Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Juma Selemani Nkamia

Supplementary Questions
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru sana Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuleta hizi fedha haraka na kujua umuhimu wa wananchi wa Chemba na Kondoa kutokana na tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningeomba hizi shilingi milioni 600 anazosema Mheshimiwa Waziri, ziliingia akaunti ya DAWASCO Dodoma toka Januari mwaka jana, mpaka leo hiyo fedha haijaingia katika Halmashauri ya Kondoa. Je, yuko tayari sasa, kusukuma ili fedha hii iingie kati ya leo na kesho?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ucheleweshwaji wa miradi mingi ya maji umechangiwa sana na flow ya fedha kutoka Hazina kwenda kwenye Halmashauri. Je, Wizara sasa iko tayari kupeleka fedha hizi haraka ili miradi mingi nchini iweze kukamilika hasa hii ya maji ambayo wakandarasi wengi wameanza kutishia sasa kwenda Mahakamani?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kwa rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali anasema, Serikali ilifanya maamuzi lakini swali langu lilikuwa Serikali ina mpango gani wa kununua mashine kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili? Mashine anayoizungumzia Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ni mashine ambayo imechukuliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma, katika Chuo Kikuu cha Dodoma, ikahamishiwa Muhimbili. Swali la kwanza, je, anaweza kukiri kwamba ni kweli hiyo mashine anayoizungumzia ni ile iliyochukuliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa katika Chuo Kikuu cha Dodoma kupelekwa Muhimbili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Dodoma pia kuna wagonjwa. Unapohamisha mashine ya CT-Scan kutoka Dodoma kupeleka Muhimbili na unakuja hapa unasema ziko mbili sasa, unataka watu wa Dodoma wafe? (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Nina swali moja dogo tu. Wilaya nyingi mpya za Tanzania hazina Hospitali za Wilaya ikiwemo Wilaya ya Chemba ninakotoka mimi. Je, Serikali itatuhakikishia ndani ya Bunge hili kwamba katika bajeti inayokuja wametenga fedha kujenga hospitali mpya katika Wilaya zote mpya Tanzania?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja dogo la nyongeza. Katika usambazaji wa umeme kwenye hii REA Phase II, Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba, umeme ule umepelekwa kwenye nyumba ya Mkuu wa Wilaya tu. Pia katika vijiji vya Gwandi, Farko na Kwamtoro ambavyo vilikuwepo kwenye programu hii havijapelekewa hata nguzo. Mheshimiwa Waziri naomba anihakikishie hapa kwamba je, mpaka kufika Juni miradi hii itakuwa imekamilika?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kutuona hasa sisi watu wa huku nyuma. Mimi nina swali moja tu. Kipande cha barabara cha kilometa nane kutoka Chuo cha Mipango hadi Msalato, huu ni mwaka wa tatu hakijakamilika na wakandarasi walishaondoka eneo hilo, tunavyozungumza hivi barabara ya kutoka njiapanda ya Usandawe pale Zamahero hadi Bonga karibu inakamilika, lakini kilometa nane hizi hakuna chochote kinachoendelea.
Mheshimiwa Waziri atuhakikishie hapa wananchi wa Dodoma na Wabunge wote hapa, lini kipande hicho kitakamilika?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza. Mji wa Dodoma ni Mji unaokua kwa haraka sana na leo tunategemea asilimia mia moja ya maji kutoka katika visima vilivyoko pale Mzakwe. Moja kati ya juhudi zilizokuwa zimebuniwa na Serikali ni pamoja na kutengeneza bwawa la Farkwa, ambalo litaleta maji hapa Dodoma kupeleka Bahi, Chemba na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie Watanzania na wananchi wote wa Dodoma, kwamba ni lini mradi huu wa bwawa la Farkwa utaanza kujengwa kwa sababu sasa hivi tayari wananchi wameshaambiwa wasiendeleze nyumba zao na miradi yao mingine wakisubiri ujenzi uanze. Naomba Mheshimiwa Waziri atuhakikishie ni lini bwawa hili litaanza kujengwa na lini wananchi wataanza kulipwa fidia?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nkamia, kwanza umeuliza swali mara mbili lakini naona kama kuna maswali matatu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi unisamehe tu kwa leo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba ujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nkamia.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba unisamehe tu, maswali yangu yatakuwa marefu kidogo kwa mara ya kwanza katika historia yangu ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kabisa Mheshimiwa Naibu Waziri anachosema humu ndani ni majibu aliyoandikiwa kutoka huko huko kwenye matatizo, waliomwandikia ndiyo chanzo cha mgogoro huu. Sasa swali la kwanza; je, yuko tayari kwenda mwenyewe badala ya kusubiri majibu anayoandikiwa kutoka huko Kiteto?
