Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Supplementary Questions
MHE. CAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutambua tatizo la maji Mradi wa Maji wa Makonde na kutenga fedha za kutosha kutokana na mkopo uliopatikana kutoka Serikali ya India. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza; kitakachoondoa tatizo la maji Mradi wa Maji Makonde ni utekelezaji wa huu mradi mkubwa wa fedha ambazo tumepata mkopo kutoka India. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini utekelezaji utaanza wa huo mradi mkubwa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, jirani na chanzo cha maji Mitema kama alivyosema Mheshimiwa Waziri ambako kuna maji ya kutosha, kuna mji mdogo wa Kitangari na watu wengi, pana Kituo cha Afya, Chuo cha Ualimu, sekondari mbili, watu wengi sana pale, soko kubwa lakini Mji ule ambao uko kama kilometa tatu tu kutoka chanzo cha maji hawapati maji. Maji yanafika Tandahimba, yanafika Mtwara Vijijini, pale kwenye chanzo cha maji hawapati maji. Je, Serikali inajua tatizo hili na kama inajua tatizo hili inawaahidi nini wananchi wa Mji Mdogo wa Kitangari?
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni taratibu dunia nzima katika mfumo wa vyama vingi Ilani ya Chama kilichoshinda uchaguzi ndiyo inayotekelezwa. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba elimu hiyo au uelewa huo unawafikiwa viongozi wa vyama vyote vilivyosajiliwa katika nchi hii?
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kushukuru majibu mazuri ya Serikali, lakini pia napenda nishukuru ushirikiano tulioupata kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege; kama walivyosema, walifika Newala na wameelekeza kiwanja kikaeje na wametueleza ukubwa wa eneo linalohitajika. Nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa kuwa taratibu za Kimataifa zinataka kabla hatujahamisha uwanja ule wa ndege, ule uwanja wa mwanzo ufutwe; na kwa kuwa Halmashauri imeandikiana sana na Wizara na viwanja vya ndege kutaka kufuta ule uwanja wa zamani, jambo ambalo halijafanyika mpaka sasa. Je, Serikali inaweza kutuhakikishia kwamba kazi ya kufuta ule uwanja itafanyika mara moja?
Swali la pili, kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ametupa majukumu Halmashauri ya Mji kufanya tathmini ili eneo lile liweze kutwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kazi ambayo tutakwenda kuisimamia mara baada ya kutoka hapo. Je, Halmashauri ya Mji ikishamaliza suala la tathmini na kwa kuwa viwanja vya ndege ni mali ya Serikali Kuu, siyo mali ya Halmashauri, Serikali itakuwa tayari kuwafidia wale wananchi wachache ambao walikuwa wanalima pale kwa kuzingatia kwamba gharama hazitakuwa kubwa kwa sababu pale hakuna mazao ya kudumu?
MHE. KAPT. (MST.) GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Napenda kuipongeza Serikali kwa kusambaza umeme (REA II) vijiji karibu Tarafa zote sita za Wilaya ya Newala. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa
Naibu Waziri yanaonesha kwamba tatizo la umeme maeneo ya Mtwara Mjini, Lindi yataisha na tumeshuhudia juzi Rais ameweka jiwe la msingi, lakini upande mwingine Naibu Waziri
anakubali kwamba Wilaya za Tandahimba, Newala, Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na Ruangwa hali ya upatikanaji wa umeme si nzuri na kule tatizo si kwamba umeme haupo tatizo
ni miundombinu. Nyaya zimekatika, ikinyesha mvua nguzo imeanguka, ni lini Serikali itachukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba kukatikakatika kwa umeme na kuanguka nguzo kuna malizwa mara moja ili Wilaya hizi nazo
zifaidi umeme kama wanavyofaidi Wilaya zingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili,
pamekuwepo na matamshi mengi upande wa Serikali juu ya gharama halisi za mwananchi wa kawaida kuingiza umeme katika nyumba yake. Nini kauli ya leo ya Serikali kwamba kijiji fulani kinataka kuingiza umeme pale Newala, yule mwananchi wa kawaida anatakiwa alipe shilingi ngapi kwa sababu matamko ya huko nyuma hayafanani na gharama halisi ambazo zimekuwa zikilipwa? Nakushukuru.
