Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Supplementary Questions
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Licha ya hivyo, nina maswali mawili madogo.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kuona umeanzishwa Mfuko wa Dhamana wa kuwasaidia akina mama hawa kupata mikopo. Kwa upande mwingine kuna mabenki mengine pamoja na taasisi ambazo bado wanatoa mikopo, lakini yenye riba kubwa.
Je, kwa upande wa Serikali kuna mikakati gani ya kushauri hizi taasisi na mabenki kutoa riba ndogo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa upande wa masoko ya uhakika, kwa upande wa Morogoro, kulikuwepo kiwanda cha matunda kinachotengeneza juice, lakini mpaka sasa hivi hakifanyi kazi. Je, kuna mkakati gani wa Serikali kushauri hiki kiwanda kiweze kufanya kazi au kuwezesha wawezeshaji waweze kujenga kiwanda Mkoani Morogoro kuwasaidia wanawake wanaolima matunda na wananchi wa Mkoa wa Morogoro kupata soko la uhakika pamoja na wajasiriamali? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, licha ya kuongeza ujazo wa mita za maji katika Manispaa ya Morogoro bado kuna sehemu za Lukobe, Kihonda, Kilakala, Folkland, SUA, Mbuyuni na sehemu zingine ambazo hawapati maji. Je, kwa nini hawapati maji wakati wote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Manispaa ya Morogoro inakua na watu wanaongezeka. Licha ya mradi wa Milenia wa Halmashauri ambao umepita, je, kuna mkakati gani wa kubuni mradi mwingine wa maji kusudi maji yaweze kutosheleza Manispaa ya Morogoro?
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara kwa mara umekuwepo usumbufu wa walimu wa awali kupata mishahara yao kwa wakati.
Je, kuna mkakati gani wa kuwapatia mishahara yao kwa wakati?
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Licha ya kupata majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mkoa wa Morogoro hauna hata hicho kituo cha kutolea mikopo na mafunzo ya ujasiriamali, je, kuna mikakati gani ya kuanzisha kituo hicho kwenye Mkoa wa Morogoro?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, kituo hicho kitaanzishwa lini? Ahsante
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Barabara ya Bigwa – Kisaki, Wilaya ya Morogoro Vijijini ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Awamu ya Tano kujengwa kwa lami. Mpaka sasa hivi hata kwenye bajeti iliyopita sikuona kitu chochote kinachoelezea kuwa itajengwa. Je, barabara hii kwa niaba ya wananchi wa Morogoro Vijijini itajegwa lini kwa kiwango cha lami? Ahsante
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hospitali ya Tumbi ni hospitali ambayo ilikuwepo tangu enzi za Nordic countries, wakati huo ikiwa chini ya Nordic countries kama chini ya shirika. Ilikuwa inatoa huduma nzuri sana, lakini mpaka sasa hivi huduma yao imefifia, je, Serikali ina mpango gani wa kufuatilia huduma za Hospitali ya Tumbi ambayo inatolewa kwa wananchi?
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mradi wa maji ni tatizo kweli, katika Wilaya ya Morogoro Vijijini, katika vijiji vya Furwe, Mikese, Gwata waliahidiwa mradi wa maji kwa muda wa miaka mingi, na wananchi wanateseka kwa maji kwa muda mrefu. Je, naomba kuuliza wananchi hawa ambao wameteseka kwa muda na wameahidiwa mradi wa maji watapata lini maji na mradi huu utatekelezwa lini?
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru sana kwa majibu ya Naibu Waziri kwa swali la msingi, lakini ningependa kuuliza kuwa kwa sababu Morogoro Vijijini hatuna mpaka sasa hivi Hospitali ya Wilaya na majibu yametolewa, naomba kuulizia je, inawezekana pia kuboresha Kituo cha Afya cha Dutumi ambacho mpaka sasa hivi na chenyewe kinatumika kwa kutupatia vitendea kazi? Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Wananchi wa Tarafa ya Mikese, Wilayani Morogoro Vijijini, wameahidiwa muda mrefu mradi wa maji, lakini mpaka sasa wanapata taabu sana kwa kupata maji.
Je, ni lini wananchi wa Mikese watapata maji kusudi waondokane na tatizo hilo?
