Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Richard Mganga Ndassa

Supplementary Questions
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nishukuru kwa majibu ya utangulizi, lakini naomba tu kuiambia Serikali kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya uchumi pamoja na kijamii. Pia niseme barabara hii ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne na wakati barabara hii inaahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne, Rais wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwepo. Sasa hili suala la upembuzi yakinifu, ni lini hasa kwa sababu swali hapa la msingi, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia kwamba hii ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hapa Tanzania tunayo mazao makuu ya biashara, ambayo yalikuwa yanajulikana katika kuongeza uchumi wa nchi yetu ambayo ni pamba, kahawa, korosho pamoja na katani.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mazao haya ambayo yalikuwa yanatoa ajira kubwa, uchumi kwa nchi yetu, kwamba mazao haya sasa yanatafutiwa soko lenye uhakika hasa pamba ambayo zaidi ya Mikoa 14, Wilaya 42 zilikuwa zinategemea zao la pamba, Serikali ina mpango gani hasa? (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri sana inayofanya ya kusambaza umeme kupitia REA, REA I, REA II na REA III kwa sasa. Swali langu kwa sababu kuna vishoka wamejitokeza ambao wanaharibu sifa nzuri ya TANESCO, wanaojifanya kwenda kutandaza nyaya kwenye nyumba za watu lakini wanachukua pesa zao halafu hawa hawarudi tena kwa ajili ya kusambaza huo umeme. Je, Serikali inaweza ikawaagiza Mameneja wa Kanda, Mameneja wa Mikoa, Mameneja wa Wilaya ili kusudi waende wawabaini hao vishoka wasiwaibie wananchi hasa katika Jimbo la Sumve?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ahadi ya Serikali na Waziri mwenyewe humu Bungeni aliwaahidi Watanzania kwamba Miradi ya REA II itakamilika yote Juni, 2015; siyo mara moja wala mara mbili; ni sababu ipi iliyopelekea miradi hii kutokukamilika kama Mheshimiwa Waziri alivyosema? (Makofi)
La pili, kwa sababu huyu Mkandarasi mara kwa mara amekuwa akiwachangisha Watanzania shilingi 200,000/= au shilingi 300,000/= kwa kila nguzo ya umeme wale wanaohitaji; Serikali inatoa tamko gani ili kusudi wananchi hao wapate huduma hii kama ilivyotarajiwa? (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba nisahishe jina langu hapa inasomeka Ngassa, siyo Ngassa ni Ndassa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba Serikali itambue kwamba suala la maji ni suala kila Mtanzania, kila mwananchi anahitaji maji na ndiyo maana unaona Wabunge wote wanasema kuhusu maji.
(a) Swali langu, kwa sababu Serikali katika mwaka 2000 na 2004 iliamua, maamuzi magumu yenye tija, kuyatoa maji ya Ziwa Victoria kuyapeleka Kahama, Shinyanga. Je, Serikali ina mpango gani mrefu wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Mikoa tisa ili maji hayo yawanufaishe Watanzania na mikoa hiyo ni Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu, Singida na Dodoma. Serikali ina mpango gani kwa sababu mahitaji ya maji ni makubwa na maji ya Ziwa Victoria yapo hayana kazi nyingine. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha kwamba maji yanafika katika maeneo hayo?
(b) Mheshimiwa Waziri wa Maji, wananchi wa Jimbo la Sumve katika Kata ya Nkalalo na Mabomba wanashida kubwa ya maji, naomba nikuombe pamoja na maelezo haya utembelee tuende ukajionee mwenyewe jinsi wananchi wa Tanzania wa Jimbo la Sumve wanavyopata taabu ya maji katika Jimbo langu.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Maji ni uhai, ningependa kuiuliza Serikali, kwa sababu iko ahadi ya kupeleka maji katika maeneo ya Sumve, Malya, Mwagini kupitia Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria, ningependa Serikali iniambie ni lini hasa mradi huo mkubwa ambao utanufaisha zaidi ya vijiji 40, utaanza kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na maelezo mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini Serikali imekuwa ikiahidi kwamba itajenga Mahakama za Mwanzo kwa muda mrefu sana. Chikawe one aliahidi, akaja Chikawe two, mama Nagu, Kairuki, ahadi ni ile ile. Sasa ningependa kujua Mahakama ya Nyamikoma, Kata ya Iseni, Jimbo la Sumve Wilaya ya Kwimba itakuwa lini kwenye mpango wa kujengwa?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, anajua kwamba Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria unaanzia katika Kitongoji cha Ihelele, Kijiji cha Nyahumango. Cha kusikitisha Mheshimiwa Waziri, sina tatizo na maji kwenda Nzega, kwenda Kahama au sehemu nyingine, pale kwenye chanzo cha maji Ihelele penye matanki makubwa kuna kituo kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, hivi ungekuwa wewe ndiyo mwenye Jimbo hilo na una Waziri ungejisikiaje?
