Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Abdallah Dadi Chikota

Supplementary Questions
MHE.ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 20 ni fedha ndogo sana inayopelekwa kijijini na kama wataamua kumlipa Mwenyekiti wa Kijiji, Serikali ya Kijiji haitafanya kitu chochote kingine. Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kubeba jukumu hili la kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji?
Swali langu la pili, kutokana na umuhimu sasa wa kundi hili na malalamiko yaliyopo kila kona nchini Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kutoa waraka maalum ambao utatoa maelekezo kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhusu malipo ya Wenyeviti hawa na kuweka kiwango cha chini cha posho hiyo, badala ya kila Halmashauri kutekeleza jinsi wanavyoona wao inafaa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Swali langu la nyongeza namba moja, ni kwa nini sasa kwa kuwa, kila kitu kimekamilika na mchakato wa manunuzi umekamilika na barabara hii ni muhimu kwa usafirishaji wa korosho, ujenzi wa barabara hii usianze mara moja badala ya kusubiri mwaka wa fedha 2016/2017, hii maana yake tutaanza Julai na wakati wananchi wanasubiri ujenzi huu uanze mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba Naibu Waziri atupe Kauli ya Serikali kuhusu kilometa 160 zilizobaki, kwa sababu barabara hii ina kilometa 210 na amesema ujenzi utaanza kwa kilometa 50. Naomba majibu?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la usambazaji wa maji linalokabili mradi wa Mbwinji, Nachingwea, linafanana na tatizo la usambazaji wa maji wa mradi wa Makonde hususan chanzo cha maji Mitema. Kwa hiyo, nataka niulize, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati mkubwa ili Miji inayonufaika na mradi ule; Nanyamba, Kitangari na Tandahimba wapate maji ya kutosha.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Mchinga linafanana sana na tatizo la Halmashauri ya Tandahimba iliyopo Mkoani Mtwara, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kugawanya Halmashauri ya Tandahimba ili kuwe na Halmashauri mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, Wilaya ya Mtwara sasa hivi ina Halmashauri tatu, Mtwara Manispaa, Halmashauri ya Mtwara na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, je, Serikali ina mpango gani kumpunguzia mzigo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, ili kuanzisha Wilaya mpya ya Nanyamba?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mamlaka za Maji Mijini ndiyo vyombo vyenye dhamana ya kuhakikisha upatikanaji wa maji mijini na kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imeanzishwa kisheria mwaka 2015, je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha uundwaji wa Bodi ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Nanyamba ili kuhakikisha maji katika Mji wa Nanyamba yapatikana kwa kirahisi?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
16
Kwa kuwa hapo awali Serikali ilikuwa na chombo ambacho kinadhibiti education materials yaani EMAC na kwa kuwa ilivunjwa rasmi huko nyuma na kutamka kwamba wataunda chombo kingine kwa ajili ya kudhibiti vifaa vinavyoingia katika mfumo wa elimu pamoja na vitabu.
Je, Serikali inaukakasi gani wa kuunda chombo hicho maana mpaka leo hakijaundwa bado?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa elimu kwa wakati wa Mtwara na Lindi ili wapate uelewa juu ya mradi huu?
Lakini pili, waweze kujiandaa kutumia fursa zitakazopatikana baada ya ujenzi wa kiwanda hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili, maeneo ambayo yalianishwa na mradi huu ni mawili, eneo la kwanza ni kwa ajili ya ujenzi wa kile kiwanda cha LNG, eneo la pili ni industrial park kwa ajili ya viwanda vingine ambavyo vitajengwa hapo baadaye.
