Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Abdallah Hamis Ulega

Supplementary Questions
MHE. ABDALLAH HAMISI ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali naomba sasa niulize majibu ya maswali mawili ya nyongeza.
(a) Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda Jimboni Mkuranga katika vijiji hivi vya Magawa, Msonga Makumbeya na vinginevyo pata athari hii ili aweze kujionea yeye mwenyewe na kuona namna iliyobora zaidi ya kutusaidia?
(b) Ningeomba niulize Serikali sasa ipo tayari kuhakikisha kwamba viuatilifu kwa maana ya sulfur, iweze kupatikana kwa wingi na kwa wakati katika Jimbo letu la Mkuranga ili kuepusha madhara haya ya ugonjwa wa mikorosho na kuhakikisha uzalishaji mkubwa zaidi ili kuwaondolea wananchi wangu umaskini?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwa kuwa, tatizo hili la Ushetu la mawasilinao lipo pia katika Jimbo langu la Mkuranga katika vijiji kama vile vijiji vya Mkuruwiri, Nyanduturu, Kibesa, Msolwa, Kibewa na kwingineko. Je, Serikali ina mipango gani ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wa vijiji nilivyovitaja na vinginevyo viweze kupata mawasiliano ya simu na wao waweze kuwasiliana na ndugu zao na shughuli zao zingine za kijamii na kiuchumi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Jimbo langu la Mkuranga liko tatizo la wafanyakazi wanaofanya kazi katika viwanda hivyo vya Wachina, kulipwa malipo madogo kwa muda mrefu wa kazi. (Makofi)
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja Mkuranga kuonana na vijana wale wanaofanya kazi katika viwanda vile na kuzungumza nao na hatimaye kuweza kuwapa matokeo ya kuweza kuwasaidia kama Serikali?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo hili la kifaa cha x- ray katika Hospitali ya Nyamagana ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amelijibu na sisi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Mkuranga linatusumbua; je, Serikali inaweza kutuhakikishia kwamba katika mgao huo wa vifaa tiba hivi hospitali ya Wilaya ya Mkuranga itakuwa ni miongoni mwa hospitali zitakazopata kifaa hiki cha x-ray ili kuwaondoa wana Mkuranga na adha ya kusafiri umbali mrefu mpaka Dar es Salaam katika Hospitali ya Temeke? Ahsante.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la wafanyakazi hasa vijana kufukuzwa kazi kiholela, kutokulipwa stahiki pindi wapatapo ajali kazini, kulipwa ujira mdogo sana wa shilingi 4,500 kwa kutwa ya siku, kufanyishwa kazi kwa muda mrefu kinyume cha sheria na taratibu za nchi lipo pia katika Wilaya yangu ya Mkuranga.
Je Serikali ina mpango gani wa kuwalinda vijana hawa wafanyakazi ili waweze kazi zao kuwa ni kazi zenye staha? Ahsante.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii uliyonipatia.
Kwa kuwa tatizo la ujambazi linaloipata Mikoa ya Kagera na Kigoma lipo pia tatizo la namna hiyo katika Jimbo letu na Wilaya yetu ya Mkuranga ambapo hapa karibuni tulipata tatizo la uvamizi wa majambazi katika Benki yetu ya NMB, Bupu na pale Mbagala Rangitatu na mengineyo.
