Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Supplementary Questions
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imekiri kuwa kuna upungufu wa nyumba 1,183 za kuishi walimu na sasa tayari wananchi wa Wilaya ya Magu wameshajenga maboma 27 yapo tayari kukamilishwa; je, Serikali inaweza kutusadia fedha za kukamilisha ili walimu waingie kwenye nyumba hizo kupunguza uhaba wa nyumba za walimu?
Swali la pili, kwa kuwa nyumba hazitoshi, je, Serikali inaonaje kuwasaidia walimu ambao wanapanga nje mitaani kuwaongeza mishahara kidogo ili waweze kumudu upangaji wa nyumba mitaani? (Makofi)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninashukuru majibu ya Serikali. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna upungufu wa vitendea kazi, kwa maana ya magari na mafuta; je, ikiongeza kununua magari, italipatia Jeshi la Polisi Wilaya ya Magu hasa Kituo cha Kabila gari lingine?
(b) Kwa kuwa Jeshi la Polisi ni walinzi wa mali na raia lakini maisha yao ni magumu sana, hata wanapostaafu, wanaendelea kuwa na maisha magumu.
Je, Serikali kwa sababu askari katika Wilaya ya Magu wako 135 na nyumba wanazoishi askari kumi ziko tano tu; Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba Wilaya ya Magu? Nipatiwe majibu ni nyumba ngapi zitakazojengwa. (Makofi)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pia nashukuru majibu ya Serikali na kuwapongeza Wizara hii kwa jinsi wanavyoshughulikia masuala haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara inatambua kwamba Magu bado vijiji 85 na 34 vitaingizwa kwenye mpango wa REA III, je, Wizara inaonaje kuviingiza vijiji vyote vilivyobaki kwenye mpango huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa REA II inaendelea na miradi kule Magu na kwa sababu baadhi ya vijiiji mkandarasi ameondoa nguzo ambazo zilikuwa zinategemewa na wananchi na wananchi wengine hawajawekewa, je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuambatana nami kwenda Jimboni kwangu kutembelea vijiji hivyo pamoja na Vijiji vya Mahaha, Nobola, Bungilya, Mwamabanza na Matale? (Makofi)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa Mwanza tuna Kiwanda cha Tanneries ambacho sasa kimegeuzwa kuwa chuo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukirudisha hicho kiwanda ili kiweze kufanya kazi iliyokusudiwa?
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza msitu unaozungumzwa haupo, hata athari zinazozungumzwa kwamba vijiji vinavyozunguka watapata athari ya upepo siyo kweli, kwa sababu hata wewe ukisimama mle mita mia tatu unaonekana huo ni msitu?
(a) Je, Serikali kwa sababu inasema ni chujio haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kulipunguza eneo hilo ikawapa wananchi upande mwingine, na upande mwingine ili wakaendelea na shughuli za kijamii na eneo linalobaki wakaliboresha kwa kupanda wenyewe misitu endelevu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu majibu haya ni ya kudanganywa, je, Naibu Waziri yupo tayari kuambatana nami kwenda kuliona eneo ambalo linasemwa ni hifadhi?
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa Kituo hiki cha Afya kinahudumia maeneo makubwa katika eneo la Ilemela, Usagara Wilaya ya Misungwi, pamoja na Jimbo la Sumve na ni Kituo cha Afya ambacho kiko highway, wakati wowote watu wanapata matatizo wanaposafiri wanahitaji huduma hii kubwa. Kwa kuwa sera ya mwaka 2007 ni kama imepitwa na wakati ukilinganisha na mazingira:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kubadilisha ili angalau kulingana na mazingira ya Kituo hiki cha Afya cha Kisesa, kiweze kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya ili kiweze kuhudumia maeneo makubwa?
