Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Susan Anselm Jerome Lyimo

Supplementary Questions
MHE. SUZAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni wazi kwamba Tanzania imeathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, lakini vilevile sababu kubwa pamoja na kwamba kuna sababu za nje, lakini kuna sababu za ndani ambayo kubwa ni ukataji hovyo wa miti, lakini Serikali kwa muda mrefu imekuwa na kaulimbiu ya kusema kwamba kata mti panda miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa nasikiliza au naangalia vyombo vya habari hapa Dodoma ambapo ni kati kati ya nchi na Makao Makuu, Mkuu wa Mkoa alikuwa anapanda miti na ikatolewa taarifa kwamba katika miti milioni mbili na laki tatu iliyopandwa ni miti mia tisa tu imeota, sawa na asilimia 0.039. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba wanafuatilia ili miti inapopandwa iweze kuota ili kuondoa tatizo la mabadiliko ya tabianchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, najua kwamba vyanzo vya kipindupindu hasa ni uchafu na hasa katika maeneo ya mikusanyiko kama vile kwenye masoko. Kwenye haya masoko huwa watu wanalipa kodi, lakini Serikali inashindwa kufanya usafi au kuzoa takataka. Je, Serikali sasa haioni kwamba yenyewe ndiyo chanzo cha kipindupindu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi kuna tahadhari kubwa sana ya ugonjwa wa homa ya zika ambayo homa hii sasa hivi iko kule Marekani ya Kusini, lakini Tanzania siyo kisiwa na wote tunajua kwamba zika ilianzia Uganda kwenye Milima ya Zika miaka hiyo ya 1920 au 1930 huko. Kwa hiyo, bado jana nimemsikia mtendaji mkuu wa World Health Organization akisema kwamba, kuwe na tahadhari.
Je, Tanzania kama nchi imejiandaaje hasa ukizingatia kwamba, wakati ugojwa wa ebola umetokea zile specimen zilipelekwa Nairobi, je, sasa hivi ukitokea hapa Tanzania tumejiandaje kama Serikali?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 20 Oktoba, 2015 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne alipokea magari ya washawasha 399 kati ya magari 777. Kati ya magari hayo ni magari 50 tu yalitumika. Nime-google bei ya gari moja ni sawa kabisa na kipimo cha MRI na Scanner kwa maana ya kwamba gari moja ni kama dola 400 na hiyo mashine bei yake ni hiyohiyo.
MWENYEKITI: Dola 400?
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Dola 400,000. Je, ni kwa nini sasa Serikali haioni kwamba huo ni upotevu mkubwa wa fedha na kutokuwajali wananchi na kwamba fedha hizo zingetosha kununua Scanner na MRI kwa nchi nzima kwenye Hospitali zote za Rufaa? (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ninataka kujua hii Hospitali ya Wilaya ambayo inajengwa hapo Kivule inagharimu kiasi gani kwa sababu mpaka sasa hivi anasema zimeshatoka shilingi milioni 1.9?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla una idadi kubwa sana ya wananchi na hospitali nyingi zimepandishwa hadhi. Kwa mfano, Hospitali ya Amana - Ilala ambapo wananchi wa Kivule wanakwenda pale, lakini mpaka leo huduma za afya bado ni mbovu sana.
Je, sasa Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba hospitali hizi zinazopandishwa hadhi ikiwemo na hii inayojengwa, inakidhi mahitaji ili wananchi waweze kupata huduma ya afya ambayo ni haki yao ya msingi?
