Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Stanslaus Shingoma Mabula

Supplementary Questions
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kilichokuwa hasa kinatakiwa kipatiwe ufafanuzi, pamoja na majibu mazuri, tunafahamu namna ambavyo mapato ya Serikali yanapatikana kutoka Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Sasa tunachouliza hapa, miradi mingi ambayo imekuwa ikianzishwa kutoka kwenye Halmashauri inayotegemea fedha kutoka Serikali Kuu, fedha hizi haziji kwa wakati na badala yake miradi mingi sana inakuwa mwaka unaisha, miradi inakaa miaka mitano haikamiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunataka tu kufahamu, miradi hii mingine ambayo kwa kweli ingekamilika ingekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi; kwa mfano, kwenye Jimbo la Nyamagana, uko mradi wa maji wa Fumagila, una zaidi ya miaka mwili sasa na umebakiza fedha kidogo sana kutoka Serikali Kuu, kiasi cha shilingi milioni 256 hazijapatikana mpaka leo. Ni lini fedha hizi zitapatikana ili maji yanayokadiriwa kusaidia watu zaidi ya 16,000 yaweze kuwasaidia kwa wakati na kupunguza mzigo kwa akina mama? Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyonyooka, ningependa sana kujua swali langu la kwanza kwamba, pamoja na fedha zilizotengwa, ni kiasi gani cha fedha hasa kilichotengwa kwa sababu hiyo ingetusaidia kuwa uhakika na hii bajeti kwamba fedha hizi zilizotengwa zitakwenda kukamilisha majengo haya, ili kuwafanya Askari hawa waliosubiri takribani miaka minne sasa walau hizi familia ishirini zipate makazi bora na salama ya kukaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu tunafahamu Nyamagana ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza, nyumba hizi zinazotarajiwa kukamilika zinaweza kukidhi mahitaji ya familia zisizozidi ishirini na tano. Ukweli ni kwamba Askari ni wengi na umuhimu wa kambi hii ni mkubwa sana kwenye Mkoa wa Mwanza. Sasa ningependa tu kujua mpango wa Serikali, kuongeza nyumba zingine kwa muda na wakati ili Askari hawa wanaoishi kwenye kambi hiyo ya Mabatini na familia zao ambao sasa ina mwingiliano mkubwa na wananchi wa kawaida waweze kupata makazi mengine bora zaidi ili waweze kuwa kwenye mazingira salama nakushukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya namna ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo, machinga, mama lishe na wengine wanaofanana na biashara hizo wanatengenezewa mazingira mazuri ya kibiashara; lakini tungependa hasa kufahamu kwa mfano, habari za uwezeshaji wa mitaji inawezekana ikawa ni njia rahisi sana ya kuwa-contain machinga hawa pamoja na maeneo wanayopewa ili waweze kufanya biashara zao kwa uhakika kwa sababu tayari wanakuwa na kipato kizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu matatizo ya haya ya Dar es Salaam yanafanana sana na matatizo yaliopo Jiji la Mwanza, Wilayani Nyamagana, ambako pia kumekuwa na changamoto kubwa sana. Pamoja na maeneo mengi kupangwa, lakini Halmashauri zimefika sehemu zinakuwa zinabeba mzigo mzito kuona namna ya kuwawezesha hawa wafanyabiashara ndogo ndogo. Yako maeneo mengi yamepangwa, lakini uwezo wa wafanyabiashara hawa kwenda kule kutokana na miundombinu ambayo inakuwa siyo rafiki sana, maana Halmashauri inaweza ikatengeneza eneo vizuri, lakini miundombinu mingine ili iweze kufikika sawasawa inahitaji nguvu ya ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali na Wizara inatuhakikishia kwamba iko tayari kushirikiana na Halmashauri hizi kuwatengenezea wafanyabiashara ndogo ndogo, machinga na mama lishe ili waweze kupata kipato na maeneo yao yawe sahihi?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo ya Nachingwea yanafanana na matatizo yalioko kwenye Jimbo la Nyamagana, ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri, kauli ya Serikali juu ya barabara ya kutokea Kata ya Buhongwa kupita Kata ya Lwanima, Mitaa ya Sawa, Kanindo, Kishili, kutokea Igoma, lakini kutoka hiyo barabara inayokwenda Mkuyuni – Kanyerere – Tambuka Reli, kutokea Buzuruga kwa sabubu imekuwa ni ahadi ya muda mrefu na tunatambua namna ambavyo Jiji la Mwanza limekuwa likikua kwa kasi kila wakati. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi wa barabara hizi zitakazopunguza msongamano kwa kiwango kikubwa?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yaliyopo kwenye Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Mwanza pia ni moja kati ya mikoa iliyotajwa kuwa mikoa maskini, sasa ningependa kujua mikakati ya Serikali mbali ya majibu mazuri na mipango ya miaka mitano na mwaka mmoja, ina mkakati gani wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kuwa sehemu ya kuhakikisha na wao wanakuwemo kwenye mpango wa kuhakikisha umaskini huu unatoweka wakiwa wana nafasi nzuri ya kufanya biashara zao kwa uhuru?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa mara ya kwanza Wizara hii imeonesha uhalisia wake kwa kutoa majibu kwa vitendo nawapongeza sana.
