Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Supplementary Questions
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo.
Kwa kuwa, katika swali la msingi suala zima linaloongelewa ni juu ya elimu na faida inayotokana na faida na ulipaji wa kodi. Kwa kuwa tumekuwa mashuhuda katika baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa tukipata fedha kutoka kwa wafadhili nikitolea mfano wa barabara iliyojengwa kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga unakuta kuna vibao ambavyo vimeandikwa kwamba pesa hii imetokana na walipa kodi wa Marekani.
Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kwa ile miradi ambayo inakamilishwa kwa pesa ya ndani, vikawekwa vibao ili kuhamasisha ulipaji wa kodi kwamba miradi hii inatokana na ulipaji kodi ya Watanzania?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza naomba nishukuru majibu ambayo yametolewa na Naibu Waziri na naipongeza Serikali kwa utendaji mahiri wa kazi ambazo zinakuwa zinaletwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, kwa kuwa, umuhimu wa barabara kwa suala zima la kiuchumi halina mbadala; na kwa kuwa, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa imeachwa nyuma kwa maana ya ukosefu wa barabara kwa kiwango cha lami, na kwa kuwa, umuhimu wa barabara kwa junction ya kuanzia Kangesa, kwenda Liapona, Kazila, unapita Mwaze pale anapotoka Muadhama Polycarp Pengo, hadi kwenda kufika Kijiji cha Mozi ambapo ndiyo customs, ni ya muhimu sana na iko chini ya TANROADS. Je, Serikali iko tayari kuiingiza katika mpango wa kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa katika bajeti ya 2016/2017 barabara hii haijaingizwa kwa ujenzi wa kiwango cha lami: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari nimkabidhi barua ya maombi maalum ili iingizwe katika mpango wa kuanza usanifu kwa 2017/2018?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni matarajio yangu makubwa kwamba, Serikali inakuwa na majibu ambayo hayabadiliki kutokana na muda. Swali kama hili nimeliuliza na Serikali ikakiri umuhimu wa barabara hii kwa sababu inaondoa takribani kilometa 100 na wakatutaka tutume ombi maalum. Je, ni lini Serikali itajenga kipande hiki ili barabara hii iendelee kutumika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipofika Kalambo kuja kuomba kura tarehe 25/8 akiambatana na Mheshimiwa Lukuvi, alimtaka Mkurugenzi atangaze haraka kabisa ujenzi wa kivuko cha Mto Kalambo kwa sababu ya umuhimu wake. Je, ni lini kandarasi hii itatangazwa ili kivuko hicho kiweze kujengwa?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili kama ifuatavyo:-
(a) Mpaka sasa Wizara imeweza kutoa leseni ngapi za utafiti wa madini katika Wilaya ya Kalambo?
(b) Kwa kuwa kuna taarifa kwamba kuna uwezekano mkubwa sana wa kupatikana mafuta hasa ndani ya Ziwa Tanganyika ambalo linafika mpaka Kalambo, je, Serikali imefanya jitihada gani za makusudi kuhakikisha kwamba utafiti huu unafanyika na kukamilika ili tuweze kupata mafuta ndani ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kwa ujumla wake?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa kulikuwa na mpango ambao ulisemekana kwamba Serikali ilikuwa inanunua meli tatu Korea Kusini na sasa hivi katika majibu ambayo yanatolewa na Serikali ni kama mpango ule umekufa kabisa.
