Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Supplementary Questions
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na hayo, Serikali imekiri kwamba ni kweli jambo hili limechukua muda mrefu. Zaidi ya miaka 18 watu hawa wanaishi katika mazingira magumu; na baadhi ya wananchi pale sasa vibanda vyao walivyojenga kwa sababu hawaruhusiwi kuongeza, familia zao wamekwenda kuwekeza kwa ndugu zao; wanaishi tofauti na familia zao.
Mheshimiwa Spika, swali; Serikali itakuwa tayari kuwaonea huruma watu hawa na kuwalipa fidia haraka ili waweze kuishi jirani na familia zao?
Mheshimiwa Spika, la pili. Kwa kuwa wananchi hawa wamejichagua na wawakilishi wao watatu, leo wanakuja hapa, yuko tayari sasa kukutana na mimi, Waziri na Waziri Mkuu na Waziri wa Ardhi, ili tukae pamoja tuwape majibu hawa wawakilishi wa wananchi ambao wanakuja? Nakushukuru?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, vilevile niishukuru kauli ya Serikali kwa kunipa matumaini kwamba sasa wananchi wangu wangu wa Makambako watapona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Makambako ni la muda mrefu takribani zaidi ya miaka 30 na kitu, mradi ambao tunao pale ulikuwa unahudumia watu 15,000 na sasa tumeshaongezeka na tumefikia zaidi ya watu 160,000. Je, Serikali imejipangaje kuona sasa tatizo hili linatatuliwa mapema na kama Rais alivyokuja alituahidi kwamba tatizo hili atalitatua?
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Waziri mwenye dhamana alikuwepo siku ile wakati Rais anazungumza kwamba, atakapomteua Waziri aanzie Makambako leo unawaambiaje watu wa Makambako?
La pili…
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali kwa mpango mzuri ambao sasa unatupa matumaini. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa, suala hili limechukua muda mrefu wa mradi huu wa REA na wa Songea na wa Makambako kwenda Songea ambao ulikuwa unaunganisha Kijiji cha Lyamkena na Kiumba. Je, ili kuwapa matumaini wananchi wangu kwa sababu suala hili kama nilivyosema limechukua muda mrefu, Waziri sasa atakuwa tayari baada ya kwisha Bunge tuende tukafanye mkutano atuambie kwamba alivyosema Machi mradi unaanza?
Swali la pili, kutoka ofisi ya TANESCO pale Makambako, kuna mita kama 400 hivi 500 kwenda kwenye Kijiji au Mtaa wa Kivavi na Mtaa wa Kibagange. Tunashukuru Serikali mlishatupa transfoma na nguzo zilianza kujengwa ni muda mrefu sasa zimesimama tumekwama nguzo za kumalizia na wire. Serikali itakuwa tayari sasa kutupa wire na nguzo ili tumalizie mradi huu wananchi waweze kufaidika?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na mimi kupata nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kijiji cha Ikelu kinafanana kabisa na swali la Korogwe; kuna mradi wa kutoka Tove kuja Mtwango mpaka Ilunda, bomba la maji limepita lakini kijiji cha Ikelu ni kilometa mbili tu hakina maji. Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea maji wananchi hawa hasa ikizingatiwa kuwa wako kilometa mbili tu toka bomba lilipo?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, kwanza nianze sana kwa kumpongeza Rais John Pombe Magufuli, Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji, pamoja na wataalam wa Wizara hii, kwa namna walivyotutengea bajeti ya Wizara ya Maji katika Halmashauri yetu ya Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu wametutengea fedha nzuri, hasa ukizingatia za mradi mkubwa ule wa Makambako ambao kwa muda mrefu wananchi wa Makambako wamekuwa wakipata tabu sana juu ya kupatikana kwa maji. Anawaambia nini wananchi wangu wa Halmashauri ya Makambako, kwamba baada ya kutenga bajeti ile mwaka wa fedha unaanza keshokutwa, ili fedha zile ziweze kwenda kujenga mradi ule mkubwa lakini ukiwepo pamoja na Kijiji cha Kiumba, Mutulingara yenyewe pamoja na Ikelu na vijiji vingine ambavyo vimekosa maji. Ni lini sasa fedha hizi tulizozitenga zitakwenda? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Makambako tuna Bodi ya Maji, kwa muda mrefu Halmashauri ilishapitisha majina ya kuja katika Wizara, mwaka mmoja na nusu sasa Bodi ya Makambako haijateuliwa katika vyombo vinavyohusika. Sijajua ni TAMISEMI au ni Wizara ya Maji. Je, ni lini sasa mtateua ili watu hawa waendelee kufanya kazi katika Bodi ya Mji wa Makambako?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa sababu tatizo la Mpwapwa linalingana kabisa na tatizo kubwa la Makambako. Mji wa Makambako una wakazi wengi zaidi ya laki moja, na tatizo la maji ni kubwa sana. Wananchi wa Mji wa Makambako alipopita Mheshimiwa Dkt. Magufuli kipenzi chao na kipenzi cha watanzania, walimueleza tatizo la maji katika Mji wa Makambako, kuna mradi ambao ulishasanifiwa wenye gharama ya zaidi ya bilioni 57, na Waziri wa Maji ambaye yupo sasa alikuwepo siku hiyo wakati anaahidi.