Pamoja na majibu haya mazuri ya vitendo, Halmashauri ya Jiji la Mwanza kama ambavyo imekuwa ikishiriki kwa asilimia kubwa katika kuboresha michezo, tayari imeshaandaa ramani ya uwanja mzima na imeshaanza kupita ngazi mbalimbali. Ninataka kupata tu maoni kutoka kwenye Serikali kwamba uwanja huu pamoja na kwamba utakuwa umetengenezwa eneo la kuchezea, lakini bado tutakuwa na changamoto kubwa katika eneo la mzunguko mzima kwa ajili ya kupata vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, lakini jukwaa kuu na maeneo ya kukaa ili uwanja ukamilike na kuwa uwanja wa kisasa. (Makofi)
Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kusaidia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha uwanja wa Nyamagana unakuwa ni wa kisasa na ambao unaweza kutumika na mechi za Kimataifa? (Makofi)
Swali dogo la pili tayari vifaa vimeshafika, ni lini ….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Stanslaus naomba hilo swali la pili ufupishe kwa sababu la kwanza umelifanya refu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini TFF waithibitishie Wizara watakuwa tayati kukamilisha uwanja huu maana tumesubiri sana na tunahitaji kuutumia haraka tunavyoweza? Nakushukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu matatizo ya Jimbo la Igalula ni sawa na matatizo ya Jimbo la Nyamagana, nigeomba pia kutumia nafasi hii kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri.
Katika Jimbo la Nyamagana ziko nyumba za polisi ambazo zimejengwa toka mwaka 2010 tarehe 24 Mei zilitarajiwa kukamilika baada ya wiki 36. Lakini kwa masikitiko makubwa mpaka hivi ninavyozungumza leo nyumba zile hazijakamilika. Wangeweza kukaa askari zaidi ya 24 na familia zao na Jeshi la Polisi likaonesha motivation kubwa kwa askari hawa kuishi kwenye mazingira bora na salama ili waweze kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri ananithibitishia nyumba hizi zitajengwa na kukamilika kama ambavyo mkataba wa mkandarasi unavyosema miaka minne baadaye?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na nishukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Makambako yanafanana sana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Nyamagana katika Kata za Kishiri na Igoma. Majibu ya Mheshimiwa Waziri ni mazuri sana ila nilitaka tu kupata uhakika kutoka kwake na sisi ambao tuna matatizo ya kupata huduma kati ya Kata ya Kishiri na Igoma tukirudia mchakato huu upya kuanzia kwenye ngazi zote ambazo amezitaja tukaleta kwake tutapata approval ya kufanya marekebisho kwa wakati? Nashukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimwa Naibu Spika, hoja yangu bado iko pale pale kwamba pamoja na majibu mazuri ya Serikali na utaratibu mzima ambao Jiji la Mwanza unao sasa wa master plan ya miaka 20 ijayo lakini kama tunavyofahamu, pamoja na master plan bado kuna suala la fidia. Luchelele sasa ni takriban miaka kumi tangu wamethaminishwa na fidia wanaambiwa kila leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imefika hatua sehemu wananchi wanachoka. Sasa ukopaji wa fedha hizi umeanza muda mrefu; ulianzia TIB ukashindikana; umehamia CRDB; lakini ili fedha ziweze kupatikana CRDB ni lazima kibali cha Serikali kutoka TAMISEMI kipatikane. Sasa lazima tuliweke vizuri, ni lini Serikali itakuwa tayari kutoa kibali cha fedha ili Halmashauri ipate fedha iende kulipa fidia na mipango inayotarajiwa hata ya master plan ifikie kwenye wakati wake na ikubalike vizuri na wananchi? Nakushukuru sana.