Je, Serikali sasa iko tayari kuhakikisha kwamba Wilaya yetu ya Mkuranga inapata nyongeza ya vifaa kazi lakini pia na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nasi wananchi wa Mkuranga tumeomba miradi ya umeme katika baadhi ya vijiji vyetu zaidi ya 30, vikiwemo Vijiji vya Mlamleni, Lugwadu, Mkola, Kazole, Lukanga, Mwajasi, Vianzi, Malela na vinginevyo, je, miradi hii itakamilika katika muda gani ili wananchi wale waweze kujiandaa kupokea miradi hii ya umeme?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu haya, ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Kama Serikali ilivyosema kwamba tunayo barabara ya lami ya kutuunganisha na Dar es Salaam. Sisi watu wa Mkuranga tunataka barabara itakayotuunganisha, Kisarawe mpaka Kibaha moja kwa moja, uwezekano wa kufanya hivyo upo, tunayo barabara ya kutoka Kimanzichana mpaka Mkamba, Mkamba mpaka Mkuluwili, Mkuluwili inapita katika Bonde la Saga, na kwenda kutokea Msanga, takapofika pale Msanga, itakwenda kuungana na barabara ya Manelomango inayotoka Mzenga, Mlandizi, inakwenda mpaka Mloka.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo imeahidiwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Namuomba Waziri aichukue barabara hii, aziagize mamlaka zinazohusika ziweze kutuunganisha sisi watu wa Mkuranga, Kibiti, Rufiji kwa pamoja na Wilaya ya Kisarawe mpaka Kibaha.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza, matatizo haya ya watu wa Tarime Vijijini ni sambamba na matatizo ya watu wa Jimbo la Mkuranga kuhusu barabara ya kutoka Mkuranga Mjini mpaka Kisiju kwani ni barabara inayounga wilaya mbili za Mafia, ni barabara inayobeba uchumi wa korosho, ni barabara inayobeba watu zaidi ya laki moja na ni barabara ambayo itakuwa ni tegemezi katika uchumi wa viwanda vitakapojengwa katika Kata ya Mbezi. Je, kwa kuwa hii pia ni barabara iliyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano, ni lini na yenyewe itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo haya ya mawasiliano yaliyopo katika Jimbo la Korogwe Vijijini, yako pia katika Jimbo langu la Wilaya ya Mkuranga katika Kata ya Panzuo, katika Vijiji vya Mkuruwili, Kibesa na Kibuyuni, Kisegese, Chamgoi; Kata ya Kitomondo katika Kijiji cha Mpera na Mitandara na katika Kata ya Bupu katika Kijiji cha Mamdi Mkongo, Mamdi Mpera na hata kule Tundu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Mheshimiwa Waziri aniambie, ni lini wananchi hawa wa vijiji nilivyovitaja katika Wilaya ya Mkuranga watapata mawasiliano ili na wao waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa MWenyekiti, pamoja na majibu hayo mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo langu la Mkuranga utafiti ulishafanyika na ikagundulika gesi asilia katika kijiji cha Kiparang‟anda na kisima kiko pale. Naomba sasa Serikali inieleze ina mpango gani wa kuhakikisha kisima kile cha gesi kilichopo pale Mkuranga kinatumika kwa manufaa ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha gesi hii inatumika ipasavyo katika kuzalisha umeme wa uhakika ili kikidhi haja ya viwanda na makazi yanayokuwa kwa kasi katika Jimbo hili la Mkuranga? Ahsante
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la dogo nyongeza. Barabara ya kutoka Mkuranga Mjini mpaka Kisiju Pwani ni miongoni mwa barabara ambayo zimekuwa zikiahidiwa pia kuwekwa lami na Awamu ya Nne na hata Awamu hii ya Tano. Barabara hii inapita katika Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Mkuranga lakini pia inapita katika Hospitali yetu Kuu ya Wilaya ya Mkuranga. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itatusaidia kuhakikisha barabara hii inawekwa lami kutoka Mkuranga Mjini kupita Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Hospitali ya Wilaya mpaka Kisiju Pwani?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kwa namna ya kipekee kabisa wakati nikijielekeza kuuliza swali hilo niipongeze sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya ya kuwalinda wakulima wetu na wananchi wetu wa hali ya chini. Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hiyo pia nimpongeze Mkuu wetu wa Mkoa Engineer Evarist Ndikiro kwa kazi nzuri aliyoifanya mwaka wa jana wa kuyalazimisha Makapuni mawili ya Alpha Choice na Kaisari ambayo yaligoma kuwalipa kwa wakati wakulima wa korosho wa vijiji vya Msonga, Kalole, Mkuranga mjini na Kimanzichana Kusini. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri anaeleza kwamba wanapochelewesha…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Ahsante sana. Wanapochelewesha kulipa malipo ya wakulima wa korosho huchelewa. Je, Serikali ipo tayari sasa kuhakikisha inawasimamia ipasavyo na madhubuti kabisa wanunuzi hao ili wawe wanaondoa mazao yao katika maghala yetu mapema iwezekanavyo ili mzigo mwingine wa wakulima uingie kwa wakati na waweze kupata pesa za kuinua maisha yao?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ningeomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie sawa na jibu lake la msingi ya kwamba kazi mojawapo ya Polisi ni ulinzi wa raia na mali zao. Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Wilaya hii ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji juu ya usalama wao na wa mali zao kipindi hiki cha operesheni ya kutafuta wahalifu ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru bila ya kubigudhiwa? Ahsante.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa rufsa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya yaliyopo kwenye Mkoa wa Katavi yako pia katika imo jimbo langu la Mkururanga kilometa 60 tu kutoka katika Mkoa wa Dar-es salaam ambapo kata za Kwanzuo Kisegese, Mkamba na kwingineko ikiwa ni pamoja na kijiji ambacho wewe unalima kijiji cha Koragwa Tundani na pale Mkuranga maeneo ya Kiguza. Yote yana shida ya mawasiliano.