Je, sasa tatizo hili la mradi mkubwa wa bilioni 57 litatatuliwa lini ili wananchi wa Makambako waendelee kupata maji.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru majibu mazuri ya Waziri ya kutununulia baadhi ya vifaa vya upasuaji ili tupate huduma hii. Kama nilivyosema vifaa hivi vimekaa tu haviwezi kufanya kazi, ni sawa na mifugo umechukua majike umeyaweka hujapeleka madume hakuna kitu ambacho kitaendelea pale. Serikali haioni sasa uko umuhimu wa kupeleka kwa mfano hizi dawa za usingizi ili shughuli za upasuaji ziweze kuanza? (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Rais alipopita pale aliahidi kuwaondolea kero wananchi wa Makambako ili wasiende kufanyiwa upasuaji Njombe na Kibena kama nilivyouliza kwenye swali la msingi. Hawaoni sasa iko haja ya kuchukua fedha za dharura kununua vifaa hivi pamoja na vile vilivyopelekwa ili shughuli za upasuaji zianze?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba niulize swali la nyongeza ambalo linalingana kabisa na lile la Morogoro Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za kutoka Njombe – Mdandu - Iyayi na kutoka Njombe - Lupembe -Madeke, zilishafanyiwa upembuzi na usanifu miaka miwili, mitatu iliyopita:-
Je, ni lini sasa barabara hizi zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Makete ndipo ambapo kituo kinachozalisha mitamba katika wilaya hiyo na wananchi wa Wilaya ya Makete ndiyo wamekuwa miongoni mwa wanaofaidi na mikoa mingine jirani kama alivyosema:-
Swali, hivi sasa Serikali imejipangaje kuona sasa Halmashauri jirani za Mkoa wa Njombe hususan Wilaya ya Wanging‟ombe, Njombe, Ludewa, Halmashauri ya Mji wa Makambako na Lupembe zinafaidika kupata mikopo ya kuwakopesha mitamba hii ili iweze kuzalisha katika halmashauri hizi wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Makete walitoa eneo kubwa sana kwa kituo hiki na eneo hilo bado kubwa halitumiki, Serikali imejipangaje kuona wananchi wa Wilaya ya Makete wanakopeshwa mitamba hii ili waweze kupata eneo ambalo limekaa tu halitumiki waweze kunufaika nalo? (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, niulize swali la nyongeza linalolingana na Wilaya ya Uyui. Katika mji wa Makambako kipolisi ni Wilaya ya Kipolisi, pamoja na maelezo ambayo Serikali imetoa mazuri. Je, Serikali ina mpango gani hasa hususani kituo cha Makambako ambacho ndicho kiko barabarani yaani kiko njia panda ya kwenda Mbeya, Songea na askari hawa hawana nyumba kabisa hata moja ya kuishi?