MHE: STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya vyumba vya upasuaji yako pia kwenye Wilaya ya Nyamagana hasa, kwenye Hospitali yetu ya Sekou Toure ambayo Miundombinu yake ya theatre iliyopo sasa iko mbali kutoka kwenye Jengo ambalo ni labour ward. Pale kwenye jengo la labour ward tayari kuna jengo ambalo lilishaandaliwa lakini halina vifaa kabisa. Ni lini Serikali itakuwa tayari kupeleka vifaa vya upasuaji kwenye jengo hilo ambalo liko karibu sana na chumba wanachojifungulia akinamama, tukiamini kupatikana kwa vifaa hivi kutasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto yanajitokeza hasa wakati wa kujifungua?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, lakini pamoja na maswali mawili ya nyongeza, nikiri kwamba sijaridhishwa kabisa na majibu ya Mheshimiwa Waziri na wala sikubaliani nayo kwa sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu, Nyamagana ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza na ni mji unaokua kwa kasi sana, barabara hii haijasemwa leo, imesemwa sana, sasa tukisema mwaka 2017/2018 ndiyo tuanze upembuzi yakinifu tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Jimbo la Nyamagana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe Naibu Waziri na akumbuke kwamba iko sasa hivi mikakati ya kuboresha miji ukiwemo Mji wa Mwanza, barabara hii itakuwa muhimu sana kwa mkakati wa Serikali wa ukusanyaji mapato, ni lini watakuwa tayari kutumia fedha za dharura kuhakikisha hii shughuli ya kufanya upembuzi yakinifu inafanyika kwa mwaka huu na mwaka ujao barabara hii ianze kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa sababu zilezile kwamba Mji wa Mwanza ni mji unaokua kwa kasi na mara nyingi tumekuwa tukitumia fedha nyingi wakati wa dharura, tunaposubiri mvua nyingi zinanyesha na kuharibu barabara. Je, ni lini sasa fedha hizi za dharura zitatumika kuimarisha barabara ikiwemo barabara ya kutoka Mkuyuni kwenda Nyangurugulu kutokea Mahina, Buzuruga, lakini ya kutoka Mkolani kwenda Saint Augustine University kupitia Luchelele na Nyegezi Fisheries?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kutokana na sababu ya msingi kwamba tatizo la Machinga, yaani wafanyabiashara ndogo ndogo pengine linaweza kuwa endelevu, hasa kwenye Halmashauri zenye miji mikubwa ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo ipo Jimbo la Nyamagana, napenda tu kuiuliza Serikali kwamba, pamoja na utaratibu huu mzuri ambao inaelekeza, Halmashauri zetu zimekuwa na changamoto kubwa ya kifedha. Je, Serikali sasa iko tayari kupitia Wizara ya TAMISEMI kuzisaidia Halmashauri kwa namna moja au nyingine kuweza kuboresha maeneo haya na yawe rafiki kwa hawa wafanyabiashara?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ningependa tu kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kwamba pamoja na mikakati hii mizuri ambayo Serikali inayo katika kuwasaidia watumishi wakiwemo Walimu kupata mikopo ya muda mrefu, sasa ni lini Serikali itazishauri au itazielekeza hizi Halmashauri zetu zote nchini kuhakikisha kwamba kila zinapofanya zoezi la upimaji wa ardhi Walimu wanapewa kipaumbele katika kupata maeneo ambayo pamoja na mkopo watakaopata basi ardhi isiwe kikwazo kwao na waweze kumudu ujenzi huu wa sasa? Nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa hawa waajiriwa 779 walikuwa tayari wapo nchini wanafanya kazi kinyume na utaratibu jambo ambalo ni batili, ni hatua gani ambazo Serikali ilikwishachukua dhidi yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swal la pili, je, anafahamu kwamba utoaji wa vibali unaoendelea, unaendelea kunyima fursa vijana wengi wa Kitanzania kama alivyokiri kwamba wanazo sifa na wamemaliza vyuo vikuu, lakini wanakosa fursa za kuajiriwa kwa wakati kutokana na waajiriwa wengi kutoka nje kupata nafasi? Nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili madgo ya nyongeza.
