Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Supplementary Questions
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa tatizo la kivuko cha Kitunda, Lindi linafanana sana na tatizo la kivuko baina ya Kilindoni na Nyamisati katika Wilaya ya Rufiji; na kwa kuwa, wananchi wa Mafia kupitia Mbunge wao, tuliiomba Wizara itupatie iliokuwa MV Dar es Salaam, ambayo kwa sasa imepaki pale Navy, Dar es Salaam ili ije itusaidie Mafia kuunganisha baina ya Kilindoni na Nyamisati. Je, ni lini Wizara itaridhia ombi hilo?
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwa kuwa, tatizo la Nyamagana la nyumba za makazi ya Polisi linafanana sana na tatizo la makazi kwa Polisi wa Kisiwa cha Mafia. Je, Mheshimiwa Naibu waziri anaweza kulitolea maelezo gani tatizo la makazi kwa Polisi wa Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Kwa kuwa gati ya Bukondo linafanana sana na kesi iliyopo kwenye gati la Nyamisati na la Kilindoni kule Mafia.
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Gati la Nyamisati, na lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la abiria kwa Gati la Kilindoni?
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwanza Naibu Waziri anakiri kwamba barabara ile imejengwa chini ya kiwango;
lakini Naibu Waziri atakubaliana na mimi, alipotembelea Mafia tuliikagua barabara hii mimi na yeye. Barabara hii si ya kufanyiwa matengenezo makubwa, ni ya kurudiwa upya.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, ng’ombe akikatisha kwenye barabara anaacha mashimo, barabara ya lami! Gari likipata
puncture ukipiga jeki, jeki inakwenda chini kama unapiga jeki kwenye tope, kule Mafia wanaiita barabara ya big G
(chewing gum).
Mheshimiwa Spika, sasa nina maswali mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali inakiri kwamba mkandarasi
huyu ameijenga chini ya kiwango, ni hatua gani za kimkataba na za kisheria zimechukuliwa dhidi ya huyu
mkandarasi aliyeisababishia Serikali hasara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa maeneo ya Kilindoni, Kiegeyani na Utende ambao wahanga wa kubomolewa nyumba zao, wengine walikuwa ni wahanga wa kubomolewa nyumba zao, wengine wamekatiwa minazi yao na mikorosho yao na mazao yao mbalimbali, mpaka leo wengi wao hawajalipwa fidia kutokana na ujenzi wa barabara ile, ningependa nisikie kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, nini hatma ya waathirika hawa wa fidia? Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Wilaya ya Mafia imezungukwa na bahari na hakuna Police Marine na kuna matishio ya Maharamia wa Kisomali. Je, ni lini sasa Serikali itafikiria uwezekano wa kuleta doria ya Police Marine katika Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kumuuliza swali moja Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari Mafia, imeshindwa kazi yake ya msingi ya kuzuia uvuvi haramu na uhifadhi na hivi sasa inauza visiwa na maeneo Wilaya Mafia. Je, Sasa Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuondoa uongozi wa juu pale na kubadilisha kuleta uongozi mwingine?Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la Songea Mjini linafanana sana na tatizo lililopo katika Wilaya ya Mafia. Wilaya nzima ya Mafia haina hata Kituo kimoja cha Afya. Ukizingatia kwamba alipokuja Waziri Mkuu tulimwomba suala hili na mchakato tumeshauanza katika ngazi ya Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itatupatia Kituo cha Afya angalau kimoja pale Kilongwe kwa kuongeza hadhi ile zahanati iliyopo pale?
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru pia ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii sio ahadi tu ya Rais Mstaafu na kwenye Ilani ya Uchaguzi bali pia ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea Wilaya ya Mafia mwezi Septemba, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mafia kwa kuwa ni kisiwa, hali ya upatikanaji wa udongo ni ndogo sana. Udongo unapatikana katika kijiji kimoja cha Bweni na wataalam wanasema baada ya miaka miwili udongo huo utakuwa umekwisha kabisa. Kwa hiyo, mtakapokuwa tayari kuja kujenga barabara ya lami, udongo Mafia utakuwa umekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, sasa kwa kuwa Ilani ya CCM inasema mwaka huu mtaanza na usanifu na katika majibu yako hujasema hata kama usanifu utafanyika, swali la kwanza; kwa nini usanifu usifanyike mwaka huu ili ujenzi ufanyike mwakani?
La pili; ni kwanini sasaSerikali isitilie maanani hili suala la ukosefu wa udongo na kuharakisha ujenzi huu ifikapo mwakani? Ahsante.(Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya vituo vya reli yanafanana sana na matatizo ya vituo vya boti vinavyomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari - TPA. Kituo cha boti cha Nyamisati hakina vyoo, maji na migahawa. Je, ni lini Naibu Waziri ataielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari - TPA wakajenge vyoo, maji, umeme pamoja na masuala mengine ya kijamii? Ahsante sana.(Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mafia ina vivutio vingi sana akiwemo huyu samaki wa ajabu anayeitwa Potwe au whale shark. Vile vile Mafia kuna maeneo mazuri sana ya scuba diving, sports fishing na kuna fukwe tulivu. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mafia kama Wilaya mpaka leo haina Afisa wa Utalii. Sasa swali la kwanza, ni lini Serikali itatupatia Afisa wa Utalii katika Wilaya ya Mafia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itaruhusu
au itaifungulia ile hoteli ambayo Mheshimiwa Simbachawene alikuja akaifunga ya Chole Mjini, ambapo wananchi wanapata pale ajira, Serikali inapata kodi na wale wawekezaji pale walikuwa wanasomesha vijana wengi katika kisiwa cha Chole, sasa ni nini tamko la Serikali juu ya kuondoa tofauti zilizokuwepo ili ile hoteli iendelee kufanya kazi? Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa fursa hii.