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri na Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya ngongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 75 ya wakulima hapa Tanzania wakiwemo wakulima wa Mkoa wa Morogoro wanategemea kilimo kwenye uchumi wao. Serikali ina mkakati mzuri wa kupunguza bei kwenye mbolea kusudi iweze kuwa nafuu kwa wakulima. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha viwanda vya mbolea hapa nchini sambamba na Kiwanda cha Minjingu na Kiwanda cha Mtwara kinachotegea kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mbolea hasa ya DAP pamoja na UREA ni mbolea ambayo zinatumika sana kwenye kilimo chetu, DAP ikiwa ni mbolea ya kupandia na UREA ikiwa ni mbolea ya kukuzia. Hapa nchini tuna mbolea ya Minjingu ambayo inazalishwa Manyara.
Je, mbona haijawekwa kwenye mkakati huu kusudi wananchi waweze kupata hamasa ya kutumia mbolea ya Minjingu? Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ni mpango wa Serikali kuanzisha Vyuo vya VETA katika kila Wilaya: Je, kuna mkakati gani wa kuanzisha mkondo wa kilimo na uvuvi katika kila Chuo cha VETA kinachoanzishwa kwenye Wilaya zetu ili kuongeza Maafisa Ugani hawa wa kilimo na uvuvi ambao wanaweza kufanya kazi kwenye vijiji vyetu na kuinua kilimo chetu na uvuvi?
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Manispaa ya Morogoro kumekuwa na tatizo kubwa la maji hasa kwenye mitaa kama mitaa ya Mlima Kola, Lukobe, Foko land, Manyuki na mitaa mingine na kwa kuwa Serikali inafanya vizuri; naishukuru Serikali ya Ufaransa na ya Tanzania kwa kupata fedha hizo Euro milioni 70; lakini napenda kujua mradi huo ni lini utakamilika ili wananchi ambao wamepata matatizo ya maji kwa muda mrefu wapate subira ya kupata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pli, miradi ya maji katika Mji Mdogo wa Mikumi imechukua muda mrefu kiasi wananchi wa Mji wa Mikumi wana matatizo makubwa ya maji. Je, ni lini miradi hii itakamilika kusudi na wananchi waweze kupata maji safi na salama ya kutosha? Ahsante.(Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo lakini nina maswali mawili mafupi. Swali la kwanza, kuwa wakulima wengi sasa hivi wamechangamkia kilimo cha miembe na kwa kuwa Serikali imetoa mwongozo wa mafunzo kwa Maafisa Kilimo 117 tu; na kwa kuwa ni vikundi 19 tu vimepewa mafunzo; je, Serikali haioni haja kuweka mpango wa kutoa mafunzo zaidi ya maafisa kilimo ili kuweza kueneza kilimo hiki cha miembe ambacho kimechangamkiwa sana na wananchi sasa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa imeanza utafiti, naipa pongezi na kwa kuwa mpaka sasa hivi Serikali imetoa starter kit kwa kikundi cha wakulima ambacho kinalima maembe tu. Hiki kikundi cha wakulima sana kimejikita Mkoa wa Pwani ambapo Mikoa ya Morogoro, Tanga mpaka Zanzibar, Tabora wanalima maembe na kwa kuwa ni lita 560 tu za kivutia wadudu zimetolewa tu. Je Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kutoa starter kit angalau moja kwa mikoa hii inayolima miembe na kuongeza hii dawa ya kivutia wadudu kwa mikoa hii ili wakulima waweze kuendelea na kilimo hiki cha miembe?
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nawapa hongera sana vijana wangu wa SUA na wajasiriamali na Chuo cha SUA ambao wanaeneza miche ya miembe, hongereni sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa ni sera na mpango wa Serikali kila wilaya kuwa na hospitali, je, ni lini ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini utaanza licha ya jitihada nyingi za Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero utakamilika?
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, licha ya elimu kutolewa lakini bado kuna matatizo kuhusu haki ya ardhi. Sasa Serikali inaonaje kutoa kipindi maalum, narudia, kipindi maalum kwa muda muafaka kwenye luninga au kwenye redio kusudi elimu hii iwafikie hasa wanawake kwa wakati muafaka na kwa muda muafaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi inatumiwa sana na wanawake; kama asilimia 70 wanawake wanatumia hii ardhi hasa kwa uzalishaji mali hasa kwa kilimo. Hata hivyo wanawake hawa hawana maamuzi kuhusu ardhi hii. Je, Serikali inatoa kauli gani hasa ya kueneza elimu hii na kutokana na kwamba kwenye makabila mengine bado kuna mfumo dume ambao hauwapi ridhaa wanawake kumiliki ardhi? ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's