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi, lakini lazima ni-admit kwamba nimefedheheshwa sana na majibu ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba elimu imeporomoka kama ambavyo amekiri lakini hajatupa mikakati. Katika majibu yake ya msingi anasema kwamba Walimu wamekuwa na morali, ni wazi kwamba Serikali labda haijui maana ya motivation theories na hawa Walimu wanapata motive gani. Ni wazi hilo suala la umeme miaka ya 60, 70 hapakuwa na umeme lakini nyumba za Walimu zilionekana. Sasa hivi mtoto anaona aibu kusema yeye ni mtoto wa Mwalimu, anaona afadhali hata aseme ni mtoto wa Mmachinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavyoongea Walimu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Susan, naomba uende kwenye swali tafadhali.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye swali, nataka kujua kama tuna tatizo kubwa la Walimu, Walimu wame-graduate toka mwaka jana mwezi wa tano mpaka leo tunapoongea hawajaajiriwa, hiyo ndiyo motisha? Kwa hiyo, naomba kujua ni lini Walimu waliomaliza masomo yao wanapata ajira zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, moja ya mikakati ni kuhakikisha kwamba Walimu wanapata mafunzo, lakini ukisoma ripoti ya CAG inaonesha Walimu hawajakwenda mafunzo, ni asilimia 11 ya Walimu wa sekondari ndiyo tu wanapata in-service program na Walimu wa primary ni asilimia 30. Ni lini Walimu hawa watapata in service training ili waweze kuendana na mazingira halisi ya ualimu na hasa kuhakikisha kwamba elimu yetu haiporomoki?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema samaki mkunje angali mbichi. Ujenzi wa kituo hicho hautakuwa na maana kama hatujawekeza huku chini. Tunatambua kwamba wakati Serikali inapanua elimu walihakikisha kabisa viwanja katika shule zetu za msingi havipo kwa maana kwamba walijenga shule za pili. Je, Serikali inasema nini kuhakikisha kwamba shule zetu za msingi zina viwanja ili watoto waanze kucheza riadha au michezo mingine ili sasa hivi vituo wanavyovijenga huku juu viwe na maana?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niulize swali moja dogo la nyongeza. Ukiangalia katika majibu amesema kwamba, mabadiliko haya yanafanywa baada ya utafiti, baada ya wataalam kuleta taarifa mbalimbali. Naomba kujua GPA imetumika kuanzia mwaka 2013 na sasa 2015 tayari imebadilika imekuwa madaraja, yaani ilikuwa madaraja ikaja GPA within a year, sasa naomba kujua huo utafiti ulifanywa lini hasa ikizingatiwa wataalam walioko Baraza la Mitihani ni wale wale kuanzia Mtendaji Mkuu? Kwa hiyo, naomba kujua huo utafiti umefanywa wapi na mazingira ya jamii ni watu gani walitaka hasa wabadilishwe kutoka madaraja kwenda GPA na kurudi tena kwenye madaraja?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli sijaridhikia kwa sababu ukiangalia kwa miaka takribani kumi toka wameanza kujenga hivi vipande vidogo vidogo wamejenga kilometa 19 tu, ina maana hizi kilometa 96 labda zitatumia miaka mingine 30.
Swali, kwa kuwa barabara hii sasa ilianza kujengwa kwa vipande vya lami toka mwaka 2008 ambapo lami zile ziliziba kabisa makalavati hali inayopelekea wananchi wa Ndungu na Maore ama kufariki au mazao yao kuharibika kutokana na mvua au maji yale yanayotuama.
Je, ni lini sasa mtahakikisha kwamba makalavati yale yanajengwa ili watani zangu kule wasipate matatizo pamoja na vifo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naelekea kwangu sasa, kwa kuwa barabara ya Kawawa hadi Marangu Mtoni ilijengwa kwa lami mpaka kiasi cha nusu, lakini cha ajabu barabara hiyo imejengwa kiwango cha lami madaraja yote hayajajengwa hali ambayo inapelekea magari kuanguka na watu wameshafariki, ni lini madaraja katika barabara hiyo yatajengwa hasa ukizingatia land scape ya Kilimanjaro?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo wote tunajua kuna tatizo kubwa sana la madawati na Halmashauri nyingi sasa hivi zinatengeneza madawati. Swali langu la msingi ni kwamba, je, ni nani anayedhibiti ubora wa madawati hayo? Kwa sababu yawezekana kabisa mbao hizo wakati mwingine zinaweza zikawa hazijakauka vizuri na maana yake ni kwamba hayo madawati hayatadumu. Swali langu ni nani anayedhibiti kuhakikisha kwamba mbao zinazotengeneza madawati hayo ni bora na zimekauka ili isiwe tunafanya kazi ya zimamoto? Nashukuru.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia suala la uhaba wa bajeti lakini naomba kuuliza; Benjamin Mkapa Foundation wamejenga vituo vya afya kule mkoa wa Rukwa ambako kuna matatizo makubwa sana; kwa mfano kuna Zahanati ya Kala - Nkasi, Milepa – Sumbawanga, Ngorotwa – Kalambo pamoja na ile ya Kishapu na wamekabidhi kwa Halmashauri toka Juni 2014, lakini mpaka leo havijatumika wakati kuna matatizo makubwa sana, ni kwa nini Serikali haijaweza kuvitumia vituo hivyo?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, disability is not inability. Kwa muda mrefu tumepiga kelele sana kwamba majengo hasa madarasa yawe disabaility friendly ili watoto wenye ulemavu waweze kusoma, lakini mpaka leo tunashuhudia madarasa yanajengwa hayana ngazi za kuwasaidia au ramps ili hawa watoto waweze kusoma kama wenzao na kwa kufanya hivyo suala la kwamba waongezewe muda wa kustaafu halitakuwepo. Serikali inatoa kauli gani kuhakikisha kwamba majengo yote ya Serikali yanakuwa disability friendly ili watoto waweze kuingia madarasani toka wakiwa na umri mdogo?