Sasa nataka nijue hatua iliyofikia katika kutwaa eneo hili ambalo litajegwa viwanda vingine yaani eneo la industrial park kwamba je, wananchi wameshafidiwa au bado hawajafidiwa hadi sasa? (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba miundombinu ya kiwanja cha ndege ni pamoja na barabara inayoingia uwanjani na barabara hii sasa imechakaa. Sasa nataka kuuliza kwamba Serikali ina mpango gani wa ukarabati wa barabara inayoingia uwanja wa ndege wa Mtwara kutoka Magomeni Mjini Mtwara hadi uwanja wa ndege?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amesema kwamba kuna master plan ambayo inaandaliwa; sasa nilitaka kuuliza kwamba kwa kuwa Serikali ina mpango gani wa kutwaa eneo la ardhi kwa sababu sehemu kubwa ya uwanja huo wa ndege imepakana na eneo la Jeshi; sasa kwa vyovyote vile watahitaji eneo la kijiji cha Naliendele; wamejiandaaje kutwaa eneo hili ili kuepusha migogoro ya wananchi wa Naliendele hapo baadaye?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kipo! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa Mfuko wa Mawasiliano umenufaisha Kata chache sana katika Jimbo la Nanyamba; je, Serikali ipo tayari sasa kuingiza Kata ya Nyuundo na Kata nyingine ambazo hazina mawasiliano katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 badala ya kutuambia siku za usoni ambazo hatujui itakuwa ni lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kuna Makampuni ya Simu yamefunga minara katika baadhi ya kata zetu lakini upatikanaji wa mitandao bado ni hafifu kama vile Kata ya Njengwa na Milangominne.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari sasa kuyaagiza sasa makampuni hayo kutuma wataalamu ili wakaangalie matatizo ya minara hiyo?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kuhusu uboreshaji wa elimu lazima tuzingatie mafunzo kazini kwa walimu. Sasa nataka niulize, Wizara ina mpango gani wa kufufua Vituo vya Walimu ambavyo vilianzishwa huko nyuma chini ya Mpango wa Kuboresha Elimu Ngazi ya Wilaya (District Based Support to Education(DBSPE) ambavyo kwa sasa hivi havitumiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili morale kwa Walimu ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba, dhana hii ya elimu bure inafanikiwa. Kwa hiyo, sasa nataka kujua kwamba, Serikali ina mpango gani kuhakikisha madeni kwa Walimu hayajirudii pamoja na kwamba, tupo kwenye sera ya kubana matumizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu ya maswali haya ya nyongeza.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali la nyongeza, kwa kuwa, hali ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango, FDC inafanana na kile cha Mtawanya, kilichopo Mkoani Mtwara, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha miundombinu ya chuo hicho lakini pia kuboresha utoaji wa taaluma katika Chuo hicho cha Maendeleo ya Wananchi Mkoani Mtwara?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwaa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la vyoo katika shule zetu za msingi linafanana na tatizo la nyumba za Walimu kwa shule zetu na tatizo hili sasa hivi kama limeachiwa Halmashauri ndiyo watatue tatizo hili, lakini kwa mapato ya Halmashauri nina uhakika mkubwa kwamba tatizo hilo haliwezi kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Naibu Waziri kwamba Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hili katika kipindi kifupi kijacho?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama alivyosema kwenye jibu lake la msingi kwamba kituo hiki kinafanya tafiti mbalimbali lakini wanashindwa kuhaulisha yale maarifa wanayopata kwenye tafiti zao kwa wakulima kwa sababu hawana fedha za kutosha za kuweza kwenda kwa wakulima Mtwara, Lindi na Pwani na kuwapa matokeo mapya ya utafiti. Serikali ina mpango gani wa kukiongezea fedha kituo hiki ili waweze kuwafikia wakulima wengi wa korosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kiuatilifu muhimu katika uzalishaji wa zao la korosho ni sulfur dust. Napenda kujua mpango wa muda mfupi wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inawashawishi wawekezaji wakubwa waje kujenga kiwanda cha kutengeneza sulfur Mikoa ya Lindi na Mtwara ili sulfur hiyo iuzwe kwa bei ya chini kama ilivyo sasa hivi kwa viwanda vya mbolea badala ya kuagiza sulfur hii kwa fedha nyingi za kigeni kutoka nchi za nje?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mosi, kuhusu Mradi wa Kitere pamoja kwamba majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanasema mradi umekamilika, lakini mradi huo umekamilika lakini haufanyi kazi kama unavyotakiwa na mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri shahidi amepita pale na hakuona hizi ekari 3,000 zimelimwa.
