Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Maryam Salum Msabaha

Supplementary Questions
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa huu Mradi wa REA umesambazwa sana vijijini na nguzo zimewekwa sana vijijini, lakini nguzo hizi zimeanza kuoza. Je, ni lini Serikali itahakikisha nguzo hizi zinawekwa na wananchi wa vijijini wanapata umeme? Ahsante sana.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu ya Waziri na amekuwa mfuatiliaji sana wakati nauliza maswali yanahusu Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya jeshi inalindwa na Wanajeshi wenyewe, je, ni kwa nini kuna vikosi ambavyo vinavaa nguo za jeshi na kulinda mipaka ya jeshi na kuchafua taswira ya Jeshi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar, kipindi cha uchaguzi kumekuwa na vikosi vingi sana na vingine havina taaluma ya kutumia silaha na wamekuwa wakiwadhuru wananchi kwa silaha za moto na waliodhurika wengine ni wazee wakongwe wa miaka 60 na kuwapatia ulemavu wa kudumu. Je, Serikali ina mikakati gani kuunda Kamati Teule kukichunguza hiki kikosi cha Mazombe ili tutambue kwa mujibu wa sheria kimesajiliwa na Serikali ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naona Mheshimiwa Naibu Waziri sijui alikuwa kalala, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kambi hii niliyoitaja hasa hii Mesi ya Ulinzi na Usalama ipo katika mazingira ambayo siyo rafiki sana na jamii iliyowazunguka, upande kuna Skuli ya SOS na upande kuna Msikiti, pia kunakuwa na vitendo ambavyo vinaendelea pale ambavyo siyo rafiki na jamii inayowazunguka. Je, ni lini Serikali itahakikisha inatenga fedha za kutosha ili kukarabati Kambi hii na hasa hii Mesi ya Jeshi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vikosi vingi vya Ulinzi na Usalama vinaishi uraiani na vinakuwa siyo rafiki sana na wananchi hasa wananchi ambao siyo waadilifu na nchi yao. Je, ni lini Serikali itahakikisha vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vinajengewa makazi bora na yenye sifa kama vikosi vya Ulinzi na Usalama?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa huu umeme wa REA wananchi wengi hawajapata elimu ya kusaidiana na Serikali katika kutoa maeneo ya kuweka huu umeme wa REA. Je, Serikali mna mpango gani kuhakikisha mnakwenda kijijini kutoa hii elimu ili wananchi watoe maeneo haya ya kupitisha umeme wa REA?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya vituo vingi Zanzibar ni vibovu na majengo ni chakavu na askari hawana vitendea kazi wanapokamata wahalifu kama wino wa kuchapisha barua na mahitaji mengine muhimu na hata wahalifu wale hawapati hata mkate kwa sababu siyo wahalifu wote wana jamaa wa kwenda kuwaangalia kwenye vituo vya polisi wanapokuwa mahabusu.
Je, ni lini Serikali itahakikisha vituo vyote vinapatiwa huduma stahiki za kuendesha kazi zao kwa wakati muafaka.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa watumishi hawa wanaohamishwa katika sekta ya afya wanacheleweshewa mafao yao huko wanakopelekwa. Je, Serikali itahakikishaje wanapata stahiki zao kwa wakati muafaka?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimwulize Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza kutokana majibu yake kuwa marefu sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bandari bubu zipo mipakani; vyombo vya ulinzi na usalama huwa vinakutana na changamoto kwenye bandari hizi. Je, Serikali mnatambua kama vyombo hivi vinakutana na changamoto kubwa kudhibiti silaha na hata magendo? Mna mpango gani kuongezea vyombo vya ulinzi na usalama, stahiki zao na hata vifaa vya utendaji kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa majahazi ndiyo yanayotumika kufanya sana uhalifu, kubeba madawa ya kulevya na hata kutorosha bidhaa haramu kama pembe za ndovu: Je, Serikali mna mikakati gani kukagua majahazi na kudhibiti vyombo hivi vya majahazi ndani ya bahari na ukaguzi wa mara kwa mara?
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na pole sana. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa rehma. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi za wenzetu kama kwa mfano nchi za jirani South Africa na nchi nyingine wametenga maeneo kwa ajili ya mama lishe, maeneo rafiki na wanauza vyakula vyao bila kubughudhiwa.
