Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Azza Hilal Hamad

Supplementary Questions
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu wa kisima kirefu cha maji Mji Mdogo wa Tinde gharama yake halisi iliyotolewa na SHIWASA ilikuwa ni milioni 400 na mpaka sasa hivi Serikali imeshatoa milioni 300 kwa awamu.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kutoa milioni 100 ili kukamilisha mradi huo?

Swali la pili, mradi huu wa maji, unategemewa kuhudumia zaidi ya watu 10,000 katika Mji mdogo wa Tinde. Vituo vilivyowekwa vya kuchotea maji havitoshelezi kabisa ukilinganisha na idadi iliyopo.

Je, Serikali haioni kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza vituo vya kuchotea maji ili wananchi waweze kuchota maji hayo bila bugudha?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo ya Busokelo yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, na kwa kuwa, wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini tumeanzisha kwa nguvu zetu wenyewe ujenzi wa Hospitali ya Wilaya toka mwaka 2007, na mapato ya Halmashauri ni kidogo, Halmashauri imekuwa ikijenga kidogo kidogo kwa kushirikiana na wananchi wake, lakini ukamilishaji wa hospitali hii umekuwa ni mgumu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuipa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ombi maalum la fedha ilizoomba kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hii?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu yake lakini nitumie fursa hii kumpa pole kwa ajali aliyoipata jana, hakika Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya gharama zake ni kubwa sana na kwa kutegemea bajeti ya Halmashauri inaonesha wazi Hospitali hii haitakamilika kwa wakati. Toka ujenzi huu umeanza ni takribani miaka saba leo na Hospitali haijaanza kufanya kazi. Je, ni lini Serikali itaipa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ombi la fedha maalum kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hii?
Swali la pili, kwa kuwa Naibu Waziri amefika Shinyanga na akajionea hal halisi ya matatizo ya huduma ya afya na katika Mkoa mzima wa Shinyanga ni Wilaya moja tu ambayo inatoa huduma za Hospitali ya Wilaya, je, ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba inausaidia Mkoa wa Shinyanga na kuhakikisha Hospital ya Wilaya ya Shinyanga na Hospitali ya Wilaya ya Kishapu zinapewa kipaumbele kwa kuanza kutoa huduma kwa majengo yaliyokamilika na kuwapa watumishi?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Tatizo la Benki ya Wanawake limekuwa ni kubwa katika mikoa yote, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni kwanini Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto isikae na kukubaliana na benki ambazo zinapatikana kwa kila mkoa kama NMB, CRDB na NBC ili waweze kuweka angalau dirisha moja kwa kila mkoa kuweza kutoa huduma hizi?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na
majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji nina maswali
mawili ya nyongeza. Naibu Waziri amekiri miradi hii imechukua muda mrefu
kutoka 2012 mpaka leo hii haijakamilika; Je, Wizara haioni sasa ni muda muafaka
wanapokuwa wamepelekewa certificate waweze kulipa malipo haya kwa
muda muafaka kwa sababu wanawachelewesha wakandarasi. (Makofi)
Swali la pili; miradi hii imechukua muda mrefu sana mpaka muda huu
imefikia asilimia 70 ya utekelezaji. Mheshimiwa Naibu Waziri haoni ni muda
muafaka sasa wa kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hii?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kijiji cha Ishololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kilitengewa fedha kwa ajili ya Mradi wa Umwagiliaji, zaidi ya shilingi bilioni moja. Mradi huu haujaweza kukamilika na Mkandarasi kuweza kuondolewa na Serikali kwa sababu, mradi huu haukuisha kwa wakati. Je, Mheshimiwa Waziri, uko tayari sasa kuja katika Kijiji cha Ishololo na kuona mashimo tuliyoachiwa na mkandarasi yule na mradi huu kuwa hauna tija kwa wananchi wetu?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Awali ya yote nianze kuishukuru sana Serikali kwa sababu, swali hili leo ni mara ya nne naliuliza ndani ya Bunge lako.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaendelea katika Kituo cha Wazee cha Kolandoto. Natumia fursa hii kuishukuru sana na kuipongeza Serikali kwa kazi ambayo wanaifanya, wamesikia kilio cha wananchi na wazee wa Kolandoto.
Mheshimiwa Spika, naomba nimwulize Naibu Waziri swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, jengo hili linaonekana litapendeza sana baada ya kukamilika. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha wanawapelekea wazee hawa vitanda na magodoro ili waweze kuishi kwa raha mustarehe?
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikuliza swali hili toka nilivyoingia ndani ya ukumbi huu mwaka 2010. Ujenzi wa hospitali hii umeanza toka mwaka 2007 mpaka hivi tunavyoongea fedha inayoonekana hapo ndiyo ambayo imeshafika katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, lakini wakati nauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nipongeze Serikali kwa hatua kubwa ambayo wameamua kuchukua katika uboreshaji wa vituo vya afya kikiwemo Kituo cha Afya cha Tinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali inawaahidi nini wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuhusu ukamilishwaji wa ujenzi huu kwa kuwa umekuwa ni wa muda mrefu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, Serikali imeweka mpango gani madhubuti ili kuhakikisha kwamba pindi ujenzi huu wa vituo vya afya unapokuwa umekamilika unaweza kupata wataalam wa kutosha katika majengo yetu ya upasuaji na huduma zingine zinazostahili? Nakushukuru. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amejibu lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kituo hiki cha Buhangija kimekuwa na msongamano kutokana na wimbi kubwa la mauaji ya Albino na kukifanya kituo hiki kuwa na watoto wengi zaidi na hatimaye watoto wale kuweza kuishi pale shuleni. Je, ni lini Serikali itakiangalia kituo hiki na kukipelekea fedha ya kutosha ili kiondokane na tatizo kubwa la chakula linalokuwa linakikumba kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha kwa ajili ya watoto wasioona, wasiosikia na wasiosema? Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's