Kwa hiyo, naomba kauli ya Serikali kwamba, kuna mkakati gani wa kukamilisha mapungufu yaliyopo ili mradi huo sasa uweze kufanya kazi pasavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kupitia Ofisi za Umwagiliaji Kanda, kuna miradi mingi hapa nchini ambayo haifanyi kazi. Juzi Kamati yetu ya LAAC ilikuwa Tabora, kuna mradi haufanyi kazi, kuna mradi Liwale, kuna mradi Mkuranga na miradi mingine. Sasa Serikali ina kauli gani kuhusu ushauri unaotolewa na ofisi hizi za umwagiliaji kanda ambazo miradi mingi ambayo inabuniwa na ofisi hizi huwa haifanyi kazi ipasavyo?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri
ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Ni wazi kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mfumo huu una upungufu na una changamoto nyingi ambazo nimeelezea mojawapo. Sasa nataka commitment ya Serikali kwamba hiyo Version 11 itaanza kutumika lini? Swali langu la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; changamoto nyingine ya mfumo huu ni kwamba, unasimama peke yake (stand
alone system) na wakati ukiangalia kwenye taasisi zetu, kwa mfano Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kuna mifumo mingi, tulitegemea kwamba mifumo hii ingekuwa inaongea; kuna EPICA, kuna LGMD, sasa je, Mheshimiwa Waziri atanihakikishia kwamba mfumo huu mpya Lawson Version 11 utakuwa unaongea na mifumo mingine?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Matatizo ya Mawasiliano ambayo yanalikabili Jimbo la Kilwa Kaskazini yanafanana na yale ya Jimbo la Nanyamba kwa sababu kuna kata za Njengwa, Nyundo, Nitekela na Kiyanga ambayo hayana mawasilinao. Na nilishawahi kuuliza swali hili hapa Bungeni nikaambiwa kwamba Mfuko wa Mawasiliano utapeleka mawasiliano huku na mradi huo bado mpaka sasa hivi haujatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipate majibu ya Serikali kuhusu miradi hii?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa suala la udhibiti wa elimu huwezi kutofautisha na udhibiti wa vitabu vinavyoingia kwenye mfumo wa elimu na kwa kuwa imeonekana wazi kwamba taasisi ya elimu ambayo imepewa jukumu la kuthibiti ubora wa vitabu vinavyoingia kwenye mfumo wa elimu imeonekana kuna dosari kubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha chombo cha ithibati kama ilivyokuwa EMAC huko nyuma ili kudhibiti vitabu vinavyoingia katika mifumo yetu ya elimu na kuacha madudu yanayoendelea sasa hivi?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Changamoto ya huduma ya afya iliyopo Kigamboni na Ubungo inafanana na ile iliyopo Jimbo la Nanyamba ambako hakuna kituo cha afya hata kimoja, hakuna hospitali ya wilaya, hakuna ambulance na hakuna DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya). Sasa nataka kujua Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kutatua changamoto hizi?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa wananchi wa Majimbo ya Mtama, Newala Vijijini na Newala Mjini kwa ajili ya usafirishaji wa korosho, choroko na mihogo. Je, ni lini sasa Serikali itaanza maandalizi haya ya ujenzi kwa kiwango cha lami, yaani kwa kufanya feasibility study? Watuambie ni lini wataanza sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; naipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala na Masasi. Hata hivyo, barabara hii ni kilometa 210, lakini ujenzi ambao umeanza ni kilometa 50 tu, wananchi wa Nanyamba, Tandahimba na Mtwara wanataka kusikia Serikali ina kauli gani kuhusu kilometa 160 zilizobaki?
MHE ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa shahidi kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria kwa sababu kuna watendaji wengi wa hizo AMCOS ambao hawana sifa zilizotajwa kisheria. Kwa hiyo, napenda kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu AMCOS ambazo zimeajiri watendaji ambao hawana sifa?
Mheshimiwa Spika, pili, kutokana na kazi kubwa ambazo wanazifanya watendaji hawa wa AMCOS hasa wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi ambao sasa hivi wanashughulikia zao la korosho na wanashughulika na fedha nyingi sana, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo kwa kuandaa mafunzo maalum ili kupunguza ubadhirifu na upotevu wa pesa ambao siyo wa lazima? (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa pembejeo za ruzuku hazitoshelezi mahitaji yote ya zao la korosho, Serikali inampango gani sasa zile pembejeo zingine ambazo mkulima atahitaji azipate sokoni kuagiza kwa pamoja (bulk purchase) kama itakavyofanya mbolea katika msimu huu kwa mwaka 2017/2018?