Je, Serikali mna mikakati gani kuhakikisha mnatenga maeneo maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo hasa mama lishe?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zama hizi tumeona askari wakifanya mazoezi katika barabara wakiwa na silaha za moto na kwa mujibu wa sheria vikosi vyote vya ulinzi na usalama wana maeneo yao maalum ya kufanyia mazoezi. Je, Serikali haioni kwamba wanawapa maadui nafasi kuona udhaifu wa askari wetu na kuingiza maadui kupambana na vyombo vya ulinzi na usalama? Ni kwa nini vyombo hivi visibaki sehemu zao za kufanyia mazoezi huko huko vilikopangiwa?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Zanzibar kumekuwa na matukio ambayo yanaendeshwa na vikosi vya Janjaweed; na kama Kikosi cha Polisi mna taarifa hiyo, ni kwa nini kikosi hiki kimekuwa kikifanya matukio ya kuumiza wananchi na kuwasababishia ulemavu wa kuendelea na hata kutokujitafutia riziki kwa mahitaji yao ya kila siku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali kipindi cha uchaguzi kunakuwa na matukio mengi sana ya kupiga wananchi ambao hawana silaha na mnapambana nao na kuwaachia ulemavu wa kudumu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu ya Serikali.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, hili tatizo la matundu ya choo hasa shule ambazo ziko pembezoni, shule za vijijini siyo rafiki sana na watoto wa kike pamoja na wanafunzi kwa ujumla. Ni lini Serikali itahakikisha tatizo hili la matundu ya choo linakwisha mara moja?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na tabia ya wananchi au vyombo vya ulinzi na usalama na wengine ambao wanakwenda kwenye mafunzo ambayo siyo halali kutesa raia wasiokuwa na hatia na kuwasababishia maumivu makali na hatimaye kupelekwa rumande bila kupatiwa huduma za kiafya. Je, Serikali hamuoni kama mnavunja haki za binadamu na utawala bora?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda na mimi nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa hii michezo ya kamari imekuwa ikichezwa kwenye stendi kubwa na sehemu za starehe na kupelekea watu kufilisika na wengine kufikia hatua hata ya kujiua. Je, hamwoni sasa ni wakati muafaka wa kukataza michezo hii isichezwe na wale wanaochezesha michezo hii wachukuliwe hatua?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wajasirimali wadogo wadogo hasa mama lishe na wamachinga na ambao wengine wana vipato vya chini wamekuwa wakikopa mikopo kwa ajili ya biashara zao na kutozwa riba kubwa na kushindwa kurejesha mikopo ile na kufilisiwa.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya Wajasiriamal wadogo wadogo na kuwatoza riba ambayo inaendana na biashara zao?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Nami naomba nimuulize Naibu Waziri swali
dogo la nyongeza. Kwa kuwa ongezeko la watoto wa
mitaani linachangiwa na akinababa kukataa mimba na
kukataa familia zao. Je, Serikali inaweza kusema mpaka sasa
hivi ni akinababa wangapi wameshatiwa hatiani na
kufunguliwa mashtaka ili kutunza familia zao?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Watanzania wengi
wanategemea bandari na kumekuwa na ukiritimba wa kutozwa kodi mara kwa mara wafanyabiashara sasa hivi wanakwepa bandari zetu, je, Serikali ina mikakati gani kuweka utaratibu mzuri wa utozaji kodi katika mizigo ya wafanyabiashara ili biashara zipate kupita katika bandari zetu?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba nimwulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna wananchi ambao wanakamatwa kwa uhalifu mbalimbali, aidha wa kubandikiziwa kesi na kupata kipigo kikali sana na kufanyiwa majeraha kwenye miili yao na kufikishwa kwenye vyombo vya mahabusu bila kupatiwa huduma za afya, hamuoni kama mnakiuka haki za binadamu?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna migodi ambayo inakuwa imeshafungwa na inakuwa si salama kwa wachimbaji wadogowadogo na hawa wachimbaji wadogowadogo wamekuwa wakikiuka sheria na kuvamia migodi hii na kuhatarisha maisha yao. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha uvamizi huu wa wachimbaji wadogowadogo unakwisha na kuchukulia hatua za kisheria?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sambamba na kuokoa tatizo la akina mama katika uzazi salama bado akina mama hao wamekuwa wamachinga wa kubeba vifaa mbalimbali wakati wa kwenda kujifungua. Je, kama Serikali mnatambua tatizo hili ni lini Serikali mnahakikisha mnatenga bajeti ya kutosha katika hospitali zote za akina mama na akina mama wakifika kule kujifungua wapate huduma salama? (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, lakini kuna genge la wahuni ambalo hatujui wanapata wapi silaha za kijeshi na kushambulia raia wasiokuwa na hatia.