Je, Serikali ituambie ina mpango gani kuhakikisha kwamba hizo meli ambazo zilikuwa zinunuliwe kutoka Korea Kusini zinanunuliwa na kupelekwa katika maziwa yote matatu?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa sababu swali la msingi limeongelea kuhusiana na tatizo kubwa la umeme na Wilaya ya Kalambo ni miongoni mwa Wilaya chache ambazo zilikuwa na umeme sifuri, je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini wananchi wa Kalambo juu ya vijiji vile ambavyo havijapata umeme kupatiwa umeme kabla hatujaenda awamu ya III?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali ambayo kimsingi sijaridhika sana, naomba kwanza niifahamishe Serikali kwamba maporomoko ya Kalambo ni ya pili Afrika yakifuatiwa na maporomoko ya Victoria. Kwa hiyo, yana unyeti na upekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuifahamisha Serikali, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mazungumzo yalikuwa yameshaanza kati ya Halmashauri ya Kalambo na TANAPA wakijua umuhimu wa maporomoko haya. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuhakikisha kwamba anayasukuma mazungumzo haya na ili maporomoko ya Kalambo yapandishwe hadhi na kuchukuliwa na TANAPA? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa maporomoko ya Kalambo yapo mpakani mwa Tanzania na Zambia na wenzetu wa upande wa Zambia wamekuwa wakiyatumia na kuyatangaza maporomoko haya na wakinufaika pamoja na kwamba scenery nzuri iko upande wa Tanzania. Je, Serikali iko tayari kuweka mkakati mahsusi kuhakikisha kwamba maporomoko haya yanafanyiwa promotion ya pekee?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya
nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakati naandika swali hili, nilitaka lijibiwe na Wizara ya Fedha na si kwamba nilikuwa nimekosea kwa kuitaka Wizara ya Fedha ijibu swali hilo.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika na Serikali wanakiri pale ambapo mwekezaji unampunguzia badala
ya kulipa asilimia 25 akalipa asilimia 10 maana yake hiyo ni pesa ambayo ingeweza kwenda kwa Watanzania, ni tax ambayo ilitakiwa kuwa imekusanywa, haikukusanywa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, isingekuwa busara nafasi hiyo inekuwa imetolewa kwa Mtanzania awae
yeyote ambaye ananunua mabasi ya aina hiyo either anapeleka Mwanza, anapeleka Sumbawanga akaweza
kupata fursa kama hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, katika utaratibu wa Serikali kujenga barabara hizi kwa awamu ya kwanza
ambayo imeshakamilika sasa tunaenda awamu ya pili na mpak aya tatu, ni wazi kwamba Serikali itaendelea kuwekeza na katika hali ya kawaida ili muweze kugawana lazima kila mmoja aoneshe rasilimali ambayo amewekeza. Je, ni busara kwamba pamoja na uwekezaji ambao utaendelea kuwekwa na Serikali, bado mwekezaji huyu aendelee kumiliki asilimia 51 na Serikali ibaki na asilimia 49?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la moja. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameonesha utayari wa kutembelea vivutio mbalimbali na kimsingi hajakuwa na ziara hivi karibuni ya kutembelea Nyanda za Juu Kusini ili akajionee maporomoko ya pili Afrika ya Kalambo pamoja na Ngome ya Bismark iliyoko Kasanga. Je, katika mwezi huo Agosti aliojipanga atatembelea na Nyanda za Juu Kusini?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali. Kwa kutambua na kukiri umuhimu wa mradi huu, naomba nipatiwe majibu; lini mradi huu utakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba commitment ya Serikali kwamba hiyo 2018/2019 hakika pesa itatengwa kwenye bajeti.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika awamu iliyotangulia Wilaya ya Kalambo ilipatia umeme vijiji vichache sana kutokana na scope ya kazi iliyokuwa imetolewa. Je, Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba vile vijiji ambavyo vilikuwa viwe kwenye REA Awamu ya Pili vinaanza kuwekewa umeme haraka iwezekanavyo, ikiwepo kijiji cha Mwazi ambacho tayari transfoma iko pale ni suala la kushusha umeme pamoja na kijiji cha Kazila? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri ni shuhuda, tulienda naye, akaenda kijiji cha Samazi na Ukanda wa Ziwa Tanganyika, miundombinu ya kule alikiri jinsi ambavyo iko haja kubwa ya kuhakikisha kwamba umeme unafika maeneo yale.
Je, yupo tayari kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapatiwa umeme haraka iwezekanavyo?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's