Je, Mheshimiwa Naibu yuko tayari yeye na hao viongozi wa huo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kushirikiana name kuhakikisha maeneo haya yanapata mawasiliano? (Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaondoa migogoro hii ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kwetu sisi wakulima wa korosho, hapa juzi Serikali imetutangazia kutupatia sulphur kwa maana ya pembejeo ya kilimo bure. Je, Serikali imejipangaje katika usambazaji wa sulphur hii ya bure ili iweze kutufikia kwa wakati na ya kutosha?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kuhusiana na ujenzi wa kituo cha mabasi ya Kusini katika eneo la Jimbo la Mkuranga; na kwa kuwa uratibu wa zoezi zima la ujenzi wa kituo cha mabasi ya Kusini linasimamiwa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuhakikisha wanashirikiana vema, Wizara ya TAMISEMI, Maliasili na nyingine zinazohusika kuhakikisha kituo hiki cha mabasi ya Kusini kinapatikana kwa haraka katika eneo la Wilaya ya Mkuranga hasa maeneo ya msitu ule wa Vikindu? (Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa ni wa muda mrefu sasa, wao wenyewe wameridhi kutoka kwa wazazi wao ambao wameshafariki, na wao wenyewe miongoni mwao wanaelekea kuwa watu wazima sasa, ni lini Serikali itawalipa haki zao wananchi hawa, ilimradi wale warithi wao wasisumbuke kama ambavyo wao sasa hivi wanavyoishi, wakiwa hawaelewi ni lini watalipwa pesa zao? (Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, asante sana, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake lenye kuleta matumaini ya kwamba siku moja na sisi watu wa Mkoa wa Pwani tunaweza tukapata madini ya dhahabu, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ninependa kujua ni lini sasa Wizara itaanza kukitumia kisima cha gesi kilichopo katika eneo la kijiji cha Kiparang’anda ndani ya Wilaya ya Mkuranga ili kiweze kupata na kutuletea faida watu wa Mkuranga na Taifa letu kwa ujumla?
Swali la pili, ningeomba Naibu Waziri wa Nishati na Madini anieleze Wilaya ya Mkuranga tunachimba madini ya aina ya mchanga, madini ambayo kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam hayachimbwi yanachimbwa tu Mkuranga. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na sisi watu wa Mkuranga kuboresha ushuru na tozo mbalimbali ili madini haya yaweze kuleta tija kwa watu wa Mkuranga?
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu katika majibu ya msingi ameeleza kwamba Wilaya za Kibiti, Rufiji na Wilaya yangu ya Mkuranga ni miongoni mwa Wilaya ambazo wavuvi wake hajaomba mikopo. Inawezekana kabisa kutokuombwa kwa mikopo hii ni kutokana na ukosefu wa elimu ya kuweza kuwafahamisha na kuwawezesha waweze kuwa na uelewa wa kuomba hii mikopo.
Sasa swali langu, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie moja kwa moja ni lini tunaweza tukashirikiana sisi na wao ili kwa haraka zaidi Watanzania hawa wa Kisiju, Kibiti Delta na Rufiji mpaka Bagamoyo waweze kutumia fursa hii ya mikopo inayotolewa? (Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kupata fursa hii. Kama ilivyoshida ya walimu katika jimbo la ndugu zangu wa Mbagala na sisi watu wa Mkuranga tunashida kubwa ya upungufu wa walimu. Serikali inanipa ahadi gani ya kuhakikisha kwamba upungufu ule wa walimu unapungua? Ahsante.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mji wa Mkuranga ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi sana; na kwa kuwa visima vya maji vilivyoko katika Mlima Kurungu vilishachimbwa na maji yanamwagika kuelekea mashambani; na kwa kuwa tumeshaomba shilingi milioni 800 Serikalini ya kuhakikisha tunayatoa maji yale ya Mto Kurungu kuyaleta Mkuranga Mjini na Vijiji vya jirani vya Kiguza, Dundani, Kiparang’anda, Magoza, Tengelea na kwingineko. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kunihakikisha kwamba milioni 800 zile tutazipata kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mkuranga na vijiji hivyo vingine nilivyovitaja?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's