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
6
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali iko hatua za mwisho, mkataba wa kujenga jengo la X-ray, jengo la upasuaji, limeanza mwaka 2013. Kama ni hatua za mwisho, leo ni miaka mitatu. Serikali haioni kwamba hii ni aibu, miaka mitatu inajenga majengo haya bila kukamilika na yanasubiri tu shilingi milioni 77 ili yaweze kukamilika? Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuniambia hizi shilingi milioni 77 zikipatikana hata kesho ili huduma hizi zianze kutolewa, yuko tayari kunipa fedha hizi?
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nazidi kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kadri anavyochapa kazi kuhakikisha kwamba anatoa majibu yanayoridhisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wa kuwa zahanati hizi wananchi walizijenga, Nyang‟hanga, Salongwe, Bundilya, Nsola, Nyamahanga, Nyashigwe, Chabula, Ikengele, Isangijo, Langi na Lutale; na ziko hatua za kukamilisha ili waweze kupata huduma; na kwa kuwa bajeti ya mwaka 2015/2016 inaelekea mwisho; je, Serikali inaweza kutupatia fedha hizi kwa haraka ili tuweze kukamilisha miradi hii na wanachi wapate huduma?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasema kila kijiji kiwe na zahanati, na wananchi wetu wamekuwa wakiwahi kutimiza wajibu wao kwa maana ya kujenga maboma haya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha utekelezaji wa ilani hii ili wananchi waweze kupata huduma hiyo?
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali iliongeza mipaka yake ikawafuata wananchi katika vijiji vinane vya Mwamumtani, Mwalali, Ndung‟wa, Ndinho, Ntantulu, Kiliju, Longalombogo na Shishani na haikuwashirikisha wananchi, je, ni lini sasa eneo hili litarudi kwa wananchi kwa kuwashirikisha wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa amesema umegaji wa eneo hili haujaleta tija na haujamaliza changamoto ya wananchi na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni akiwa kwenye Kijiji cha Nanga katika Kata ya Kinameli aliliona hili na alitaja Sheria ya Ardhi, Na.4 akasema kwamba akiwa Rais eneo hili atalirudisha kwa wananchi. Je, kwa nini Mheshimiwa Naibu Waziri anapingana na ahadi ya Rais?
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na kadri ambavyo imeanza kushughulikia jambo hili hasa kwa kuamini kwamba katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tulifanya ahadi na wananchi, lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wazee hawa wengi ni wakulima ambao wakati wote Serikali inapokuwa na hali mbaya ya chakula huzuia mazao yao kuuzwa mahali popote ili kukidhi mahitaji ya nchi, kwa hiyo, hawa wazee wamechangia sana katika Taifa hili.
Je, ni lini sasa Serikali pamoja na hatua nyingine ambazo imezichukua itakamilisha mpango huu ili wazee hawa waweze kulipwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sisi sote tuliopo humu ni wazee watarajiwa, je, Serikali inaweza kutuambia hapa itaanza kwa kutoa kiasi gani kila mwenzi na kwa kila mzee?
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo ya Magu yanafanana sana na matatizo ya Nyamagana, Barabara ya Ngudu – Magu – Ngumarwa, usanifu umeshakwisha kukamilika, sambamba na Barabara ya Airport – Igombe – Kayenze – Kongolo – Nyanguge ili kupunguza msongamano wa kuingia Jiji la Mwanza na kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, je, barabara hizi zitaanza kujengwa lini kwa kiwango cha lami? (Makofi)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, je, Serikali ina mpango gani wa kuzielekeza Halmashauri kutumia force account ili miradi midogo midogo kama hii iweze kutengenezwa kwa fedha ndogo na iweze kuleta impact?