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na sababu ambazo Mheshimiwa Waziri amezizungumza, naamini kabisa baadhi ya ajali, tena ajali nyingi sana zinatokea kwa sababu ya kutokuwa na alama barabarani pamoja na matuta makubwa sana. Tulishasema hapa Bungeni matuta yawe na standards. Ni lini Serikali itafanya matuta nchi nzima yawe ya standard ili kuepusha ajali ambazo siyo za lazima?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la shule hasa Kidato cha Tano na cha Sita ni la Kitaifa na hii inatokana na azma ya Serikali ya kuongeza Shule za Kata ambazo zilianzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne. Nimeshangaa sana Naibu Waziri alipozugumzia kwamba hizi Shule za Kidato cha Tano na cha Sita ni za Kitaifa lakini hapo hapo anazungumzia habari ya Halmashauri kuendelea kujenga shule hizi. Je, anaweza akatuambia baada ya shule hizi za Kata, kuanzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne, Serikali imeshajenga shule ngapi za Kidato cha Tano na cha Sita?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Tatizo la uhaba wa umeme ni kubwa sana nchi nzima, na hili linatokana na gharama kubwa ya nguzo. Nilikuwa naomba kujua ni lini Serikali itachukua ushauri kwamba nguzo ziwe ni gharama za Serikali lakini zile gharama nyingine ziwe ni za watu binafsi kama ilivyokuwa kwenye masuala mazima ya simu, kwamba nguzo za simu zilikuwa bure, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu huo ili wananchi wengi waweze kupata umeme?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitwa Susan Lyimo. Nashukuru kwa majibu mafupi sana ambayo hayana uelekeo; nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati ya UKIMWI ilipotembelea MSD, pamoja na mambo mengine ilipata taarifa kwamba kuna shehena kubwa sana ya dawa za UKIMWI ambayo ilikwama bandarini kwa sababu ya kutokulipa VAT, nataka kujua kama dawa zile tayari yameshaondoka bandarini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; natambua kwamba wafadhili wengi walisema watajitoa na hivyo Serikali ikaanzisha Mfuko wa UKIMWI, nataka kujua mpaka sasa hivi mfuko huo una kiasi gani cha fedha hasa ikizingatiwa kwamba wagonjwa hawa au waathirika hawa wakishaanza kutumia madawa wanapaswa kuendelea kuyanywa mpaka mwisho wa maisha yao. Nataka kujua mfuko huo toka umeanzishwa mpaka leo una kiasi gani cha fedha na tusipewe ahadi za uongo kama ambavyo tumesikia?
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Ni wazi kwamba suala la Palliative Care yaani Tiba Shufaa hapa nchini halijaeleweka kabisa, naamini hata wewe labda huelewi na vilevile Wabunge wengi sana hawaelewi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa yuko tayari, kutoa semina kwa Wabunge wote ili wapate uelewa wa maana ya Palliative Care? Vilevile, elimu hii pia itolewe kwa wananchi wote ili waweze kulielewa na waweze kuwasaidia wagonjwa wetu ambao wanakufa katika mazingira magumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba tuna tatizo kubwa la wahudumu wa afya, ambao pia hawana huo uelewa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, kuna haja kubwa sasa ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na curriculum ya Palliative Care katika courses za undergraduate kama wanavyofanya wenzetu wa Kenya na Uganda ili sasa tuwe na wataalam wa kutosha kwa hii huduma, hasa tukizingatia sasa kwamba kuna magonjwa mengi ya kusendeka (chronic diseases) ambayo yako nyingi na kwa maana hiyo, wagonjwa ni wengi na hawapati huduma hiyo?
MHE. SUSAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Katika siku hizi za karibuni, Tanzania tumepata sifa kubwa sana ya kuwa na chuo kikubwa sana Afrika Mashariki na Kati, Chuo Kikuu cha Dodoma; na chuo hiki kinaweza kuchukua takribani wanafunzi 40,000. Kwa mshangao mkubwa sana, leo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kufanya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa sehemu ya majengo ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Serikali kwa kuleta utaratibu wa kubadili au wa kuchanganya wanafunzi na majengo ya Serikali (Wizara), maana yake ni kwamba tunachukua wanafunzi wetu kuwapekeleka kwenye simba. Nataka kujua huu ndiyo utaratibu wa kuhamia Dodoma kwa maana ya kubadilisha miundombinu ya elimu kuwa Ofisi za Serikali? Naomba majibu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa suala hili linahusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, nilitaka kujua je, wastaafu wa Afrika Mashariki wa nchi nyingine walishalipwa lakini Tanzania imekuwa inasuasua na kuna sintofahamu wakati ambapo wengine wanasema wameshalipwa, bado tunatambua kuna wastaafu wengi wa Tanzania hawajalipwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka tamko la Serikali, je, wastaafu hao ni kweli wamelipwa wote na kama bado kuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wastaafu wao au warithi wao wanapata fedha zao? Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's