Swali la pili, ni ukweli usiopingika kwamba korosho mwaka huu imeingiza fedha nyingi sana za kigeni ni zao ambalo linaongoza, je, Benki ya Maendeleo ya Wakulima Tanzania ni lini itafungua tawi Mkoani Mtwara ili iweze kuwahudumia wakulima wa korosho wa Mikoa ya Mtwara na Lindi. Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa upungufu huo wa Maafisa Ugani ni mkubwa sana kwenye Halmashauri ambazo zimeanzishwa hivi karibuni, kama Halmashauri ya Mji wa Nanyamba; je, Serikali ina mpango gani wa upendeleo kwa mamlaka hizi mpya za Serikali za Mitaa ambazo zimeanzishwa hivi karibuni?
Swali langu la pili, ukiangalia takwimu za ajira zilizotolewa hivi karibuni kwa Maafisa Ugani, na kwa kuwa nchi yetu ina takribani vijiji zaidi ya 12,000 utaona kwamba kuna vijiji vingi sana vinakosa Maafisa Ugani.
Je, Serikali ina mpango gani au mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba kila kijiji katika nchi yetu kinakuwa na Afisa Ugani ili kuleta mapinduzi ya kweli katika kilimo?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hatua inayochukua katika kusimika mifumo mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kurahisisha uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pamoja na pongezi hizo, nampongeza vilevile Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, changamoto kubwa katika utumiaji wa mifumo hii ni upatikanaji wa wataalam wa TEHAMA katika Mamlaka za Serikali zetu za Mitaa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri wataalam wa kutosha wa TEHAMA hasa katika halmashauri mpya ambazo zimeanza hivi karibuni kama Nanyamba na Halmashauri ya Mji wa Newala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba kwenye Mfumo wa EPICOR kuna changamoto nyingine ambayo inapatikana hususan wakati wa kutayarisha final account katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kiasi kwamba wataalam hulazimika kutafuta taarifa nyingine nje ya mfumo. Je, Serikali ina mpango gani wa ku--repair changamoto hii ili tunapoandaa hesabu za mwisho kwa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa wataalam wategemee taarifa za kwenye system tu na si kuchukua nyingine kutoka nje?
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya matibabu kwa magonjwa ya UKIMWI na TB yanafanana sana na magonjwa ambayo yameibuka siku hizi, yale ambayo yanatokana na mtindo wa maisha hususani kisukari na shinikizo la juu la damu. Nataka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwenye dawa za magonjwa hayo kwa sababu mgonjwa akishapata ugonjwa huo ataendelea kutumia dawa hizo mpaka mwisho wa maisha yake. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku au kutoa bure kabisa dawa za magonjwa hayo? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo la Nanyamba kuna kata saba ambazo hakuna mawasiliano ya uhakika ya simu, Kata ya Hinju, Nitekela, Nyundo, Mnima, Kitaya, Kilomba na Kianga. Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea mawasiliano ya simu wananchi wa maeneo hayo? (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kila tunapouliza kuhusu ukarabati mkubwa wa Mradi wa Makonde tunaambiwa kwamba kuna dola za Kimarekani milioni 84 ambazo ni za mkopo kutoka Serikali ya India, lakini kila siku tunaambiwa majadiliano yanaendelea. Sasa nilitaka nipate commitment ya Serikali, majadiliano hayo yataisha lini na mkataba utasainiwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mradi huu wa Makonde unahusisha Halmashauri nne; Newala Vijijini, Newala Mjini, Tandahimba na Nanyamba, lakini majibu ya Naibu Waziri yanazungumzia Halmashauri tatu tu. Sasa nilitaka nipate maelezo ya Serikali kuhusu mpango wa Serikali kutoa maji Mitema na kupeleka Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameonesha kwamba huduma hizi sasa zinaanza kutolewa kuanzia Hospitali ya Wilaya, na ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wetu wengi wapo vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha huduma hizi katika vituo vya afya ili kupunguza adha ya wananchi wetu kutembea kwenda Hospitali ya Wilaya?
Swali la pili, miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na kisukari, hivi sasa kuna ujenzi unaoendelea wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kule Mtwara, amesema kwamba hospitali za rufaa za kanda zitatoa vilevile huduma hii katika ngazi ya kanda.
Je, Serikali imejiandaaje sasa itakapofunguliwa Hospitali ya Kanda ya Kusini ambayo inajengwa Mtwara, kwamba huduma ya saratani pia itatolewa katika hospitali hiyo ili kuwapunguzia adha Wanamtwara kwenda Hospitali ya Ocean Road iliyopo Dar es Salaam? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Makame Kassim Makame

Mwera (CCM)

Contributions (1)

Profile

View All MP's