwenye kilimo?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kama Serikali ilivyosema katika jibu lake la msingi kwamba kuna vijiji saba ambavyo umeniongeza kwa hiyo, je, nataka kuvijua vijiji hivi saba ni vipi na ni lini vitaanza kupatiwa umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, katika Kata ya Mkulazi kuna miradi miwili nya kielelezo inayofanyiwa kazi sasahivi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Kiwanda cha Mkulazi cha Sukari pia na ujenzi wa Bwawa la Kidunda, je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika kata hii yenye vijiji vinne na Kijiji cha Kwaba, ambavyo ni vijiji vya Kwaba, Kidunda pamoja na Usungura?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkoa wa Morogoro wenye Wilaya saba na Halmashauri tisa ina Hospitali za Wilaya mbili tu ambazo ni Ulanga na Kilosa. Kwa kuwa katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Morogoro hususani katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini katika Kata ya Mvuha.
Je, ni lini Serikali italeta hizi shilingi milioni 500 ili tuanze ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Mvuha?
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tulipata vijiji 17 kati ya vijiji 64 katika miradi ya umeme ya REA Awamu ya Kwanza na REA Awamu ya Pili, na kwa kuwa katika awamu zote hizo utekelezaji wake wa miradi hiyo kuna taasisi za umma kama vile shule, zahanati, vituo vya afya na nyumba za ibada na vijiji na vitongoji vingi kwa mfano, Kijiji cha Tomondwe, Mfumbwe, vitongoji vya Misala vilirukwa.
Je, Serikali huu mradi wa densification utafika lini Morogoro hususan katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili vijiji na vitongoji hivi vilivyorukwa vipatiwe umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na majibu hayo nataka niweke kumbukumbu sawa. Swali kama hili niliuliza katika Bunge lililopita katika swali la nyongeza na swali la msingi Bunge lingine lililopita. Serikali ilinipa majibu katika jimbo langu wamenipa vijiji 20 na si 14; mpaka sasa hivi huyo mkandarasi ameshafika na amefanya survey ya vijiji vyote 20. Hata hivyo kwa kuwa amefanya vijiji saba amepata mkataba wa kufanya survey pamoja na kujenga miundombinu ya umeme. Lakini vijiji 13 ameambiwa tu afanye survey ukizingatia ndani ya vijiji hivyo ndiko kunakojengwa kiwanda kikubwa cha sukari ambacho kitaanza ujenzi mwaka huu pamoja na Bwawa la Kidunda.
Je, Serikali imejipanga vipi ili kumalizia na ujenzi katika vijiji hivi 13 na vijiji vile vingine vya Tomondo na sehemu zingine? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's