Je, Serikali haioni sasa imefika wakati muafaka kufanya doria katika sehemu zote za mipaka na barabarani na hata katika vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha genge hili halina nguvu kwa sababu linachafua taswira ya Tanzania katika medali za kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa bado silaha hizi zinaendelea kuuzwa sehemu za starehe kama vile minadani na sehemu mbalimbali na kuhatarisha amani ya ambao wanafika katika kupata huduma katika sehemu hizo.
Je, Serikali ina mikakati gani ya ziada kuhakikisha suala hili kuuza silaha holela linakomeshwa na wale wanaokamatwa wachukuliwe sheria kali ili suala hili likome mara moja? (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakijiajiri kwa kupitia uvuvi wa bahari kuu, lakini vijana hawa hawana mitaji ya kuendeleza sekta hii ya uvuvi.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha vijana hawa wanapatiwa angalau mikopo ya bei nafuu ili wapate kujiendeleza katika sekta hii ya uvuvi?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Ziwa Tanganyika kumekuwa na tatizo la wavuvi wengi kuvamiwa hasa kutoka nchi za jirani kama Congo, wale wavuvi wamekuwa wakipata shida sana. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha hawa wavuvi wanaotoka upande wa Kigoma nao angalau wanaridhika na rasilimali zao na kutokunyanyaswa na raia ambao wanatoka Congo na nchi jirani za Burundi? (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Ziwa Tanganyika kulikuwa na uharamia, wale wavuvi walikuwa wakivamiwa na maharamia kutoka nchi za jirani na kuwapokonya nyavu zao na hata mitumbwi yao. Je, Serikali imedhibiti vipi maharamia hawa katika Ziwa Tanganyika?(Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi nipate kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na tatizo la watoto wa mitaani hasa kwenye miji mikubwa kwa mfano, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na kadhalika na watoto hawa wamekuwa wakitumiwa kwenye masuala ya uhalifu kama madawa ya kulevya na kadhalika. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha watoto hawa wanarudi shuleni na kupata angalau malezi bora? (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kuwa haya maswali tumekuwa mara kwa mara tunauliza na hakuna utekelezaji. Je, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri nusu mwaka wa fedha unakwishwa. Ni majengo mangapi yamekarabatiwa kwa upande wa Zanzibar na ni vituo vingapi vya kambi vya Kambi za Jeshi kwa upande wa Zanzibar vimekarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa hivi vituo vya afya tunavyoviulizia ambavyo vipo kwenye makambi ya Jeshi havihudumii tu majeshi na familia zao, zinahudumia pia na jamii zilizowazunguka na hasa hichi kituo nilichokiulizia kiko sehemu ambapo ajali zinatokea mara kwa mara.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha vituo vyote vya majeshi vinapata dawa kwa wakati muafaka na sitahiki zinazofaa kwa wakati muafaka? Ahsante.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa vijana wetu wanaanza vipaji wakiwa mashuleni, je, Serikali ina mpango gani kuipa sekta ya michezo hasa mashuleni ili angalau vijana hao tuwakuze katika vipaji vya michezo ili tuweze kufikia kama nchi ya Brazil?
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Mwenyezi Mungu akupe wepesi katika siku hii ya leo kwa sababu Wabunge umewafurahisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, kuna watu wanafanya makusudi kabisa kuambukiza wenzao ugonjwa huu. Mtu anajua kama ni muathirika wa UKIMWI lakini anambukiza watu kwa makusudi hata watoto wadogo ambao ni wanafunzi wa vyuo. Je, Serikali ina mikakati gani kwa hawa ambao wanafanya maambukizi ya makusudi kwa wanafunzi wa vyuo na hata kwa ambao hawajaambukizwa maradhi haya? Naomba tamko la Serikali. (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's