Swali la kwanza, pamoja na jitihada kubwa ambazo zimeshafanywa na Halmashauri yangu ya Jiji la Mwanza, namshukuru sana tu Mkurugenzi kwa jitihada zake anazozifanya kuhakikisha anasaidia wanawake na vijana wa Jiji la Mwanza kujikomboa.
Mheshimiwa Spika, niulize tu kwamba inawezekana haya yanafanyika vizuri kwenye Halmashauri ambazo Wakurugenzi wengi wana utashi wa kusaidia makundi haya. Ni nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba fedha hizi zinapaswa kutolewa siyo kwa hiyari, iwe ni kwa lazima kwa mujibu wa makusanyo ya mapato ya ndani ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, je, Serikali haioni sasa ni wakati muhimu wa kuongeza asilimia hizi kutoka 10 mpaka 15 kwa sababu ni ukweli usiofichika kwamba vijana na wanawake wanaendelea kuongezeka zaidi hasa katika masuala mazima ya kujitafutia riziki na familia zao pia ili waweze kujikwamua kiuchumi? Nakushukuru. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa inaonekana utaratibu wa usambazaji maji unakuwa mgumu sana na ziko mamlaka za maji kwa mfano mamlaka ya MWAUWASA pale jiji la Mwanza; Serikali ina mpango gani kuziwezesha mamlaka hizi ili ziweze kuwa zinatatua changamoto za maji zinakabiliana nazo kwenye maeneo zilizopo? Hii itakuwa msaada mkubwa sana kwa Halmashauri hizi lakini pia kwa wananchi wenyewe. Nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibnu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Serikali inaendelea kufanya kazi nzuri kupitia miradi ya REA, lakini nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba yako maeneo mengine kwenye miji na majiji bado yanazo sura za vijiji; kwa mfano kwenye Jimbo la Nyamagana iko mitaa inafanana kabisa bado na maeneo ya vijijini kama Fumagila, Rwanima, Isebanda, Kakebe na maeneo mengine kama Nyakagwe. Ni lini Serikali itakuwa na utaratibu wa kuhakikisha na maeneo haya yanapatiwa umeme wa REA ili yaweze kupata sawasawa na mengine? Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Natambua Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla wewe ni mtaalam na unafahamu kabisa kwamba katika prevention za malaria kuna primary prevention na kuna secondary prevention, nashukuru umeelezea vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri kiwanda cha viuadudu kama tutaweza kufanikiwa, dawa ikasambaa vya kutosha tuka-control wale vector kwenye hiyo level ya wale wadudu kutafuna larva, huoni kwamba tutakuwa tume-eradicate kabisa malaria na ni wajibu wa kila Hamashauri kununua zile dawa ili kusudi kile kiwanda kifufuke na tuweze kuzuia malaria? Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara ya lami inayotoka Nela kuelekea Kiwanja cha Ndege. Niulize swali dogo, kwa kiwango hicho hicho ni lini Serikali sasa itaanza mpango wa kuboresha barabara kwa kiwango cha njia nne kutoka mjini katikati kwa maana ya barabara ya Kenyatta kwenda Shinyanga kupitia Kata za Mkuyuni, Igogo, Mkolani, Nyegezi pamoja na Buhongwa ili na yenyewe iweze kufanana na yale mazingira yaliyopo? Nakushukuru. (Makofi)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kulichukulia kwa uzito suala hili na kutenga fedha hiyo. Imani yangu ni kwamba kifaa hiki kitakamilika na kitafika kwa wakati kwenye Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana inao ujenzi wa jengo kubwa lenye ghorofa mbili kwa ajili ya wodi ya