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwamba itakuwa ni Serikali ya viwanda, je, Selikali ina mpango gani wa kuanza kufufua viwanda hivi ambavyo vilikufa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichoko katika Wilaya ya Lushoto, Jimbo la Bumbuli, kimefungwa kwa takribani miaka mitatu sasa na mpaka sasa hakijaanza uzalishaji. Mara ya mwisho wakati Msajili wa Hazina anakuja pale alituambia kwamba zimeandaliwa shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji na kwenye randama ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara fedha hiyo hatujaiona. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kufunguliwa kwa kiwanda hiki?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri zinatofautiana kimapato na Kituo cha Afya cha Nyambiti hakina gari, ni utaratibu gani sasa utumike ili kituo hiki kiweze kupata gari kwa sababu uwezo ni mdogo?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mwanza hapo awali kulikuwa na zaidi vinu 15 vya kuchambulia pamba, kikiwepo na cha Nyambiti Ginnery, Ngasamo. Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilishaongea na Mheshimiwa Waziri Marehemu Abdallah Kigoda, pia niliongea na Waziri aliyekuwepo wakati huo Mheshimiwa Mama Nagu; ni lini sasa angalau Nyambiti Ginnery iweze kutengeneza pamba nyuzi?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Tanzania tunayo makampuni binafsi mawili yanayotoa huduma za ndege kwa wasafiri hapa nchini, FastJet pamoja na Precision.
Mheshimiwa Spika, lakini ningependa kujua ni utaratibu gani wa gharama za nauli wanazotumia kupanga. Kwa sababu gharama ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kurudi inakaribia shilingi 800,000 vivyo hivyo gharama ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya inakaribia shilingi 800,000 sawasawa na nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dubai kwa ndege za Emirates. Nataka kujua, ni utaratibu gani unaotumika kupanga gharama za nauli kwa wasafiri hasa kwa Dar es Salaam, Mwanza pamoja na Mbeya, routes za ndani hizi ni nani anayepanga nauli hizi?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Katika maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba ruzuku ya pembejeo pia inapelekwa kwenye zao la pamba. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba mpaka leo hakuna ruzuku yoyote inayopelekwa kwenye zao la pamba, kwenye mbolea pamoja na mbegu?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba, nakumbuka ulifanya ziara mkoani Mwanza na ulizungumza na wadau wa pamba. Msimu wa pamba umeanza Jumatatu, bei elekezi tunaambiwa ni shilingi 1,000, lakini wapo wanunuzi wengine wanasema hawawezi kununua pamba kwa bei ya shilingi 1,000.
Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu bei ya pamba, kwa sababu viwanda vyote hivyo Manonga, MWATEX, vinahitaji pamba ya kutosha; na ili wakulima wa zao la pamba waweze kulima zaidi lazima bei iwe nzuri, nini msimamo wa Serikali kuhusu bei ya pamba?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu Wakala wa Madini (TMAA) wanafanya kazi nzuri sana. Mwaka 2010 na mpaka mwaka 2015 waliweza kukamata madini yenye thamani ya Dola bilioni mbili, lakini pia kwa upande wa shilingi, jumla ya shilingi bilioni 64 zilikamatwa. Je, kwa utaratibu huo huo Serikali ina mpango gani wa kuzuia wachimbaji katika migodi hasa katika usafirishaji wa ule mchanga kwenda kupimwa nje?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. TBC na Radio ya Taifa ndiyo visemeo vya Serikali. Je, wakati mnaboresha mitambo, Serikali ina utaratibu gani wa kuwapeleka wafanyakazi wa TBC na Radio ya Taifa kwenda nje kujifunza ili kusudi waendane na teknolojia ya sasa, kuwapeleka nje kwenda kusoma?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu kazi ya ujenzi wa zahanati ni kazi nyingine, ujenzi wa vituo vya afya ni kazi nyingine, upelekaji wa tiba ni kazi nyingine. Je, Serikali kwa sababu inajua kwamba upo upungufu mkubwa sana wa wataalam katika ngazi zote, imejipanga namna gani kuhakikisha kwamba zahanati na vituo vyote vile vinakuwa na waganga wa kutosha?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Miji ya Sumve, Nyamatala, Malya, Nyambiti, Hungumarwa inakua kwa kasi sana. Mheshimiwa Waziri katika ziara yake aliyoifanya Kwimba nilimuomba vitendea kazi kama gari na vifaa vya kupimia. Nataka kujua ombi letu hilo limefikia wapi?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mwaka 2013 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuchimba visima vinane katika vijiji vinane, lakini hadi sasa shilingi milioni 184 tu zilizopelekwa.
Naiuliza Serikali ni lini sasa kwa sababu azma ya Serikali ilikuwa ni kuchimba visima vinane; ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya visima hivyo?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ujasikia vizuri swali? Mheshimiwa Ndassa sehemu ya mwisho ya swali ni lini?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Katika Jimbo la Sumve na Jimbo la Kwimba Serikali ilipanga kuchimba visima vinane katika vijiji vinane vya Isunga, Kadashi, Gumangubo, Shilima, Mande na Izimba A. Fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 3.6 lakini hadi juzi ni shilingi milioni 185 tu ndizo zilizopelekwa, kwa hiyo, miradi hii imekwama, ni lini sasa Serikali imepeleka fedha hizo?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, tarehe 11/10/2014 ilikuwa siku ya Jumamosi saa 5.32; Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne wakiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, walizindua daraja la Mto Simiyu kule Maligisu na kuahidi kwamba mita 50 kuingia kwenye daraja na mita 50 kutoka kwenye daraja itawekewa lami. sasa nataka kujua, je, ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa lini?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza. REA Awamu ya II imebakiza siku 27, je, wameshafanya tathmini ya kutosha nchi nzima? Kama jibu ni ndiyo utekelezaji wake ni asilimia ngapi?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Wizara hii inashughulika na habari, utamaduni, sanaa na michezo. Kwa idhini
yako, naomba uniruhusu niulize swali la michezo. Timu yetu ya vijana under 17
imebahatika kwenda kwenye fainali itakayofanyika Gabon Aprili, ni mwezi
mmoja tu sasa umebaki. Je, Serikali pamoja na TFF tunajiandaa namna gani ili
timu yetu hii isiende kushiriki bali iende kushindana na kuleta ushindi katika nchi
yetu?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana, naomba nimuulize bwana Waziri; katika Wilaya ya Kwimba kuna vijiji kumi ambavyo vilipangiwa kupelekewa maji katika mradi wa vijiji kumi, zaidi ya miaka kumi leo,