Swali la pili, hivi sasa wapo wakulima kutoka Chemba, Kongwa, Kondoa na maeneo mengine ambayo wafugaji wameamua kwenda kuchunga mashamba yao wakati yakiwa na mazao shambani na hakuna chochote kinachofanywa na mamlaka ya utawala wa Kiteto. Je, kama ninyi Waheshimiwa Mawaziri mmeshindwa kutatua tatizo hili, mko tayari sasa kuturuhusu tumwombe Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli akamalize tatizo hili?
niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, lakini kabla ya hayo kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Dada yangu na Shemeji yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake, pamoja na Wizara nzima kwa hatua za haraka walizochukua baada ya ugonjwa wa hatari kuibuka kule Wilayani Chemba, kwa kweli nawashukuru sana na wanafanya kazi yao vizuri sana.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, bei ya dawa za binadamu hasa kwenye maduka ya watu binafsi imekuwa ni kubwa mno, kiasi kwamba watu wenye kipato cha chini wanashindwa kumudu gharama. Je, chombo hicho cha kudhibiti dawa kitaundwa lini?
Swali la pili, katika maduka mengi ya dawa, hasa vijijini dawa nyingi hazina ubora, lakini nyingi zinauzwa zikiwa tayari muda wake wa matumizi umekwisha na inawezekana wananchi wetu wengi wanatumia dawa hizi zikiwa tayari zime-expire. Je, Serikali hili inaliona? Kama inaliona inachukua hatua gani?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Shule ya Sekondari ya Kuryo, iliyoko Wilayani Chemba ina historia ndefu sana. Shule hii inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya ya Wazazi kimeshindwa kuiendesha shule hii na sasa hivi imefungwa na ina miundombinu yote, je, Serikali iko tayari sasa kuichukua shule hii kutoka mikononi mwa Chama cha Mapinduzi na kuikabidhi Halmashauri ya Chemba ili iweze kufanya kazi yake vizuri?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Maji wa Ntomoko ambao chanzo chake kipo Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya vijiji vya Wilaya ya chemba, na Wilaya ya Kondoa. Mradi huu haujakamilika hadi sasa na tumeambiwa kwamba vijiji viwili, kijiji cha Jangalo na Madaha hawatapata maji, licha ya kwamba fedha hizi zilitolewa ili na wao wapate maji kwenye mradi huu.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana kwenda kukutana na Mkurugenzi wa Kondoa na Chemba ili tufanye makubaliano sasa pesa zile zilizokuwa zikamilishe mradi huu zisogezwe ili tuchimbe visima walau viwili kwa ajili ya Jangalo na Madaha
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Nkamia, ahsante. Najua umenikosea kwa sababu leo niko tofauti kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nina swali moja tu la nyongeza. Wala sina tatizo lolote na Wakuu wa Wilaya, lakini kama Serikali Kuu inashindwa kumhudumia Mkuu wa Wilaya, anakwenda kuomba Halmashauri ambayo inaongozwa na Mkurugenzi, hiyo checks and balances inatoka wapi? Haoni kwamba Wakuu wengi wa Wilaya watakuwa ni ombaomba sasa kwa sababu OC wanazopata ni kidogo na matokeo yake wanaishi kwa kutegemea fadhila za Wakurugenzi?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la usalama ni jambo la msingi sana kwa raia wa Tanzania, kumekuwa na matukio mengi sana ya watu kupigwa na wengine kuuawa katika mpaka wa Kiteto na Chemba. Polisi wa eneo hili hasa wale wa Wilaya ya Chemba walioko Mrijo wanashindwa kufuatilia matukio haya kutokana na ukosefu wa vifaa ikiwemo magari, wengi wanaazima pikipiki na wakati mwingine baiskeli. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vifaa vinapatikana katika maeneo ambayo kuna matatizo kama haya ili kunusuru wananchi na mali zao?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Maswali mengi kuhusu hizi milioni 50 tunaulizwa sisi Wabunge kwenye majimbo yetu. Wakati mwingine tunashindwa kutoa majawabu sahihi kwa sababu Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu utoaji wa hizi shilingi milioni 50. Je, Mheshimiwa Waziri Serikali iko tayari sasa kwenda front na kutangaza kwamba wananchi wasubiri mpaka Baraza la Mawaziri likae ili liweze kutoa utaratibu wa kutoa hizi fedha ili sisi Wabunge tusipate wakati mgumu tunapokuwa Majimboni mwetu kuulizwa suala la shilingi milioni 50?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja tu dogo la nyongeza. Katika mwaka huu wa fedha kuna baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Chemba vimeorodheshwa kwamba vitapata umeme. Nataka Mheshimiwa Waziri na Serikali nzima hii inihakikishie mradi huu utaanza kutekelezwa lini?