Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa

Supplementary Questions
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyokuwa kwa Nzega Mjini, Mheshimiwa Rais wetu alipokuwa kwenye kampeni katika Jimbo la Bagamoyo aliwaahidi wananchi kuikabidhi kambi ya mkandarasi iliyopo Daraja la Makofia kwa wananchi wa Bagamoyo ili waweze kuanzisha shule ya msingi. Naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri taratibu zimefikia wapi?
MHE. DKT. SHUKURU KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ingawa ni majibu ambayo mimi na wananchi wangu wa Bagamoyo yanatupa matatizo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kama atakubali kuielekeza timu hii ya pamoja iliyoundwa ili iweze kukutana na wawakilishi wa wananchi hawa akiwemo Mbunge na Waheshimiwa Madiwani wa jimbo la Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, TANAPA inawatoza fedha wananchi wa Makurunge na Matipwili wanapovuka daraja eneo la Gama katika Mto wa Wami wanapokuwa wanafanya shughuli zao, mtu Shilingi 5,000 na gari Shilingi 25,000, je, nini kauli ya Serikali kuhusu uhalali wa tozo hiyo?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa changamoto za Jimbo la Busega zinafanana na zile za Jimbo langu la Bagamoyo, vijiji viwili, Kijiji cha Kongo na Kijiji cha Kondo ambavyo vilikuwa ndani ya mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya II ambapo mpaka hivi sasa havijaanza kuwekewa umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie kuna mkakati gani wa kuwezesha vijiji hivi kuwekewa umeme kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa vile tatizo la maji katika Mji Mkongwe wa Tukuyu linafanana sana na tatizo la upatikanaji wa maji katika Mji Mkongwe zaidi Bagamoyo, ambapo huduma ya maji iko chini, maeneo mengi hayapati maji hasa eneo la Mji Mkongwe upatikanaji wake wa maji ni mdogo hata Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo iko katika ratiba ya mgao wa maji ambapo inasababisha huduma kuwa nzito katika Hospitali hiyo na maeneo mengine kama Kisutu na Nia Njema hakuna hata mtandao wa maji. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuboresha upatikanaji maji katika Mji wa Bagamoyo? (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Moja, kwa vile Waziri amekiri kwamba maji yanapatikana kwa mgao: Je, Waziri atakuwa tayari kuiagiza DAWASCO ili iiondoe hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo katika utaratibu wa mgao ili kuweza kuboresha huduma ya afya katika hospitali hii ya Wilaya?
Swali la pili; je, mradi huo wa usambazaji mabomba utajumuisha kata zote tisa za Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bagamoyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, isipokuwa nina maswali mawili ya nyongeza ya kuuliza. Moja, Mheshimiwa Waziri katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, tulitengewa fedha jumla ya sh.82,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa wodi kwenye Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, lakini mpaka hapa tunapoongea fedha hizi hazijapelekwa katika Halmashauri. Je, Mheshimiwa Waziri atatuhakikishia Bagamoyo kwamba fedha hizi zitaweza kutolewa kabla ya mwaka huu kumalizika ili tuweze kuboresha huduma katika hospitali hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amenijibu kuhusu ujenzi wa OPD kwa kutumia fedha za (own source) za kwetu wenyewe, lakini OPD hii ni mbovu sana; haina uwezo wa kuhudumia wagonjwa kwa kadri ambavyo ingeweza kutoa huduma ile ambayo wanasema inafaa kwa wananchi wale wa Bagamoyo. Inahitaji ujenzi mpya kabisa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari ku-commit kiasi cha fedha ili angalau tuweze kuijenga upya OPD hiyo?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Bagamoyo, vijiji vya Kondo na Kongo vilikuwa kwenye REA Awamu ya Pili lakini miradi hii haikutekelezwa na katika REA Awamu ya Tatu miradi ya vijiji hivi haimo. Nilishamsikia Mheshimiwa Naibu Waziri akitamka hapa Bungeni kwamba miradi yote ile ambayo haikutekelezwa kwenye Awamu ya Pili ndiyo itapata kipaumbele katika Awamu ya Tatu.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambiaje wananchi wa vijiji vya Kongo na Kondo waliokwemo kwenye Awamu ya Pili lakini wamefutwa kwenye Awamu ya Tatu?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye kutia moyo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; nilijulishwa na uongozi wa REA kwamba Vijiji vya Kongo na Kondo ambavyo havikutekelezewa miradi yake katika awamu ya pili vimeingizwa kwenye orodha ya miradi ya nyongeza kwenye REA-III ambayo imeombewa kibali kwa ajili ya utekelezaji. Sasa swali; je, lini kibali hicho kitaweza kutolewa ili miradi hiyo itekelezwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kufuatana na orodha ya miradi ya REA Awamu ya Tatu kwenye Jimbo la Bagamoyo, vijiji vingi katika Kata za Fukayosi, Makurunge, Mapinga, Kerege na Zinga havitopata umeme. Je, Serikali ina mkakati gani kuweza kuvipatia umeme vitongoji hivyo?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Bagamoyo imepata hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo mwaka 2005 na miaka 10 baadaye mwaka 2015 baada ya kujitathimini na kuona tumetimiza vigezo tumeomba kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji. Je, Serikali inatupa jibu gani kuhusu Bagamoyo kupandishwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mwezi Septemba, 2015 Serikali iliwalipa fidia wananchi wanaopisha mradi wa bandari katika Vijiji vya Pande na Mlingotini. Miongoni mwao wananchi 687 walibainika kwamba walipunjwa fidia zao; kwa hivyo Serikali iliwafanyia uhakiki mwezi wa kwanza mwaka jana ili kubaini fidia stahiki za wananchi hao. Je, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia zao stahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tarehe 22 Mwezi wa sita mwaka jana wakati anazindua kiwanda cha Elvin katika Kata ya Mapinga, Mheshimiwa Rais aliwatangazia wananchi wanaopisha mradi wa EPZ Bagamoyo kwamba wale wote ambao hawajalipwa fidia zao wanaweza wakarudi sasa katika maeneo yao wayaendeleze maeneo yao. Je, ni lini EPZA na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo itawaruhusu wananchi hao kumiliki maeneo yao kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais?
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani za wananchi wa Bagamoyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa namna ambavyo amesimamia ujenzi wa tenki kubwa la maji Bagamoyo, swali langu ni kuwa, je, lini mradi wa usambazaji wa mabomba ya maji katika Mji wa Bagamoyo pamoja na kata zote za Bagamoyo utaanza?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's