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzijenga nyumba katika kituo cha Polisi cha Makambako na wakati eneo la kujenga nyumba lipo? Nakushukuru
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini naomba niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali langu la msingi nimeelezea namna ambavyo wananchi wa Kata ya Saja, Kijiji cha Nyigo na Mtewele namna wanavyopata tabu kwani huduma zote zinapatikana Makambako na kwenda kwenye Halmashauri yao kutoka Saja kwenda Wanging‘ombe ni kilometa 88 na kwenda Makambako ni kilometa 20 na kutoka Mtewele ni kilometa tano na Waziri amekiri ni kweli katika suala la upatikanaji wa huduma ni mbali. Kwa nini Waziri asiagize shughuli hii ya vikao ianze kufanyika? Siku za nyuma vilishafanyika na kupelekwa kwenye vikao vinavyohusika vya mkoa na hivi juzi tu tulikaa kwenye kikao na mkoa tayari walianza kushughulikia. Niombe Waziri sasa ashughulikie suala hili na kuagiza kwamba waweze kukaa vikao ili wananchi hawa wapate huduma jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Kijiji cha Nyigo, GN ambayo iko katika Halmashauri ya Makambako inaonyesha Kijiji cha Ngigo mpaka wake mwisho ni barabara ya zamani ya Mgololo. Hata hivyo, uongozi wa Iringa umewahi kwenda pale na kutaka kupotosha ukweli. Niombe sasa Waziri asimamie na afuatane na mimi ili tukaone ile GN ambayo tulipewa Halmashauri ya Mji wa Makambako ili wananchi wale waweze kupata huduma jirani na Mji wa Makambako. Nakushukuru.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, suala la Monduli linafanana na suala la Makambako.
Mheshimiwa Spika, Makambako kuna eneo linaloitwa Kipagamo ambalo miaka ya huko nyuma wananchi waliipa Jeshi kwa ajili ya matumizi ya shabaha. Maeneo hayo sasa tayari wananchi tumejenga shule na tayari kuna makazi ya watu na matumizi hayo sasa hayatumiki kama ambavyo yalivyokuwa yamekusudiwa huko nyuma kwa sababu pana shule na makazi ya watu.
Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuwarudishia wananchi eneo lile ili liendelee kutumika kwa shule na makazi ya watu na kwa sababu barua tulishaiandika kupitia Serikali ya Kijiji na nilimpa mwenyewe Waziri mkono kwa mkono, je, ni lini sasa Serikali itarudisha eneo hilo hilo liendelee kutumika kwa wananchi? Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Rais alipotembelea Mji wa Makambako aliwaahidi Wanamakambako kwamba atatoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la Mji wa Makambako kupatiwa maji; naishukuru Serikali kwamba na kwenye bajeti zilitengwa fedha za kutoka India: Mheshimiwa Waziri anawaambia nini Wanamakambako kuhusu fedha ambazo zimetengwa kutoka Serikali ya India kutatua tatizo la Mji wa Makambako kupata maji?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupewa
nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu
mazuri ya Serikali nina maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kwa kuwa lengo la Serikali ilikuwa ni
kujenga VETA kila Wilaya ili vijana wetu waweze kupata mafunzo, vijana ambao
wanakuwa wameshindwa kuendelea na vyuo vikuu na kadhalika. Je, sasa
Serikali imejipangaje kuhakikisha inakamilisha azma yake iliyopanga ya kujenga
chuo cha VETA kila Wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na majibu mazuri kama
nilivyosema ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali kwa majibu yake imesema kule
Njombe tuna Chuo cha Ulembwe pale ambacho kinamilikiwa na Wilaya yetu ya
Njombe. Je, Serikali sasa kwa majibu haya imejipangaje kuhakikisha chuo hiki
kinaboreshwa kama walivyosema ili wananchi wa Wilaya ya Njombe hususan
pamoja na Jimbo la Makambako, vijana hawa waweze kwenda kusoma chuo
hiki cha VETA ambacho kiko pale Ulembwe?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika,
nashukuru na mimi kunipa nafasi niulize nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inafanya kazi nzuri ya kuwapelekea umeme wananchi katika nchi yetu; na kwa kuwa kipindi kilichopita Serikali kwenye Jimbo la Makambako hususan vijiji vya Ikwete, Nyamande, Manga, Utengule, Mlowa, Mahongole, Kitandililo na Kifumbe iliahidi kutuletea umeme katika Awamu ya Pili na mkandarasi ambaye tulikuwa tumepewa alikuwa ni LAC Export na mkandarasi huyu baadae Serikali kupitia Bunge hili walisema
wamemuondoa kwa sababu alikuwa hakidhi vigezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali