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya viongozi katika ngazi za Wilaya, hasa ma-DC na ma-DAS, wengi wao wamekuwa wababe na wamekuwa wakitumia madaraka yao kuwanyanyasa wananchi kwa kisingizio eti wao ni Marais wa Wilaya. Wakati nafahamu katika uchaguzi uliopita tumemchagua Rais mmoja tu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Je, Serikali haioni hili linaweza kuwa ni tatizo kubwa sana? Na inawezekana kama tutaendelea bila kufanya utafiti wa kutosha na kuwachunguza watu hawa wanaweza kuharibu hata imani ya wananchi kwa Chama cha Mapinduzi?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza. Tatizo la Hifadhi ya Ngorongoro linafanana sana na lile tatizo la Hifadhi ya Swagaswaga ambalo linaunganisha Wilaya za Kondoa na Chemba. Kumekuwa
na matatizo watu wengi wamezuiwa kulima na
nilishakwenda mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri katika eneo hilo na akatoa maagizo kwamba, ufanyike utaratibu wa kuweka mipaka upya, lakini jambo hili halijafanyika hadi sasa. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuweka mipaka ili
wananchi wa Lahoda, Kisande, Iyoli pamoja na Handa waweze kuondokana na tatizo hili?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekuwa ikipeleka fedha kidogo kidogo kwenye Halmashauri hizi ambazo ni mpya. Je, haioni kwamba sasa hakuna sababu ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala kabla ya kumaliza maeneo ambayo tayari yameshaanzishwa na uendeshaji wake unasuasua?
Swali la pili, kuendesha Halmashauri ni gharama
kubwa; kunahitaji huduma za afya, miundombinu na
vinginevyo. Je, Serikali iko tayari sasa kuongeza bajeti kwenye
Halmashauri mpya zote nchini ili kuziondoa kabisa katika hali
ambayo sio nzuri sana kwa sasa na kuacha kabisa zoezi la
kuanzisha maeneo mapya ya utawala?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza. Gereza la Kondoa linahudumia Wilaya ya Chemba na Wilaya ya Kondoa. Gereza hili limejengwa mwaka 1919, lina hali mbaya sana.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa pengine hata Waziri aende tu aone pale kama kweli hawa wafungwa bado ni binadamu, lakini wanaishi kwenye mazingira mabaya sana. Askari wana hali mbaya sana, hata Mkuu wa Gereza anatembea na boda boda. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari hata kwenda tu?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mradi wa Ntomoko ambao ulipangwa kuhudumia Wilaya za Kondoa na Chemba unaonekana dhahiri ni kama umechezewa. Je, Serikali iko tayari sasa kupokea ushauri wangu kwanza kusimamisha malipo ya mkandarasi aliyekuwepo na ifanye ukaguzi wa kutosha kwa sababu mradi huu ni kama hauna manufaa yoyote kwa wananchi?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri na ya uhakika ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nilikuwa na swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya Chemba ni moja kati ya Wilaya kubwa sana katika Mkoa huu wa Dodoma na pengine kwa Tanzania kwa ujumla. Je, Serikali wakati inasubiri kujenga jengo la Mahakama katika Makao Makuuya Wilaya iko tayari sasa kuimarisha mahakama za Mrijo na kwa Mtoro ili kupunguza adha inayowafanya wananchi kutembea zaidi ya kilometa 170 kufuata huduma za mahakama Wilayani Kondoa?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali dogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi ndani ya Bunge kwamba ingeweza kumaliza migogoro ya wananchi na mapori ya hifadhi mwezi Desemba mwaka jana. Moja kati ya maeneo ambayo yanakabiliwa na mgogoro mkubwa sana ni pamoja na eneo la Swagaswaga katika Wilaya ya Chemba ambako wananchi wamekuwa wakifukuzana na askari wanyamapori kila siku.
Ningeomba kauli ya Serikali, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri anajiandaa kwenda Urambo, hapa Chemba ni karibu sana, yuko tayari kwenda Chemba pale kabla ya kwenda Urambo?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali moja dogo tu la nyongeza.
Nheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaipongeza Serikali kwa kutoa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi wa maji wa Ntomoko kule Kondoa na Chemba.
Swali langu ni kwamba pamoja na Serikali kutoa fedha hizi mradi ule umehujumiwa Serikali inajua na wananchi wa Kondoa na Chemba wanajua na waliohujumu mradi huu wamehamishwa kutoka Halmashauri ya Kondoa kwenda Halmashauri nyingine. Nilitaka kujua ni nini kauli ya Serikali kuhusu hali hii? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Job Yustino Ndugai

Kongwa (CCM)

Contributions (1)

Profile

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Kiembesamaki (CCM)

Questions / Answers(3 / 0)

Contributions (6)

Profile

View All MP's