naomba leo nijue katika hivi vijiji vya Kadashi, Isunga, Shirima na Mhande mkandarasi hayupo site mpaka leo na kwa sababu nilishafanya mawasiliano na Mheshimiwa Waziri wa Maji mwenyewe kwa muda mwingi, nataka leo anipe majibi kazi hii ya miradi hii ya maji katika Wilaya ya Sumve na Kwimba lini itakamilika?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa sababu tunao uwanja wetu wa Taifa (Dar es Salaam) ambao ni wa kimataifa na ili kuutangaza uwanja huo, na ili kutangaza utalii na kuongeza ajira kwa nini Serikali sasa isije na mpango wa kuziomba Balozi zetu nje ili timu zao za Taifa huko ziliko zije kuutumia uwanja wetu wa mpira wa uwanja wa Taifa, na wakimaliza kucheza mpira au baada ya kucheza mpira wachezaji hao waende kwenye hifadhi zetu ili watangaze utalii wa nchi yetu kupitia uwanja wa Taifa?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu TBC 1 na TBC Redio ni visemeo vya Taifa, ndiyo spika ya Serikali. Je, kwa sababu matatizo ni mengi, usikivu karibu nchi nzima hawasikii vizuri, Je, Mheshimiwa Waziri hivi unatambua kwamba TBC1 na Redio TBC 1, televisheni ni kisemeo cha Taifa. Kwa nini sasa Serikali isiwekeze ili kuondoa kutokusikia vizuri katika maeneo mbalimbali?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Matatizo yaliyopo Mbozi Vwawa yanafanana sana na Kituo cha Afya cha Malya. Kituo cha Afya cha Malya kinahudumia Maswa, Malampaka na Kwimba. Kwa sababu Kituo cha Afya cha Malya kwa sasa kimezidiwa, miundombinu ya majengo na vyumba vya kusaidia wazazi havitoshi, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwekeza angalau adha zilizopo pale ziweze kupungua?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. TASAF awamu ya pili ilianzisha mradi wa barabara ya Bungurwa-Msunga; leo ni zaidi ya miaka 10 na yapo makalvati yapo tayari zaidi ya 50. Je, ni lini sasa mradi huo au ujenzi wa barabara hiyo utatekelezwa?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya Mradi wa Maji Sumve, Madya na Malampaka, mwaka 2017/2018 ilitenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huo. Sasa Mheshimiwa Waziri katika majibu yake, kwa sababu ili maji yafike Mji wa Malampaka ni lazima yafike Sumve na Malya. Sasa nataka kujua, tulitegemea kwamba ungetaja, angalau kwamba Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huo, lakini hukutaja hata kidogo. Sasa swali Mheshimiwa Waziri, pesa zilizotengwa sasa hivi hazipo tena au mradi huo umeshakufa?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna utaraibu mzuri wa kuzuia hizo nyavu zisizoruhusiwa, lakini samaki katika maziwa yetu; Ziwa Victoria kuna samaki aina ya sato, nembe, sangara na samaki wengine; lakini kuna utaratibu mzuri katika bahari yetu hasa uvunaji wa samaki aina ya kamba, kwamba wanavunwa baada ya muda fulani halafu wanasimama. Ili samaki hawa waweze kukua katika Ziwa Victoria; sato na samaki wengine; kwa nini sasa tusiwe na utaratibu wa kuzishirikisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania ili kusudi samaki hawa wawe na tija, badala ya kuvua samaki wadogo wadogo tuwe na muda wa kuwavuna? Ahsante.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niiulize Serikali, katika Wilaya ya Kwimba visima 188 vimeharibika, havifanyi kazi kutokana na kuzeeka lakini vingine vimechakaa na vimekauka.
Sasa naomba kuuliza, kwa sababu wananchi wa Kata za Mwabomba na hasa Nkalalo pale center wanashida kubwa sana ya maji kutokana na visima hivi kuharibika, je, Serikali sasa ina mpango gani wa kusaidia ili visima hivyo viweze kufanya kazi wakati tunasubiri mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria? (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, katika kuitikia wito wa Serikali wananchi wa mikoa ya Mwanza, Simiyu katika majimbo mbalimbali ikiwemo na Jimbo la Bariadi, Misungwi, Sumve pamba imelimwa kwa wingi sana.
Swali langu Mheshimiwa Waziri, endapo wanunuzi wa pamba watashindwa kuinunua pamba yote kwa sababu pamba imelimwa kwa wingi sana msimu huu. Je, Serikali imejipangaje kuwanusuru wakulima hawa ambao wameitikia wito wa Serikali wa kulima Pamba kwa wingi?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Serikali imesema kwamba itakarabati vituo 205 kikiwemo pia na Kituo cha Afya cha Malya, ninapenda kujua Mheshimiwa Waziri, ni formula gani mnayotumia kupelekwa kwa baadhi ya vituo vya afya shilingi milioni 500 na vingine milioni 400 wakati mlichagua kwamba vituo vyote 205 vikarabatiwe kwa pamoja. Ni formula gani mnayotumia? Lakini ni lini pesa zingine ambazo mliahidi kwamba mtapeleka shilingi milioni 500 kwa kila kituo, kwa nini 400 na kwa nini 500? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's