itatupeleka katika vijiji hivi nilivyovitamka umeme Awamu hii ya Tatu ili wananchi hawa waweze kupata umeme kama ambavyo wanapata sehemu zingine? Nakushukuru.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la Lulindi linafanana kabisa na tatizo lililoko katika jimbo la Makambako. Makambako kuelekea usawa wa kwenda Mbeya ni kilometa mbili eneo moja linaitwa Majengo hakuna mawasiliano. Kilometa tano kuelekea usawa wa kwenda Njombe kijiji chenye eneo la Kyankena Kiumba hakuna mawasiiano; Kitandililo Mawandea hakuna mawasiliano. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka minara hii ilimawasiliano yaweze kupatikana katika maeneo hayo?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami niulize swali fupi. Hospitali yetu ya Makambako ilipandishwa hadhi tangu 2013 na kuwa hospitali kutoka kituo cha afya, lakini mgao wa dawa mpaka sasa tunapata kama kituo cha afya. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kupeleka mgao kama ambavyo ilipandisha kuwa hospitali kwa sababu wataalam, Madaktari wapo na chumba cha kufanyia upasuaji kinaanza mwezi huu?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeonesha nia nzuri ya kutatua tatizo kubwa la maji lililoko katika Mji wa Makambako. Swali la kwanza, kwa sababu Serikali imetenga fedha hizo dola ambazo amezitaja hapo, dola milioni 38, nataka kujua ni lini sasa mradi huu utaanza ili wananchi wa Makambako waepukane na tatizo kubwa wanalopata Makambako na hata wawekezaji wa viwanda inashindikana kwa sababu maji hatuna?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu mradi huu mdogo ambao kama alivyosema tenda imetangazwa ambao ni kwa ajili ya bwawa dogo la Makambako, nilipofuatilia Mkoani wanasema tayari iko Wizarani lakini Wizara bado haijarudisha kule ili mkandarasi aanze kazi. Je, ni lini sasa mkandarasi huyu ataanza kazi kwa mradi huu kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.
Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kupitia Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya wajasiriamali wakiwemo wa Makambako juu ya Soko la Kimataifa, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, lakini kabla sijauliza niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuteuliwa kwake, vile vile kutokana na majibu mazuri ambayo yamelenga utekelezaji wa Ilani ya CCM kutatua kero za wananchi, kwa majibu haya nimefarijika sana, ni imani yangu kwamba tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu eneo hili bomba la mafuta linapita nyuma ya Hospitali yetu ya Mji wa Makambako na linapita eneo la polisi pale na linapita kwenye maeneo ya wananchi kama ambavyo swali la msingi limesema.
Je, sasa kutokana na kwamba amesema atawatuma watu wa TANROADS ili waweze kwenda kuona na kushughulikia. Ni lini sasa hao watu wa TANROADS waende mapema ili kusudi kabla ya mvua za Disemba hazijaanza kunyesha ili kutatua kero ambayo ipo kwa sababu wananchi wanashindwa kupita na magari katika maeneo haya ambayo nimeyataja?
Mheshimiwa Mweyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi baada ya kumalizika Bunge hili, ili akaone maeneo ambayo yametajwa katika maeneo hayo? Nakushukuru.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mwaka jana tumepitisha kwenye bajeti miradi 17 mikubwa nchini Tanzania, ikiwemo 16 Tanzania Bara na mmoja Zanzibar, ikiwemo na Makambako, kutokea fedha za kutoka India. Je, Waziri anawaambia nini wananchi wa Makambako juu ya ule mradi mkubwa ambao utajengwa katika Mji wa Makambako, lini utaanza ili wananchi hawa waweze kuondokana na adha na tabu ya maji wanayoipata katika Mji wa Makambako?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa nia ya Serikali ni kumtua mama ndoo, kumsogezea huduma jirani ili kuweza kupata maji hasa vijijini na mijini; na kwa kuwa kuna miradi 17 mikubwa ya maji hasa fedha za kutoka India ambazo zilipitishwa kwenye bajeti hapa; na kwa kuwa Mji wa Makambako umekuwa ni miongoni mwa miji ya kupata mradi huu mkubwa wa maji katika miji ile 17.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wangu wa Mji wa Makambako ili waweze kupata maji, ni lini miradi hii itaanza?
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Kituo cha Polisi Makambako ni kituo cha kiwilaya na kwa sababu Makambako ndipo katikati ya kwenda Songea, Mbeya na Iringa; na kwa sababu, Waziri alituahidi kutupatia kitendea kazi cha gari. Je, ahadi yake ya kutupatia gari iko pale pale ili shughuli za kipolisi pale ziweze kufanyika kwa ufanisi mzuri?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's