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasubiri ruhusa yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo si mazuri sana kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Hata hivyo, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nataka niwapongeze Waheshimiwa Wabunge vijana wa Bunge la 10 ambao kwa hiari yao walijiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa, walionesha kwamba kuongoza ni kuonesha njia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Baba wa Taifa alituandalia akafanya JKT kama ndiyo jando, mahali pa kuwafunda, kuwaandaa vizuri vijana wa Tanzania kimaadili, kiuzalendo na kiulinzi; na kwa kuwa sasa inaonekana vijana wengi hawaendi tumeporomoka kutoka asilimia 75 mpaka mwaka huu 23. Je, kwa kutokuwapeleka hawa vijana JKT, Serikali haioni kwamba inachangia kuwaunda vijana ambao hawana maadili, legelege, ambao hawana uzalendo katika nchi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa changamoto zilizoelezwa na Wizara nimezipitia zote ziko ndani ya uwezo wa Serikali. Je, Serikali inaweza kuliahidi Bunge hili kwamba itaunda kikosi maalum cha kupitia changamoto hizi, kuziondoa na kuhakikisha kwamba vijana wote wanakwenda Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria na kwamba hata kama ikibidi kuomba pesa walete maombi hapa Bungeni; kwa sababu Watanzania tuna uzoefu wa kushughulikia matatizo mbalimbali kaa UPE; na kama mwaka wa jana tulivyopeleka watoto wote kutoka darasa la kwanza mpaka form four wamekwenda bila malipo? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. KAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa huruma yako kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwanza nataka niipongeze Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya ya kujenga kwa kiwango cha lami katika maeneo korofi kama Mlima Kinombedo na Kitangari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini swali langu ni hili; kwa sababu ni sera ya Serikali kwamba mikoa iunganishwe kwa barabara za lami, barabara hii inaunganisha Mikoa ya Mtwara na Lindi, barabara hii inategemewa sana na wananchi wa Tandahimba, Newala na nchi ya Msumbiji wale wanaovuka. Nini kauli ya Serikali, tunajua kwamba sasa hivi inatafutwa fedha. Je, Serikali inaweza kutoa kauli hapa kwamba sasa kuanzia bajeti ijayo wataanza kutenga pesa za kufanya upembuzi yakinifu wakati fedha zinatafutwa? (Makofi)
MHE. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri kwa majibu aliyoyatoa. Majibu ambayo mimi na wananchi wa Newala wanaomsikiliza, yametukatisha tamaa kwa sababu swali la msingi halijajibiwa.
Mheshimiwa Spika, swali langu nimeuliza, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha viwanda hivi vinafanya kazi? Ndiyo swali la msingi, lakini majibu ya Mheshimiwa Waziri yanaeleza, mwekezaji atafanya hiki, atafanya hiki. Tangu miaka 14 huko nyuma; tumesubiri miaka 14, bado Serikali inaridhika na maelezo yake, atafanya hiki, atafanya hiki, atafanya hiki.
Mheshimiwa Spika, nataka nikwambieni Serikalini, hawa watu waliochukua viwanda vya Newala walivigeuza kuwa warehouse stores wakavikodisha. Hiyo shilingi milioni 75 waliyolipa imerudi siku nyingi.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri: kwa kuwa, huyu mtu ameshindwa kutekeleza mkataba baina yake na Serikali kwa zaidi ya miaka 10; na kwa kuwa kuna watu wengi waliokuja Newala kuomba wanunue kiwanda hiki. Je, sasa Serikali iko tayari kumnyang’anya kiwanda hiki na kuwauzia watu ambao wakipewa leo leo wanaanza kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kile Kiwanda cha Newala II ni kweli kinafanya kazi na tunamshukuru kwa hapo alipofika, lakini kiwanda kile nimekitembelea, kuna matatizo makubwa mawili; moja maslahi ya wale akinamama wanaobangua korosho pale; pili, hawana hata gloves, zile zana za kufanyia kazi ya kubangua korosho. Je, Serikali iko tayari kumtuma wiki hii Mkaguzi wa Viwanda aende Newala akakague mazingira wanayofanya kazi akinamama wa Newala wanaobangua korosho? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's