wanaume. Nataka commitment ya Serikali, je, watakuwa tayari baada tu ya jengo hili kukamilika mapema mwakani mwezi wa tatu kutusaidia kwa ajili ya kupata vitanda na vifaa tiba vingine ili kutoa huduma iliyo bora kuendana na kasi ya Awamu ya Tano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Wilaya ya Ilemela haina Hospitali ya Wilaya ya Ilemela lakini ni wilaya mpya na ujenzi wa hospitali yake umeanza kwa kusuasua sana. kwenye bajeti ya shilingi bilioni nne sasa hivi imeshapata milioni 500 peke yake. Nataka kujua je, Serikali itakuwa tayari kuhakikisha fedha zipatikane na kwenda kukamilisha ujenzi wa hospitali hii ya Wilaya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Ilemela?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Pamoja na kazi nzuri na jitihada za Serikali katika kuhakikisha miji inapangwa na zoezi zima la urasimishaji wa makazi ikiwemo upimaji shirikishi, naomba tu kujua Serikali inayo mkakati gani kuhakikisha kwamba pamoja na upimaji huu unaofanyika sasa ile gharama ya premium inaonekana kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi na matokeo yake wanashindwa kufikia hatua ya kupewa hati miliki, hivyo inawapelekea kubaki katika maeneo ambayo yamepimwa bila hati hizo.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuondoa kabisa hizi asilimia 2.5 zilizopunguzwa japo ilikuwa Saba ikapunguzwa, nini mkakati wa Serikali kuondoa hizi lakini kuongeza muda wa upimaji shirikishi ili wananchi wengi zaidi waweze kupimiwa kuhakikisha maeneo yao yote yamekamilika? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba biashara ya bodaboda imekuwa ni sehemu kubwa sana ya ajira kwa vijana, lakini naomba tu kufahamu ukichukulia Jimbo la Nyamagana peke yake zipo bodaboda takribani 6,700 lakini vijana hao wenye uwezo wa kujiajiri ni asilimia 30% peke yake, ni nini mkakati wa Serikali kutumia walau fedha za Mfuko wa Vijana na Fedha za Uwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waweze kukopeshwa na fedha hizi watumie kama sehemu ya ajira yao ili kuepusha migogoro na waajiri wao na mikataba isiyokuwa rafiki kwao? Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na mikakati mizuri ya Serikali katika kusaidia wavuvi kuwawezesha kwa namna mbalimbali kwa mikopo na vifaa, kwa Kanda ya Ziwa na Ziwa Victoria kwa sasa hali imekuwa tofauti. Hivi tunavyozungumza wananchi wavuvi wa Kanda ya Ziwa, Mikoa ya Ziwa Victoria wanapata taabu kutokana na zana zao, nyavu, mitumbwi kuchomwa moto na faini zisizokuwa rafiki kwa maisha yao halisi na kazi wanayoifanya.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na suala hili la uvuvi haramu kutokufika kwenye kiwango cha kumuumiza mvuvi ambaye tunataka tumsaidie afike mbali zaidi? (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa tunafahamu kwamba soko la kahawa bei yake imekuwa ikipanda na kushuka, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuanzisha ruzuku maalum kwa ajili ya wakulima wa kahawa ili hata soko linapoporomka mkulima asipate maumivu sana kwenye upande wa mauzo? (Makofi)
Pili, tunaamini kwamba Vyama vyetu vya Ushirika vinayo nafasi kubwa sana ya kuhakikisha wakulima wan chi hii wananufaika. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinaimarika na kuwa msaada kwa wakulima? Ahsante. (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's