Swali la pili, kwa kuwa jambo hili linafanana kabisa
na vituo vya afya vilivyoko Jimbo la Magu katika kituo cha afya Lugeye pamoja na Nyanguge. Serikali ina mpango gani wa kuvijengea majengo ya upasuaji ili wananchi waweze kupata huduma karibu? Ahsante sana.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali pamoja na mikakati mizuri ambayo Serikali inaiweka lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa nina imani kwamba Waziri na Maprofesa wote mlioko ndani humu mmesoma bure A-Level na kwa sababu watoto hawa wanachaguliwa, wengine wanashindwa kuendelea na masomo haya kwa kukosa fedha, kwa sababu bado ni watoto wa maskini na wengine wamefaulu vizuri masomo ya sayansi pamoja na hesabu, je, Serikali haioni kwamba inapoteza vijana wazuri ambao wanaweza kusaidia Taifa?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hawa watoto wanaochaguliwa kuendelea na A-level ni wachache kuliko wale ambao wanahudumiwa na Serikali kwa maana ya O-Level, je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuleta bajeti ili tuweze kuwasaidia watoto hawa wa maskini ili waweze nao kusoma bure wafaidi matunda ya Serikali hii? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DESTERY B. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na hasa niendelee kuanidka Kiswaga. Kwa kuwa swali langu linafanana kabisa na suala hili la Kigamboni, Wilaya ya Magu ambayo ni Jimbo lina vijiji 82, ni vijiji 29 tu vina umeme. Je, vijiji 53 ni lini vitapatiwa umeme ambavyo hata Mheshimiwa Dkt. Kalemani anavifahamu? (Makofi)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali.
Kwa kuwa Serikali imekiri kufuta leseni 423 yenye eneo la hekta 69,652.88; je, Serikali iko tayari kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo eneo hili ambalo limefanyiwa utafiti ili waweze kujiajiri na kujipatia ajira na waweze kulipa kodi stahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Serikali iko tayari kuwanunulia vifaa vinavyohusiana na wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kukodisha kuliko ilivyo sasa wanachimba bila utaalam na vifaa vinavyostahili?
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa, mkandarasi anaendelea na mkataba mpaka kuezeka. Je, Serikali ina mpango gani wa ku-lease fedha ambazo zitahitajika, ili halmashauri isikiuke mkataba?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa, hatua ya kuezeka inakwenda kukamilika na jengo hili limechukua muda mrefu. Je, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa mwaka ujao wa fedha, fedha za kutosha ili kukamilisha jengo hilo?
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwanza naishukuru Serikali kwa kutupa mradi wa maji pale Magu Mjini, mkandarasi yuko site; lakini pia nipongeze Kampuni ya Alliance Ginnery, mwekezaji amechimba kisima kirefu pale salama na kinatoa lita 9,000 kwa saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala hili la Nyamagana linafanana kabisa na Jimbo la Magu, kijiografia na kwa fursa zilizopo. Katika Tarafa ya Sanyo kwa maana ya Kisesa yote na vijiji vyake pamoja na Tarafa ya Ndagalu kuna hali mbaya sana ya maji katika Vijiji vya Ng’aya, Salama, Ndagalu, Nyabole, Kabila na Mahala...

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa sababu Halmashauri tumeomba dharura, ni lini Serikali sasa itatupatia fedha kwa ajili ya kuchimba visima virefu ili tuweze kusaidia wananchi hao?
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kwamba uchumi ukiwa nzuri tutaongeza, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa majibu yanaonesha kwamba kila baada ya miaka miwili Serikali ilikuwa ikiongeza posho za Waheshimiwa Madiwani mpaka 2015 na leo tuko 2017 tayari miaka miwili. Je, Serikali haioni kwamba kulingana na mazingira wanayofanyia kazi Waheshimiwa Madiwani pamoja na kupanda kwa maisha, sasa ni muda muafaka wa kuongeza posho angalau kidogo ili waweze kumudu maisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mikopo hii wanayokopa kwenye mabenki ni kutokana na posho yao, Serikali haioni kwamba hizi fedha ni ndogo zaidi, hawawezi hata kupeleka kwenye usafiri. Je, Serikali kwa nini isiweke ruzuku kama inavyotoa kwa Waheshimiwa Wabunge nusu ili Waheshimiwa Madiwani waweze kumudu usafiri? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's