Tatizo la mgogoro wa shamba la Madaba linafanana sana na tatizo la shamba la Kigomani na Utumaini lililopo Wilayani Mafia.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuja Mafia kukaa na wadau wa Halmashauri pamoja na Viongozi wengine kutatua tatizo hilo?
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Kwa kuwa Serikali imepiga marufuku uvuvi wa majongoo bahari Kisiwani Mafia; wakati huo huo majongoo bahari yanavunwa kule Zanzibar upande wa pili wa Muungano.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kuruhusu uvuvi wa majongoo bahari kuendelea Mafia?
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Tatizo la viboko lililopo katika Jimbo la Ulanga linafanana sana na tatizo la viboko lililopo Kisiwani Mafia. Wananchi wa kata za Ndagoni, Baleni na Kirongwe wameharibiwa mazao yao na ng’ombe wao wameuwawa na viboko waharibifu. Kutokana na ongezeko kubwa sana la viboko hawa na Kisiwa cha Mafia ni eneo dogo, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutoa ruhusa tuanze kuwavuna viboko hawa kwa sababu kule ni kitoweo pia? Ahsante. (Kicheko)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri na yenye kutia matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Jibondo kimejengeka kutokana na mawe na miamba mikubwa, huwezi ukachimba kisima pale ukapata maji. Wananchi wa Jibondo wamekuwa kwenye kadhia ya ukosefu wa maji toka dunia hii iumbwe, wanapata maji ya bahari na mara chache maji ya mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba usanifu pamoja na ujenzi utaanza mwaka ujao wa fedha.
Nilikuwa naomba aliahakikishie Bunge lako, ujenzi huu utaanza lini? Kwa sababu usanifu na ujenzi vyote vimewekwa pamoja, utaanza lini na utachukua muda gani ili nikitoka hapa niende nikawaambie wananchi wa Jibondo kwamba tarehe fulani maji yataanza kutoka Jibondo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuingia katika vitabu vya historia na kuwa Waziri wa pili kufanya ziara katika Kisiwa cha Jibondo toka Mzee Malecela alipofanya hivyo miaka ya 1970 akiambatana na mimi Mbunge wa Jimbo? Ahsante. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri hapa kwamba kutokana na jiografia yake kisiwa cha Mafia, kiwanja cha ndege ni muhimu sana katika kukuza uchumi. Lakini mimi nataka nimuongezee, kuna ziada pia masuala ya jamii. Hivi ukiwa Mafia ikifika saa kumi na mbili na ukapata dharura ya ugonjwa huna namna ya kutoka kwenda katika Hospitali ya Rufaa kwa sababu kiwanja hakina taa.
Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba usanifu na upembuzi ulishafanyika toka mwaka 2009 na leo ni miaka minane kwa hesabu za haraka bado unakuja kutuambia kwamba pesa hazija patikana?
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini hizi pesa zitapatikana ili ujenzi wa kuweka taa katika uwanja wa Mafia na jengo la abiria ufanyike?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kurukia na kutua yani runway ya kiwanja cha Mafia ina mita kama 800 hivi, hivyo ndege kubwa haziwezi kutua na unasema kuna fursa za kitalii pale.
Je, ni lini sasa Serikali itaongeza urefu wa uwanja ule kwenda mpaka kilometa mbili ili kuruhusu ndege kubwa zitue moja kwa moja kutoka Ulaya na kuleta watalii Mafia? Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya wavuvi wadogo katika Ziwa Tanganyika yanafanana sana na matatizo ya wavuvi wadogo katika Kisiwa cha Mafia. Taasisi ya Hifadhi ya Bahari Mafia imekuwa ikiwanyanyasa na kuwabambikia kesi wavuvi wadogo wa Mafia na kuwanyang’anya nyavu zao. Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kufanya ziara Mafia na kutukutanisha sote ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili?
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri sambamba na Waziri mwenye dhamana wamekuwa mara kadhaa wakijibu maswali hapa na kuahidi kwamba, visiwa vidogo vyote nchi nzima vitapatiwa umeme wa solar. Sasa ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini umeme wa solar utakwenda katika Visiwa vya Jibondo, Chole, Juani na Bwejuu? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya usafiri wa baharini ya Bumbwini yanafanana sana na matatizo ya usafiri baina ya Bandari ya Kilindoni, Mafia na Bandari ya Nyamisati, Kibiti. Wananchi wa Mafia wamekuwa wakisafiri katika maboti ya mbao ambayo si salama na hayana bima.
Je, ni lini Serikali itainunulia Wilaya ya Mafia boti ya kisasa kuondokana na tatizo la usafiri baina ya Bandari ya Nyamisati na Kilindoni ili kuepusha maafa? (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, hali ya usalama wa abiria na mizigo katika bandari ya Kilindoni kwa zaidi ya miezi mitatu sasa iko mashakani kufuatia kukatika kwa ngazi katika gati la Kilindoni. Abiria wanalazimika kupanda kwa kutumia mitumbwi na viboti vidogo vidogo kwenda kupanda boti kubwa hali ambayo ni hatari sana kwa usalama wao.
Sasa je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuhakikishia Wananchi Mafia kwamba atawaelekeza watu wa Mamlaka ya Bandari waje watengeneze warekebishe gati lile ili lianze kutumika? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la kutoanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo linafanana sana na tatizo la kutokuanza ujenzi wa Bandari ya Nyamisati katika Wilaya ya Kibiti. Bandari ya Nyamisati ni Bandari ambayo ni kiungo baina ya wananchi wa Mafia wanapokuja Dar es salaam. Mkandarasi ameshapatikana toka mwaka jana mpaka leo hajafika site, ni nini kauli ya Serikali kuhusu Mkandarasi huyu? Nakushuru.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's